Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 21 August 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..35


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu, Baba yetu ametupa kibali cha kuendelea kuiona,Mfalme wa Amani tunaanza nawewe kwa kila jambo..

Asante Baba yetu Mungu wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
Jehovah..!Yahweh..!Baba wa Upendo,Baba wa Rehema,Baba wa Baraka..
Muweza wa yote,Alfa na Omega..!Hakuna kama wewe Mungu wetu..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa..
Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..
Unatosha Mungu wetu..!

Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine..Mfalme wa Amani tunaomba ukatawale katika maisha yetu..
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.
Siku moja, watozaushuru na wenye dhambi wengi walikwenda kumsikiliza Yesu. Mafarisayo na waalimu wa sheria wakaanza kunungunika: “Mtazameni mtu huyu! Anawakaribisha wenye dhambi, na tena anakula nao.” Yesu akawajibu kwa mfano: “Hivi, mmoja wenu akiwa na kondoo 100, akigundua kwamba mmoja wao amepotea, atafanya nini? Atawaacha wale tisini na tisa mbugani, na kwenda kumtafuta yule aliyepotea mpaka ampate. Akimpata, atambeba mabegani kwa furaha. Anapofika nyumbani, atawaita rafiki zake na kuwaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimempata yule kondoo wangu aliyepotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo kutakavyokuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya kutubu kwa mwenye dhambi mmoja, kuliko kwa ajili ya watu tisini na tisa wanaojiona kuwa wema, wasiohitaji kutubu. “Au mwaonaje? Tuseme mwanamke fulani ana sarafu kumi za fedha, akipoteza moja, atafanya nini? Atawasha taa, ataifagia nyumba na kuitafuta kwa uangalifu mpaka aipate. Akiipata, atawaita rafiki na jirani zake na kusema, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata ile sarafu yangu iliyopotea.’ Kadhalika nawaambieni, ndivyo watakavyofurahi malaika wa Mungu kwa sababu ya mwenye dhambi mmoja anayetubu.” Yesu akaendelea kusema, “Kulikuwa na mtu mmoja mwenye watoto wawili wa kiume. Yule mdogo alimwambia baba yake: ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Naye akawagawia mali yake. Baada ya siku chache, yule mdogo aliuza urithi wake, akasafiri na fedha aliyopata, akaenda nchi ya mbali ambako aliitumia ovyo. Alipomaliza kutumia kila kitu, kukatokea njaa kali katika nchi ile, naye akaanza kuhangaika. Akaomba kazi kwa mwananchi mmoja wa huko naye akampeleka shambani mwake kulisha nguruwe. Alitamani kula maganda waliyokula wale nguruwe, ila hakuna mtu aliyempa kitu. Alipoanza kupata akili, akafikiri: ‘Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kusaza, nami ninakufa njaa? Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ Basi, akaanza safari ya kurudi kwa baba yake. Alipokuwa bado yu mbali, baba yake alimwona, na kwa moyo wa huruma alimkimbilia, akamkumbatia na kumbusu. “Mwanae akamwambia: ‘Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.’ Lakini baba yake akawaambia watumishi wake: ‘Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike! Mvisheni pete na viatu! Mchinjeni ndama mnono; tule na kusherehekea! Kwa sababu huyu mwanangu; alikuwa amekufa, kumbe yu hai; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kufanya sherehe. “Wakati huo kaka yake alikuwa bado shambani. Alipokuwa akirudi na kukaribia nyumbani, akasikia vifijo na ngoma. Akamwita mmoja wa watumishi, akamwuliza: ‘Kuna nini?’ Huyo mtumishi akamwambia: ‘Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.’ Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. Lakini yeye akamjibu: ‘Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwanambuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu! Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.’ Baba yake akamjibu: ‘Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako. Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”




Ndugu zangu Mungu wetu atupe neema ya kuweza kuwasamehe wengine ili nasi atusamehe..
Haijalishi umepitia nini,umeumizwa kiasi gani,umetendwaje..
Tumuombe Mungu atupe roho ya kusamehe na kumaliza..
Atupe neema ya kuchukuliana na kuwa makini tutakapo maliza jambo hilo ili tusirudie tena makosa..
Mangapi tumekwenda kinyume na Mungu?
Mara ngapi tumeanguka na Mungu wetu ametuinua?
Mungu kama angehesabu ni mara ngapi tumekosea leo hii tungekuwa wapi? Jiulize Mungu amekuokoa na mangapi?Mungu amekutendea mangapi ambayo kwa macho au mawazo yako ulishashindwa?
Mungu wetu akatupe neema ya kuonyana kwa hekima na busara..
tukatue mizigo isiyo yetu..Tumuombe Mungu akatende leo na siku zote tukapate kupona rohoni..


Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti, huwapa hekima wasio na makuu. Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa, huufurahisha moyo; amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi, humwelimisha mtu. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema, na la kudumu milele; maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa, yote ni ya haki kabisa. Yatamanika kuliko dhahabu; kuliko dhahabu safi kabisa. Ni matamu kuliko asali; kuliko asali safi kabisa. Yanifunza mimi mtumishi wako; kuyafuata kwaniletea tuzo kubwa. Lakini nani aonaye makosa yake mwenyewe? Ee Mungu, niepushe na makosa nisiyoyajua. Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi, usikubali hayo yanitawale. Hapo nitakuwa mkamilifu, wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa. Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu na mkombozi wangu!

Mungu wetu tunaomba ukatutakase Miili yetu na Akili zetu na ukatufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Mungu wetu ndiyo mkombozi wetu..

Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Jehovah tukatende sawasawa na mapenzi yako..

Ukabariki Nyumba zetu/Ndoa,Watoto wetu/familia,Ndugu/jamaa na wote wanaotuzunguka Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu..

Mungu wetu tusipungukiwe katika mahita yetu Baba wa Mbinguni ukatupe kama inavyokupendeza wewe..
Yahweh ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..

Mfalme wa Amani tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa,wenye shida/tabu na wote waliokatika vifungo mbalimbali Mungu wetu ukawaongoze na kuwapa neema ya kusimamia Neno lako nao wakapate kuwa huru..

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Ukaonekane Mungu wetu popote tupitapo,tunenapo tukanene yaliyo yako..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama ipasavyo kupitia Neno lako, Amri na sheria zako..

Sifa na utukufu  tunakurudishia Mungu wetu.
kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Baba wa upendo akawaongoze katika yote na upendo wenu usiwe bure..
Nawapenda.



Miji ya Walawi

1 Taz Yosh 21:1-42 Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose katika tambarare za Moabu, ngambo ya mto Yordani karibu na Yeriko, akamwambia, 2“Waamuru Waisraeli kwamba kutokana na urithi watakaomiliki, wawape Walawi miji ya kukaa na sehemu za malisho kandokando ya miji hiyo. 3Miji hiyo itakuwa yao, nao watakaa humo na malisho yake yatakuwa kwa ajili ya ng'ombe na mifugo yao pamoja na wanyama wao wengine. 4Malisho ya maeneo mtakayowapa Walawi kandokando ya miji yataenea kila upande umbali wa mita 450 kutoka kwenye kuta za miji hiyo. 5Kwa hiyo, eneo hilo la malisho litakuwa la mita 900, na litaenea kila upande wa mji, mji wenyewe ukiwa katikati. Eneo hilo litakuwa malisho yao kandokando ya miji yao. 6Mtawapa Walawi miji sita ya makimbilio ambapo mtu akimuua mwenzake bila kukusudia ataruhusiwa kukimbilia. Pamoja na hiyo, mtawapa miji mingine arubaini na miwili. 7Jumla ya miji mtakayowapa Walawi itakuwa arubaini na minane; mtawapa miji hiyo pamoja na sehemu za malisho yake. 8Idadi ya miji mtakayowapa Walawi katika urithi wa Waisraeli itategemea ukubwa wa kabila; kabila kubwa litatoa miji mingi na kabila dogo litatoa michache. Kila kabila litatoa miji yake kwa ajili ya Walawi kulingana na eneo litakalorithi.”

Miji ya makimbilio

(Kumb 19:1-13; Yosh 20:1-9)

9Mwenyezi-Mungu akaongea na Mose, akamwambia, 10Waambie Waisraeli kwamba wakati mtakapovuka mto Yordani na kuingia nchini Kanaani, 11mtachagua miji itakayokuwa miji ya makimbilio ambamo kama mtu akimuua mwenzake bila kukusudia ataweza kukimbilia. 12Miji hiyo itakuwa mahali pa kukimbilia usalama ili huyo mwuaji asiuawe na mwenye kulipiza kisasi kabla ya kuhukumiwa na jumuiya. 13Mtajitengea miji sita kwa ajili ya makimbilio. 14Kati ya miji hiyo sita mtakayoitenga, mitatu iwe mashariki ya Yordani, na mitatu iwe katika nchi ya Kanaani. 15Miji hii itakuwa ya makimbilio kwa ajili ya Waisraeli na wageni wa kudumu au wa muda wanaokaa pamoja nao. Mtu yeyote akimuua mwingine bila kukusudia anaweza kukimbilia huko.
16“Lakini mtu akimpiga mwenzake kwa kitu cha chuma, akafa, mtu huyo ni mwuaji na ni lazima auawe. 17Mtu yeyote akimpiga mwenzake kwa jiwe, akifa, mtu huyo ni mwuaji, na lazima auawe. 18Kama akimpiga mwenzake kwa silaha ya mti ambayo yaweza kusababisha kifo, akafa, mtu huyo ni mwuaji, na ni lazima auawe. 19Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi. Huyu atakapokutana na huyo mwuaji, atatekeleza hukumu ya kifo.
20“Hali kadhalika, kama mtu anamchukia mwenzake halafu, akamsukuma au kumtupia kitu kwa kumvizia, 21au kwa kumpiga ngumi akafa, basi mtu huyo aliyempiga mwenzake ni mwuaji na ni lazima auawe. Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi atakapokutana naye.
22“Lakini kama mtu akimsukuma mwenzake kwa ghafla bila chuki au kumtupia kitu bila kumvizia 23au mtu akirusha jiwe linaloweza kusababisha kifo, akamuua mtu bila kukusudia, ingawa hakuwa adui yake wala hakutaka kumdhuru, 24basi, jumuiya itaamua kati ya huyo mwuaji na jamaa ya mtu aliyeuawa anayetaka kulipiza kisasi, kulingana na sheria hizi. 25Jumuiya itamwokoa mtu huyo aliyeua mikononi mwa jamaa ya mtu aliyeuawa, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alimokuwa amekimbilia. Atakaa huko mpaka kifo cha kuhani mkuu wa wakati huo aliyeteuliwa kwa kupakwa mafuta matakatifu. 26Lakini huyo aliyeua akitoka nje ya mji aliokimbilia wakati wowote ule, 27halafu jamaa ya mtu aliyeuawa akampata nje ya mipaka ya mji huo wa makimbilio akamuua, huyo hatakuwa na hatia ya kuua. 28Maana huyo aliyeua ni lazima akae ndani ya mji wa makimbilio mpaka kuhani mkuu atakapofariki; lakini baada ya kifo cha kuhani mkuu anaweza kurudi nyumbani.
29“Sheria hizi zitatumika katika vizazi vyenu vyote, mahali popote mtakapokaa.
30 Taz Kumb 17:6, 19:15 “Mtu yeyote atakayeua mtu, atahukumiwa kifo kutokana na ushahidi wa mashahidi wawili au zaidi; mtu yeyote hawezi kuhukumiwa kifo kutokana na ushahidi wa mtu mmoja.
31“Msipokee fidia yoyote kuokoa maisha ya mwuaji aliyepatikana na hatia, akahukumiwa kifo; mtu huyo lazima auawe. 32Msipokee wala msikubali fidia yoyote kutoka kwa mtu aliyekimbilia mji wa makimbilio ili kumruhusu arudi kukaa nyumbani kwake kabla ya kifo cha kuhani mkuu. 33Mkifanya hivyo mtakuwa mnaitia unajisi nchi ambayo mnakaa. Umwagaji damu huitia nchi unajisi, na hakuna sadaka iwezayo kuitakasa nchi iliyofanyiwa mauaji isipokuwa kwa kumuua mwuaji huyo. 34Msiitie unajisi nchi ambayo mnakaa, nchi ambayo mimi ninakaa; maana mimi Mwenyezi-Mungu ninakaa miongoni mwenu Waisraeli.”



Hesabu35;1-34



Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: