Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 7 August 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2Mambo ya Nyakati 35...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?


Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu kila wakati
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe ee Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Uhimidiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako yanatisha
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu..

Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!



Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika kuungana na Bwana. Sichoki kurudia yale niliyokwisha andika pale awali, maana yatawaongezeeni usalama. Jihadharini na hao watendao maovu, hao mbwa, watu wanaosisitiza kujikata mwilini. Watu waliotahiriwa kikweli ni sisi, si wao; kwani sisi twamwabudu Mungu kwa njia ya Roho wake, na kuona fahari katika kuungana na Kristo Yesu. Mambo ya nje tu hatuyathamini. Mimi pia ningeweza kuyathamini hayo mambo ya nje; na kama yupo mtu anayefikiri kwamba anaweza kuyathamini hayo mambo ya nje, mimi ninayo sababu kubwa zaidi ya kufikiri hivyo: Mimi nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa kwangu; mimi ni wa taifa la Israeli, kabila la Benyamini, Mwebrania halisi. Kuhusu kuizingatia sheria mimi nilikuwa Mfarisayo,


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona

Kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona...



na nilikuwa na bidii sana hata nikalidhulumu kanisa. Kuhusu uadilifu unaopatikana kwa kuitii sheria, mimi nilikuwa bila hatia yoyote. Lakini hayo yote ambayo ningeweza kuyafikiria kuwa ni faida, nimeyaona kuwa ni hasara, kwa ajili ya Kristo. Naam, wala si hayo tu; ila naona kila kitu kuwa ni hasara tupu, kwa ajili ya jambo bora zaidi, yaani kumjua Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa ajili yake nimekubali kutupilia mbali kila kitu; nimeyaona hayo yote kuwa ni takataka, ili nimpate Kristo na kuunganishwa naye kabisa. Mimi sitaki tena uadilifu unaotokana na kuitii sheria. Sasa ninao ule uadilifu unaopatikana katika kumwamini Kristo; uadilifu utokao kwa Mungu na ambao unategemea imani. Ninachotaka tu ni kumjua Kristo na kuiona nguvu ya ufufuo wake, kushiriki mateso yake na kufanana naye katika kifo chake, nikitumaini kwamba nami pia nitafufuliwa kutoka kwa wafu.




Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii

 Mungu wetu ukatupe akili ya kutambua mema na mabaya
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye barua  njema ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...






Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu. Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo. Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa. Ndugu zangu, fuateni mfano wangu. Tumewapeni mfano mwema, na hivyo wasikilizeni wale wanaofuata mfano huo. Nimekwisha waambieni jambo hili mara nyingi, na sasa narudia tena kwa machozi: Watu wengi wanaishi kama maadui wa msalaba wa Kristo. Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia. Lakini sisi ni raia wa mbinguni, na twatazamia kwa hamu kubwa Mwokozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. Yeye ataibadili miili yetu dhaifu na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu, kwa nguvu ile ambayo kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya utawala wake.


Baba wa Mbinguni tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee  kama inavyokupendeza wewe
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
sawasawa na mapenzi yake....

Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na Upendo 
wa Mungu Baba ukae nanyi daima....
Nawapenda.



Yosia aadhimisha Pasaka

(2Fal 23:21-23)

1Mfalme Yosia aliadhimisha Pasaka mjini Yerusalemu, wakachinja wanakondoo wa Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. 2Aliwateua makuhani kwa kazi zao ambazo walihitajika kufanya katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na kuwatia moyo wazifanye kikamilifu. 3Pamoja na hayo, aliwapa Walawi waliowafundisha watu wa Israeli na ambao walikuwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, maagizo yafuatayo: “Liwekeni sanduku takatifu ndani ya nyumba ambayo Solomoni mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli alijenga; hamhitaji kulibebabeba tena mabegani. Sasa mtumikieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu na watu wake Waisraeli. 4Timizeni wajibu wenu kulingana na koo zenu, kufuatana na maagizo ya Daudi mfalme wa Israeli na Solomoni mwanawe. 5Simameni pia mahali patakatifu kama wawakilishi wa jamaa za koo zenu wasiofanya kazi za ukuhani, na kila mmoja aiwakilishe jamaa moja ya Walawi.35:5 maana katika Kiebrania si dhahiri. 6Mchinjeni mwanakondoo wa Pasaka, mjitakase, halafu itayarisheni kwa ajili ya ndugu zenu, ili waweze kutimiza agizo la Mwenyezi-Mungu lililosemwa na Mose.”
7Kisha Yosia aliwapa watu, wanambuzi wapatao 30,000, na mafahali 3,000, wote hawa walitolewa kwenye mifugo ya mfalme. 8Nao maofisa wake, kwa hiari yao, walitoa mchango wao wakawapa watu, makuhani na Walawi. Hilkia, Zekaria na Yehieli, maofisa wa nyumba ya Mungu, waliwapa makuhani wanakondoo na wanambuzi 2,600 na mafahali 300 kwa ajili ya sadaka za Pasaka. 9Naye Konania na nduguze wawili, Shemaya na Nethaneli, pamoja na Hashabia, Yeieli na Yozabadi, waliokuwa viongozi wa Walawi, nao pia waliwapa wanakondoo na wanambuzi 5,000 na mafahali 500, kwa ajili ya sadaka za Pasaka.
10Baada ya matayarisho yote ya Pasaka kumalizika, makuhani walisimama mahali pao, na Walawi katika makundi yao; sawasawa na amri ya mfalme. 11Walimchinja mwanakondoo wa Pasaka, nao makuhani walinyunyiza damu, waliyopokea kutoka kwao nao Walawi waliwachuna wanyama. 12Halafu walitenga sadaka za kuteketeza ili waweze kuzigawa kulingana na jamaa zao walio makuhani ili wamtolee Mwenyezi-Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mose. Nayo mafahali waliwafanya vivyo hivyo. 13Walimchoma mwanakondoo wa Pasaka juu ya moto kama ilivyoagizwa, na pia walizitokosa sadaka takatifu katika vyungu, masufuria na kwenye vikaango, na kuwagawia upesiupesi watu wasiofanya kazi ya ukuhani. 14Baadaye, Walawi wakajiandalia sehemu zao na za makuhani kwa maana makuhani wa uzao wa Aroni walikuwa wanashughulika na utoaji wa sadaka za kuteketeza, na vipande vya mafuta, mpaka usiku; kwa hiyo Walawi waliandaa kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Aroni. 15Nao waimbaji wazawa wa Asafu walishika nafasi zao, kwa mujibu wa maagizo ya mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni, mwonaji wa mfalme. Nao mabawabu walikuwa kwenye malango; hawakuhitajika kuziacha nafasi zao za kazi kwa kuwa ndugu zao Walawi waliwaandalia Pasaka. 16Hivyo basi, huduma yote ya Mwenyezi-Mungu ilitayarishwa siku hiyo, ili kuiadhimisha Pasaka na kutoa sadaka za kuteketeza kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamuru mfalme Yosia. 17Wakati huo watu wote wa Israeli waliohudhuria waliiadhimisha sikukuu hiyo ya Pasaka na sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, kwa muda wa siku saba. 18Pasaka kama hiyo ilikuwa haijasherehekewa katika Israeli yote tangu siku za nabii Samueli. Hapajatokea mfalme hata mmoja wa Israeli aliyeadhimisha Pasaka kama hii iliyoadhimishwa na mfalme Yosia pamoja na makuhani, Walawi na watu wote wa Yuda, watu wa Israeli na wakazi wa Yerusalemu. 19Pasaka hiyo iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake mfalme Yosia.

Mwisho wa utawala wa Yosia

(2Fal 23:28-30)

20Baada ya haya yote aliyofanya mfalme Yosia kwa ajili ya hekalu, Neko, mfalme wa Misri, aliongoza jeshi lake kwenda kushambulia Karkemishi kwenye mto Eufrate. Naye mfalme Yosia alitoka kumkabili, 21lakini mfalme Neko akamtumia ujumbe usemao: “Vita hivi havikuhusu wewe hata kidogo ewe mfalme wa Yuda. Sikuja kupigana nawe bali dhidi ya maadui zangu, na Mungu ameniamuru niharakishe. Acha basi kumpinga Mungu, ambaye yu upande wangu, la sivyo atakuangamiza.” 22Lakini Yosia hakukubali kumwachia. Alikataa kuyasikiliza maneno aliyonena Mungu kwa njia ya Neko, kwa hiyo akajibadilisha ili asitambulike, kisha akaingia vitani katika tambarare ya Megido.
23Nao wapiga upinde walimpiga mshale mfalme Yosia; basi ndipo mfalme alipowaambia watumishi wake: “Niondoeni! Nimejeruhiwa vibaya sana.” 24Watumishi wake walimtoa katika gari lake la farasi, wakambeba na gari lake la pili hadi Yerusalemu. Hapo akafariki dunia na kuzikwa katika makaburi ya kifalme. Watu wote wa Yuda na Yerusalemu waliomboleza kifo cha Yosia.
25Nabii Yeremia pia alitunga shairi la maombolezo kwa ajili ya kifo chake; nao waimbaji wote, wanaume kwa wanawake, humtaja Yosia katika maombolezo yao, mpaka leo. Imekuwa desturi kufanya maombolezo haya katika Israeli. Hayo yameandikwa katika Maombolezo. 26Matendo mengine ya Yosia na matendo yake mema kama yalivyoandikwa katika sheria ya Mwenyezi-Mungu, 27na matendo yake tangu mwanzo hadi mwisho, hayo yameandikwa katika Kitabu cha Wafalme wa Israeli na Yuda.





2Mambo ya Nyakati35;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: