Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 19 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 11...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku/wiki  nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Si kwamba sisi ni wema sana kuliko wengine waliotangulia/kufariki
leo hii,Si kwamba sisi ni wazuri mno,si kwa nguvu zetu wala utashi
wetu,si kwa akili zetu wala uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Asante kwa jinsi tulivyo Mungu wetu ni kwa neema zako tuu..
Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa Baba wa Mbinguni
Unastahili kuabudiwa Yahweh,Unastahili kuhimidiwa Jehovah
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu,Mamtendo yako
yanatisha,Hakuna linaloshindikana mbele zako,Hakuna lililo gumu mbele zako Mungu wetu,Neema yako yatutosha Mungu wetu...


Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki. Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio. Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki. Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie. Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako Mungu wetu
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote wealiotukosea
Mungu wetu usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazaret yeye aliteseka kwanza li sisi tupate
kupona...


Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia. Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa. Usiku huo, Paulo aliona maono ambayo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: “Vuka, uje Makedonia ukatusaidie.” Mara baada ya Paulo kuona maono hayo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwahubirie Habari Njema.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza 
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
ukatupe kama inavyokupendeza wewe....


Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ndoa/nyumba zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu tukawe salama rohoni,Baba wa Mbinguni tunaomba
ukatupe macho ya kuona,Masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako,Yahweh
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba
upo Baba wa Mbinguni,Neema na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Yahweh ukatupe neema ya kutambua mema na mabaya..
Mkono wako wenye nguvu ukaguse maisha yetu
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli. Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa. Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo. Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema. Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, “Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae.” Akatuhimiza twende.


Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako kila mmoja na
mahitaji yake,Jehovah ukaonekane katika shida zao Mungu wetu ukawaongoze na kuwaokoa Baba wa Mbinguni ukawape neema ya
kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru
Yahweh tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawasimamishe na kuwalinda,Jehovah ukawaponye
kimwili na kiroho pia,Ee Baba tunaomba ukasikie  kuomba kwetu na
ukapoke sala/maombi yetu,Mungu wetu naukawatendee sawasawa na 
mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu mwenye nguvu na baraka akawaguse kwa mkono wake wenye
nguvu na akawatendee kama inavyompendeza yeye..
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba
ukawe nanyi daima...
Nawapenda.



Solomoni anamwasi Mungu

1Solomoni alipenda sana wanawake wa kigeni: Binti Farao, wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni, na Wahiti; 2wanawake wa mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza Waisraeli akisema, “Msioe kwao wala wao wasioe kwenu kwa sababu wanawake hao watapotosha mioyo yenu ili muitumikie miungu yao.” Solomoni aliwapenda sana wanawake hao. 3Solomoni akawa na wanawake 700, wote mabinti wa kifalme; na masuria 300. Hao wanawake wakampotosha. 4Maana, alipokuwa mzee, wake zake walimpotosha hata akaitumikia miungu mingine, wala hakuwa mwaminifu kabisa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama baba yake Daudi alivyokuwa mwaminifu. 5Solomoni alimtumikia Ashtarothi aliyekuwa mungu wa kike wa Wasidoni, na alimfuata Milkomu11:5 Milkomu (aya 5) na Moleki (aya 7): Ni majina ya mungu yuleyule. chukizo la Waamoni. 6Hivyo, Solomoni alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wala hakufuata kwa ukamilifu matakwa ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake Daudi alivyokuwa amefanya. 7Juu ya mlima ulio mashariki ya Yerusalemu, Solomoni alijenga mahali pa kumtambikia Kemoshi, chukizo la Wamoabu, na mahali pa kumtambikia Moleki, chukizo la Waamoni. 8Kadhalika, aliwajengea wake zake wote wa kigeni mahali pa kufukizia ubani na kuitambikia miungu yao.
9Basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alimkasirikia Solomoni, kwa sababu alikuwa amemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, ingawa yeye alikuwa amemtokea mara mbili, 10na kumwamuru asiiabudu miungu ya kigeni; Solomoni hakutii amri ya Mwenyezi-Mungu. 11Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akamwambia Solomoni, “Kwa kuwa umeamua kufanya hivyo, ukavunja agano langu nawe, na kuasi amri zangu nilizokupa, hakika nitakunyanganya huo utawala na kumpa mtumishi wako. 12Hata hivyo, kwa ajili ya baba yako Daudi, sitafanya hivyo maishani mwako, bali nitauondoa utawala huo mikononi mwa mwanao. 13Hata yeye sitamnyanganya milki yote, bali nitamwachia mwanao kabila moja, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu.”

Maadui wa Solomoni

14Ndipo Mwenyezi-Mungu akamfanya Hadadi aliyekuwa wa ukoo wa mfalme wa Edomu, kuwa adui ya Solomoni. 15Wakati Daudi alipowaangamiza Waedomu Yoabu, mkuu wa jeshi la Daudi, alikwenda huko kuwazika waliouawa. Yoabu aliwaua wanaume wote wa Edomu. 16(Yoabu alikaa huko na wanajeshi wake kwa muda wa miezi sita, apate kuwaangamiza kabisa wanaume wote wa Edomu.) 17Lakini Hadadi ambaye wakati huo alikuwa kijana alitorokea Misri pamoja na Waedomu kadhaa, watumishi wa baba yake. 18Hadadi na wenzake walisafiri kutoka Midiani, wakawachukua watu wengine huko Parani, wakaenda nao mpaka Misri, kwa Farao mfalme wa nchi hiyo. Farao akampatia Hadadi nyumba, akaamuru awe akipewa chakula, akampa na ardhi. 19Farao alipendezwa sana na Hadadi. Hivyo Farao akamruhusu shemeji yake, mdogo wa malkia Tapenesi, aolewe na Hadadi. 20Huyo dada wa Tapenesi akamzalia Hadadi mwana aliyeitwa Genubathi. Genubathi alilelewa na Tapenesi katika nyumba ya Farao, pamoja na wana wa mfalme.
21Lakini Hadadi aliposikia huko Misri kwamba Daudi na Yoabu mkuu wa jeshi, walikuwa wamefariki, alimwambia Farao, “Uniruhusu niondoke nirudi nchini kwangu.” 22Lakini Farao akamwuliza, “Nimekunyima nini hata uamue sasa kurudi nchini kwako?” Naye Hadadi akamsihi akisema, “Uniache tu niende.”
23Vilevile, Mungu alimfanya Rezoni mwana wa Eliada, awe adui ya Solomoni. Rezoni alikuwa amemtoroka bwana wake, mfalme Hadadezeri wa Soba. 24Baada ya Daudi kufanya mauaji huko Soba, Rezoni alikusanya watu na kuunda genge la maharamia, naye mwenyewe akawa kiongozi wao. Basi, wakaenda Damasko, wakakaa huko na kumfanya Rezoni mfalme wa Damasko. 25Rezoni alikuwa adui wa Israeli siku zote za utawala wa Solomoni, akamsumbua sana Solomoni kama naye Hadadi alivyomsumbua. Basi, Rezoni aliidharau Israeli, naye alitawala nchi ya Aramu.

Ahadi ya Mungu kwa Yeroboamu

26Yeroboamu mwana wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumishi wa Solomoni, ambaye mama yake mjane, aliitwa Zerua, pia alimwasi mfalme. 27Kisa cha uasi huo ni hiki: Solomoni alipokuwa akishughulika na kusawazisha sehemu ya Milo, na kuimarisha kuta za mji wa baba yake Daudi, 28Yeroboamu alionekana kuwa kijana hodari na shujaa. Ndipo Solomoni alipoona kwamba huyo kijana alikuwa mwenye bidii, akamweka awe msimamizi wa kazi za kulazimishwa zilizofanywa na watu wa ukoo wa Yosefu. 29Siku moja, Yeroboamu alipokuwa akisafiri kutoka Yerusalemu, nabii Ahiya wa Shilo alikutana naye njiani. Ahiya alikuwa amevaa vazi jipya. Wote wawili walikuwa peke yao mashambani. 30Mara, Ahiya akalivua vazi lake jipya, akalirarua vipande kumi na viwili, 31halafu akamwambia Yeroboamu, “Jitwalie vipande kumi maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Tazama, karibu nitaurarua ufalme na kuuondoa mikononi mwa Solomoni, nami nitakupa wewe makabila kumi.’ 32Lakini yeye nitamwachia kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu katika makabila yote ya Israeli. 33Nitafanya hivyo kwa sababu Solomoni ameniacha, akaabudu miungu ya kigeni: Ashtarothi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi, mungu wa Wamoabu na Milkomu mungu wa Waamoni. Solomoni ameniasi, ametenda maovu mbele yangu, na wala hakutii sheria zangu na maagizo yangu kama Daudi baba yake alivyofanya. 34Hata hivyo, sitamnyanganya milki yote, wala sitamwondolea mamlaka maishani mwake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi ambaye nilimchagua, na ambaye alifuata amri zangu na maongozi yangu. 35Lakini, nitamnyanganya mwanawe ufalme huo, nami nitakupatia wewe Yeroboamu makabila kumi. 36Huyo mwanawe Solomoni nitamwachia kabila moja, ili wakati wote mzawa wa mtumishi wangu Daudi awe anatawala Yerusalemu, awe taa inayoangaza daima mbele yangu katika mji ambao nimeuchagua uwe mahali pa kuniabudia. 37Basi, wewe Yeroboamu, nitakufanya kuwa mfalme wa Israeli, nawe utatawala kama upendavyo. 38Na kama utazingatia yote nitakayokuamuru, kama utaishi kulingana na matakwa yangu, kama utatenda mema mbele zangu kwa kushika maongozi yangu na amri zangu, kama mtumishi wangu Daudi alivyofanya, mimi nitakuwa pamoja nawe daima. Na nitakupatia nchi ya Israeli na kuufanya utawala wako uwe thabiti kama nilivyomfanyia Daudi. 39Kutokana na hayo, nitawaadhibu wazawa wa Daudi, lakini si daima.”
40Kwa sababu hiyo, Solomoni alijaribu kumuua Yeroboamu; lakini Yeroboamu akakimbilia Misri kwa Shishaki mfalme wa Misri, akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki.

Kifo cha Solomoni

(2Nya 9:29-31)

41Mambo mengine ya Solomoni, yote aliyotenda na hekima yake, yameandikwa katika Kitabu cha Matendo ya Solomoni. 42Kwa muda wa miaka arubaini, Solomoni aliitawala nchi yote ya Israeli; makao yake yakiwa Yerusalemu. 43Hatimaye, Solomoni alifariki, akazikwa katika mji wa baba yake Daudi. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, akatawala mahali pake.



1Wafalme11;1-43


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: