Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 16 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 14...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba  wa Mbingu na Nchi
Muumba vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana
Baba wa Upendo,Baba wa Faraja,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mfalme wa amani,Kweli wewe ni Mungu uliyefichika,Mungu wa Israel,Mungu Mwokozi,Wewe ni Mungu unayetenda maajabu,Wewe ni Mungu wangu nami ninakushuru, ninakutukuza ee Mungu wangu..
Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa rehema na huruma,ni mvumilivu, ni mwingi wa fadhila na uaminifu,Neema yako yatutosha ee Baba wa Mbinguni..!!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima na kwakuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu Tunakurudishia Baba wa Mbinguni...


Jishughulishe na biashara hata kama kwa kubahatisha; yawezekana baadaye ukapata chochote kile. Wagawie watu saba hata wanane sehemu yako, maana, hujui balaa litakalofika duniani. Mawingu yakijaa maji, mvua hunyesha; mti ukiangukia kusini au kaskazini, hapo uangukiapo ndipo ulalapo. Anayengoja upepo hatapanda mbegu, anayesubiri mawingu yatoweke, hatavuna kitu.

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni
Yahweh tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote walio tukosea
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
Kwakupigwa kwakwe sisi tumepona,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....

Usivyojua jinsi uhai unavyoingia katika mifupa ya mtoto tumboni mwa mamake, kadhalika huwezi kuelewa matendo ya Mungu, ambayo hufanya kila kitu. Panda mbegu asubuhi na jioni usiache kupanda, maana, hujui zipi zitaota; za asubuhi, za jioni, au zote zitakuwa nzuri. Mwanga wafaa, na kuliona jua kwapendeza macho. Mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie miaka hiyo yote; lakini akumbuke kuwa siku za giza zitakuwa nyingi, na kwamba yote yatakayofuata ni bure.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji....
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Baba wa Mbinguni ukatuongoze tuingiapo/tutokapo,Jehovah ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo..
Baba wa Mbinguni tukawe salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Jehovah ukaonekane popote tupitapo Yahweh na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,Amani ikatawale,Upendo ukadumu kati yetu,utu wema na fadhili na tukatende yanayokupendeza wewe ee Mungu wetu..
Ukatufanye chombo chema Baba wa Mbinguni nasi tukatumike kama inavyo kupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Ewe kijana, furahia ujana wako, moyo wako, uchangamke wakati ungali kijana. Fuata mapenzi ya moyo wako na upeo wa macho yako. Lakini kumbuka kwamba Mungu atakuhukumu kadiri ya hayo yote. Ondoa mahangaiko moyoni mwako, jikinge, usipate maumivu mwilini kwa sababu ujana na mwisho wa maisha ni bure kabisa.

Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu  watoto wako wanaokutafuta na kukuomba kwa bidii na imani
Yahweh ukaonekane katika maisha yao Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru,ukawape macho ya rohoni Yahweh ukawape neema ya kutambua/kujitambua,Mungu wetu ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe ukawape neema ya kutambua walipokesea/walipoanguka Mungu wetu ukawaongoze...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu aendelee kuwabariki katika yote na akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.


Yoabu anapanga kumrudisha Absalomu

1Yoabu mwana wa Seruya, alitambua kwamba maelekeo ya moyo wa Daudi yalikuwa kwa Absalomu tu. 2Hivyo alituma watu huko Tekoa ili wamtafutie mwanamke mwenye hekima. Walipomleta, akamwambia, “Jisingizie unafanya matanga. Vaa nguo za kuomboleza, usijipake mafuta, ila ujifanye kama mwanamke ambaye amekuwa katika maombolezo ya wafu kwa muda mrefu. 3Halafu nenda kwa mfalme ukamwambie yale ninayokuambia.” Kisha Yoabu akamwambia maneno ya kumwambia mfalme. 4Huyo mwanamke kutoka Tekoa akaenda kwa mfalme, akaanguka kifudifudi, mbele ya mfalme, akasujudu, akamwambia, “Ee mfalme, nisaidie.”
5Mfalme akamwambia, “Una shida gani?” Yule mwanamke akajibu, “Nasikitika, mimi ni mjane, mume wangu amekufa. 6Nilikuwa na watoto wa kiume wawili. Siku moja, walipokuwa mbugani, walianza kugombana. Kwa vile hapakuwa na mtu yeyote wa kuwaamua, mmoja akampiga mwenzake, akamuua. 7Sasa ndugu zangu wote wamenigeuka mimi mtumishi wako; wanataka nimtoe kwao mtoto aliyemuua mwenzake ili wamuue kwa kuyaangamiza maisha ya ndugu yake. Hivyo, watamuua huyu ambaye sasa ndiye mrithi. Wakifanya hivyo, watazima kabisa tumaini langu lililobakia, na mume wangu hataachiwa jina wala mzawa duniani.”
8Mfalme akamwambia yule mwanamke, “Rudi nyumbani nitaamuru jambo lako liangaliwe.” 9Yule mwanamke kutoka Tekoa akasema, “Bwana wangu mfalme, hatia yote na iwe juu yangu na juu ya jamaa ya baba yangu. Hivyo, wewe na ufalme wako msiwe na hatia.”
10Mfalme akamwambia, “Mtu yeyote akikutishia mlete kwangu na hatakuja kukugusa tena.” 11Yule mwanamke akamwambia, “Tafadhali, mfalme, niombee kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili yule ndugu yangu ambaye angelipiza kisasi cha mauaji ya mwanangu asifanye hatia nyingine kubwa ya kumwua yule mtoto wangu mwingine.” Mfalme Daudi akamwambia, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, hakuna hata unywele mmoja wa mwanao utakaoanguka chini.” 12Yule mwanamke akamwambia, “Nakuomba, mimi mtumishi wako, uniruhusu niseme neno moja kwako mfalme.” Mfalme akamwambia, “Sema”. 13Yule mwanamke akamwambia, “Kwa nini basi, umepanga uovu huu dhidi ya watu wa Mungu? Kulingana na uamuzi wako juu ya jambo hilo wewe mwenyewe umejihukumu kuwa na hatia kwa sababu humruhusu mwanao arudi nyumbani kutoka alikokimbilia. 14Sisi sote lazima tutakufa. Sisi ni kama maji yaliyomwagika chini ambayo hayazoleki. Hata Mungu hafanyi tofauti kwa mtu huyu na tofauti kwa mwingine; yeye hutafuta njia ili waliopigwa marufuku, wakakimbia, wapate kurudi. 15Mimi nimekuja kuzungumza nawe, bwana wangu mfalme, kwani wamenitisha. Basi, mimi mtumishi wako, niliwaza kuwa, ‘Afadhali nikazungumze na mfalme, huenda akanitimizia mahitaji yangu mimi mtumishi wake. 16Maana mfalme atanisikiliza na kuniokoa mikononi mwa mtu ambaye anataka kuniangamiza mimi pamoja na mwanangu kutoka urithi wa Mungu’. 17Nami mjakazi wako nilifikiri kuwa, ‘Neno lake bwana wangu mfalme litanipa amani moyoni, kwani wewe bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu katika kupambanua mema na mabaya.’ Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, awe pamoja nawe.”
18Ndipo mfalme alipomjibu yule mwanamke, “Usinifiche jambo lolote nitakalokuuliza.” Yule mwanamke akasema, “Sema bwana wangu mfalme.” 19Mfalme akamwuliza, “Je, Yoabu anahusika katika jambo hili?” Yule mwanamke akasema, “Kama uishivyo, bwana wangu mfalme, mtu hawezi kukwepa kulia au kushoto kuhusu jambo ulilosema bwana wangu mfalme. Yoabu yule mtumishi wako ndiye aliyenituma. Ni yeye aliyeniambia maneno yote haya niliyokuambia mimi mtumishi wako. 20Yoabu alifanya hivyo ili kubadilisha mambo. Lakini, wewe bwana wangu, una hekima kama ya malaika wa Mungu hata unaweza kujua mambo yote yaliyoko duniani.”
21Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.”
22Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.” 23Hivyo, Yoabu aliondoka, akaenda Geshuri kumleta Absalomu mjini Yerusalemu. 24Lakini mfalme akasema, “Absalomu aishi mbali nami; aishi nyumbani kwake. Asije hapa kuniona.” Hivyo, Absalomu akawa anaishi mbali, nyumbani kwake na hakumwona mfalme Daudi.

Absalomu na mfalme Daudi wapatana

25Katika Israeli yote, hakuna yeyote aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Tangu nyayo zake hadi utosini mwake, Absalomu hakuwa na kasoro yoyote. 26Kila alipokata nywele zake, (na kila mwishoni mwa mwaka alikata nywele zake kwani zilikuwa nzito), alipozipima, zilikuwa na uzito wa kilo mbili kulingana na vipimo vya kifalme. 27Absalomu alizaa watoto watatu wa kiume pamoja na binti mmoja jina lake Tamari. Tamari alikuwa mwanamke mzuri.
28Basi, Absalomu aliishi mjini Yerusalemu kwa muda wa miaka miwili mizima bila kumwona mfalme Daudi. 29Kisha, Absalomu alimtumia ujumbe Yoabu, ili aende kwa mfalme kwa niaba yake, lakini Yoabu akakataa. Absalomu akatuma ujumbe mara ya pili lakini Yoabu akakataa. 30Basi, Absalomu akawaambia watumishi wake, “Angalieni Yoabu ana shamba la shayiri karibu na langu. Nendeni mkalichome moto.” Kwa hiyo watumishi wa Absalomu wakalichoma moto shamba la Yoabu. 31Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu akamwuliza, “Kwa nini watumishi wako wamechoma moto shamba langu?” 32Absalomu akamjibu, “Tazama, nilikupelekea ujumbe, uje huku ili nikutume kwa mfalme, ukamwulize: ‘Kwa nini niliondoka Geshuri? Ingekuwa bora kwangu kubaki huko’. Sasa nisaidie nipate kumwona mfalme. Kama nina hatia basi, na aniue!” 33Kwa hiyo Yoabu akaenda na kumweleza mfalme maneno hayo yote, naye akamwita Absalomu, naye akaingia kwa mfalme, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme. Na mfalme akambusu Absalomu.


2Samweli14;1-33

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: