Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 28 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 22...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote....

Asante Baba wa mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu...
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Yahweh,Uabudiwe Jehovah...!!
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako yanatisha,Matendo yako ni ya ajabu,Neema yako yatutosha ee Baba wa Mbinguni....

Basi, tuyaache nyuma yale mafundisho ya mwanzomwanzo juu ya Kristo, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa, na sio kuendelea kuweka msingi kuhusu kuachana na matendo ya kifo, na juu ya kumwamini Mungu; mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele. Hilo tutafanya, Mungu akipenda. Maana watu waliokwisha kuangaziwa, wakaonja zawadi za mbinguni, wakashirikishwa Roho Mtakatifu na kuonja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao, kisha wakaiasi imani yao, haiwezekani kuwarudisha hao watubu tena. Hao wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu kwa makusudi na kumwaibisha hadharani.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyotenda
kwakuwaza,kwakunena,Kwakutenda,kwakujua/kutojua...
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni
utuokoe na yule mwovu  na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima imebarikiwa na Mungu. Ardhi ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto. Ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tuna uhakika wa kupewa mambo mema zaidi: Yaani wokovu. Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mliyoonesha kwa ajili yake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake. Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aoneshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia. Hivyo msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu, wakapokea yale aliyoahidi Mungu.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe maarifa na ubunifu katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji...
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni tuaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote
tunavyovimiliki,Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu tukawe salama moyoni Baba wa Mbinguni ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii....
Jehovah ukaonekane  katika maisha yetu Mungu wetu popote tupitapo
na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni...
Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba ukavitakase na 
kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo....
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu...
Mungu wetu ukatufanye barua njema nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...



Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa. Mungu alisema: “Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi.” Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo akapokea kile alichoahidiwa na Mungu. Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu kuliko wao, na kiapo husuluhisha ubishi wote. Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake. Basi, kuna vitu hivi viwili: Ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu. Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo lapenya mpaka mahali patakatifu mbinguni. Yesu mwenyewe ametangulia kuingia humo kwa ajili yetu na amekuwa kuhani mkuu milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.



Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
watoto wako wanaokuita,wanaokungojea,wanaokulilia na kukuomba
kwa bidii na imani...
Yahweh ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
nazo ziwaweke huru,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Amani ikatawale,Baba wa Mbinguni ukawasamehe wale waliokwenda kinyume nawe...
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie kulia kwao
Yahweh ukawafute machozi yao Mungu wetu ukasikie 
na ukapokee sala/maombi yetu Jehova ukajibu sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele...
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika kristo Yesu kwa kuwanami/kunisoma
Mungu wetu akawabariki nakuwatendea kama inavyompendeza yeye
Nawapenda.

Wimbo wa ushindi wa Daudi

1Daudi alimwimbia Mwenyezi-Mungu maneno ya wimbo ufuatao siku ile Mwenyezi-Mungu alipomkomboa mikononi mwa adui zake, na mkononi mwa Shauli. 2Alisema,
“Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu,
ngome yangu, na mkombozi wangu.
3Mungu wangu, mwamba wangu, ninayemkimbilia usalama;
ngao yangu, nguvu ya wokovu wangu,
ngome yangu na kimbilio langu.
Mwokozi wangu; unaniokoa kutoka kwa watu wakatili.
4Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie,
nami naokolewa kutoka kwa adui zangu.
5“Maana mawimbi ya kifo yalinizingira,
mafuriko ya maangamizi yalinivamia;
6kamba za kuzimu zilinizinga,
mitego ya kifo ilinikabili.
7“Katika taabu yangu, nilimwita Mwenyezi-Mungu;
nilimwita Mungu wangu.
Toka hekaluni mwake aliisikia sauti yangu,
kilio changu kilimfikia masikioni mwake.
8“Hapo, dunia ikatetemeka na kutikisika,
misingi ya mbinguni ikayumbayumba na kuruka,
kwani Mungu alikuwa amekasirika.
9Moshi ulifuka kutoka puani mwake,
moto uunguzao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake.
10Aliinamisha anga, akashuka chini;
na wingu jeusi chini ya miguu yake.
11Alipanda kiumbe chenye mabawa22:11 kiumbe chenye mabawa; Kiebrania: Kerubi. na kuruka,
alionekana juu ya mabawa ya upepo.
12Alijizungushia giza pande zote,
kifuniko chake kilikuwa mawingu mazito na mkusanyiko wa maji.22:12 makala ya Kiebrania si dhahiri.
13Umeme ulimulika mbele yake,
kulilipuka makaa ya moto.
14Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni,
Mungu Mkuu akatoa sauti yake.
15Aliwalenga adui mishale, akawatawanya,
alirusha umeme, akawatimua.
16Mwenyezi-Mungu alipowakemea,
kutokana na pumzi ya puani mwake,
vilindi vya bahari vilifunuliwa,
misingi ya dunia ikaonekana.
17“Mungu alinyosha mkono wake toka juu, akanichukua,
kutoka kwenye maji mengi alininyanyua.
18Aliniokoa kutoka kwa adui yangu mwenye nguvu,
aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia
maana walikuwa na nguvu nyingi kunishinda.
19Walinivamia nilipokuwa taabuni,
lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu.
20Alinileta, akaniweka mahali pa usalama,
alinisalimisha, kwani alipendezwa nami.
21“Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu;
alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia.
22Maana, nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu,
wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu.
23Nimeshika maagizo yake yote,
sikuacha kufuata masharti yake.
24Mbele yake sikuwa na hatia,
nimejikinga nisiwe na hatia.
25Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu,
yeye anajua usafi wangu.
26“Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu,
mwema kwa wale walio wema.
27Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu,
lakini mkatili kwa watu walio waovu.
28Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu,
lakini wawaangalia wenye majivuno kuwaporomosha.
29Ee Mwenyezi-Mungu, wewe u taa yangu,
Mungu wangu, unayefukuza giza langu.
30Kwa msaada wako, wakishambulia kikosi;
wewe wanipa nguvu ya kuruka kuta zake.
31Anachofanya Mungu hakina dosari!
Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika;
yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia.
32“Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu?
Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu?
33Mungu huyu ndiye kimbilio langu imara,
na ameifanya njia yangu iwe salama.22:33 makala ya Kiebrania si dhahiri.
34Ameiimarisha miguu yangu22:34 yangu: Au yake. kama ya paa,
na kuniweka salama juu ya vilele.
35Hunifunza kupigana vita,
mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba.
36Umenipa ngao yako ya kuniokoa;
msaada wako umenifanya mkuu.
37Umenirahisishia njia yangu;
wala miguu yangu haikuteleza.
38Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza,
sikurudi nyuma mpaka wameangamizwa.
39Niliwaangamiza, nikawaangusha chini
wasiweze kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita;
uliwaporomosha adui chini yangu.
41Uliwafanya adui zangu wakimbie,
na wale walionichukia niliwaangamiza.
42Walitafuta msaada, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa,
walimlilia Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwajibu.
43Niliwatwanga na kuwaponda kama mavumbi ya nchi,
nikawaponda na kuwakanyaga kama matope barabarani.
44“Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu,22:44 sehemu ya aya hii makala ya Kiebrania si dhahiri.
umenifanya mtawala wa mataifa.
Watu nisiowajua walinitumikia.
45Wageni walinijia wakinyenyekea,
mara waliposikia habari zangu walinitii.
46Wageni walikufa moyo;
wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka.22:46 wakitetemeka: Kiebrania: Wamejifunga wenyewe.
47“Mwenyezi-Mungu yu hai!
Asifiwe mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu.
48Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi
na kuyatiisha mataifa chini yangu.
49Ameniokoa kutoka adui zangu.
Ee Mwenyezi-Mungu, ulinikuza juu ya wapinzani wangu
na kunisalimisha mbali na watu wakatili.
50“Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa,
ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako.
51Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa;22:51 Mungu … mkubwa: Au yeye ni mnara wa wokovu.
humwonesha fadhili zake huyo aliyemweka wakfu,
naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.”


2Samweli22;1-51

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 27 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 21...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa vyote vilivyomo
vinavyoonekana na visivyoonekana,Mungu mwenye nguvu,
Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mume wa wajane,Baba wa Yatima
Muweza wa yote hakuna kama wewe,wewe ni Alfa na Omega...

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Wengi walitamani Baba wa Mbinguni lakini haikuwezekana
Si kwasababu wao ni waovu na si kwamba wao wametenda mabaya sana
zaidi ya sisi uliyetupa nafasi hii/uhai na kuwa wazima mpaka leo hii..
Si kwa uwezo wetu si kwa nguvu zetu si kwamba sisi ni wema sana au
sisi ni wazuri mno sikwamba sisi niwajuaji na tuna akili sana
hapana ni kwa neema/rehema zako ni kwa mapenzi yako Mungu wetu
sisikuwa hivi tulivyo leo hii...
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu.....!!


Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nenda katika ikulu ya mfalme wa Yuda, uwape watu ujumbe huu: Wewe mfalme wa Yuda unayekikalia kiti cha enzi cha mfalme Daudi, pamoja na watumishi wako na watu wako wanaopita katika malango haya, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tendeni mambo ya haki na uadilifu. Mwokoeni mikononi mwa mdhalimu mtu yeyote aliyenyanganywa mali zake. Msiwatendee vibaya au ukatili wageni, yatima na wajane wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia mahali hapa. Kama mkishika neno hili nililowaambia basi, wafalme wanaokikalia kiti cha enzi cha Daudi wataendelea kuingia kwa kupitia malango ya ikulu hii. Watapita pamoja na watumishi wao na watu wao, wakiwa wamepanda farasi na magari ya farasi. Lakini kama hamtatii maneno haya, mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwa nafsi yangu kwamba mahali hapa patakuwa magofu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Mwenyezi-Mungu asema hivi kuhusu ikulu ya mfalme wa Yuda: “Ingawa waonekana kuwa mzuri kama nchi ya Gileadi kama kilele cha Lebanoni, Lakini naapa kuwa nitakufanya uwe jangwa, uwe mji usiokaliwa na watu. Nitawatayarisha waangamizi dhidi yako, kila mmoja na silaha yake mkononi. Wataikata mierezi yako mizuri, na kuitumbukiza motoni. “Kisha watu wengi wa mataifa watapita karibu na mji huu, na kila mmoja atamwuliza mwenzake: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameutenda hivi mji huu mkubwa?’ Wenzao watawajibu, ‘Ni kwa sababu waliliacha agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, wakaiabudu miungu mingine na kuitumikia.’”


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akaili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona
Kwakupigwa kwake sisi tumepata kuwa huru...

Msimlilie mtu aliyekufa, wala msiombolezee kifo chake. Bali mlilieni kwa uchungu yule aendaye mbali, kwa kuwa hatarudi tena kuiona nchi yake. Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Shalumu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, aliyetawala baada ya Yosia baba yake, na ambaye aliondoka mahali hapa: “Shalumu hatarudi tena mahali hapa, bali atafia hukohuko walikomchukua utumwani. Kamwe hataiona tena nchi hii.


Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Baba wa Mbinguni nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji...
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu
Mungu wetu tunaomba ukawabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia Baba wa Mbinguni tunaomba 
ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba ukabariki
vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah ukavitakase na ukavifunike
kwa Damu ya mwanao mpendwa bwana na Mwokozi wetu Yesu kristo
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu Jehovah ukaonekane 
popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Tukanene yaliyo yako,tukapate kutambua/kujitambua Mungu wetu tukawe salama moyoni Yahweh tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote
za maisha yetu,Jehovah ukatupe macho ya kuona Yahweh ukatupe masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu amani,furaha,
upendo kati yetu ukadumu....
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.....
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


“Ole wako Yehoyakimu wewe unayejenga nyumba kwa dhuluma na kuiwekea ghorofa bila kutumia haki. Unawaajiri watu wakutumikie bure wala huwalipi mishahara yao. Wewe wasema: ‘Nitalijenga jumba kubwa, lenye vyumba vikubwa ghorofani.’ Kisha huifanyia madirisha, ukafunika kuta zake kwa mbao za mierezi, na kuipaka rangi nyekundu! Unadhani umekuwa mfalme kwa kushindana kujenga kwa mierezi? Baba yako alikula na kunywa, akatenda mambo ya haki na mema ndipo mambo yake yakamwendea vema. Aliwapatia haki maskini na wahitaji, na mambo yake yakamwendea vema. Hii ndiyo maana ya kunijua mimi Mwenyezi-Mungu. Lakini macho yako wewe na moyo wako, hungangania tu mapato yasiyo halali. Unamwaga damu ya wasio na hatia, na kuwatendea watu dhuluma na ukatili. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu ya Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda: Wakati atakapokufa, hakuna atakayemwombolezea akisema, ‘Ole, kaka yangu!’ ‘Ole, dada yangu!’ Hakuna atakayemlilia akisema, ‘Maskini, bwana wangu!’ ‘Maskini, mfalme wangu!’ Atazikwa bila heshima kama punda, ataburutwa na kutupiliwa mbali, nje ya malango ya Yerusalemu.”

Tazama wenye shida/tabu,Wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio kata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka,walio katika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,waliorudinyuma/walioanguka,wenye uchungu moyoni,wanaotafuta watoto,wanaotafuta kazi,wanaotaka kurudi shule,waliokwama kibiashara,walio umizwa rohoni,walio dhulumiwa na wote  wanaokuita/kuhitaji,wanaokutafuta kwa bidii na imani....
 Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia
Yahweh ukawasamehe na kuwasimamisha tena,Mungu wetu ukabariki
kazi za mikono yao,mashamba yao,masomo yao na ukawape unachoona kinawafaa Baba wa Mbinguni....
Ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako Mungu wetu
Nuru yako ikaangze katika maisha yao,ukaonekane Mungu wetu katika
maisha yao,ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni ukawafute machozi yao
Mungu wetu ukasikie,ukapokee sala/maombi yetu Baba wa Mbinguni ukajibu na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina...!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu wetu akawatendee na kuwabariki katika yote sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.


Wazawa wa Shauli wanauawa

1Wakati mmoja kulitokea njaa kali nchini Daudi akiwa mfalme. Njaa hiyo ilidumu miaka mitatu mfululizo. Daudi alimwomba Mwenyezi-Mungu shauri. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Shauli na jamaa yake wana hatia ya kumwaga damu kwa sababu aliwaua Wagibeoni.” 2Hivyo, mfalme Daudi akawaita Wagibeoni21:2 Wagibeoni: Makala ya Kiebrania: Wagibeoni na akawaambia. (Wagibeoni hawakuwa Waisraeli ila walikuwa mabaki ya Waamori. Ingawa watu wa Israeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Shauli alijaribu kuwaua wote kwani alikuwa na bidii ya upendeleo kwa watu wa Israeli na wa Yuda). 3Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitalipaje kwa maovu mliyotendewa ili mpate kuibariki nchi hii na watu wake Mwenyezi-Mungu?” 4Wagibeoni wakamwambia, “Kisa chetu na Shauli pamoja na jamaa yake si jambo la fedha au dhahabu. Wala si juu yetu kumwua yeyote katika nchi ya Israeli.” Mfalme akawauliza tena, “Sasa mnasema niwatendee nini?” 5Wao wakamwambia mfalme, “Shauli alikusudia kutuua sisi na kutuangamiza, asiache mtu wetu yeyote katika eneo lote la Israeli. 6Basi, tukabidhi watu saba kati ya wanawe wa kiume, nasi tuwanyonge mbele ya Mwenyezi-Mungu mlimani Gibea, kwa Shauli aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu.” Mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”
7Lakini mfalme alimnusuru Mefiboshethi mwana wa Yonathani kwa sababu ya kiapo ambacho Daudi na Yonathani mwana wa Shauli walikuwa wamekula kati yao kwa jina la Mwenyezi-Mungu. 8Lakini mfalme aliwachukua wana wawili ambao Rispa binti Ahiya alimzalia Shauli, Armoni na Mefiboshethi,21:8 Mefiboshethi: Au Meri-baali. pamoja na watoto wote watano wa kiume wa Mikali, binti Shauli ambao alimzalia Adrieli mwana wa Barzilai Mmeholathi. 9Watoto hao saba wa kiume Daudi aliwakabidhi kwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele ya Mwenyezi-Mungu, wote saba wakafa pamoja. Watoto hao waliuawa mwanzoni mwa mavuno ya shayiri.
10Kisha, Rispa binti Aya alichukua nguo ya gunia, akajitandikia mwambani. Alikaa hapo tangu mwanzo wa mavuno mpaka wakati wa mvua ulipowadia na kuinyeshea maiti. Wakati huo wote, aliwafukuza ndege wa angani na wanyama wa porini, usiku na mchana, ili wasifikie maiti hizo. 11Daudi aliposikia yale aliyofanya Rispa binti Aya, suria wa Shauli, 12alikwenda na kuichukua mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka wakazi wa Yabesh-gileadi, waliokuwa wameiiba kutoka mtaani huko Beth-sheani, ambako Wafilisti walikuwa wamemtundika Shauli na Yonathani siku ile Wafilisti walipomuua Shauli mlimani Gilboa. 13Basi, Daudi akairudisha mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka huko; halafu wakakusanya mifupa ya vijana saba waliotundikwa. 14Basi, watu wa Daudi wakaizika mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Sela katika kaburi la Kishi baba yake Shauli. Walifanya kila kitu ambacho mfalme aliamuru. Baada ya hayo, Mungu akayasikiliza maombi kuhusu nchi yao.

Vita dhidi ya majitu ya Wafilisti

(1Nya 20:4-8)

15Kisha Wafilisti walifanya vita tena na Waisraeli. Naye Daudi na watu wake wakaenda kupigana na Wafilisti. Daudi alichoka sana siku hiyo. 16Ishbi-benobu, mmojawapo wa wazawa wa majitu ambaye mkuki wake wa shaba ulikuwa na uzito wa karibu kilo tatu na nusu na aliyekuwa amejifunga upanga mpya alisema atamuua Daudi. 17Lakini Abishai mwana wa Seruya, alikwenda kumsaidia Daudi. Abishai alimshambulia yule Mfilisti na kumwua. Hivyo, watu wakamwapia Daudi wakisema, “Hutakwenda tena nasi vitani, la sivyo utaizima taa ya ufalme katika Israeli.”
18Baada ya hayo, kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Huko Sibekai, Mhushathi, alimuua Safu aliyekuwa mmojawapo wa wazawa wa Warefai. 19Kulitokea tena mapigano na Wafilisti huko Gobu. Naye Elhanani mwana wa Yaareo-regimu, Mbethlehemu, alimuua Goliathi Mgiti, ambaye mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo. 20Baadaye kulitokea tena vita huko Gathi ambako kulikuwa na mtu mmoja alikuwa mkubwa kwa kimo, na mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake vidole ishirini na vinne. Yeye pia alikuwa mzawa wa majitu. 21Alipowadhihaki Waisraeli, Yonathani mwana wa Shimei, nduguye Daudi, alimuua. 22Hao wanne walikuwa wazawa wa majitu huko Gathi, nao waliuawa na Daudi pamoja na watumishi wake.


2Samweli21;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 26 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 20...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo wetu,Si kwamba sisi ni wema sana au ni wazuri mno,Si kwa utashi wetu wala akili zetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii ni kwa neema/rehema zake ni kwa mapenzi yake Mungu Baba..
Tumshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake kwetu wakati wote..
Asante Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe ee Jehovah,Uabudiwe Yahweh,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu,Neema yako yatutosha ee Mungu wetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Baba wa Mbinguni...


Mnamo siku ya ishirini na moja, mwezi wa saba mwaka huohuo, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Hagai. Alimwambia Hagai aongee na mkuu wa Yuda, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki na watu wote waliorudi kutoka uhamishoni awaambie hivi: “Je, kuna yeyote kati yenu asiyekumbuka jinsi hekalu hili lilivyokuwa la fahari? Sasa mnalionaje? Bila shaka sasa mnaliona kama si kitu! Hata hivyo, usife moyo, ewe Zerubabeli. Jipe moyo, kuhani mkuu Yoshua mwana wa Yehosadaki. Jipeni moyo nanyi watu wote wa nchi hii. Fanyeni kazi, maana mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nipo pamoja nanyi. Mlipotoka Misri niliwaahidi kwamba daima nitakuwa pamoja nanyi. Basi, ningali pamoja nanyi, kwa hiyo, msiogope kitu. “Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema, hivi karibuni nitazitikisa mbingu na dunia, bahari na nchi kavu. Nitayatikisa mataifa yote na hazina zao zote zitaletwa humu, nami nitalifanya hekalu hili kuwa la fahari. Mimi nimesema. Fedha na dhahabu yote duniani ni mali yangu. Hekalu jipya litakuwa lenye fahari zaidi kuliko lile la awali, na mahali hapo ndipo nitakapowapa watu wangu fanaka.” Asema Mwenyezi-Mungu wa majeshi.


Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu baba wa Mbinguni tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilimjia nabii Hagai, akamwambia: “Waambie makuhani watoe uamuzi juu ya jambo hili: Kama mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha akagusa kwa upindo wa vazi hilo mkate au chakula kilichopikwa, au divai, au mafuta au chakula cha aina yoyote ile, je, chakula hicho kitakuwa kitakatifu?” Makuhani wakamjibu, “La, hasha.” Hagai akawauliza tena, “Je, mtu aliye najisi kwa kugusa maiti, akigusa baadhi ya vyakula hivi, chakula hicho kitakuwa najisi?” Makuhani wakamjibu, “Ndiyo, kitakuwa najisi.” Hapo Hagai akawaambia, “Mwenyezi-Mungu asema kwamba, hivyo ndivyo ilivyo kwa watu wa taifa hili na kila kitu wanachofanya; kadhalika na kila wanachotoa madhabahuni ni najisi.

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,Mungu wetu tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia Yahweh ukatubariki tuingiapo/tutokapo Jehovah ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu tunaomba ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..
Yahweh tukawe salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia Neno lako na kulitii...
Mungu wetu tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako Jehovah tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kama upo Baba wa Mbinguni.....
Mungu wetu ukatupe neema ya Hekima,Busara,Amani,Upendo,Furaha,Huruma,Shukrani,Fadhili,Utuwema na yote yanayokupendeza wewe..
Jehovah ukatufanye chombo chema Baba wa Mbinguni nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....

“Lakini sasa angalieni mambo yatakayotukia. Kabla ya kuanza kujenga upya hekalu langu, hali yenu ilikuwaje? Mliliendea fungu la nafaka mkitarajia kupata vipimo ishirini, lakini kulikuwa na vipimo kumi tu. Mliliendea pipa la divai mkitarajia kujaza vyombo hamsini, lakini mlikuta ishirini tu. Niliwapiga kwa ukame, ukungu na mvua ya mawe, nikaharibu kila mlichojaribu kupanda, lakini hata hivyo hamkunirudia. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu. Leo ni siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, siku ambayo msingi wa hekalu umekamilika. Basi, ngojeni mwone yale yatakayotokea tangu leo. Ingawa sasa hamna nafaka ghalani, nayo mizabibu, mitini, mikomamanga na mizeituni haijazaa kitu, lakini tangu leo, nitawabariki.”

Mungu wetu tunarudisha Shukrani,Sifa,Utukufu una wewe
Yahweh asante kwa matendo yako makuu kwetu
Baba wa Mbinguni asante kwa baraka zako,Uponyaji wako Yahweh kwa kufungua njia/milango kwenye maisha yetu
Baba wa Mbinguni mkono wako wenye nguvu na uponyaji umegusa maisha yetu Yahweh tulikuita ukaitika,Jehovah tulikwambia ukasikia,Baba wa Mbinguni tulikuomba umetupa sawasawa na mapenzi yako
Yahweh umekuwa faraja Mungu wetu umekuwa mtetezi wetu Baba wa Mbinguni umeonekana kwenye maisha ya watoto wako waliokuomba kwa bidii na imani Yahweh tukurudishie nini kwa wema wako na fadhili zako?
Hakuna neno zuri linalo faa na kutosha kulifikisha kwako Mungu wetu
zaidi ya kukusifu,kukuabudu na kufuata njia zako ee Mungu wetu uzidi kutuongoza....!!



Siku hiyohiyo ya ishirini na nne, mwezi wa tisa, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Hagai mara ya pili: “Ongea na Zerubabeli mkuu wa Yuda, umwambie hivi: Niko karibu kuzitikisa mbingu na dunia, kuangusha falme na kukomesha nguvu zao. Nitayapindua magari yao ya farasi na wapandafarasi wake, nao wataanguka na kuuana wao kwa wao. Siku hiyo, nitakuchukua wewe mtumishi wangu Zerubabeli mwana wa Shealtieli, na kukuteua ili utawale kwa jina langu. Wewe ndiwe niliyekuchagua.” Mwenyezi-Mungu wa majeshi amesema.
Yahweh tazama na wengine wanaokuhitaji na kukutafuta kwa bidii na imani,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Jehovah ukawaponye na kuwaongoza katika mapito yao
Yahweh ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako nazo zitawaweka huru...
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukasikie kulia kwao Mungu  wetu ukawafute machozi yao Yahweh ukapokee sala/maombi yetu Mungu wetu ukatende kama inavyokupendeza wewe....
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele....
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu mwenye nguvu akawaguse kwa mkono wake na Mkabarikiwe muingiapo/mtokapo Jehovah akawape sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda

Uasi wa Sheba

1Sasa ikawa kwamba huko Gilgali kulikuwa na mtu mmoja mlaghai aitwaye Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini. Basi Sheba alipiga tarumbeta, na kusema,
“Hatuna fungu lolote kwa Daudi,
hatuna sehemu yetu katika huyo mwana wa Yese.
Enyi watu wa Israeli,
kila mmoja na ajiendee hemani kwake!”
2Hivyo, watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi, wakamfuata Sheba mwana wa Bikri. Lakini watu wa Yuda walimfuata mfalme Daudi kwa uaminifu toka mto Yordani mpaka mjini Yerusalemu. 3Hatimaye, Daudi aliwasili nyumbani kwake mjini Yerusalemu. Mfalme aliwachukua masuria wake kumi ambao alikuwa amewaacha kuangalia nyumba yake, akawaweka kwenye nyumba moja chini ya ulinzi, akawatunza vizuri, lakini hakulala nao. Hivyo, masuria hao wakawa wametiwa ndani hadi siku za kufa kwao, wakaishi kana kwamba, walikuwa wajane.
4Kisha, mfalme akamwambia Amasa, “Nikusanyie watu wote wa Yuda katika siku tatu, na wewe mwenyewe uwepo.” 5Basi, Amasa akaenda kuwaita watu wa Yuda. Lakini akachelewa kurudi katika wakati ule aliopangiwa na mfalme. 6Daudi akamwambia Abishai, “Sasa, Sheba mwana wa Bikri, atatuletea madhara kuliko Absalomu. Chukua watumishi wangu, umfuatie Sheba asije akaingia kwenye miji yenye ngome akaponyoka, tusimwone tena.” 7Abishai akatoka akiwa pamoja na Yoabu, Wakerethi na Wapelethi pamoja na mashujaa wote. Hao wote waliondoka Yerusalemu kwenda kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. 8Walipofika kwenye jiwe kubwa lililoko huko Gibeoni, Amasa akatoka kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa vazi la kijeshi, na ndani ya vazi hilo kulikuwa na mkanda ulioshikilia upanga kiunoni mwake ukiwa kwenye ala yake. Yoabu alipokuwa anakaribia, upanga wake ulichomoka alani ukaanguka chini. 9Yoabu akamwambia Amasa, “Je, hujambo ndugu yangu?” Yoabu akamshika Amasa kidevuni kwa mkono wa kulia kana kwamba anataka kumbusu. 10Lakini Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu. Basi, Yoabu akamchoma Amasa upanga tumboni, matumbo yake yakatoka nje, akafa. Yoabu hakumchoma upanga mara mbili.
Kisha, Yoabu na nduguye Abishai wakaendelea kumfuatilia Sheba mwana wa Bikri. 11Mtu mmoja wa Yoabu akaja akasimama karibu na mwili wa Amasa, akasema, “Yeyote anayempenda Yoabu na yeyote anayempenda Daudi, na amfuate Yoabu!” 12Amasa alikuwa bado anagagaa kwenye damu yake katikati ya barabara kuu. Kwa hiyo, kila mtu aliyepita hapo, alipomwona, alisimama.20:12 kwa hiyo … alisimama: Sehemu imechukuliwa toka mwisho wa aya. Lakini yule mtu alipoona kwamba watu wote walikuja na kusimama hapo, aliuondoa mwili wa Amasa barabarani, akaupeleka shambani na kuufunika kwa nguo. 13Amasa alipoondolewa kwenye barabara kuu, watu wote sasa waliendelea kumfuata Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14Sheba alipitia katika makabila yote ya Israeli mpaka mji wa Abeli wa Beth-maaka.20:14 wa Beth-maaka: Makala ya Kiebrania: Na Beth-maaka. Watu wote wa ukoo wa Bikri20:14 Bikri: Makala ya Kiebrania: Wabikri. wakakusanyika na kumfuata. 15Watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakaenda kumzingira Sheba akiwa katika mji huo wa Abeli wa Beth-maaka. Walirundika kuuzingira mji, na ngome; halafu wakaanza kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini. 16Kisha, mwanamke fulani mwenye hekima alisikika kutoka mjini akisema, “Sikieni! Sikieni! Mwambieni Yoabu aje nizungumze naye.” 17Yoabu akaenda karibu naye, huyo mwanamke akamwambia, “Je, wewe ni Yoabu?” Yoabu akasema, “Naam! Ni mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Nisikilize mimi mtumishi wako.” Yoabu akamwambia, “Nasikiliza.” 18Huyo mwanamke akamwambia, “Hapo kale watu walikuwa wakisema, ‘Waacheni watake shauri kutoka mji wa Abeli’. Ndivyo watu walivyoweza kutatua matatizo. 19Mimi ni mmojawapo wa wale wanaopenda amani na uaminifu katika Israeli. Sasa wewe unakusudia kuuharibu mji ambao ni kama mama katika Israeli. Kwa nini sasa unataka kuuangamiza mji ulio mali yake Mwenyezi-Mungu?” 20Yoabu akamjibu, “Kamwe maishani mwangu! Sina nia kuangamiza wala kuharibu. 21Ulivyosema si kweli! Lakini mtu mmoja kutoka sehemu ya milima ya Efraimu aitwaye Sheba mwana wa Bikri anataka kumwasi mfalme Daudi. Mtoeni huyo kwangu nami nitaondoka mjini kwenu.” Yule mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake kitarushwa kwako kupitia ukutani.” 22Kisha, huyo mwanamke akaenda kwa watu wote mjini kwa busara yake. Wakamkata kichwa Sheba mwana wa Bikri, wakakitupa nje kwa Yoabu. Kwa hiyo, Yoabu akapiga tarumbeta, na kuwatawanya watu wake kutoka mji huo wa Abeli; kila mtu akaenda nyumbani kwake. Kisha Yoabu akarudi kwa mfalme Daudi, mjini Yerusalemu.
Orodha ya wasaidizi wa Daudi
23Sasa Yoabu alikuwa mkuu wa jeshi lote la Israeli. Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi. 24Adoramu alikuwa msimamizi wa kazi za kulazimishwa; Yehoshafati alikuwa mwandishi wa kumbukumbu. 25Shausha alikuwa katibu; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani. 26Ira, Myairi alikuwa pia kuhani wa Daudi.



2Samweli20;1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.