Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 20 August 2020

Kikombe Cha Asubuhi; Mathayo 5 ....

 


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Mungu wa walio hai,Mungu  mwenye huruma,Mungu wa upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!


Ndugu aliye maskini anapaswa kufurahi wakati Mungu anapomkweza,

Yakobo 1:9

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako,
Tukijinyenyekeza,tukijiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunamomba utusamehe dhambi zetu
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
 ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea

Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


naye tajiri anapaswa kufurahi anaposhushwa na Mungu. Maana tajiri atatoweka kama ua la porini.

Yakobo 1:10

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomna ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Yahwe ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Baba wa Mbinguni  tunaomba ukatupe neema ya kufuata
njia zako,tukasimamie Neno lako,amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu,ukatufanye chombo chema
ee Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Jua huchomoza na kwa joto lake kali hukausha mimea, nayo maua yake huanguka, na uzuri wake wote huharibika. Vivyo hivyo, tajiri ataangamizwa katika shughuli zake.

Yakobo 1:11

Tazama watoto wako wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipo kwenda kinyume nawe
Yahweh tunaomba ukawape neema ya kuweza kujiombea,kufuata njia zako nazo zikawaweke huru...
Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...

Nawapenda.
Hotuba mlimani 
1Yesu alipoyaona makundi ya watu, alipanda mlimani, akaketi. Wanafunzi wake wakamwendea, 2naye akaanza kuwafundisha: 

Furaha ya kweli 
(Luka 6:20-23) 
3“Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao. 4Heri walio na huzuni, maana watafarijiwa. 5 Taz Zab 37:11 Heri walio wapole, maana watairithi nchi. 6Heri wenye njaa na kiu ya kufanya atakavyo Mungu, maana watashibishwa. 7Heri walio na huruma, maana watahurumiwa. 8 Taz Zab 24:3-4 Heri wenye moyo safi, maana watamwona Mungu. 9Heri wenye kuleta amani, maana wataitwa watoto wa Mungu. 10Heri wanaoteswa kwa sababu ya kufanya atakavyo Mungu, maana ufalme wa mbinguni ni wao. 11“Heri yenu nyinyi watu wakiwatukana, wakiwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. 12Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu. 

Chumvi na mwanga 
Marko 9:50; Luka 14:34-35 
13“Nyinyi ni chumvi ya dunia. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake itakolezwa na nini? Haifai kitu tena, ila hutupwa nje na kukanyagwa na watu. 14“Nyinyi ni mwanga wa ulimwengu! Mji uliojengwa juu ya mlima hauwezi kufichika. 15Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa debe, ila huiweka juu ya kinara ili iwaangazie wote waliomo nyumbani. 16Vivyo hivyo, ni lazima mwanga wenu uangaze mbele ya watu, ili wayaone matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

 Kuhusu sheria
 17“Msidhani kuwa nimekuja kutangua sheria na mafundisho ya manabii. Sikuja kutangua bali kukamilisha. 18Kweli nawaambieni, mpaka hapo mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata nukta moja au sehemu ndogo kabisa ya sheria itakayoondolewa, mpaka yote yametimia. 19Basi, yeyote atakayevunja hata amri moja ndogo kuliko zote, na kuwafundisha wengine wafanye hivyo, huyo atakuwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Lakini yule atakayezishika na kuwafundisha wengine, huyo atakuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. 20Ndio maana nawaambieni, wema wenu usipozidi ule wa waalimu wa sheria na wa Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. 

Kuhusu hasira 
(Luka 12:57-59) 
21“Mmekwisha sikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa: ‘Usiue! Atakayeua lazima ahukumiwe.’ 22Lakini mimi nawaambieni, yeyote anayemkasirikia ndugu yake, lazima ahukumiwe. Anayemdharau ndugu yake atapelekwa mahakamani. Anayemwita ndugu yake: ‘Pumbavu’ atastahili kuingia katika moto wa Jehanamu. 23“Basi, ukipeleka sadaka yako mbele ya madhabahu na hapo ukakumbuka kwamba ndugu yako ana ugomvi nawe, 24iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako, ndipo urudi utoe sadaka yako. 25“Patana na mshtaki wako upesi mkiwa bado njiani kwenda mahakamani. La sivyo, mshtaki wako atakukabidhi kwa hakimu, naye hakimu atakukabidhi kwa askari, nawe utafungwa gerezani. 26Kweli nakuambia, hutatoka humo mpaka umelipa senti ya mwisho.

 Kuhusu uzinzi 
27“Mmesikia kwamba watu waliambiwa: ‘Usizini!’ 28Lakini mimi nawaambieni, atakayemtazama mwanamke kwa kumtamani, amekwisha zini naye moyoni mwake. 29Basi, kama jicho lako la kulia linakukosesha, lingoe ukalitupe mbali. Afadhali zaidi kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu. 30Na kama mkono wako wa kulia unakukosesha, ukate ukautupe mbali. Afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote uende katika moto wa Jehanamu.

 Kuhusu talaka 
(Mat 19:9; Marko 10:11-12; Luka 16:18) 
31“Ilikwisha semwa pia: ‘Anayemwacha mke wake, yampasa ampe hati ya talaka’. 32Lakini mimi nawaambieni, anayempa mkewe talaka, isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, anamfanya azini; na mwanamume akimwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini. 

Kuhusu kiapo 
33“Tena mmesikia kwamba watu wa kale waliambiwa: ‘Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.’ 34Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; 35Taz Zab 48:2 wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. 36Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37Ukisema, ‘Ndiyo’, basi iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu. 

Kuhusu kulipiza kisasi 
(Luka 6:29-30) 
38“Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’ 39Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia la pili. 40Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako. 41Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili. 42Akuombaye mpe, wala usimpe kisogo anayetaka kukukopa kitu.

 Kuwapenda maadui
 (Luka 6:27-28,32-36)
 43“Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Mpende jirani yako, na kumchukia adui yako.’ 44Lakini mimi nawaambieni, wapendeni maadui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu nyinyi, 45ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu. 46Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda nyinyi? Hakuna! Kwa maana, hata watozaushuru hufanya hivyo! 47Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo. 48Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Mathayo5;1-48

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe

No comments: