Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 14 June 2019

Kikombe Cha Asubuhi ;Zaburi 147...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante  Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu


Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni

Neema yako yatutosha  Mungu wetu..!

Kisha nikaona kwamba katika lile anga juu ya vichwa vya viumbe wenye mabawa kulikuwa na kitu kinachofanana na johari ya rangi ya samawati, umbo lake kama kiti cha enzi. Mungu akamwambia yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani, “Nenda katikati ya magurudumu yaliyo chini ya viumbe wenye mabawa, ukaijaze mikono yako makaa ya moto ulioko katikati yao na kuyatawanya juu ya mji.” Nikamwona akienda.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea,Usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote,Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa  Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Wale viumbe wenye mabawa walikuwa wamesimama upande wa kusini wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu yule mtu alipoingia ndani; wingu likaujaza ua wa ndani. Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukapaa juu kutoka kwa wale viumbe wenye mabawa ukaenda kwenye kizingiti cha nyumba hiyo, na lile wingu likaijaza nyumba, na ua ukajaa mngao wa utukufu wa Mwenyezi-Mungu.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe



Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu  wetu ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo 

Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Ukatufanye barua njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Mlio wa viumbe wenye mabawa uliweza kusikika hata kwenye ua wa nje, kama sauti ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi anapoongea. Mwenyezi-Mungu alipomwamuru yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani achukue moto toka katikati ya magurudumu yaliyokuwa chini ya viumbe wenye mabawa, yule mtu alikwenda na kusimama pembeni mwa gurudumu mojawapo. Kiumbe mmoja akanyosha mkono wake kuchukua moto uliokuwa katikati ya viumbe wenye mabawa, akatwaa sehemu yake na kuutia mikononi mwa yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani; naye alipoupokea, akaenda zake.
Tazama wenye shida/tabu,Mungu wetu tunaomba
 ukawaguse kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,macho ya rohoni,masikio yakusikia sauti yako,wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni tunomba ukawafute machozi yao
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!!


Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana
kwakuwanami/kunisoma

Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima....
Nawapenda.

Yafaa kumsifu Mungu
1Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu!
Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa.
2Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu;
anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni.
3Anawaponya waliovunjika moyo;
na kuwatibu majeraha yao.
4Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota,
na kuzipa zote majina yao.
5Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi;
maarifa yake hayana kipimo.
6Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu,
lakini huwatupa waovu mavumbini.
7Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani,
mpigieni kinubi Mungu wetu!
8Yeye hulifunika anga kwa mawingu,
huitengenezea nchi mvua,
na kuchipusha nyasi vilimani.
9Huwapa wanyama chakula chao,
na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia.
10Yeye hataki nguvu za farasi,
wala hapendezwi na ushujaa wa askari;
11lakini hupendezwa na watu wamchao,
watu wanaotegemea fadhili zake.
12Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee Yerusalemu!
Umsifu Mungu wako, ee Siyoni!
13Maana yeye huimarisha milango yako,
huwabariki watu waliomo ndani yako.
14Huweka amani mipakani mwako;
hukushibisha kwa ngano safi kabisa.
15Yeye hupeleka amri yake duniani,
na neno lake hufikia lengo lake haraka.
16Hutandaza theluji kama pamba,
hutawanya umande kama majivu.
17Huleta mvua ya mawe kama kokoto
na kwa ubaridi wake maji huganda.
18Kisha hutoa amri, maji hayo yakayeyuka;
huvumisha upepo wake, nayo yakatiririka.
19Humjulisha Yakobo ujumbe wake,
na Israeli masharti na maagizo yake.
20Lakini hakuyatendea hivyo mataifa mengine;
watu wengine hawayajui maagizo yake.
Msifuni Mwenyezi-Mungu!


Zaburi147;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: