Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 5 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; Leo tunaanza kitabu cha -1 Wafalme 1....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Nisiku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na 
 kutupa kibali cha kuendelea  kuiona leo hii...
Tunamshukuru Mungu wetu katika yote..

Leo tunaanza kitabu kingine baada ya kumaliza/kupitia 
kitabu cha "2Samuel" leo tunaanza kitabu cha "1Wafalme"
Mungu akatuongoze katika kusoma,kuelewa,kujifunza,kukumbuka,
na akatupe macho ya rohoni, tukatunze tunachojifunza
ikawe faida kwetu na kwa wengine....
Ee Baba tunaomba ukatupe shauku/hamu ya kukujua wewe zaidi...!


Yesu alianza kufundisha tena akiwa kando ya ziwa. Umati mkubwa wa watu ulimzunguka hata ikambidi aingie katika mashua na kuketi. Watu wote wakawa wamekaa katika nchi kavu, kando ya ziwa. Aliwafundisha mambo mengi kwa mifano, na katika mafundisho yake aliwaambia, “Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu. Alipokuwa akipanda mbegu, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila. Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi, zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina. Jua lilipochomoza, zikateketea; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka. Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga, nazo hazikuzaa nafaka. Nyingine zilianguka katika udongo mzuri, zikamea, zikakua na kuzaa: Moja punje thelathini, moja sitini na nyingine mia.” Kisha akawaambia, “Mwenye masikio na asikie!”

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo....
wewe si Mungu wa wafu ni Mungu wa wote walio hai
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma,Baba wa upendo,
Baba wa Baraka,Baba wa Yatima,Mume wa wajane...
Jehovah..!Yahweh..!Adonai..!Elohim..!Elyona..!El Olam..!
El Qanna..!El Shaddai..!Emanuel-Mungu pamoja nasi..!!!


Yesu alipokuwa peke yake, baadhi ya wale waliomsikia walimwendea pamoja na wale kumi na wawili, wakamwuliza juu ya hiyo mifano. Naye akawaambia, “Nyinyi mmejaliwa kujua siri ya ufalme wa Mungu, lakini wale walio nje wataambiwa kila kitu kwa mifano, ili, ‘Watazame kweli, lakini wasione. Wasikie kweli, lakini wasielewe. La sivyo, wangemgeukia Mungu, naye angewasamehe.’”


Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako ...
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni tunaomba nasi utupe neema ya kuweza 
kuwasamehe wale wote walio tukosea..
Yahweh tunaomba usitutie katika majaribu Mungu wetu 
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona...


Basi, Yesu akawauliza, “Je, nyinyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? Mpanzi hupanda neno la Mungu. Watu wengine ni kama walio njiani ambapo neno lilipandwa. Lakini mara tu baada ya kulisikia, Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu walisikiapo hilo neno hulipokea kwa furaha. Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno, mara wanakata tamaa. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaosikia hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia.”

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa
katika utendaji Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji...



Yesu akaendelea kuwaambia, “Je, watu huwasha taa wakaileta ndani na kuifunika kwa debe au kuiweka mvunguni? La! Huiweka juu ya kinara. Basi, kila kilichofichwa kitafichuliwa, na kila kilichofunikwa kitafunuliwa. Mwenye masikio na asikie!” Akawaambia pia, “Sikilizeni kwa makini mnachosikia! Kipimo kilekile mnachowapimia watu wengine, ndicho mtakachopimiwa; tena mtazidishiwa. Aliye na kitu atapewa zaidi; asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.”

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,Jehovah tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka...
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah ukavitakase na kuvifunika
kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia Yahweh tukawe salama
moyoni Baba wa Mbinguni ukaonekane katika maisha yetu
Jehovah popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Yahweh Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe neema ya kufuata njia zako Jehovah tukasimamie Neno lako
amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Jehovah ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.” Tena, Yesu akasema, “Tuufananishe Ufalme wa Mungu na nini? Tuueleze kwa mifano gani? Ni kama mbegu ya haradali ambayo ni ndogo kuliko mbegu zote. Lakini ikisha pandwa, huota na kuwa mmea mkubwa kuliko mimea yote ya shambani. Matawi yake huwa makubwa hata ndege wa angani huweza kujenga viota vyao katika kivuli chake.” Yesu aliwahubiria ujumbe wake kwa mifano mingine mingi ya namna hiyo; aliongea nao kadiri walivyoweza kusikia. Hakuongea nao chochote bila kutumia mifano; lakini alipokuwa pamoja na wanafunzi wake peke yao alikuwa akiwafafanulia kila kitu.

Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wote wakutafutao kwa bidii na imani..
Mungu wetu ukaonekane na ukawape neema ya kujiombea,kufuatanjia zako,kuisimamia Neno lako nalo litawaweka huru..
Yahweh tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda
 kinyume nawe,Mungu wetu ukawaokoe na kuwalinda Yahweh
tunaomba Nuru yako ikaangaze katika masiha yao,Baba wa Mbinguni
wakapate kutambua/kujitambua...
Mungu wetu tunaomba ukapokee sala/maombi yetu
Baba wa Mbinguni ukawajibu sawasawa na mapenzi yako


Jioni, siku hiyohiyo, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Tuvuke ziwa, twende ngambo.” Basi, wakauacha ule umati wa watu, wakamchukua Yesu katika mashua alimokuwa. Vilevile mashua nyingine zilimfuata. Basi, dhoruba kali ikaanza kuvuma, mawimbi yakaipiga ile mashua hata ikaanza kujaa maji. Yesu alikuwa sehemu ya nyuma ya mashua, amelala juu ya mto. Basi, wanafunzi wakamwamsha na kumwambia, “Mwalimu, je, hujali kwamba sisi tunaangamia?” Basi, akaamka, akaukemea ule upepo na kuyaamrisha mawimbi ya ziwa, “Kimya! Tulia!” Hapo upepo ukakoma, kukawa shwari kabisa. Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mbona mnaogopa? Je, bado hamna imani?” Nao wakaogopa sana, wakawa wanaulizana, “Huyu ni nani basi, hata upepo na mawimbi vinamtii?”

Kwakuwa ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Kristo Yesu ikawe nanyi Daima....
Nawapenda.



Siku za mwisho za mfalme Daudi

1Mfalme Daudi, wakati alipokuwa mzee sana, watumishi wake walimfunika kwa mablanketi, lakini hata hivyo, hakuweza kupata joto. 2Kwa hivyo wakamwambia, “Bwana wetu mfalme, afadhali tukutafutie msichana akutumikie na kukutunza; alale pamoja nawe kusudi akupatie joto.”
3Basi, wakatafutatafuta msichana mzuri kote nchini Israeli. Akapatikana msichana mmoja mzuri aitwaye Abishagi, Mshunami; wakamleta kwa mfalme. 4Msichana huyo, alikuwa mzuri sana. Basi, akaanza kumtumikia na kumtunza mfalme; lakini mfalme hakulala naye.

Adoniya anajitakia ufalme

5Wakati huo, Adoniya, mwana wa Daudi na Hagithi, akaanza kujigamba kwamba yeye ndiye atakayekuwa mfalme. Basi, akajitayarishia magari ya kukokotwa, wapandafarasi na wapiga mbio hamsini wa kumtangulia na kumshangilia. 6Lakini baba yake, Daudi, hakuwa amemkemea mwanawe hata mara moja na kumwuliza kwa nini alikuwa amefanya hivyo. Adoniya, ama kwa hakika, alikuwa mwenye sura ya kupendeza sana; na alikuwa amemfuata Absalomu kwa kuzaliwa. 7Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari; nao wakamfuata na kumuunga mkono. 8Lakini kuhani Sadoki, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na nabii Nathani na Shimei, Rei pamoja na walinzi wa Daudi, hawakumuunga mkono Adoniya.
9Siku moja, Adoniya alitoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono kwenye Jiwe la Nyoka, karibu na chemchemi iitwayo Enrogeli. Akawaalika kwenye karamu ya sadaka hiyo ndugu zake wote, yaani wana wengine wa mfalme, na watumishi wote wa mfalme waliokuwa wa kabila la Yuda. 10Lakini, nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Solomoni ndugu yake hakuwaalika.

Solomoni anatawazwa kuwa mfalme

11Hapo, Nathani akamwendea Bathsheba mama yake Solomoni, akamwuliza, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwanawe Hagithi, amejinyakulia mamlaka ya ufalme na bwana wetu Daudi hana habari? 12Basi, kama ukitaka kuyaokoa maisha yako na ya mwanao Solomoni, nakushauri hivi: 13Mwendee mfalme Daudi, umwulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi mtumishi wako ukisema, “Mwana wako Solomoni atatawala mahali pangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?” Imekuwaje basi, sasa Adoniya anatawala?’ 14Na utakapokuwa bado unaongea na mfalme, mimi nitaingia na kuyathibitisha maneno yako.”
15Basi, Bathsheba alimwendea mfalme chumbani mwake (wakati huo mfalme alikuwa mzee sana, naye Abishagi, Mshunami alikuwa akimhudumia). 16Bathsheba aliinama, akamsujudia mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Unataka nini?” 17Bathsheba akamjibu, “Bwana wangu, uliniapia mimi mtumishi wako mbele ya Bwana Mungu wako, ukisema: ‘Mwana wako Solomoni atatawala baada yangu, na ataketi juu ya kiti changu cha enzi.’ 18Sasa, tazama, Adoniya anatawala ingawa wewe bwana wangu mfalme hujui kuhusu hayo. 19Ametoa sadaka ya ng'ombe, ya vinono, na kondoo wengi, na kuwaita wana wote wa mfalme, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini mtumishi wako Solomoni hakumkaribisha. 20Na sasa, bwana wangu mfalme, Waisraeli wote wanakungojea, ili uwaambie yule atakayeketi juu ya kiti chako baada yako, bwana wangu mfalme. 21La sivyo, itatokea ya kwamba, wakati ambapo wewe bwana wangu, mfalme, utakapofariki mimi pamoja na mwanangu Solomoni tutahesabika kama wenye hatia.” 22Wakati Bathsheba alipokuwa akizungumza na mfalme, nabii Nathani aliingia ikulu. 23Nao watu wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Naye alipomfikia mfalme, alimwinamia mfalme mpaka uso ukafika chini udongoni. 24Ndipo Nathani aliposema, “Bwana wangu, je, ulisema, ‘Adoniya atatawala baada yangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?’ 25Kwa maana leo ameteremka, akatoa sadaka ya ng'ombe, vinono na kondoo wengi na amewakaribisha wana wa mfalme, Yoabu jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari, na, tazama, wanakula na kunywa mbele yake, na kusema, ‘Uishi mfalme Adoniya!’ 26Lakini hakunialika mimi, mtumishi wako wala kuhani Sadoki, wala Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni. 27Je, yote haya umeyafanya wewe bwana wangu, mfalme, bila kuwaambia watumishi wako mtu atakayekaa juu ya kiti chako cha enzi baada yako?” 28Naye mfalme Daudi akajibu, “Niitie Bathsheba.” Bathsheba alimwendea mfalme na kusimama mbele yake. 29Halafu mfalme aliapa akisema, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, aliyekomboa roho yangu katika taabu nyingi, 30kama nilivyokuapia mbele za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nikisema, ‘Mwanao Solomoni atatawala baada yangu, na kwamba atakaa juu ya kiti changu cha enzi badala yangu,’ ndivyo nitakavyofanya leo.” 31Ndipo Bathsheba alipoinama mpaka chini, akamsujudia mfalme, na kusema “Bwana wangu, mfalme Daudi, aishi milele!” 32Kisha mfalme Daudi akasema, “Niitie kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Nao wakamjia mfalme. 33Naye mfalme akawaambia, “Nenda na watumishi wangu mimi bwana wako, umpandishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu, umpeleke Gihoni; 34halafu umruhusu kuhani Sadoki na nabii Nathani wampake mafuta kuwa mfalme wa Israeli; baadaye pigeni tarumbeta na kusema, ‘Mfalme Solomoni aishi!’ 35Nanyi mtamfuata, naye atakuja na kuketi juu ya kiti changu cha enzi badala yangu; nami nimemteua kuwa mtawala juu ya Israeli na juu ya Yuda.” 36Ndipo Benaya mwana wa Yehoyada alipomjibu mfalme, “Amina! Bwana Mungu wa bwana wangu mfalme, na anene vivyo hivyo. 37Kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa na bwana wangu mfalme, awe pia na Solomoni, na akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme Daudi.” 38Basi, kuhani Sadoki, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada, na Wakerethi na Wapelethi, wote walishuka wakampandisha Solomoni kwenye nyumbu wa mfalme Daudi, na kumpeleka mpaka Gihoni. 39Kisha kuhani Sadoki alichukua pembe za mafuta kutoka hemani na kumpaka mafuta Solomoni kuwa mfalme. Kisha walipiga tarumbeta; na watu wote wakasema, “Aishi mfalme Solomoni!” 40Halafu watu wote walimfuata, wakipiga mazomari, wakafurahi kwa shangwe kubwa, hata nchi ikatikisika kwa sauti zao. 41Basi, Adoniya pamoja na wageni waliokuwa naye walisikia hao watu walipomaliza sherehe. Naye Yoabu aliposikia sauti ya tarumbeta alisema, “Makelele hayo mjini ni ya nini?” 42Alipokuwa akisema, kumbe, Yonathani mwana wa kuhani Abiathari akaingia; kisha Adoniya akasema, “Karibu, kwani wewe u mtu mwema; unaleta habari njema.” 43Ndipo Yonathani alipomjibu Adoniya, “Hapana, kwa sababu mfalme Daudi amemtawaza Solomoni kuwa mfalme; 44naye mfalme amempeleka pamoja na kuhani Sadoki, nabii Nathani, Benaya mwana wa Yehoyada na Wakerethi na Wapelethi, nao wamempandisha juu ya nyumbu wa mfalme, 45kisha kuhani Sadoki na nabii Nathani wamemtia mafuta kuwa mfalme kule Gihoni; halafu wametoka hapo wakifurahi; ndicho kisa cha makelele hayo unayosikia. 46Sasa Solomoni anaketi juu ya kiti cha kifalme. 47Zaidi ya hayo, watumishi wa mfalme walikuja kumpongeza bwana wetu mfalme Daudi wakisema, ‘Mungu wako alifanye jina la Solomoni kuwa maarufu kuliko lako; pia akikuze kiti chake cha enzi kuliko kiti chako.’ Halafu mfalme akainama kitandani, 48na kuomba akisema, ‘Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, ambaye amemfanya mzawa wangu kuwa mfalme mahali pangu, na ambaye amenipa maisha hata nimeyaona haya.’”
49Basi, wageni wa Adoniya wakaogopa sana, wakaondoka na kutawanyika. 50Naye Adoniya, kwa kuwa alimwogopa Solomoni, akakimbilia katika hema la Mwenyezi-Mungu akazishika pembe za madhabahu apate kusalimika. 51Mfalme Solomoni akapata habari kwamba Adoniya alikuwa amekimbilia hemani, na kwamba anashikilia pembe za madhabahu akisema, “Sitaondoka hapa mpaka mfalme Solomoni atakaponihakikishia kwamba hataamuru niuawe.” 52Mfalme Solomoni akasema, “Nikimwona kuwa mwaminifu basi, hatapata madhara yoyote. Lakini nikimwona kuwa mwovu, lazima afe.” 53Basi, mfalme Solomoni akaagiza Adoniya aitwe kutoka hemani, aje kwake. Adoniya akafika mbele ya mfalme, akainama kwa heshima. Mfalme akamwambia, “Nenda zako nyumbani.”




1Wafalme1;1-53


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: