Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 25 August 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 8....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Lakini mtu anayeangalia kwa makini sheria kamilifu ambayo huwapa watu uhuru, mtu anayeendelea kuizingatia, na si kuisikia tu na kuisahau baadaye, bali anaitekeleza, mtu huyo atabarikiwa katika kila kitu anachofanya.

Yakobo 1:25

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Kama mtu akijiona kuwa ni mtu mwenye dini, lakini hawezi kuutawala ulimi wake, dini yake haifai kitu, na anajidanganya mwenyewe.

Yakobo 1:26

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Dini iliyo safi na isiyo na hitilafu mbele ya Mungu Baba ni hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika shida zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu huu.

Yakobo 1:27

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.



Yesu anamponya mtu mwenye ukoma 
(Marko 1:40-45; Luka 5:12-16)
 1Yesu aliposhuka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata. 2Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia na kusema, “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!” 3Yesu akanyosha mkono, akamgusa na kusema, “Nataka! Takasika.” Mara huyo mtu akapona ukoma wake. 4Kisha Yesu akamwambia, “Angalia, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajioneshe kwa kuhani, na kutoa sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona.” 

Yesu anamponya mtumishi wa jemadari Mroma 
(Luka 7:1-10) 
5Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, jemadari mmoja alimwendea, akamsihi 6akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana.” 7Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.” 8Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. 9Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, ‘Nenda!’ Naye huenda; na mwingine, ‘Njoo!’ Naye huja; na mtumishi wangu, ‘Fanya kitu hiki!’ Naye hufanya.” 10Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, “Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli mwenye imani kama hii. 11Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika ufalme wa mbinguni. 12Lakini wale ambao ufalme huo ni wao watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno.” 13Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile. 

Yesu anaponya watu wengi 
(Marko 1:29-34; Luka 4:38-41) 
14Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali. 15Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia. 16Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa. 17Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: “Yeye mwenyewe ameuchukua udhaifu wetu, ameyabeba magonjwa yetu.”

 Wanaostahili kuwa wafuasi
 (Luka 9:57-62) 
18Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ngambo ya ziwa. 19Mwalimu mmoja wa sheria akamwendea, akamwambia, “Mwalimu, mimi nitakufuata kokote utakakokwenda.” 20Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia.” 21Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu.” 22Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao.”

 Yesu anaamuru dhoruba itulie 
(Marko 4:35-41; Luka 8:22-25) 
23Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye. 24Mara, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu lakini alikuwa amelala usingizi. 25Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, “Bwana, tuokoe, tunaangamia!” 26Yesu akawaambia, “Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?” Basi, akainuka, akaukemea upepo na lile ziwa; kukawa shwari kabisa. 27Watu wakashangaa, wakasema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na bahari vinamtii!” 

Yesu anaponya watu wawili wenye pepo 
(Marko 5:1-20; Luka 8:26-39) 
28Yesu alifika katika nchi ya Wagadara8:28 Wagadara: Au Wagerase., ngambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita njia hiyo. 29Nao wakaanza kupiga kelele, “Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?” 30Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa. 31Basi, hao pepo wakamsihi, “Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale.” 32Yesu akawaambia, “Haya, nendeni.” Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa majini. 33Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa. 34Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.

Mathayo8;1-34

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: