Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 15 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 13...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Mungu wetu Muumba wetu,Baba yetu,Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Baba wa Yatima ,Mume wa wajane,Baba wa upendo,Baba wa Baraka,Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyooneka,Muweza wa yote,Jehovah..!Yahweh..!Adonai..!Elohim..!El Elyon..!El Olam..!El Qanna..!El Shaddai..!Emanueli-Mungu pamoja nasi...!!!



Hapo mwanzo, Mungu aliumba mbingu na dunia. Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji na roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji. Mungu akasema, “Mwanga uwe.” Mwanga ukawa. Mungu akauona mwanga kuwa ni mwema. Kisha Mungu akautenganisha mwanga na giza, mwanga akauita “Mchana” na giza akaliita “Usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya kwanza. Mungu akasema, “Anga liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.” Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo. Mungu akaliita anga “Mbingu.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili.



Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Baba wa Mbinguni...!

Mungu akasema, “Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nchi kavu itokee.” Ikawa hivyo. Mungu akapaita mahali pakavu “Nchi” na kusanyiko la maji akaliita “Bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Nchi na ioteshe mimea. Mimea izaayo mbegu, na miti izaayo matunda yenye mbegu.” Ikawa hivyo. Basi, nchi ikaotesha mimea izaayo mbegu kwa jinsi yake, na miti izaayo matunda yenye mbegu kwa jinsi yake. Mungu akaona kuwa ni vyema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tatu.


Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya Yahweh na kesho ni siku nyingine Jehovah..
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako 
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...

Mungu akasema, “Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka, na ingae angani na kuiangazia dunia.” Ikawa hivyo. Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia, ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne. Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.” Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema. Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano.


Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu 
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji...
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu ukatawale katika maisha yetu,Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Jehovah ukatuongoze tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukabariki vyote tunavyenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo...
Yahweh tunaomba amani yako ikatawale,upendo ukadumu kati yetu,utu wema na fadhili,hekima na busara na tukatende yote yanayokupendeza wewe Yahweh tukawe salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni....
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Utufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...

Mungu akasema, “Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina.” Ikawa hivyo. Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema. Kisha Mungu akasema, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.” Basi, Mungu akaumba mtu kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba. Aliwaumba mwanamume na mwanamke. Mungu akawabariki na kuwaambia, “Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani.” Kisha Mungu akasema, “Tazama, nawapeni kila mmea duniani uzaao mbegu, na kila mti uzaao matunda yenye mbegu; mbegu zao au matunda yao yatakuwa chakula chenu. Nao wanyama wote duniani, ndege wote wa angani, viumbe vyote vitambaavyo, naam, kila kiumbe chenye uhai, chakula chao kitakuwa majani yote ya mimea.” Ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya sita.

Yahweh tunarudisha shukrani sifa na utukufu una wewe
Asante kwa uwepo wako Mungu wetu,Asante kwa matendo yako makuu
Asante kwa uponyaji wako,Asante kwa kujibu maombi yetu Baba wa Mbinguni,Asante kwa amani yako kwa watoto wako Yahweh Asante kwa kuwafungua Mungu wetu na kuwaongoza,Umekuwa Mwema Yahweh umesikia kilio chao umewatendea kwa wakati unaofaa Yahweh umewapa sawasawa na mapenzi yako Mungu wetu,mkono wako wenye nguvu na uponyaji umegusa maisha ya  watu wako Jehovah.... Ee Baba wa Mbinguni tunashukuru...!!

Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu na  wengine wanaohitaji uponyaji wako,watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Jehovah ukawasikie kulia kwao Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako Yahweh ukawatendee sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma..
pendo lenu si bure Mungu akawabariki katika yote na akawape kinacho wafaa..
Nawapenda.

Amnoni na Tamari
1Absalomu, alikuwa na dada yake mzuri aliyeitwa Tamari. Muda si muda, Amnoni, mtoto mwingine wa kiume wa Daudi, akampenda sana Tamari. 2Amnoni aliteseka sana hata akajifanya mgonjwa kwa sababu ya dada yake Tamari hasa kwa vile Tamari alikuwa bikira, na ilionekana jambo lisilowezekana kwa Amnoni kufanya chochote naye. 3Lakini Amnoni alikuwa na rafiki aliyeitwa Yonadabu, mtoto wa Shama, ndugu ya Daudi. Yonadabu alikuwa mtu mwerevu sana. 4Yonadabu akamwambia Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme, kwa nini unakonda na unaonekana huna furaha kila siku? Mbona hutaki kuniambia.” Amnoni akamwambia, “Nampenda Tamari, dada ya ndugu yangu Absalomu.”
5Yonadabu akamwambia, “Wewe jilaze kitandani ukidai kuwa u mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona, wewe msihi ukisema, ‘Mruhusu dada yangu, Tamari, aje aniletee mkate nipate kula na aniandalie chakula mbele yangu ili nikione naye mwenyewe anilishe.’” 6Hivyo, Amnoni akaendelea kulala kitandani, akijifanya mgonjwa. Mfalme alipokwenda kumwona, Amnoni alimwambia, “Nakuomba, Tamari aje hapa anitengenezee mikate michache huku nikimwangalia. Halafu yeye mwenyewe anilishe.”
7Hivyo, Daudi alipeleka ujumbe kwa Tamari kwamba aende nyumbani kwa kaka yake Amnoni, akamtengenezee chakula. 8Tamari alikwenda huko, akamkuta Amnoni amelala. Akachukua unga, akaukanda, na kuoka mikate mbele ya Amnoni. 9Mikate hiyo ilipokuwa tayari, Tamari akaiopoa kutoka kikaangoni. Akampelekea Amnoni, lakini Amnoni alikataa kula, akasema kila mmoja na atolewe nje, na wote wakaondoka. 10Kisha, Amnoni akamwambia Tamari, “Sasa niletee mikate hiyo chumbani kwangu, halafu unilishe.” Tamari aliichukua mikate aliyoiandaa na kuipeleka chumbani kwa kaka yake Amnoni. 11Hapo, alipokuwa anampatia mikate hiyo, Amnoni alimkamata na kumwambia, “Njoo ulale nami.” 12Tamari akamwambia, “Sivyo, kaka yangu, usinilazimishe. Kitendo hiki hakifanyiki katika Israeli. Usifanye kitendo hiki cha kipumbavu. 13Kwa upande wangu, siwezi kuvumilia aibu hiyo. Na kwa upande wako, utakuwa mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, mimi nakusihi uzungumze na mfalme kwani hatakukataza kunioa.” 14Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza na kwa kuwa alimzidi nguvu, alimlazimisha, akalala naye. 15Kisha, Amnoni akamchukia Tamari kupita kiasi. Akamchukia Tamari kuliko alivyompenda hapo awali. Akamwambia Tamari, “Ondoka mara moja.” 16Tamari akamjibu, “Sivyo kaka yangu;13:16 Sivyo kaka yangu: Makala ya Kiebrania si dhahiri. ovu hili kubwa la kunifukuza ni baya zaidi kuliko lile ulilonitendea.” Lakini Amnoni hakutaka kumsikiliza. 17Akamwita kijana wake aliyemtumikia, akamwambia, “Mtoe mwanamke huyu mbele yangu. Na mlango uufunge kwa komeo.” 18Amnoni na yule kijana wakamtoa nje na kuufunga mlango kwa komeo. Tamari alikuwa amevaa vazi refu lenye mikono mirefu kwani hivyo ndivyo walivyovaa13:18 ndivyo walivyovaa: Makala ya Kiebrania: Walivaa mavazi. mabikira wa mfalme zamani hizo. 19Basi, Tamari alijipaka majivu kichwani, akalipasua vazi lake, akaweka mikono yake kichwani, halafu akaondoka huku analia kwa sauti. 20Kaka yake, Absalomu, alipomwona, alimwuliza, “Je, Amnoni kaka yako amelala nawe? Tulia dada yangu. Yeye ni kaka yako. Usilitie jambo hilo moyoni mwako.” Hivyo, Tamari aliishi katika nyumba ya Absalomu akiwa na huzuni na mpweke.
21Mfalme Daudi aliposikia jambo hilo alikasirika sana. 22Absalomu alimchukia Amnoni sana hata hakusema naye, kwa sababu alimshika kwa nguvu dada yake Tamari akalala naye.

Absalomu ajilipiza kisasi

23Baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na shughuli ya kuwakata kondoo wake manyoya mjini Baal-hasori, karibu na Efraimu. Akawaalika watoto wote wa kiume wa mfalme. 24Absalomu alimwendea mfalme Daudi, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako ninao wakata-kondoo manyoya. Nakuomba wewe mfalme pamoja na watumishi wako, mwende pamoja nami, mtumishi wako.”
25Mfalme akamjibu, “Sivyo, mwanangu, tusiende wote; tusije tukawa mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alizidi kumsihi baba yake aende, lakini mfalme alikataa, ila alimpa baraka zake. 26Halafu, Absalomu akamwambia, “Kama huendi, basi, mruhusu ndugu yangu Amnoni twende naye.” Mfalme akamjibu, “Lakini kwa nini aende pamoja nanyi?” 27Lakini Absalomu alizidi kumsihi, na mwishowe mfalme akamruhusu Amnoni na wanawe wengine waende kwenye sherehe hiyo. 28Absalomu akawaambia watumishi wake, “Mwangalieni Amnoni atakapokuwa amekunywa divai na kufurahi. Nitakapowaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ muueni. Hiyo ni amri yangu kwenu. Jipeni moyo na muwe hodari.” 29Hivyo, watumishi wa Absalomu walimtendea Amnoni kama walivyoamriwa na Absalomu, kisha wana wa kiume wengine wa mfalme wakaondoka kila mmoja akapanda nyumbu wake na kukimbia.
30Walipokuwa bado njiani, Daudi alipata habari kuwa Absalomu amewaua watoto wake wote hakuna hata mmoja aliyesalia. 31Mfalme Daudi aliinuka, akararua mavazi yake kwa huzuni akalala chini. Hata na watumishi wake wote waliokuwa wamesimama karibu naye walirarua mavazi yao. 32Lakini Yonadabu, mwana wa Shimea, ndugu ya Daudi akamwambia, “Bwana wangu, usifikiri kuwa wanao wote wameuawa. Amnoni pekee ndiye aliyeuawa. Haya Absalomu aliyakusudia kuyafanya tangu wakati ule Amnoni alipomshika kwa nguvu dada yake Tamari na kulala naye. 33Hivyo, bwana wangu, usifikiri moyoni mwako kwamba watoto wako wote wamekufa. Ni Amnoni pekee ndiye aliyeuawa.” 34Lakini Absalomu alikuwa amekwisha kimbia. Naye kijana aliyekuwa na zamu ya ulinzi, mara akaona kundi kubwa la watu wanakuja kutokea mlimani katika barabara ya kutoka Horonaimu.13:34 barabara … Horonaimu: Kiebrania: Barabara nyuma. 35Yonadabu akamwambia Daudi, “Tazama mfalme, wanao wanakuja kama nilivyokuambia mimi mtumishi wako.” 36Mara tu yule mtumishi alipomaliza kusema, wana wa kiume wa mfalme wakaingia, wakaanza kulia kwa sauti. Mfalme na watumishi wake wote, wakalia kwa uchungu.
37Lakini Absalomu alikimbilia kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa mji wa Geshuri. Mfalme Daudi akamwombolezea mwanawe Amnoni kwa siku nyingi. 38Absalomu alikimbilia mjini Geshuri, akakaa huko kwa muda wa miaka mitatu. 39Baada ya mfalme Daudi kutulia kutokana na kifo cha Amnoni, alianza kutamani kumwona mwanawe Absalomu.


2Samweli13;1-39

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: