Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Swahili na Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 16 August 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..32


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu..
Asante Baba wa Mbinguni,Mungu wetu na Mlinzi wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Jehovah..!Yahweh..!Alfa na Omega..!
Utukuzwe Baba yetu,Uhimidiwe,usifiwe na uabudiwe daima..Mfalme ashangilia, ee Mwenyezi-Mungu, kwa nguvu yako, anafurahi mno kwa msaada uliompa. Umemtimizia matakwa ya moyo wake; wala hukumkatalia ombi lake. Umemjia, ukampa baraka nzurinzuri; umemvika taji ya dhahabu safi kichwani mwake. Alikuomba maisha nawe ukampa; ulimpa maisha marefu milele na milele. Kwa msaada wako ametukuka sana; wewe umemjalia fahari na heshima. Wamjalia baraka zako daima; wamfurahisha kwa kuwako kwako. Mfalme anamtumainia Mwenyezi-Mungu; kwa fadhili za Mungu Mkuu atakuwa salama.

Asante Baba wa Mbinguni kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwa nguvu zetu wala ufahamu wetu Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo..
Ni kwa neema/rehema zako Baba wa Mbinguni..


Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyeyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Muumba wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwatenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah..Nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu na nguvu za mpinga Kristo zishindwe katika Jina laYesu..

Yahweh tunaomba ututakase Miili yetu na Akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate upona..


Nani aliyeamini mambo tuliyosikia? Nani aliyetambua kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu ulihusika? Maana, mbele yake Mwenyezi-Mungu, mtumishi wake alikua kama mti mchanga, kama mzizi katika nchi kavu. Hakuwa na umbo wala sura ya kutupendeza, wala hakuwa na uzuri wowote wa kutuvutia. Alidharauliwa na kukataliwa na watu, alikuwa mtu wa uchungu na huzuni. Alikuwa kama mtu kinyaa kwa watu; alidharauliwa na tukamwona si kitu. Hata hivyo alivumilia majonzi yetu, na kubeba huzuni zetu. Sisi tulifikiri amepata adhabu, amepigwa na Mungu na kuteswa. Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu. Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai; kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote tumepotea kama kondoo, kila mmoja wetu ameelekea njia yake. Lakini Mwenyezi-Mungu alimtwika adhabu, ambayo sisi wenyewe tuliistahili. Alidhulumiwa na kuteswa, lakini alivumilia kwa unyenyekevu, bila kutoa sauti hata kidogo. Alikuwa kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, kama kondoo akaavyo kimya anapokatwa manyoya. Hakutoa sauti hata kidogo. Alidhulumiwa, akahukumiwa na kupelekwa kuuawa; na hakuna mtu aliyejali yanayompata. Alifukuzwa kutoka nchi ya walio hai, kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Walimzika pamoja na wahalifu; katika kifo aliwekwa pamoja na matajiri, ingawa hakutenda ukatili wowote, wala hakusema neno lolote la udanganyifu. Mwenyezi-Mungu alipenda kumwumiza na kumweka katika huzuni. Alijitoa mhanga kwa ajili ya kuondoa dhambi. Mtumishi wa Mungu atakuwa na wazawa; ataishi maisha marefu. Yeye ndiye atakayetimiza mpango wa Mwenyezi-Mungu. Mungu asema: “Baada ya kutaabika sana, mtumishi wangu atafurahi. Kwa kuwajibika kwake kikamilifu, atatosheka na matokeo hayo. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwadilifu atawafanya wengi wawe waadilifu Yeye atazibeba dhambi zao. Kwa hiyo, nitamweka katika cheo cha wakuu, atagawa nyara pamoja na wenye nguvu; kwa kuwa alijitolea mwenyewe kufa, akawekwa katika kundi moja na wakosefu, alizibeba dhambi za watu wengi, akawaombea msamaha hao wakosefu.”

Mfalme wa Amani tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
nasi tunaomba utupe neema yakuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Mungu wetu utuepushe katika kiburi,majivuno,Ubinafsi,chuki na vyote vinavyokwenda kinyume nawe..


Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wote wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi, zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, zikateketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikamea, zikakua na kuzaa: Moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia.” Kisha akawaambia, “Mwenye masikio na asikie!” Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano. Naye akawaambia, “Nyinyi mmejaliwa kujua siri ya ufalme wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano, ili, ‘Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe.’”

Ukaonekane Mungu wetu katika maisha yetu na popote tupitapo,tunenapo tukanene yaliyo yako,ukatupe Neema ya kusimamia Neno lako,Amri na Sheria zako wakati wote..


Basi, Yesu akawauliza, “Je, nyinyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? Mpanzi hupanda neno la Mungu. Watu wengine ni kama walio njiani ambapo neno lilipandwa. Lakini mara tu baada ya kulisikia, Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu walisikiapo hilo neno hulipokea kwa furaha. Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno, mara wanakata tamaa. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaosikia hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia.” Yesu akaendelea kuwaambia, “Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. Mwenye masikio na asikie!” Akawaambia pia, “Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.” Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.” Tena, Yesu akasema, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake.” Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Asante Mungu wetu katika yote..
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni wapendwa kwa kuwa nami..
Mungu mwenye upendo aendelee kuwatendea katika yote yampendezayo..
Nawapenda.
 


Makabila ya mashariki ya Yordani

(Kumb 3:12-22)

1Makabila ya Reubeni na Gadi yalikuwa na mifugo mingi sana. Basi, walipoona kwamba eneo la Yazeri na Gadi lilifaa kwa mifugo, 2waliwaendea Mose, kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, wakawaambia, 3“Miji ya Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni, 4nchi ambayo Mwenyezi-Mungu alishinda kwa ajili ya jumuiya ya Israeli, ni nchi nzuri kwa mifugo, nasi tunayo mifugo mingi sana. 5Basi, kama mkitukubalia tunawaomba mtupe nchi hii iwe mali yetu; msituvushe ngambo ya mto Yordani.”
6Mose akawajibu watu wa makabila ya Gadi na Reubeni, “Je, mnataka kubaki hapa huku ndugu zenu Waisraeli wanakwenda vitani? 7Mbona mnawavunja moyo Waisraeli wasiende katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu amewapa? 8Taz Hes 13:17-33 Hivyo ndivyo walivyofanya babu zenu nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea kuipeleleza nchi. 9Wao walikwenda hadi bonde la Eshkoli, wakaiona nchi, lakini waliporudi, waliwavunja moyo Waisraeli ili wasiingie katika nchi aliyowapa Mwenyezi-Mungu. 10Taz Hes 14:26-35 Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira siku hiyo, akaapa akisema, 11‘Hakika hakuna mtu yeyote kati ya watu waliotoka Misri mwenye umri wa miaka ishirini na zaidi atakayeiona nchi niliyoapa kuwapa Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwa sababu hawakunitii kikamilifu.’ 12Wote hawataiona, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, maana wao wamenitii kikamilifu. 13Mwenyezi-Mungu aliwaka hasira dhidi ya Waisraeli, akawafanya watangetange jangwani kwa muda wa miaka arubaini; kizazi kizima kilichokuwa kimefanya maovu mbele yake kikafariki. 14Na sasa, enyi kizazi cha wenye dhambi, mmezuka mahali pa wazee wenu, kuongeza tena hasira kali ya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Waisraeli. 15Kama nyinyi mkikataa kumfuata, yeye atawaacheni tena jangwani, nanyi mtasababisha watu hawa wote waangamie.”
16Basi, wakamwendea Mose, wakamwambia, “Kwanza turuhusu tuwajengee kondoo wetu mazizi, na watoto wetu miji hapa. 17Lakini sisi wenyewe tutachukua silaha zetu tayari kwenda vitani pamoja na ndugu zetu Waisraeli, na tutakuwa mstari wa mbele vitani hadi tuwafikishe mahali watakapokaa. Wakati huo watoto wetu watakaa kwenye miji yenye ngome, ili kujilinda na wenyeji wa nchi hii. 18Hatutarudi nyumbani hadi hapo Waisraeli wengine wote watakapomiliki maeneo yao waliyogawiwa. 19Hatutamiliki mali yoyote miongoni mwao ngambo ya mto Yordani, kwa sababu sisi tumepata maeneo yetu ngambo hii, mashariki ya mto Yordani.”
20Mose akawaambia, “Kama kweli mtafanya kama mlivyosema, basi papa hapa mbele ya Mwenyezi-Mungu, chukueni silaha zenu kwenda vitani. 21Kila mpiganaji wenu atavuka mto Yordani na mkiwa chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mtawashambulia adui zetu mpaka Mwenyezi-Mungu awashinde, 22na kuimiliki nchi. Mkisha fanya hayo, mtarudi, maana mtakuwa mmetimiza wajibu wenu kwa Mwenyezi-Mungu na ndugu zenu Waisraeli. Kisha Mwenyezi-Mungu atakubali nchi hii ya mashariki ya Yordani kuwa mali yenu. 23Lakini nawaonyeni kwamba msipotimiza ahadi yenu, mtakuwa mnamtendea Mwenyezi-Mungu dhambi; jueni kwa hakika kwamba mtaadhibiwa. 24Wajengeeni watoto wenu miji na kondoo wenu mazizi; lakini fanyeni kama mlivyoahidi.”
25Kisha, watu wa Gadi na wa Reubeni wakamwambia Mose, “Sisi watumishi wako tutafanya kama ulivyotuamuru. 26Wake zetu, watoto wetu na kondoo na ng'ombe, watabaki hapa katika miji ya Gileadi. 27Lakini sisi watumishi wako tuko tayari kwenda vitani chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu. Tutavuka mto Yordani na kupigana, kama ulivyosema.”
28Basi, Mose akatoa amri zifuatazo kwa kuhani Eleazari, kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kwa viongozi wa jamaa za makabila ya Waisraeli: 29“Ikiwa watu wa Gadi na wa Reubeni watavuka mto Yordani pamoja nanyi wakiwa na silaha zao chini ya uongozi wa Mwenyezi-Mungu, mkashinda na kuichukua nchi hiyo, basi mtawapa nchi ya Gileadi iwe mali yao. 30Lakini kama hawatavuka mto Yordani pamoja nanyi na silaha zao, basi watamiliki sehemu ya nchi ya Kanaani pamoja nanyi.”
31Watu wa Gadi na wa Reubeni wakajibu, “Bwana, sisi tutafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyotuambia sisi watumishi wako. 32Chini ya uongozi wake Mwenyezi-Mungu, tutavuka na silaha zetu mpaka nchini Kanaani, lakini nchi tuliyopewa hapa mashariki ya Yordani itakuwa mali yetu.”
33Basi, Mose akawapa watu wa makabila ya Gadi na Reubeni na nusu ya kabila la Manase mwana wa Yosefu, nchi yote ya mfalme Sihoni wa Waamori na nchi ya mfalme Ogu wa Bashani pamoja na miji na maeneo yaliyokuwa kandokando ya miji hiyo. 34Kabila la Reubeni likaijenga miji ya Diboni, Atarothi, Aroeri, 35Atroth-shofani, Yazeri, Yogbeha, 36Beth-nimra na Beth-harani, miji yenye ngome na mazizi ya kondoo. 37Kabila la Gadi lilijenga miji ya Heshboni, Eleale, Kiriathaimu, 38Nebo na Baal-meoni (majina ya hiyo miji yalibadilishwa), na Sibma. Miji waliyoijenga waliipa majina mengine.
39Wazawa wa Makiri, mwana wa Manase, waliishambulia nchi ya Gileadi, wakaiteka na kuwafukuza Waamori waliokuwa wanakaa humo. 40Kwa hiyo, Mose akawapa watu wa ukoo wa Makiri mwana wa Manase, nchi ya Gileadi, nao wakakaa humo. 41Yairi, wa kabila la Manase, alishambulia vijiji kadhaa vya Gileadi na kuviteka, akavipa jina Hawoth-yairi.32:41 Hawoth-yairi: Maana yake “Vijiji vya Yairi”. 42Naye Noba aliishambulia na kuiteka Kenathi na vijiji vyake, akauita Noba, jina lake mwenyewe.
Hesabu32;1-42Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: