Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 14 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Ezra 4...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu..

Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!



Jitahidini kuwa na upendo. Vilevile fanyeni bidii ya kupata vipaji vingine vya kiroho, hasa kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu. Mwenye kunena lugha ngeni hasemi na watu bali anasema na Mungu. Yeye hunena kwa nguvu ya Roho mambo yaliyofichika. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, husema na watu kwa ajili ya kuwajenga, kuwafariji na kuwatia moyo. Mwenye kunena lugha ngeni anajijenga mwenyewe. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, analijenga kanisa.


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...




Basi, ningependa nyinyi nyote mseme kwa lugha ngeni lakini ningependelea hasa muwe na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, maana mtu mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni wa maana zaidi kuliko yule mwenye kusema lugha ngeni, isipokuwa tu kama yupo hapo mtu awezaye kuyafafanua hayo mambo asemayo, ili kanisa lipate kujengwa. Hivyo, ndugu zangu, kama nikija kwenu na kusema nanyi kwa lugha ngeni itawafaa nini? Haitawafaa chochote, isipokuwa tu kama nitawaelezeni ufunuo wa Mungu au ujuzi fulani au ujumbe wa Mungu au mafundisho fulani. Ndivyo ilivyo kwa vyombo visivyo na uhai vyenye kutoa sauti kama vile filimbi au kinanda. Je, mtu anawezaje kuutambua wimbo unaochezwa kama vyombo hivyo havitoi sauti waziwazi vinapopigwa? La mgambo likilia bila kufuata taratibu zake, nani atajiweka tayari kwa vita? Hali kadhalika na nyinyi, kama ulimi wenu hausemi kitu chenye kueleweka, nani ataweza kufahamu mnayosema? Maneno yenu yatapotea hewani.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Zipo lugha mbalimbali ulimwenguni, na hakuna hata mojawapo isiyo na maana. Lakini ikiwa mimi sifahamu maana ya lugha asemayo mtu fulani, mimi ni mgeni kwake mtu huyo naye pia ni mgeni kwangu. Hali kadhalika na nyinyi, maadamu mna hamu ya kupata vipaji vya Roho, jitahidini hasa kujipatia vile vinavyosaidia kulijenga kanisa. Kwa hiyo, mwenye kunena lugha ngeni na aombe apate uwezo wa kuzifafanua. Maana, nikisali kwa lugha ngeni roho yangu ndiyo inayosali, lakini akili yangu hubaki bure. Nifanye nini, basi? Nitasali kwa roho yangu, nitasali pia kwa akili yangu; nitaimba kwa roho yangu, nitaimba pia kwa akili yangu.


Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.



Ujenzi wa hekalu wapingwa

1Kisha maadui wa watu wa Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanalijenga upya hekalu la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, 2Taz 2Fal 17:24-41 walimwendea Zerubabeli na viongozi wa koo, na kumwambia, “Tafadhali tushirikiane katika ujenzi wa hekalu. Sisi kama nyinyi tunamwabudu Mungu wenu, na tumekuwa tukimtolea tambiko tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru aliyetuleta hapa.”
3Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa koo za Israeli wakawaambia, “Sisi hatuhitaji msaada wowote kutoka kwenu ili kuijenga nyumba ya Mungu wetu. Sisi wenyewe tutamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kama mfalme Koreshi wa Persia alivyotuamuru.” 4Hapo, watu waliokuwa wanaishi mahali hapo wakaanza kuwavunja moyo na kuwatisha Wayahudi ili wasiendelee kama walivyokusudia. 5Tena waliwahonga maofisa wa serikali ya Persia wawapinge Wayahudi. Waliendelea kufanya hivyo muda wote wa utawala wa Koreshi, mpaka wakati wa utawala wa Dario.

Ujenzi mpya wa Yerusalemu wapingwa

6 Taz Esta 1:1 Mwanzoni mwa utawala wa mfalme Ahasuero, maadui wa watu waliokaa Yuda na Yerusalemu waliandika mashtaka dhidi yao.
7Tena wakati wa utawala wa Artashasta, mfalme wa Persia, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli na rafiki zao, walimwandikia barua mfalme Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa herufi za Kiaramu na kutafsiriwa.4:7 Kiebrania si dhahiri.
8Pia mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa, walimwandikia Artashasta barua ifuatayo dhidi ya Yerusalemu:
9“Kutoka kwa mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa pamoja na wenzetu, na mahakimu, maofisa wote ambao hapo awali walitoka Ereki, Babuloni na Susa katika nchi ya Elamu, 10pamoja na watu wa mataifa mengine ambao Asur-banipali, mtu mkuu na mwenye nguvu aliwahamisha na kuwaweka katika mji wa Samaria na mahali pengine katika mkoa wa magharibi ya Eufrate.”
11Barua yenyewe ilikuwa hivi:
“Kwa mfalme Artashasta: Sisi watumishi wako katika mkoa wa magharibi ya Eufrate, tunakutumia salamu. 12Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kwamba Wayahudi waliokuja hapa kutoka maeneo mengine ya ufalme wako wamekwenda Yerusalemu na wanaujenga upya mji huo mwasi na mwovu. Wanamalizia kujenga kuta zake na kutengeneza msingi. 13Tungependa ufahamu, ewe mfalme, kuwa mji huu ukijengwa upya na kuta zake zikimalizika, watu hawatalipa kodi, ushuru wala ada, na hazina yako itapungua. 14Sasa, kwa kuwa ni wajibu wetu4:14 ni wajibu wetu: Kiebrania: Tunakula chumvi katika ikulu., ee mfalme, hatungependa kuona ukivunjiwa heshima, ndiyo maana tumeona ni vizuri tukuarifu 15ili ufanye uchunguzi katika kumbukumbu za babu zako. Humo utagundua kwamba tangu zamani, mji huu ulikuwa mwasi na umewasumbua sana wafalme na watawala wa mikoa, na kuwa tangu zamani watu wake ni wachochezi sana; ndio sababu mji huo uliangamizwa. 16Kwa hiyo tunakujulisha kwamba ikiwa mji huu utajengwa upya na kuta zake zikimalizika, hutaweza kuutawala mkoa wa magharibi ya Eufrate.”
17Kisha mfalme akapeleka jibu lifuatalo:
“Kwa mtawala Rehumu, kwa Shishai, katibu wa mkoa, pamoja na wenzenu wote wanaoishi Samaria na mahali penginepo katika mkoa wa magharibi ya Eufrate.
18“Barua mliyonitumia imetafsiriwa na kusomwa mbele yangu. 19Nimetoa amri uchunguzi ufanywe na imegunduliwa kuwa ni kweli kwamba tangu zamani mji huu wa Yerusalemu umekuwa ukiwapinga wafalme na kwamba watu wake wamekuwa waasi na wachochezi wakubwa. 20Wafalme wenye nguvu wamepata kuutawala mji huo pamoja na mkoa wa magharibi ya Eufrate wakitoza kodi, ushuru na ada. 21Kwa hiyo, toeni amri watu hao waache kuujenga upya mji huo hadi hapo nitakapotoa maagizo mengine. 22Tena, angalieni sana msichelewe kufanya hivyo, nisije nikapata hasara.”
23Mara tu waliposomewa barua hii kutoka kwa Artashasta, Rehumu, katibu Shimshai na wenzao waliharakisha kwenda Yerusalemu na kuwalazimisha kwa nguvu Wayahudi waache kuujenga mji.

Ujenzi wa hekalu waanza tena

24Kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu ilisimama, na hali hiyo iliendelea mpaka mwaka wa pili wa utawala wa Dario, mfalme wa Persia.


Ezra4;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: