Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 7 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 3....



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Baba wa Mbinguni,Usifiwe ee Mungu wetu,
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na yakobo
Baba wa Upendo,Baba wa huruma,Baba wa Baraka,Baba wa uzima
Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye kusamehe,Mungu wetu si kiziwi
anasikia,Mungu wetu si kipofu anaona,Mungu wetu kiwete anaweza
Hakuna lililogumu mbele zake,Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni
Neema yako yatutosha eeMungu wetu...!!


Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu.


Tazama jana imepita leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Jehovah tnakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona......


Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea. Maana tumesikia juu ya imani yenu kwa Kristo Yesu na juu ya mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu. Imani yenu na mapendo yenu vina msingi katika tumaini mlilowekewa mbinguni. Mlipata kusikia juu ya hilo tumaini mara ya kwanza wakati mlipohubiriwa ule ujumbe wa ukweli wa Habari Njema. Injili inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu nyinyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli. Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu. Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho. Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu wakati tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa matakwa yake, pamoja na hekima yote na ujuzi wa kiroho. Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu. Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili muweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu. Na kwa furaha mshukuruni Baba, aliyewawezesha nyinyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale aliyowawekea watu wake katika ufalme wa mwanga. Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi. Kwake yeye tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu 
Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe...


Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Jehovah 
tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa 
Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
maisha yetu,Yahweh tukawe salama moyoni Mungu wetu
ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako 
na kuitii, Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia
zako Jehovah tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu..
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba
upo Baba wa Mbinguni..
Yahweh tukanene yaliyo yako Jehovah ukatupe ufahamu wa
kutambua mema na mabaya...
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Matakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.....


Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Maana kwake vitu vyote viliumbwa kila kitu duniani na mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: Wenye enzi, watawala, wakuu na wenye nguvu. Vyote viliumbwa kwake na kwa ajili yake. Yeye alikuwako kabla ya vitu vyote; vyote huendelea kuwako kwa uwezo wake. Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote. Maana Mungu alipenda utimilifu wake wote uwe ndani yake. Kwake vitu vyote vilipatanishwa na Mungu: Na kwa damu yake msalabani akafanya amani na vitu vyote duniani na mbinguni. Hapo kwanza nyinyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa maadui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu. Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awaweke mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama. Mnapaswa, lakini kuendelea na msingi imara katika imani, wala msikubali kutikiswa kutoka katika tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Injili. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Injili ambayo imekwisha hubiriwa kila mtu duniani.


Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh ukawaponye kimwili na kiroho pia
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawasamehe na ukawape neema ya 
kujiombea,kufuata njia zako nazo ziwaweke huru..
Nuru yako ikaangaze katika maisha yao.,Mungu wetu
ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni ukawafute machozi yao
Mungu wetu ukaonekane katika mapito yao Jehovah ukawaokoe
na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako...

Tunayaweka haya yote mikononi mwako Mungu wetu
tukiamini wewe ni Mungu wetu na Mwokozi wetu...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami/kunisoma
Baba wa mbinguni akawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake....
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
vikakae nanyi Daima..
Nawapenda.


Solomoni aomba hekima

(2Nya 1:3-12)

1Solomoni alifanya ushirikiano na Farao mfalme wa Misri, kwa kumwoa binti yake. Akamleta binti Farao na kumweka katika mji wa Daudi, mpaka alipomaliza kujenga nyumba yake mwenyewe, nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na ukuta wa kuuzunguka mji wa Yerusalemu.
2Kabla yake, watu walikuwa wakitoa tambiko vilimani, kwa kuwa nyumba ya Mungu ilikuwa bado haijajengwa. 3Solomoni alimpenda Mwenyezi-Mungu, akazingatia maongozi ya Daudi, baba yake; ila tu, naye ilimbidi kutoa tambiko na kufukiza ubani vilimani.
4Wakati mmoja, Solomoni alikwenda kutoa tambiko huko Gibeoni, maana palikuwa ndipo mahali maarufu pa ibada. Ilikuwa ni kawaida ya Solomoni kutoa maelfu ya sadaka za kuteketezwa katika madhabahu hiyo. 5Huko Gibeoni, Mwenyezi-Mungu alimtokea Solomoni katika ndoto usiku, akamwambia, “Omba chochote nami nitakupa.” 6Solomoni akamwambia, “Ulimwonesha mtumishi wako Daudi, baba yangu, fadhili nyingi, kwa sababu alikutumikia kwa uaminifu, uadilifu na kwa haki; na umedumisha fadhili zako kwa kumpa mwana anayeketi sasa kwenye kiti chake cha enzi. 7Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umeniweka mimi mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Daudi, ijapokuwa ningali mtoto mdogo na sijui namna ya kutekeleza wajibu huu. 8Na hapa umeniweka kati ya watu wako ambao umewachagua; nao ni wengi hata hawawezi kuhesabika kwa wingi wao. 9Kwa hiyo, nakuomba unipe mimi mtumishi wako moyo wa kusikia ili kuamua watu wako, niweze kutambua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuhukumu watu wako walio wengi hivi?”
10Ombi hili la Solomoni lilimfurahisha Mwenyezi-Mungu, 11naye akamwambia, “Kwa kuwa umetoa ombi hili, na hukujiombea maisha marefu au mali, na wala hukuomba adui zako waangamizwe, bali umejiombea utambuzi wa kutoa hukumu au kutenda haki 12basi, sasa nakutimizia kama ulivyoomba. Tazama, nakupa hekima na akili kiasi ambacho hapana mtu mwingine aliyepata kuwa nacho kabla yako, na wala hatatokea mwingine kama wewe baada yako. 13Pia, nitakupa yale ambayo hukuomba: Nitakupa utajiri na heshima zaidi ya mfalme mwingine yeyote wa nyakati zako. 14Tena kama ukifuata njia na maagizo yangu na kushika amri zangu kama alivyofanya baba yako Daudi, basi, nitakupa maisha marefu.”
15Solomoni alipoamka, alitambua kwamba ilikuwa ndoto. Ndipo akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, akamtolea tambiko za kuteketezwa na za amani. Halafu akawafanyia karamu watumishi wake wote.

Solomoni anaamua kesi ngumu

16Siku moja, wanawake wawili makahaba, walikwenda kwa mfalme Solomoni. 17Mmoja wao akasema, “Ee bwana wangu, mimi na huyu mwenzangu tunakaa nyumba moja; mimi nilijifungua mtoto wakati huyu dada yumo nyumbani. 18Siku tatu baadaye, huyu naye alijifungua mtoto. Hapakuwa na mtu mwingine nyumbani ila sisi wawili tu. 19Halafu, usiku mmoja, mtoto wake alifariki kwa sababu alimlalia. 20Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mwanangu kutoka kwangu wakati mimi nipo usingizini, akamlaza kifuani pake. Halafu akaichukua maiti ya mwanawe, akailaza kifuani pangu. 21Nilipoamka asubuhi na kutaka kumnyonyesha mwanangu, nikakuta mtoto amefariki. Nilipochunguza sana, nikagundua kuwa hakuwa mwanangu niliyemzaa.”
22Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Wa kwangu ndiye aliye hai na wa kwako ndiye aliyekufa”. Naye mwanamke wa kwanza akasema, “La! Mtoto wako ndiye aliyekufa, wangu ni huyo aliye hai!” Basi, wakaendelea kubishana hivyo mbele ya mfalme.
23Ndipo mfalme Solomoni akasema, “Kila mmoja wenu anadai kwamba, mtoto wake ndiye aliye hai na kwamba aliyekufa si wake.” 24Basi, mfalme akaagiza: “Nileteeni upanga!” Wakamletea mfalme upanga. 25Mfalme akasema: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, umpe mmoja nusu na mwingine nusu.” 26Yule mwanamke aliyekuwa mama yake huyo mtoto aliye hai alishikwa na huruma juu ya mwanawe, akamwambia mfalme, “Tafadhali mfalme, msimuue mtoto. Mpe mwenzangu huyo mtoto aliye hai, amchukue yeye.” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “La! Mtoto asiwe wangu wala wake. Mkate vipande viwili.” 27Mfalme Solomoni akasema, “Usimuue mtoto! Mpe mwanamke wa kwanza amchukue, kwani yeye ndiye mama yake.”
28Watu wote wa Israeli waliposikia juu ya hukumu ya mfalme, walimwogopa, wakatambua kwamba alikuwa na hekima ya Mungu iliyomwezesha kutoa hukumu.



1Wafalme3;1-28


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: