Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Swahili na Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 22 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli26...Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendele kuiona leo hii..
Si kwa uwezo wetu,wala si kwa nguvu zetu,Si kwamba sisi ni wema sana zaidi ya wengine waliotangulia/kufa,Si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu sisi kuwa hivi tulivyo ni kwa neema/rehema zako Baba ni kwa mapenzi yako Mungu wetu..

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu kila wakati..
Asante kwa pumzi/uzima na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe Mungu wetu,usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jejovah
Uabudiwe Yahweh,Utukufu una wewe Mungu wetu..

Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uhai wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uhai huo kabla ya mwanzo wa nyakati, na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo niutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu. Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu.


Tazama jana imepita  Mungu wetu leo ni siku mpya Yahweh na kesho ni siku nyingine Jehovah..
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendeji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu ukatubariki na kutuongoza,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawe nasi tuingiapo/tutokapo,Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia,Yahweh ukawe ndani yetu nasi tukawe ndani yako
Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu..
Jehovah  ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu tukawe salama moyoni Baba wa Mbinguni ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Yahweh tukanene yaliyo yako na tukapate kutambua/kujitambua..
Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako siku zote za maisha yetu..
Jehovah ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi. Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo. Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu. Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho sahihi na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo. Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, na wanawapotosha wengine kwa upumbavu wao. Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha. Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: “Wakrete husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!” Naye alitoboa ukweli; na kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu. Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli. Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa. Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema.


Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,walio katika magumu/majaribu mbalimbali,walio katika vifungo vya yule mwovu,waliokata tamaa,walio kataliwa,wenye hofu na mashaka,walianguka/potea na wote waliokwenda kinyume nawe Mungu wetu tunaomba ukawasamehe,Baba wa Mbinguni ukawaponye kimwili na kiroho pia,Yahweh ukaonekane katika mapito yao
Mungu wetu ukawaongoze na ukawape neema ya kujiombea..
Baba wa Mbinguni ukawe masaada wao Mungu wetu ukawaokoe na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina..!!


Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami
Mungu mwenye nguvu na kubariki akawabariki kwa kila limpendezalo
Yahweh akawaokoe katika magumu yenu..
Neema ya Kristo Yesu ikawe nayi Daima..
Nawapenda.

Daudi anamhurumia tena Shauli

1Baadhi ya wanaume kutoka mji wa Zifu walimwendea Shauli huko Gibea wakamwambia kwamba Daudi alikuwa anajificha kwenye mlima Hakila, upande wa mashariki wa Yeshimoni. 2Mara moja, Shauli alikwenda kwenye nyika za Zifu kumtafuta Daudi akiwa na askari waliochaguliwa 3,000 wa Israeli. 3Shauli akapiga kambi juu ya mlima Hakila, karibu na barabara, mashariki ya Yeshimoni. Lakini Daudi alikuwa bado huko nyikani. Daudi alipojua kwamba Shauli alikuwa amekuja nyikani kumtafuta, 4alituma wapelelezi, akafahamishwa kwamba ni kweli. 5Daudi akatoka, akaenda mahali Shauli alipopiga kambi. Akapaona mahali ambapo Shauli alikuwa amelala na Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli, alikuwa amelala karibu na Shauli. Shauli alikuwa amelala katikati ya kambi huku akizungukwa na jeshi lake.
6Daudi akamwambia Ahimeleki ambaye alikuwa, Mhiti, na Abishai ndugu yake Yoabu (mama yao aliitwa Seruya), “Nani atakwenda pamoja nami kwenye kambi ya Shauli?” Abishai akamwambia; “Mimi nitakwenda pamoja nawe.” 7Hivyo usiku, Daudi na Abishai wakaingia kwenye kambi ya Shauli, wakamkuta Shauli amelala katikati ya kambi hiyo, na mkuki wake umechomekwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri pamoja na askari walikuwa wamelala kumzunguka Shauli. 8Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Basi, niache nimbane udongoni kwa pigo moja tu la mkuki; sitampiga mara mbili.”
9Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; maana hakika Mwenyezi-Mungu atamwadhibu mtu yeyote atakayeunyosha mkono wake dhidi ya mteule wake aliyepakwa mafuta. 10Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba Mwenyezi-Mungu mwenyewe atamuua Sauli; ama siku yake ya kufa itafika, au atakwenda vitani na kufia huko. 11Lakini Mwenyezi-Mungu anakataza nisinyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye amemteua kwa kumpaka mafuta. Lakini chukua mkuki wake ulio karibu na kichwa chake pamoja na gudulia lake la maji, halafu tujiendee zetu.” 12Hivyo, Daudi alichukua ule mkuki na gudulia la maji karibu na kichwa cha Shauli nao wakajiendea zao. Lakini hakuna mtu aliyeona au kujua tukio hilo, wala hakuna aliyeamka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu aliwaletea usingizi mzito.
13Kisha, Daudi akaenda upande wa pili wa bonde hilo, akasimama juu mlimani mbali na kundi la Shauli. 14Akaliita kwa sauti jeshi la Shauli na Abneri mwana wa Neri akisema, “Abneri, je, unanisikia?” Abneri akauliza, “Ni nani wewe unayemwita mfalme?” 15Daudi akamjibu, “Je, wewe si mwanamume? Nani aliye sawa nawe katika Israeli? Mbona basi, hukumlinda bwana wako mfalme? Mtu mmoja wetu aliingia hapo kumwangamiza bwana wako mfalme! 16Ulilotenda si jambo jema. Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba unastahili kufa, kwa kuwa hukumlinda bwana wako, ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta. Sasa hebu angalia, mkuki wa mfalme na lile gudulia la maji lililokuwa karibu na kichwa chake kama vipo!” 17Shauli alitambua sauti ya Daudi, akamwuliza, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Daudi akamjibu, “Bwana wangu, mfalme, ni sauti yangu.” 18Halafu akaendelea kusema, “Lakini kwa nini, wewe bwana wangu unifuatilie mimi mtumishi wako? Nimefanya nini? Ni ovu gani nimekufanyia? 19Basi, sasa bwana wangu mfalme, usikie maneno ya mtumishi wako. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuchochea uje dhidi yangu, basi, na apokee tambiko itakayomfanya abadili nia yake. Lakini kama ni watu, basi, Mwenyezi-Mungu na awalaani watu hao kwani wamenifukuza kutoka urithi aliotupa Mwenyezi-Mungu wakisema, ‘Nenda ukaitumikie miungu mingine.’ 20Usiniache nife katika nchi ya kigeni, mbali na Mwenyezi-Mungu. Kwa nini wewe mfalme wa Israeli umetoka kuyatafuta maisha yangu26:20 kuyatafuta maisha yangu: Makala ya Kiebrania: Kutafuta kiroboto. kama mtu anayewinda kware milimani?”
21Ndipo Shauli akajibu, “Mimi nimefanya makosa. Rudi mwanangu Daudi. Sitakudhuru tena kwa kuwa leo maisha yangu yalikuwa ya thamani mbele yako. Mimi nimekuwa mpumbavu na nimekosa vibaya sana.” 22Daudi akajibu, “Ee mfalme, mkuki wako uko hapa, mtume kijana wako mmoja aje auchukue. 23Mwenyezi-Mungu humtunza kila mtu kwa uadilifu na uaminifu wake. Leo Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu, lakini mimi sikunyosha mkono wangu dhidi yako kwa kuwa wewe umeteuliwa naye kwa kutiwa mafuta. 24Tazama kama vile leo maisha yako yalivyokuwa na thamani mbele yangu, ndivyo na maisha yangu yawe na thamani mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye akaniokoe kutoka kwenye taabu zote.”
25Shauli akamwambia Daudi, “Mungu na akubariki mwanangu Daudi. Utafanya mambo makuu, nawe utafanikiwa katika yote.” Basi, Daudi akaenda zake; Shauli naye akarudi nyumbani kwake.


1Samweli26;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: