Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 19 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 15...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu na si kwamba sisi ni wazuri mno wala si kwa  akili zetu au uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Ni kwa mapenzi yake ni kwa neema/rehema zake Mungu wetu....


Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: “Heri nyinyi mlio maskini, maana ufalme wa Mungu ni wenu. Heri nyinyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri nyinyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha. “Heri yenu nyinyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu. Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.

Tumshukuru Mungu wetu kwa mema meengi aliyo tutendea/anayotutendea...
Asante  Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Baba wa Mbinguni,Usifiwe Mungu wetu,Uhimidiwe ee Jehovah,Uabudiwe Yahweh matendo yako ni makuu sana,Matendo yako niya ajabu,Hakuna kama wewe Mungu wetu,Neema yako yatutosha Baba wa Mbinguni,Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu Baba..!!


Lakini ole wenu nyinyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu. Ole wenu nyinyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu nyinyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia. Ole wenu nyinyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.


Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine jehovah
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya 
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua 
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...



“Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao.


Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji,Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe....


Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya.


Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu Yahweh tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki ....
Yahweh ukatuongoze katika yote tuingiapo/tutokapo Baba wa Mbinguni tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo....

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Yahweh tuka nene yaliyoyako Mungu wetu ukatupe macho ya rohoni na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii Jehovah tukawe salama moyoni Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuta njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukatufanye kuwa barua njema Yahweh nasi tukasokome kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



“Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.” Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako.


Asante Mungu wetu kwa uponyaji Asante kwa matendo yako makuu uliyotutendea na unayotendea,Mkono wako wenye nguvu umeponya,umebariki,umeokoa Mungu wetu umegusa watoto wako wako waliokuomba kwa bidii na imani,umeonekana katika maisha yao
Baba wa Mbinguni tunashukuru Yahweh tunarudisha sifa na Utukufu kwako ee Mungu wetu...

Jehovah tazama na wengine wanaokutafuta kwa bidi na imani
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Yahweh ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawaongoze na ukawape neema ya kujiombea, kufuata njia zako,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao amani ikatawale
Baba wa Mbinguni ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina....!!

Asanteni sana wapendwa katika BWANA kwakuwa nami/kunisoma
Asanteni kwa  sms/email,salaam na kujuana zaidi
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea katika yote yampendezayo 
na si yatupendezao sisi,Baba wa Mbinguni akawabariki muingiapo/mtokapo
Neema ya Kristo Yesu ikawe nanyi daima...
Nawapenda.



Absalomu anapanga uasi

1Baada ya tukio hilo, Absalomu alijipatia gari, farasi na watu hamsini wa kumtangulia. 2Absalomu alizoea kuamka asubuhi na mapema na kwenda kusimama kwenye njia inayoelekea kwenye lango la mji. Mtu yeyote aliyekuwa na madai ambayo alitaka kuyapeleka kwa mfalme ili kupata uamuzi wake, Absalomu humwita mtu huyo kando na kumwuliza, “Unatoka mji gani?” Kama mtu huyo akisema ametoka mji fulani wa kabila la Israeli, 3Absalomu humwambia, “Madai yako ni ya haki kabisa. Lakini hakuna mtu yeyote aliyeteuliwa na mfalme kukusikiliza.” 4Tena, Absalomu humwambia, “Laiti mimi ningekuwa mwamuzi wa Israeli! Kila mtu mwenye madai au shauri angekuja kwangu, nami ningempa haki yake!” 5Zaidi ya hayo, Absalomu alinyosha mkono wake akamkumbatia na kumbusu mtu yeyote aliyekuja kumwinamia na kumsujudu. 6Basi, hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Waisraeli wote waliokuja kutafuta uamuzi wa mfalme. Kwa kufanya hivyo, Absalomu aliiteka mioyo ya Waisraeli.
7Baada ya miaka minne,15:7 minne: Kiebrania: Arubaini. Absalomu alimwambia mfalme, “Tafadhali uniruhusu niende huko Hebroni ili kutimiza nadhiri yangu ambayo nilimwekea Mwenyezi-Mungu; 8maana, mimi mtumishi wako, nilipoishi kule Geshuri katika Aramu, nilimwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri nikisema kuwa kama Mwenyezi-Mungu atanirudisha mjini Yerusalemu basi, nitamwabudu yeye.” 9Mfalme akamwambia, “Basi, nenda kwa amani.” Absalomu akaondoka kwenda Hebroni. 10Lakini Absalomu alituma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, wakasema, “Mara moja mtakaposikia mlio wa tarumbeta, semeni, ‘Absalomu ni mfalme katika Hebroni!’” 11Absalomu alipokwenda huko Hebroni, alikwenda na watu 200 aliowaalika kutoka Yerusalemu, nao walikwenda huko kwa nia njema, wala hawakujua chochote kuhusu mpango wa Absalomu. 12Wakati Absalomu alipokuwa akitoa tambiko, alituma ujumbe mjini Gilo kumwita Ahithofeli, Mgilo, aliyekuwa mshauri wa mfalme Daudi. Uasi wa Absalomu ukazidi kupata nguvu na watu walioandamana naye wakazidi kuongezeka.

Mfalme Daudi anatoroka Yerusalemu

13Mjumbe fulani alipomwendea Daudi na kumwambia, “Watu wa Israeli wamevutwa na Absalomu!” 14Basi, Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa naye mjini Yerusalemu, “Inukeni tukimbie, la sivyo, hatutaweza kumwepa Absalomu. Tufanye haraka kuondoka asije akatuletea maafa na kuuangamiza mji kwa mapanga.” 15Lakini watumishi wake wakamwambia, “Sisi watumishi wako, bwana wetu mfalme, tuko tayari kufanya lolote unaloamua.” 16Basi, mfalme akaondoka pamoja na jamaa yake, lakini akawaacha masuria wake kumi wakishughulika na kazi za nyumbani. 17Mfalme akaondoka pamoja na watu wake wote. Lakini akatua kidogo walipofikia nyumba ya mwisho mjini. 18Watumishi wote wa mfalme, Wakerethi wote, Wapelethi wote, pamoja na Wagiti 600 waliomfuata mfalme Daudi kutoka mji wa Gathi, waliondoka pamoja naye wakimtangulia.
19Kisha, mfalme Daudi alipomwona Itai, Mgiti, alimwambia, “Kwa nini hata wewe umeondoka pamoja nasi? Rudi ukakae na huyo mfalme kijana. Maana wewe ni mgeni huku, tena ni mkimbizi kutoka nyumbani kwenu. 20Wewe ulikuja huku juzijuzi tu. Je, nikufanye mtu wa kutangatanga pamoja nasi, nikijua kuwa sijui hata kule ninakoenda? Rudi nyumbani pamoja na ndugu zako. Naye Mwenyezi-Mungu akuoneshe fadhili zake na uaminifu.” 21Lakini Itai akamjibu mfalme, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na wewe bwana wangu mfalme uishivyo, popote utakapokuwa, ikiwa ni kwa kufa au ni kwa kuishi, nami mtumishi wako nitakuwapo.” 22Basi, Daudi akamwambia Itai, “Nenda basi, endelea mbele.” Hivyo, Itai, Mgiti, akapita yeye mwenyewe pamoja na watoto wake. 23Daudi alipokuwa akipita pamoja na watu wake, watu wote nchini kote walilia kwa sauti. Mfalme Daudi akavuka kijito cha Kidroni pamoja na watu wote, wakapita kuelekea jangwani.
24Kuhani Abiathari akatoka, hata na kuhani Sadoki akatoka pamoja na Walawi wote huku wamelibeba sanduku la agano la Mungu. Wakaliweka chini lile sanduku la Mungu, mpaka watu wote walipopita kutoka mjini Yerusalemu. 25Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Lirudishe sanduku la agano la Mungu mjini. Kama ninakubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu, bila shaka atanirudisha na kunijalia kuliona tena sanduku lake na kuyaona maskani yake. 26Lakini ikiwa Mwenyezi-Mungu hapendezwi nami basi, mimi niko tayari; na anitendee lolote analoona jema kwake.” 27Mfalme Daudi akamwambia tena Sadoki, “Tazama, mchukue mwanao Ahimaasi na Yonathani mwana wa Abiathari mrudi nyumbani kwa amani.15:27 Tazama … amani: Au Je, wewe ni mwonaji? Rudini mjini kwa amani, wewe na Abiathari pamoja na wanao wawili Ahimaasi mwanao na Yonathani mwana wa Abiathari. 28Lakini nitakuwa nikingojea penye vivuko huku nyikani, mpaka nitakapopata habari kutoka kwako.” 29Kwa hiyo Sadoki na Abiathari wakalirudisha sanduku la agano la Mungu mjini Yerusalemu, wakabaki humo.
30Lakini Daudi aliendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni huku analia, bila viatu na kichwa chake kimefunikwa. Hata watu wote waliokuwa pamoja naye walivifunika vichwa vyao wakawa wanapanda mlima huku wanalia. 31Wakati huo, Daudi aliambiwa kuwa hata Ahithofeli alikuwa mmoja wa waasi waliojiunga na Absalomu. Lakini Daudi akaomba akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu nakuomba, uufanye mpango wa Ahithofeli usifanikiwe.”
32Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali pa kumwabudia Mungu, mtu mmoja jina lake Hushai kutoka Arki alikuja ili kumlaki, mavazi yake yakiwa yameraruka na kichwani pake kuna mavumbi. 33Daudi akamwambia, “Ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu. 34Lakini kama utarudi mjini Yerusalemu na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako, hapo awali’; basi utanifanyia mpango wa Ahithofeli usifanikiwe. 35Makuhani Sadoki na Abiathari wako pamoja nawe mjini! Basi, chochote utakachosikia kutoka nyumbani kwa mfalme, waambie makuhani Sadoki na Abiathari. 36Tazama, watoto wao wawili wa kiume, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao. Na chochote mtakachosikia mtanipelekea habari kwa njia yao.” 37Basi, Hushai rafiki ya mfalme Daudi, akarudi mjini na wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini Yerusalemu.


2Samweli15;1-37

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: