Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 7 August 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Zekaria 14...

 

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Upande wa ndani wa kuta za nyumba aliufunika kwa mbao za mierezi, kutoka sakafuni mpaka kwenye boriti za dari; na sakafu akaitandika mbao za miberoshi.

1 Wafalme 6:15

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Chumba cha ndani, kilichoitwa mahali patakatifu sana, kilijengwa katika sehemu ya nyuma ya nyumba. Kilikuwa kimejengwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafuni hadi darini, na urefu wake ulikuwa mita 9.

1 Wafalme 6:16

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Nyumba ile iliyokuwa mbele ya mahali patakatifu sana, ilikuwa na urefu wa mita 18. Mbao za mierezi zilizotanda ukuta wa nyumba kwa ndani zilikuwa zimepambwa kwa michoro ya mibuyu na maua yaliyochanua. Kila sehemu ilikuwa imefunikwa kwa mbao za mierezi, wala hapana jiwe lililoonekana.

1 Wafalme 6:17-18

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.


Yerusalemu na watu wa mataifa mengine 
1Tazama, siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu inakuja. Siku hiyo, enyi watu wa Yerusalemu, mali yenu itagawanywa mbele ya macho yenu. 2Mwenyezi-Mungu atayakusanya mataifa yote ili kuushambulia mji wa Yerusalemu. Mji utatekwa, nyumba zenu zitatekwa nyara, na wanawake wenu watanajisiwa. Nusu ya wakazi wa mji watapelekwa uhamishoni, lakini nusu itakayosalia haitachukuliwa nje ya mji. 3Kisha Mwenyezi-Mungu atatoka na kuyapiga vita mataifa hayo, kama afanyavyo daima siku za vita. 4Siku hiyo, atasimama kwenye mlima wa mizeituni ulio mashariki ya mji wa Yerusalemu. Mlima huo utagawanywa sehemu mbili na bonde pana sana litatokea toka mashariki hadi magharibi. Nusu moja itaelekea kaskazini na nusu nyingine kusini. 5Nyinyi mtakimbia kupitia bonde hilo, katikati ya milima miwili ya Mwenyezi-Mungu. Mtakimbia kama wazee wenu walivyokimbia tetemeko la ardhi wakati wa utawala wa mfalme Uzia wa Yuda. Kisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye. 6Wakati huo hakutakuwa baridi wala baridi kali.14:6 baridi wala baridi kali: Maana katika Kiebrania si dhahiri. 7Mchana utaendelea bila giza kuingia. Wakati huo wajulikana kwa Mwenyezi-Mungu peke yake. Hakutakuwa mchana wala usiku, kwa maana hata saa za jioni mwanga utaendelea kuwapo. 8Wakati huo, maji ya uhai yatabubujika kutoka mji wa Yerusalemu, na nusu ya maji hayo yatatiririkia kwenye bahari ya mashariki, na nusu nyingine kwenye bahari ya magharibi. Maji hayo yataendelea kububujika wakati wa kiangazi kama yalivyo wakati wa masika. 9Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye mfalme pekee wa dunia yote; naye atakuwa ndiye Mwenyezi-Mungu pekee, mmoja tu, na jina lake litakuwa ndilo jina pekee. 10Nchi yote, tangu Geba hadi Rimoni, kusini mwa Yerusalemu, itageuzwa kuwa mbuga tambarare kabisa. Lakini mji wa Yerusalemu utabaki juu mahali pake tokea lango la Benyamini mpaka lango la zamani, hadi kwenye lango la Konani, tangu mnara wa Hanareli hadi kwenye mashinikizo ya mfalme. 11Mji wa Yerusalemu utakaliwa na watu kwani ndani yake haitakuwapo laana tena; naam, watu watakaa humo kwa usalama. 12Lakini kuhusu wale watu ambao walikuja kupigana na Yerusalemu, haya ndiyo maafa ambayo Mwenyezi-Mungu atawaletea: Miili yao itaoza wangali hai; macho yao yataoza yakiwa kwenye matundu yake na ndimi zao zitaoza zikiwa vinywani mwao. 13Siku hiyo, hofu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu itawakumba watu, na kila mtu atamshambulia mwenzake. 14Watu wa Yuda watapigana kuulinda mji wa Yerusalemu; utajiri wa mataifa yote yanayoizunguka nchi ya Yuda utakusanywa: Watakusanya dhahabu, fedha na mavazi kwa wingi sana. 15Maafa makubwa yatawakumba farasi, nyumbu, ngamia, punda na wanyama wote watakaokuwamo katika kambi hizo za maadui. 16Kisha, kila mtu aliyesalimika kati ya mataifa yote yaliyokuja kuushambulia mji wa Yerusalemu, atakuwa akija Yerusalemu mwaka hata mwaka, kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, na kuadhimisha sikukuu ya vibanda. 17Iwapo taifa lolote duniani halitakwenda Yerusalemu kumwabudu Mwenyezi-Mungu wa majeshi aliye mfalme, basi, mvua haitanyesha katika nchi yao. 18Iwapo Wamisri watakataa kuiadhimisha sikukuu ya vibanda, basi, Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa ugonjwa uleule atakaowapiga nao mataifa yote yanayokataa kuiadhimisha sikukuu hiyo. 19Hiyo itakuwa ndiyo adhabu itakayolipata taifa la Misri pamoja na mataifa yote yasiyoadhimisha sikukuu ya vibanda. 20Wakati huo, kwenye njuga za farasi yataandikwa maandishi haya: “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu Vyungu vilivyomo katika hekalu la Mwenyezi-Mungu vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu. 21Kila chungu katika mji wa Yerusalemu na nchi ya Yuda kitawekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ili wote wanaotoa tambiko waweze kuvichukua na kuchemshia nyama ya tambiko. Wakati huo, hakutakuwapo mfanya biashara yeyote katika hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

Zekaria14;1-21

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: