Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Swahili na Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 9 June 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mambo Ya Walawi..11...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?

Ni siku nyingine tena Mungu ametuchagua na kutupa Kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwa uwezo wetu wala si kwa nguvu zetu,si kwamba sisi ni wema sana au wazuri mno kuliko wengine ambao leo hii wapo vitandani,wapo waliotangulia/kufa,wengine wapo hoi hata kuita Mungu au kutubu wameshindwa,wapo wanaotamani kuandika/kusoma kama si kuongea au kuacha wosia/usia kwa wapendwa wao..
Sisi tumempa nini Mungu wetu? ni kwa Neema/Rehema zake Mungu sisi kuwepo na kuwa hivi tulivyo..
Tumshukuru Mungu kwa wema na Fadhili zake na tukatumie nafasi hii aliyotupa vizuri  kwa kutenda yaliyo mema na tuzidi kumtafuta kwa maana anapatikana..
Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yake..
Asante Mungu wetu na Baba yetu uliye Mbinguni..
Asante kwa kulinzi wako wakati wote na kutuamsha salama..
Tazama Jana imepita Baba wa Mbinguni Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine..

Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mungu wetu, kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakuju/kutojua..Mfalme wa Amani..
Tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe nasi waliotukosea..
utuepushe na Majaribu Mungu wetu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake..ututakase na kutufunika kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu pia tupate kutambua/kujitambua..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.
Tunaomba utubariki na kubariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda,na ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..
Maisha yetu yapo mikononi mwako Mungu wetu..
yote tuliyoyanena na tusiyo yanena Mungu wetu unayajua na kutujua kuliko tunavyojijua sisi..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi utupe neema ya kuwabariki wanaohitaji..
Baba wa Mbinguni  tusipungukiwe katika mahitaji yetu na ukatupe sawasawa na mapenzi yako..Mimi Yuda, mtumishi wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo, nawaandikia nyinyi mlioitwa na Mungu na ambao mnapendwa naye Mungu Baba, na kuwekwa salama kwa ajili ya Yesu Kristo. Nawatakieni huruma, amani na upendo kwa wingi.

Tunarudisha Sifa na utkufu ni wako,Tunakushukuru na kukusifu Daima..
Kwakua Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu  hata Milele...
Amina..!!Kwake yeye awezaye kuwalinda msije mkaanguka, na kuwaleta nyinyi bila hatia mpaka mbele ya utukufu wake, kwake yeye aliye peke yake Mungu, Mkombozi wetu, uwe utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kwa njia ya Kristo Bwana wetu, tangu zama zote, sasa na hata milele! Amina.


Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kutembelea hapa..
Mungu akawaongoze katika maisha yenu na msipungukiwe katika mahitaji yenu na akawape sawasawa na mapenzi yake..
Sina neno zuri kwenu zaidi ya kuwaombea na kuwaambia..
Nawapenda.

Wanyama najisi na wasio najisi
(Kumb 14:3-21)

1Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, 2“Wawaambie Waisraeli hivi: 3Kati ya wanyama wote duniani, mmeruhusiwa kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua. 4Lakini msile mnyama yeyote ambaye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili, au ambaye kwato zake zimegawanyika lakini hacheui. Msile ngamia, kwani hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili. Kwenu huyo ni najisi. 5Pelele msimle; yeye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika; kwenu huyo ni najisi. 6Sungura msimle; yeye hucheua lakini kwato zake hazikugawanyika; kwenu huyo ni najisi. 7Nguruwe msimle; ana kwato zilizogawanyika lakini hacheui; kwenu huyo ni najisi. 8Kwa sababu wanyama hao ni najisi msile nyama yao wala msiguse mizoga yao.
9“Samaki yeyote wa baharini au mtoni mwenye mapezi na magamba, mnaweza kumla. 10Lakini chochote kinachoishi baharini au mitoni, ambacho hakina mapezi wala magamba, yaani viumbe vyote viendavyo majini na viumbe vingine vyote viishivyo majini ni najisi kwenu. 11Viumbe hivyo vitakuwa daima najisi kwenu. Msile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao kwani ni najisi. 12Chochote kinachoishi majini ambacho hakina mapezi na magamba ni najisi kwenu.
13“Ndege wote wafuatao ni najisi kwenu; hivyo msile: Tai, furukombe, kipungu, 14mwewe, aina zote za kozi, 15aina zote za kunguru, 16mbuni, kirukanjia, dudumizi, aina zote za kipanga, 17bundi, mnandi, bundi kubwa, 18mumbi, mwari, mderi, 19korongo, aina zote za koikoi, hudihudi na popo.
20“Wadudu wote wenye mabawa na waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu. 21Lakini, baadhi ya wadudu wenye mabawa na wanakwenda kwa miguu minne ya kurukia ardhini mnaweza kula. 22Hao ni: Kila aina ya nzige, kila aina ya senene, kila aina ya panzi na kila aina ya parare. 23Lakini wadudu wengine wote wenye mabawa na miguu minne ni najisi kwenu.
24“Kugusa wanyama fulanifulani humfanya mtu kuwa najisi; yeyote atakayegusa mizoga yao atakuwa najisi mpaka jioni. 25Mtu akichukua sehemu ya mizoga yake atakuwa najisi mpaka jioni, na mavazi yake ni lazima yafuliwe. 26Mtu yeyote akigusa mnyama mwenye kwato zilizogawanyika lakini hacheui, mtu huyo atakuwa najisi. 27Wanyama wote waendao kwa vitanga vyao ingawa wana miguu minne, ni najisi kwenu; na yeyote atakayegusa mzoga wa mnyama kama huyo atakuwa najisi mpaka jioni. 28Mtu yeyote anayebeba mzoga atakuwa najisi, naye atasafisha mavazi yake. Hao ni najisi kwenu.
29“Viumbe vifuatavyo ni najisi kwenu: Kicheche, panya, kila aina ya mjombakaka, 30guruguru, kenge, mijusi, goromwe, na kinyonga. 31Hao wote ni najisi kwenu na yeyote atakayegusa mizoga yao, atakuwa najisi mpaka jioni. 32Ikiwa mzoga wa viumbe hao unakiangukia kitu chochote, kiwe ni kifaa cha mbao au vazi au ngozi au gunia au chombo chochote kitumiwacho kwa kusudi lolote lile, chombo hicho kitakuwa najisi mpaka jioni. Ili kukifanya kiwe safi ni lazima kukiosha kwa maji. 33Ikiwa mzoga wake umeangukia chombo cha udongo, basi, chochote kilicho ndani ya chombo hicho ni najisi na lazima chombo hicho kivunjwe. 34Chakula au kinywaji chochote kilichokuwa ndani ya chombo hicho kitakuwa najisi. 35Kila kitu ambacho sehemu ya mzoga imekiangukia, kitakuwa najisi. Ikiwa ni tanuri au jiko, ni lazima kivunjwe. Vitakuwa najisi navyo ni najisi kwenu. 36Hata hivyo, kisima au chemchemi ya maji vitakuwa safi. Lakini chochote kinachogusa mzoga kitakuwa najisi. 37Iwapo sehemu ya mzoga inaziangukia mbegu za kupanda, mbegu hizo hazitakuwa najisi. 38Lakini ikiwa mbegu zimetiwa katika maji ili kuota na sehemu yoyote ya mzoga ikaziangukia, basi, mbegu hizo ni najisi kwenu.
39“Iwapo mnyama yeyote mnayeruhusiwa kula, anakufa mwenyewe, yeyote atakayegusa mzoga wake, atakuwa najisi mpaka jioni. 40Mtu yeyote akila nyama ya mzoga huo atafua mavazi yake na atakuwa najisi mpaka jioni. Na yeyote atakayebeba mzoga huo, atafua mavazi yake, naye atakuwa najisi mpaka jioni.
41“Kiumbe chochote kitambaacho duniani ni najisi kwenu, kamwe msikile. 42Chochote kiendacho kwa tumbo lake, chochote kiendacho kwa miguu yote minne au nyayo nyingi, naam, chochote kitambaacho, kamwe msikile kwa maana ni najisi kwenu. 43Hivyo msije mkawa najisi kwa kula viumbe vitambaavyo na hivyo mkawa najisi. 44#Taz Lawi 19:21; 1Pet 1:16 Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi Mungu wenu, jiwekeni wakfu na kuwa watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu. 45Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndimi niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu; kwa hiyo muwe watakatifu kwa maana mimi ni mtakatifu.”
46Hiyo basi, ndiyo sheria kuhusu wanyama, ndege na viumbe vyote hai ambavyo huishi majini na nchi kavu, 47ili kupambanua kati ya kisicho najisi na kilicho najisi; kinachoweza kuliwa na kisichoweza kuliwa.

Mambo Ya Walawi11;1-47


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: