Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 13 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Ezra 3...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!





Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?” Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.” Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.” Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.” Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.” Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki. Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.” Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa. Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.” Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema, “Tazama, harufu nzuri ya mwanangu ni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu! Mungu akumiminie umande wa mbinguni; akupe ardhi yenye rutuba, nafaka na divai kwa wingi. Jamii za watu zikutumikie, na mataifa yakuinamie kwa heshima. Uwe mtawala wa ndugu zako, watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima. Kila akulaaniye na alaaniwe, kila akubarikiye na abarikiwe!”



Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachiliaq mikononi mwako
 Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...




Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokuwa ndio tu ametoka mbele ya baba yake Isaka, Esau kaka yake Yakobo, akarudi kutoka mawindoni. Esau pia akatengeneza chakula kitamu, akampelekea baba yake, akamwambia, “Haya baba, inuka ule mawindo yangu mimi mwanao, ili upate kunibariki!” Isaka akauliza, “Wewe ni nani?” Naye akamjibu, “Ni mimi mwanao Esau, mzaliwa wako wa kwanza.” Hapo Isaka akatetemeka mno, akasema, “Ni nani basi yule aliyewinda na kuniletea mawindo, nami nimekwisha kula kabla hujaja? Tena nimekwisha mbariki; naam, amekwisha barikiwa!” Esau alipoyasikia maneno ya baba yake, akaangua kilio cha uchungu. Kisha akamwambia baba yake, “Ee baba yangu, nibariki na mimi, tafadhali!” Lakini Isaka akasema, “Ndugu yako alikuja kwa hila, naye amechukua baraka yako.” Esau akasema, “Ndio maana anaitwa Yakobo! Amechukua nafasi yangu mara mbili. Kwanza alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua baraka Zangu.” Kisha akamwuliza baba yake, “Je, hukunibakizia baraka yoyote?” Isaka akamjibu, “Nimekwisha mfanya Yakobo kuwa mtawala wako, na kumpa ndugu zake wote kuwa watumishi wake. Nimempatia nafaka na divai. Nikufanyie nini sasa, wewe mwanangu?” Esau akamwambia baba yake, “Baba, kwani una baraka moja tu? Nibariki hata mimi, ee baba!” Hapo Esau akalia kwa sauti kubwa.


Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...





Ndipo Isaka, baba yake, akamwambia, “Makao yako yatakuwa mbali na ardhi yenye rutuba, na mbali na umande wa mbinguni. Utaishi kwa upanga wako, na utamtumikia ndugu yako; lakini utakapoasi utaivunja kongwa yake shingoni mwako.” Basi, Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka aliyokuwa amepewa na baba yake. Esau akawaza, “Siku za matanga ya baba zitakapokwisha, ndipo nitakapomuua ndugu yangu Yakobo.” Lakini Rebeka alipojua nia ya mwanawe mkubwa, akamwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia, “Jihadhari, ndugu yako Esau anajifariji kwa kupanga kukuua. Kwa hiyo, mwanangu, sikiliza maneno yangu. Ondoka ukimbilie kwa kaka yangu Labani kule Harani. Kaa naye kwa muda, mpaka ghadhabu ya nduguyo itakapopoa. Ghadhabu yake itakapopoa, naye atakapokuwa amesahau uliyomtendea, nitatuma mtu akurudishe. Kwa nini nifiwe na nyinyi wote wawili siku moja?” Rebeka akamwambia Isaka, “Sina raha kabisa maishani kwa sababu ya hawa wanawake wa Esau Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mmojawapo wa wanawake hawa Wahiti, maisha yangu yana faida gani?”


Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Kuabudu kunaanza tena

1Baadaye mwezi wa saba ulipofika, na watu wa Israeli wakiwa wamekwisha kaa katika miji yao, wote walikusanyika pamoja mjini Yerusalemu. 2Taz Kut 27:1 Yeshua, mwana wa Yosadaki, pamoja na makuhani wenzake, na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, pamoja na jamaa zake, waliijenga upya madhabahu ya Mungu wa Israeli, ili waweze kumtolea sadaka za kuteketezwa kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtu wa Mungu. 3Taz Hes 29:1-8 Waliijenga madhabahu hiyo mahali palepale ilipokuwa hapo zamani, kwa kuwa waliwaogopa watu waliokuwa wanaishi katika nchi hiyo. Kisha wakawa wanamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu yake kila siku asubuhi na jioni. 4Taz Hes 29:12-38 Waliiadhimisha sikukuu ya vibanda kama ilivyoandikwa katika sheria; kila siku walitoa sadaka za kuteketezwa zilizohitajika kwa ajili ya siku hiyo. 5Taz Hes 28:11–29:39 Walitoa pia sadaka za kawaida ambazo ziliteketezwa nzima, sadaka zilizotolewa wakati wa sikukuu ya mwezi mpya na katika sikukuu nyingine zote alizoagiza Mwenyezi-Mungu. Pia, walitoa tambiko zote zilizotolewa kwa hiari. 6Ingawa msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu ulikuwa bado kuwekwa, watu walianza kutoa sadaka za kuteketezwa tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba.

Ujenzi wa hekalu waanza

7Watu walitoa fedha za kuwalipa maseremala na waashi, walitoa pia chakula, vinywaji na mafuta, ili vipelekwe katika miji ya Tiro na Sidoni kupata miti ya mierezi kutoka Lebanoni. Miti hiyo ililetwa kwa njia ya bahari hadi Yopa. Haya yote yalifanyika kwa msaada wa mfalme Koreshi wa Persia. 8Basi, watu walianza kazi mnamo mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya kufikia nyumba ya Mungu mjini Yerusalemu. Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki, ndugu zao wengine, makuhani, Walawi na watu wengine wote waliorudi Yerusalemu kutoka uhamishoni, walijiunga nao katika kazi hiyo. Walawi wote waliokuwa na umri wa miaka ishirini au zaidi, waliteuliwa ili kusimamia kazi ya kuijenga upya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 9Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi.
10 Taz 1Nya 25:1 Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli. 11Taz 1Nya 16:34; 2Nya 5:13; 7:3; Zab 100:5; 106:1; 107:1;118:1; 136:1; Yer 33:11 Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu:
“Kwa kuwa yu mwema,
fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.”
Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. 12Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha. 13Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana.



Ezra3;1-13

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: