Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 8 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 36...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..! Adonai..!Elohim..!El Olam..!El Qanna..!
El Elyon..!El shaddai..!Emanueli...!-Mungu pamoja nasi...
Unastahili sifa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Jehovah,
Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unastahili Kutukuzwa Baba wa Mbinguni....!



Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!





Mungu wa nguvu Mwenyezi-Mungu, amenena, amewaita wakazi wa dunia, tokea mawio ya jua hadi machweo yake. Kutoka Siyoni, mji mzuri mno, Mungu anajitokeza, akiangaza. Mungu wetu anakuja, na sio kimyakimya: Moto uunguzao wamtangulia, na dhoruba kali yamzunguka. Kutoka juu anaziita mbingu na dunia; zishuhudie akiwahukumu watu wake: “Nikusanyieni waaminifu wangu, waliofanya agano nami kwa tambiko!” Mbingu zatangaza uadilifu wa Mungu; kwamba Mungu mwenyewe ni hakimu.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....





“Sikilizeni watu wangu, ninachosema! Israeli, natoa ushahidi dhidi yako. Mimi ni Mungu! Mimi ni Mungu wako! Sikukaripii kwa sababu ya tambiko zako; hujaacha kunitolea tambiko za kuteketeza. Kwa kweli sina haja na fahali wa zizi lako, wala beberu wa mifugo yako; maana wanyama wote porini ni mali yangu, na maelfu ya wanyama milimani ni wangu. Ndege wote wa mwitu ni mali yangu, na viumbe vyote hai mashambani ni vyangu. Kama ningeona njaa singekuambia wewe, maana ulimwengu na vyote vilivyomo ni vyangu. Je, wadhani nala nyama ya fahali, au Kunywa damu ya mbuzi? Shukrani iwe ndio tambiko yako kwa Mungu mtimizie Mungu Aliye Juu ahadi zako.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Yahweh  tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni

Yahweh ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...






Uniite wakati wa taabu, nami nitakuokoa, nawe utaniheshimu.” Lakini Mungu amwambia mtu mwovu: “Ya nini kuzitajataja tu sheria zangu? Kwa nini unasemasema juu ya agano langu? Wewe wachukia kuwa na nidhamu, na maneno yangu hupendi kuyafuata. Ukimwona mwizi unaandamana naye, na wazinzi unashirikiana nao. Uko tayari daima kunena mabaya; kazi ya ulimi wako ni kutunga uongo. Wakaa kitako kumsengenya binadamu mwenzako, naam, kumchongea ndugu yako mwenyewe. Umefanya hayo yote nami nimenyamaa. Je, wadhani kweli mimi ni kama wewe? Lakini sasa ninakukaripia, ninakugombeza waziwazi. “Fikirini vizuri jambo hili, enyi msionijali, la sivyo nitawaangamizeni, wala hapatakuwa na wa kuwaokoeni. Anayenipa shukrani kama tambiko yake, huyo ndiye anayeniheshimu; yeyote anayedumu katika njia yangu, huyo ndiye nitakayemwokoa.”



Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao
 

Baba wa Mbinguni tunayaweke haya yote mikono mwako
tukiamini Mungu wetu utawatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!



Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu
kwakuwanami/kunisoma Mungu Baba aendelee
kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima
Nawapenda. 
 


Mfalme Yehoahazi wa Yuda

(2Fal 23:30-35)

1Watu wa Yuda walimtwaa Yehoahazi, mwana wa Yosia, wakamtawaza awe mfalme mahali pa baba yake. 2Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala kwa muda wa miezi mitatu huko Yerusalemu. 3Baadaye mfalme wa Misri alimwondoa huko Yerusalemu na akaitoza nchi kodi ya kilo 3,400 za fedha na kilo 34 za dhahabu. 4Kisha mfalme wa Misri akamweka Eliakimu, nduguye Yehoahazi, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu, akabadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu; lakini Neko akamtwaa Yehoahazi nduguye mpaka Misri.

Mfalme Yehoyakimu wa Yuda

(2Fal 23:36–24:7)

5Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, akatawala kwa muda wa miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake. 6Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alimshambulia, akamfunga kwa pingu ili kumpeleka mateka Babuloni. 7Nebukadneza pia alitwaa baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu akavipeleka Babuloni na kuviweka katika ikulu yake huko Babuloni. 8Basi, matendo mengine ya Yehoyakimu, pamoja na machukizo aliyotenda na mengine yaliyoonekana dhidi yake tazama yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda. Yehoyakini36:8 Yehoyakini: Au Yekonia. mwanawe alitawala badala yake.

Mfalme Yehoyakini wa Yuda

(2Fal 24:8-17)

9Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka minane36:9 labda miaka kumi na minane kama ilivyoandikwa katika 2Fal 24:8. alipoanza kutawala. Alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu na siku kumi. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. 10Mwaka ulipokwisha, mfalme Nebukadneza alituma wajumbe, wakamchukua Yehoyakini mateka hadi Babuloni, pamoja na vyombo vya thamani vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Akamtawaza Sedekia, nduguye, kuwa mfalme wa Yuda na Yerusalemu.

Mfalme Sedekia wa Yuda

(2Fal 24:18-20; Yer 52:3-11)

11Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka kumi na mmoja. 12Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, wala hakunyenyekea mbele ya nabii Yeremia ambaye alisema maneno yaliyotoka kwa Mwenyezi-Mungu.

Yerusalemu yaangammia

(2Fal 25:1-21; Yer 52:3-11)

13Sedekia alimwasi pia mfalme Nebukadneza aliyekuwa amemfanya aape kwa jina la Mungu kwamba hatamwasi. Alikuwa mkaidi sana na mwenye kiburi akakataa kumgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. 14Hata makuhani, viongozi wa Yuda pamoja na watu walikosa uaminifu kabisa wakiiga matendo yote ya kuchukiza ya watu wa mataifa mengine; waliichafua nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambayo yeye mwenyewe alikuwa ameitakasa huko Yerusalemu. 15Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, mara kwa mara alituma kwao wajumbe wake maana alikuwa na huruma kwa watu wake na makao yake. 16Lakini wao waliendelea kuwadhihaki wajumbe wa Mungu, wakayapuuza maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka hatimaye ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya watu wake hata kusiwe na namna yoyote ya kutoroka. 17Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu alimleta mfalme wa Wakaldayo ambaye aliwaangamiza vijana wao kwa upanga hata ndani ya mahali patakatifu; wala hakumhurumia mtu yeyote awe mvulana au msichana, mzee au mnyonge. Wote Mwenyezi-Mungu aliwatia mikononi mwake. 18Alitwaa vyombo vyote vya nyumba ya Mungu vikubwa na vidogo na hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya mfalme na maofisa wake. Alivipeleka vyote mpaka Babuloni. 19Aliichoma moto nyumba ya Mungu, akaubomoa ukuta wa Yerusalemu, akayachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu vyombo vyake vyote vya thamani. 20Watu walionusurika vitani aliwachukua uhamishoni Babuloni. Huko wakawa watumwa wake na wa wazawa wake mpaka mwanzo wa ufalme wa Persia. 21Hivyo likatimia neno la Mwenyezi-Mungu alilosema nabii Yeremia: “Nchi itabaki tupu bila kulimwa miaka sabini kulingana na muda wa pumziko ambao haukuadhimishwa.”

Koreshi awaamuru Wayahudi warudi kwao

(Ezr 1:1-4)

22Mnamo mwaka wa kwanza wa utawala wa Koreshi, mfalme wa Persia, ili litimie neno la Mwenyezi-Mungu alilolinena kwa njia ya nabii Yeremia, Mwenyezi-Mungu alimfanya Koreshi, mfalme wa Persia, atangaze amri ifuatayo katika ufalme wake wote na kuiweka katika maandishi:
23“Hivi ndivyo anavyosema Koreshi mfalme wa Persia: Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, amenipatia falme zote za ulimwenguni, na ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, nchini Yuda. Basi, sasa kila mtu katika nyinyi nyote mlio watu wake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake na awe pamoja naye, na aende.”


2Mambo ya Nyakati36;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: