Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 9 April 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Wafalme3 ......



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa 
kibali cha kuiona leo hii...
Si kwamba sisi ni wema sana wala si kwamba sisi ni wazuri mno,
Si kwa uwezo wetu wala utashi wetu si kwa akili zetu wala nguvu
zetu ni kwa neema/rehema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/zima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu.....

Utukuzwe ee Mungu  wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah,
Uabudiwe ee Yahweh,Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako niya ajabu,Matendo yako yanatisha,hakuna kama wewe ee Mungu wetu
Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni...!!


Sisi tunalo kundi hili kubwa la mashahidi mbele yetu. Kwa hiyo tuondoe kila kizuizi kinachotuzuia, na dhambi ile inayotungangania. Tupige mbio kwa uvumilivu katika mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Tumwelekee Yesu ambaye ndiye aliyeianzisha imani yetu na ambaye ataikamilisha. Kwa ajili ya furaha iliyokuwa inamngojea, yeye alivumilia kifo msalabani, bila kuijali aibu yake, na sasa anaketi upande wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishsuha na 
kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu
Jehovaha tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Mungu wetu usitutie katika majarubu Baba wa Mbinguni tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah 
tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu 
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....



Fikirini juu ya mambo yaliyompata Yesu, jinsi alivyostahimili upinzani mkubwa kwa watu wenye dhambi. Basi, msife moyo, wala msikate tamaa. Maana katika kupambana na dhambi, nyinyi hamjapigana mpaka kiasi cha kumwaga damu yenu. Je, mmesahau yale maneno ya kutia moyo ambayo Mungu anawataja nyinyi kuwa wanawe? “Mwanangu, usidharau adhabu ya Bwana, wala usife moyo anapokukanya. Maana Bwana humpa nidhamu kila anayempenda, humwadhibu kila anayekubali kuwa mwanawe.”


Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji....
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa
zetu Yahweh tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na 
wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo
vimiliki,Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo

Mungu wetu tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Jehovah tunaomba ukavitakase na ukavifunike kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo...
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Jehovah tunaomba
ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
 Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote
za maisha yetu,Yahweh ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya
Jehovah ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni,Neema yako na Nuru yako
ikaangaze katika maisha yetu
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Vumilieni adhabu kwani ni mafundisho; Mungu huwatendea nyinyi kama wanawe. Maana ni mwana gani asiyeadhibiwa na baba yake? Lakini msipoadhibiwa kama wana wengine, basi, nyinyi si wanawe, bali ni wana haramu. Zaidi ya hayo, sisi tunawaheshimu wazazi wetu waliotuzaa hata wanapotuadhibu. Basi, tunapaswa kumtii zaidi Baba yetu wa kiroho ili tupate kuishi. Wazazi wetu hapa duniani walituadhibu kwa muda, kama wao wenyewe walivyoona kuwa vema; lakini Mungu anatuadhibu kwa ajili ya faida yetu wenyewe, tupate kuushiriki utakatifu wake. Kuadhibiwa si jambo la kufurahisha bali la kuhuzunisha. Lakini wale waliofunzwa kuwa na nidhamu mwishowe watavuna tuzo la amani kutoka katika maisha adili.


Baba wa mbinguni tunawaweka mikononi mwako watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake  Yahweh tunaomba ukaonekane katika 
shida/mapito yao Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawape 
neema ya kujiombea,kufuata njia zako kusimamia Neno lako nalo
liwaweke huru,Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Jehovah
tunaomba ukawafute machozi yao,Yahweh tunaomba ukasikie na 
ukapokee sala/maombi yetu Mungu wetu ukawatendee sawasawa
na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina....!!

Asanteni sana wapendwa katika kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendesa
kama inavyompendeza yeye...
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukawe nanyi Daima....
Nawapenda.


Vita kati ya Israeli na Moabu
1Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yehoshafati wa Yuda, Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala Israeli, akatawala kutoka Samaria kwa muda wa miaka kumi na miwili. 2Yoramu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini yeye hakuwa mbaya kama baba na mama yake; maana alibomolea mbali mnara wa Baali uliofanywa na baba yake. 3Hata hivyo, Yoramu hakuacha dhambi kama mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyemtangulia ambaye alifanya dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.
4Mfalme Mesha wa Moabu alikuwa mfuga kondoo, na kila mwaka alitoa ushuru kwa mfalme wa Israeli wanakondoo laki moja na sufu ya kondoo laki moja. 5Lakini Ahabu alipofariki, mfalme wa Moabu alimwasi. 6Kwa hiyo mfalme Yoramu akaondoka Samaria, akakusanya jeshi lote la Israeli. 7Akatuma ujumbe kwa mfalme Yehoshafati wa Yuda, akamwambia, “Mfalme wa Moabu ameniasi. Je, utashirikiana nami tupigane naye?”
Mfalme Yehoshafati akamjibu, “Niko tayari! Mimi na wewe ni kitu kimoja; watu wangu ni kama wako, farasi wangu ni kama wako. 8Je, tutashambulia kutoka upande gani?” Yoramu akajibu, “Tutashambulia kutoka jangwa la Edomu.”
9Basi, mfalme Yoramu akaondoka pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kusafiri kwa muda wa siku saba, maji yakawaishia. Hawakuwa na maji kwa majeshi yao wala kwa wanyama wao. 10Hapo mfalme wa Israeli akasema, “Ole wetu! Mwenyezi-Mungu ametukusanya sote wafalme watatu atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.” 11Mfalme Yehoshafati akauliza, “Je, hakuna nabii yeyote hapa wa Mwenyezi-Mungu ambaye tunaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu?” Mtumishi mmoja wa mfalme Yoramu wa Israeli akajibu, “Elisha mwana wa Shafati yupo hapa. Yeye alikuwa mtumishi wa Elia.” 12Yehoshafati akasema, “Huyo ni nabii wa kweli.” Kisha wafalme hao watatu wakamwendea Elisha.
13Elisha akamwuliza mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda ukawatake shauri manabii ambao baba yako na mama yako waliwaendea.” Mfalme wa Israeli akajibu, “Sivyo! Mwenyezi-Mungu ndiye aliyetuita sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.” 14Elisha akasema, “Kama aishivyo Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu ambaye mimi ninamtumikia, naapa kwamba kama isingekuwa kwa heshima niliyo nayo kwa rafiki yako mfalme Yehoshafati wa Yuda, nisingekujali hata kidogo. 15Lakini sasa niletee mpiga kinanda.” Wakamletea mpiga kinanda. Ikawa alipopiga kinanda, nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elisha, 16akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Chimbeni mashimo kila mahali kote bondeni. 17Ingawa hamtaona upepo wala mvua, bonde litajaa maji, nanyi mtakunywa, nyinyi pamoja na ng'ombe wenu na wanyama wenu.’ 18Lakini hili si jambo gumu kwa Mwenyezi-Mungu; yeye atawapeni pia ushindi juu ya Moabu. 19Mtashinda kila mji wenye ngome na kila mji mzuri; mtaikata miti yao yote, mtaziba chemchemi zote za maji, na kuyaharibu mashamba yao yote yenye rutuba kwa kuyajaza mawe.” 20Kesho yake asubuhi, wakati wa kutambikia, maji yakatiririka kutoka upande wa Edomu na kujaa kila mahali bondeni.
21Wamoabu walipopata habari kwamba hao wafalme watatu wamekuja kuwashambulia, watu wote wawezao kuvaa silaha kuanzia vijana mpaka wazee, waliitwa, wakapewa silaha na kuwekwa mpakani tayari kwa vita. 22Walipoamka asubuhi iliyofuata, jua lilikuwa linametameta juu ya maji hayo; walipoyatazama yakaonekana kuwa mekundu kama damu. 23Wakasema, “Hii ni damu! Bila shaka hawa wafalme watatu wamepigana wao kwa wao na kuuana! Twendeni tukachukue nyara!”
24Lakini walipofika katika kambi ya Israeli, watu wa Israeli waliwashambulia, nao wakakimbia mbele yao. Watu wa Israeli wakawafuatia mpaka Moabu huku wakiwaua 25na kuibomoa miji yao. Kila walipopita penye shamba zuri, kila mtu alilirushia jiwe mpaka kila shamba likajaa mawe; kadhalika wakaziziba chemchemi zote za maji na kukata miti yote mizuri. Hatimaye, ukabaki mji mkuu wa Kir-haresethi peke yake, ambao pia wapiga kombeo waliuzingira na kuuteka.
26Mfalme wa Moabu alipoona kwamba vita vinamwendea vibaya, alichukua watu wake 700 wenye kupigana kwa mapanga, akikusudia kupenya majeshi ya adui zake mkabala na mfalme wa Edomu, lakini hakufaulu. 27Hapo akamchukua mwanawe wa kwanza ambaye angekuwa mfalme mahali pake, akamtoa kuwa sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Watu wa Israeli walipoona hayo, wakachukizwa mno. Wakauacha mji huo na kurudi nchini kwao.



2Wafalme3;1-27


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: