Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 7 June 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 1Mambo ya Nyakati 21...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega...!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu

Neema yako yatutosha ee Mungu wetu....!!



Mwanangu, usiyasahau mafundisho yangu, bali kwa moyo wako uzishike amri zangu. Maana yatakupa wingi wa siku, maisha marefu na fanaka kwa wingi. Utii na uaminifu visitengane nawe. Vifunge shingoni mwako; viandike moyoni mwako. Hivyo utakubalika na kusifika, mbele ya Mungu na mbele ya wanadamu. Mtumaini Mwenyezi-Mungu kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe. Umtambue Mungu katika kila ufanyalo, naye atazinyosha njia zako.

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba ukatupe neema
ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Usitutie majaribu Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu
ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Usijione wewe mwenyewe kuwa mwenye hekima; mche Mwenyezi-Mungu na kujiepusha na uovu. Hiyo itakuwa dawa mwilini mwako, na kiburudisho mifupani mwako. Mheshimu Mwenyezi-Mungu kwa mali yako, na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Hapo ghala zako zitajaa nafaka, na mapipa yako yatafurika divai mpya. Mwanangu, usidharau adhabu ya Mwenyezi-Mungu, wala usiudhike kwa maonyo yake; maana Mwenyezi-Mungu humwonya yule ampendaye, kama baba amwonyavyo mwanawe mpenzi. Heri mtu anayegundua hekima, mtu yule anayepata ufahamu. Hekima ni bora kuliko fedha, ina faida kuliko dhahabu. Hekima ina thamani kuliko johari, hamna unachotamani kiwezacho kulingana nayo. Kwa mkono wake wa kulia Hekima atakupa maisha marefu; kwa mkono wake wa kushoto atakupa mali na heshima.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji

Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe....



Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu

Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu

Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Tukawe barua njema  ee Mungu wetu nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi


Njia zake ni za kupendeza, zote zaelekea kwenye amani. Hekima ni mti wa uhai kwa wote wampatao; wana heri wote wanaoshikamana naye. Kwa hekima Mwenyezi-Mungu aliweka misingi ya dunia, kwa akili aliziimarisha mbingu. Kwa maarifa yake vilindi vilipasuka, na mawingu yakadondosha umande. Mwanangu, zingatia hekima safi na busara; usiviache vitoweke machoni pako, navyo vitakuwa uhai nafsini mwako, na pambo zuri shingoni mwako. Hapo utaweza kwenda zako kwa usalama, wala mguu wako hautajikwaa. Ukiketi hutakuwa na hofu; ukilala utapata usingizi mtamu. Usiogope juu ya tishio la ghafla, wala shambulio kutoka kwa waovu, Maana Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekutegemeza; atakuepusha usije ukanaswa mtegoni. Usimnyime mtu anayehitaji msaada, ikiwa unao uwezo wa kufanya hivyo. Usimwambie jirani yako aende zake hadi kesho, hali wewe waweza kumpa anachohitaji leo. Usipange maovu dhidi ya jirani yako, anayeishi karibu nawe bila wasiwasi. Usigombane na mtu bila sababu ikiwa hajakudhuru kwa lolote. Usimwonee wivu mtu mkatili, wala usiige mwenendo wake. Maana waovu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; lakini yeye huwafanya marafiki zake wale walio wanyofu. Mwenyezi-Mungu huapiza nyumba za waovu, lakini huyabariki makao ya waadilifu. Yeye huwadharau wenye dharau, lakini huwafadhili wanyenyekevu. Wenye hekima watavuna heshima, lakini wapumbavu watapata fedheha.

Tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani 
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake
Baba wa Mbinguni tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda
kinyume nawe Yahweh tunaomba ukawape neema ya kujiombea
Kufuata njia zako nazo zikawaweke huru
Ukawape macho ya rohoni ee Mungu wetu na masikio ya kusikia
sauti yako,Ukawaokoe na kuwalinda,ukawaponye kimwili na kiroho
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Amani ikatawale katika maisha yao,Upendo ukadumu kati yao..
Baba wa Mbinguni tunamba ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukajibu sawasawa na mapenzi yako

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Baba wa Mbinguni akawaguse kwa mkono wake wenye nguvu
akawabariki muingiapo/mtokapo
Amani ya Kristo Yesu na upendo wa Mungu Baba
ukae nanyi daima.....
Nawapenda.

Daudi anahesabu Waisraeli

(2Sam 24:1-25)

1Shetani akajitokeza kuwataabisha Waisraeli, akamshawishi Daudii awahesabu watu. 2Hivyo, Daudi akamwambia Yoabu na wale makamanda wengine, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli, kutoka Beer-sheba mpaka Dani. Nileteeni ripoti ili nijue idadi yao.”
3Lakini Yoabu akasema, “Mwenyezi-Mungu na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa! Bwana wangu mfalme, kwani hawa wote si watumishi wako? Kwa nini basi unataka kufanya jambo ambalo litawatia Waisraeli katika hatia?” 4Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu. Hivyo, Yoabu akaenda katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu. 5Yoabu akampelekea mfalme Daudi idadi ya watu: Katika Israeli yote, kulikuwamo wanaume 1,100,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga; na katika Yuda kulikuwamo watu 470,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga. 6Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme.
7Mungu hakupendezwa na jambo hilo kwa hiyo akaiadhibu Israeli. 8Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo hili nililolifanya! Lakini nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.”
9Basi, Mwenyezi-Mungu alisema na Gadi, mwonaji wa Daudi, akamwambia, 10“Nenda umwambie Daudi kwamba mimi Mwenyezi-Mungu ninampa mambo matatu. Ajichagulie mojawapo nami nitamtendea.” 11Hivyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Jichagulie mojawapo: 12Njaa ya miaka mitatu, au miezi mitatu ya maangamizi kutokana na maadui zako ambapo upanga wa maadui zako utakushinda; au siku tatu ambapo Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa upanga wake, awaletee maradhi mabaya nchini, na malaika wake apite kuwaangamiza katika nchi nzima ya Israeli. Sasa amua, ni jibu lipi nitakalompa yeye aliyenituma.”
13Daudi akamjibu Gadi, “Nimeingia katika mashaka makubwa! Lakini afadhali niadhibiwe na Mwenyezi-Mungu kwani yeye ana huruma sana. Ila nisianguke katika mkono wa mwanadamu.” 14Basi, Mwenyezi-Mungu akawaletea Waisraeli maradhi mabaya, ambayo yalisababisha vifo vya Waisraeli 70,000. 15Halafu Mungu akatuma malaika aende kuuharibu Yerusalemu; lakini kabla hajafanya hivyo, Mwenyezi-Mungu akageuza nia yake na kumwambia malaika huyo aliyetekeleza maangamizi, “Basi, yatosha!” Malaika alikuwa amesimama karibu na uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi.
16Daudi akainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama kati ya mbingu na dunia, naye ameunyosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuuangamiza. Hapo Daudi na wazee wote walikuwa wamevaa mavazi ya gunia, wakaanguka kifudifudi. 17Daudi alimwambia Mungu, “Je, si mimi niliyetoa amri watu wahesabiwe? Ni mimi niliyetenda dhambi na kufanya uovu. Lakini kondoo hawa wamefanya nini? Nakusihi sana, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mkono wako uwe dhidi yangu na dhidi ya jamaa ya baba yangu, lakini maradhi haya mabaya yasiwapate watu wako.”
18Ndipo malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwamuru Gadi amwambie Daudi aende amjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu, katika kiwanja cha kupuria nafaka cha Ornani Myebusi. 19Daudi akatii amri ya Mwenyezi-Mungu, akapanda juu kufuatana na neno la Gadi alilosema kwa jina la Mwenyezi-Mungu. 20Ornani alipogeuka na kumwona yule malaika, ndipo yeye na wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Naye Ornani alikuwa akipura ngano. 21Daudi alipomwendea Ornani, Ornani alitazama na kumwona Daudi; basi huyo Ornani alitoka kwenye uwanja wa kupuria akaenda mbele; kisha akamsujudia akiinamisha kichwa chake mpaka chini ardhini. 22Daudi akamwambia Ornani, “Nipe nafasi ya uwanja wako wa kupuria nafaka ili nimjengee Mwenyezi-Mungu madhabahu juu yake, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa kwa watu. Niuzie kwa bei yake kamili.”
23Naye Ornani akamwambia Daudi, “Kichukue kiwanja hiki, bwana wangu mfalme, na ukitumie vile unavyopenda mwenyewe. Tazama, nawatoa fahali kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, na vifaa vya kupuria kwa kuni, pamoja na ngano iwe tambiko ya nafaka. Vyote hivyo ninakupa.”
24Lakini mfalme Daudi alimwambia Ornani, “La, hasha; nitavinunua kwa thamani yake kamili; sitamchukulia Mwenyezi-Mungu kitu kilicho chako au kumtolea tambiko za kuteketezwa ambazo hazijanigharimu kitu.” 25Hivyo, Daudi alimlipa Ornani kwa kumpimia shekeli 600 kamili za dhahabu kulipia uwanja huo. 26Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu mahali hapo na kumtolea sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akakubali ombi lake kwa kuleta moto kutoka mbinguni kuiteketeza ile sadaka kwenye madhabahu.
27Halafu, Mwenyezi-Mungu alimwamuru malaika, naye akaweka upanga wake alani mwake. 28Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba Mwenyezi-Mungu amekubali ombi lake kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Ornani, Myebusi, akatoa tambiko papo hapo. 29Hema la Mwenyezi-Mungu ambalo lilitengenezwa na Mose nyikani, na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, wakati huo vilikuwa bado pale mahali pa kuabudia huko Gibeoni. 30Lakini Daudi hakuweza kwenda huko kumwomba Mungu shauri kwa sababu alikuwa anauogopa upanga wa malaika wa Mwenyezi-Mungu.



1Mambo ya Nyakati21;1-30

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: