Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 12 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli20...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyomo,vinavyoonekana na visivyooneka..
Baba wa upendo,Baba wa Yatima,Baba wa huruma,Mume wa Wajane,
Mungu wemye nguvu,Mungu wa walio hai,Muweza wa yote Alfa na Omega
Hakuna kama wewe,Matendo yako ni makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu,Neema yako yatutosha Mungu wetu..!!


Mimi Petro, mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia nyinyi wateule wa Mungu Baba, ambao mmetawanyika na mnaishi kama wakimbizi huko Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithunia. Mungu Baba aliwateua nyinyi kufuatana na kusudi lake, na mmefanywa watakatifu na Roho, mpate kumtii Yesu Kristo na kusafishwa kwa damu yake. Nawatakieni neema na amani tele.
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Si kwa nguvu zetu,wala si kwa uwezo wetu,si kwamba sisi tumetenda mema sana,si kwamba ni wazuri mno si kwa utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo ni kwa neema/rehema zako ni kwa mapenzi yako Baba wa Mbinguni sisi kuwa hivi tulivyo leo..
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni..!!


Asifiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa huruma yake kuu alitufanya tuzaliwe upya kwa kumfufua Yesu kutoka kwa wafu. Ametujalia tumaini lenye uhai, na hivyo tunatazamia kupata baraka zile ambazo Mungu aliwawekea watu wake. Mungu amewawekeeni baraka hizo mbinguni ambako haziwezi kuoza, au kuharibika, au kufifia. Hizo zitakuwa zenu nyinyi ambao kwa imani mnalindwa salama kwa nguvu ya Mungu kwa ajili ya wokovu ambao uko tayari kufunuliwa mwishoni mwa nyakati.

Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Jehovah..
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh utuepushe katika majaribu Mungu wetu tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Furahini kuhusu jambo hilo, ijapokuwa sasa, kwa kitambo kidogo, itawabidi kuhuzunika kwa sababu ya majaribio mbalimbali mnayoteseka, majaribio ambayo shabaha yake ni kuthibitisha imani yenu. Hata dhahabu yenyewe, ambayo huharibika, hujaribiwa kwa moto; hali kadhalika na imani yenu, ambayo ni ya thamani kuliko dhahabu, ni lazima ijaribiwe ipate kuwa thabiti. Hapo mtapokea sifa na utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa. Nyinyi mnampenda, ingawaje hamjamwona, na mnamwamini, ingawa hammwoni sasa. Hivyo, mnafurahi kwa furaha tukufu isiyoelezeka, kwa sababu mnapokea wokovu wa roho zenu ambao ni lengo la imani yenu. Manabii walipeleleza na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo nyinyi mngepewa. Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata. Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo nyinyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji
Baba wa Mbinguni nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh  nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatamalaki na ukatuatamie,Yahweh ukatuongoze tuingiapo/tutokapo,Mungu wetu ukabariki na kuvitakasa kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Jehovah tukawe salama moyoni,Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na amasikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Yahweh ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu tukawe barua njema na kutukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Kwa hiyo, basi, muwe tayari kabisa, na kukesha. Wekeni tumaini lenu lote katika neema ile mtakayopewa wakati Yesu Kristo atakapoonekana! Kama watoto wa Mungu wenye utii, msikubali kamwe kufuata tena tamaa mbaya mlizokuwa nazo wakati mlipokuwa wajinga. Bali mnapaswa kuwa watakatifu katika mwenendo wenu wote, kama vile yule aliyewaiteni ni mtakatifu. Maandiko yasema: “Muwe watakatifu, kwa kuwa mimi alivyo mtakatifu.” Mnapomtaja Mungu, nyinyi humwita Baba. Basi, jueni kwamba yeye humhukumu kila mmoja kadiri ya matendo yake, bila ubaguzi. Hivyo tumieni wakati wenu uliowabakia hapa ugenini katika kumcha Mungu. Maana mnajua kwamba nyinyi mlikombolewa katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliupokea kutoka kwa wazee wenu. Lakini hamkukombolewa kwa vitu vyenye kuharibika: Kwa fedha na dhahabu; bali kwa damu ya thamani ya Kristo, ambaye alikuwa kama mwanakondoo asiye na dosari wala doa. Yeye alikuwa ameteuliwa na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa, akafunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu. Kwa njia yake, mnamwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumpa utukufu; na hivyo imani na matumaini yenu yako kwa Mungu. Maadamu sasa, kwa kuutii ukweli, nyinyi mmezitakasa roho zenu na kuwapenda wenzenu bila unafiki, basi, pendaneni kwa moyo wote. Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, nyinyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele. Kama Maandiko yasemavyo: “Kila binadamu ni kama majani, na utukufu wake wote ni kama ua la majani. Majani hunyauka na maua huanguka. Lakini neno la Bwana hudumu milele.” Neno hilo ni hiyo Habari Njema mliyohubiriwa.


Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,walio katika vifungo vya yule mwovu,walikata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Mungu wetu ukawape neema ya kuomba na kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Mungu wetu ukawaponye na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako
Jehovah ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe na wakatambua,wakatubu na kukurudia wewe Mungu..
Baba ukasikie kuomba kwao,ee Mungu wetu ukapokee na kujibu na mapenzi yako yakatimie..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwa nami
Mungu Baba akawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake
Amani ya Kristo Yesu ikawe nanyi daima..
Nawapenda.



Yonathani anamsaidia Daudi

1Daudi alikimbia kutoka Nayothi katika Rama, akaenda mpaka kwa Yonathani, akamwambia, “Nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemtendea baba yako dhambi gani hata ajaribu kuyaangamiza maisha yangu?” 2Yonathani akamjibu, “Hilo na liwe mbali nawe. Hutakufa. Baba yangu hafanyi jambo lolote, liwe kubwa au dogo, bila ya kunieleza. Hata jambo hili hawezi kunificha. Sivyo ilivyo hata kidogo.”
3Daudi akaapa pia,20:3 akamjibu: Makala ya Kiebrania: Akaweka nadhiri tena. “Hakika baba yako anajua vizuri unavyonipenda; na anafikiri kukuficha juu ya jambo hili ili usihuzunike atakapolitenda. Lakini, kwa vyovyote vile, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, nawe ulivyo hai, kwamba kati yangu na mauti ipo hatua moja tu!” 4Yonathani akamwambia, “Lolote utakalosema nitakutendea.”
5Daudi akamwambia, “Kesho ni sherehe za mwezi mwandamo, nami natazamiwa kuwapo mezani kula pamoja na mfalme. Lakini niache, nikajifiche huko shambani hadi siku ya tatu jioni. 6Baba yako akinikosa mezani kwa chakula, akauliza habari zangu, basi mwambie, ‘Daudi amenisihi nimpe ruhusa ili aende mjini kwake Bethlehemu, kuhudhuria tambiko ya kila mwaka pamoja na jamaa yake’. 7Ikiwa ataona hilo ni sawa, basi, ujue kuwa mambo yangu, mimi mtumishi wako, yako sawa. La sivyo, kusudi lake juu yangu ni baya. 8Hivyo nifanyie kwa hisani yako kwani umefanya agano takatifu20:8 agano takatifu: Makala ya Kiebrania: Agano la Mwenyezi-Mungu. nami, mimi mtumishi wako, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Lakini, kama nimefanya kosa basi, na uniue wewe mwenyewe; kwa nini unipeleke kwa baba yako ili aniue?”
9Yonathani akamjibu, “Wazo hilo na liwe mbali nawe. Hakika, kama ningejua kuwa baba yangu amekusudia mabaya juu yako nisingekuficha.” 10Daudi akauliza, “Nitajuaje ikiwa baba yako atakujibu kwa ukali?”
11Yonathani akamjibu, “Njoo twende shambani!” Basi, wakaenda. 12Yonathani akamwambia Daudi, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, na awe shahidi yetu. Kesho au kesho kutwa, wakati kama huu nitamwuliza baba yangu. Ikiwa msimamo wake juu yako ni mzuri nitakueleza. 13Mwenyezi-Mungu na aniue ikiwa Shauli anakusudia kukudhuru, nami nisikutahadharishe ili uende mahali mbali ambapo utakuwa salama. Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu. 14Ikiwa nitaendelea kuwa hai basi, nioneshe ule upendo thabiti wa Mwenyezi-Mungu, ili nisife, 15tena usiache kuitendea jamaa yangu kwa uaminifu milele. Na Mwenyezi-Mungu atakapowakatilia mbali adui zako kutoka duniani, 16naomba na jina langu lisikatiliwe mbali kutoka jamaa yako. Mwenyezi-Mungu awalipize kisasi adui zako.”
17Kwa mara nyingine tena, Yonathani alimwambia Daudi aape kulingana na upendo wake kwake yeye Yonathani, kwani alimpenda Daudi kama alivyoipenda roho yake. 18Kisha akamwambia Daudi, “Kwa kuwa kesho ni sherehe za mwezi mwandamo, watu wataona wazi kwamba hupo, kwani kiti chako kitakuwa wazi. 19Tena, kesho kutwa, watu watakukosa kabisa. Siku hiyo nenda mahali ambapo ulijificha wakati jambo hili lilipokuwa bado motomoto, ukajifiche nyuma ya rundo la mawe.20:19 rundo la mawe: Makala ya Kiebrania: Jiwe la Ezeli. 20Mimi nitapiga mishale mitatu kandokando kana kwamba ninalenga shabaha fulani. 21Nitamtuma mtumishi wangu aende kuitafuta mishale hiyo. Kama nikimwambia, ‘Tazama, mishale hiyo iko upande huo wako, ichukue,’ hiyo itakuwa na maana kwamba uko salama, nawe utajitokeza kutoka mahali ulipojificha, maana naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba utakuwa salama bila hatari yoyote. 22Lakini nikimwambia, ‘Tazama, mishale iko mbele yako,’ hapo, ondoka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu atakuwa anataka uende mbali. 23Kulingana na ahadi tulizowekeana, Mwenyezi-Mungu atakuwa shahidi kati yetu milele.”
24Basi, Daudi akajificha shambani. Wakati wa sherehe za mwezi mwandamo, mfalme Shauli akaketi mezani kula. 25Kama ilivyokuwa kawaida yake, mfalme aliketi kwenye kiti chake kilichokuwa karibu ukutani. Yonathani akaketi mkabala na mfalme na Abneri akaketi20:25 akaketi: Makala ya Kiebrania: Akasimama karibu na mfalme. Lakini mahali pa Daudi pakawa wazi. 26Siku hiyo, Shauli hakusema lolote, kwani alifikiri kuwa labda Daudi amepatwa na tatizo au yeye si safi kuhudhuria sherehe hiyo. 27Siku ya pili, baada ya sherehe za mwezi mwandamo, bado mahali pa Daudi palikuwa wazi. Shauli akamwuliza mwanawe Yonathani, “Kwa nini Daudi mwana wa Yese, hakuja kwenye chakula, jana na leo?” 28Yonathani akamjibu, “Alinisihi sana nimruhusu aende Bethlehemu. 29Aliniambia, ‘Niruhusu niende kwa jamaa yangu, kwa kuwa wanafanya karamu ya tambiko huko mjini, na ndugu yangu amenitaka niwepo. Hivyo kama ni sawa kwako niruhusu niende kwa ndugu zangu’. Ndio maana hayuko hapa kushiriki chakula cha mfalme.”
30Hapo Shauli akawaka hasira dhidi ya Yonathani, akamwambia, “Mwana wa mwanamke mpotovu na mwasi wewe! Ninajua kuwa umejichagulia mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe, na kumwaibisha mama yako! 31Je, hujui kwamba Daudi awapo hai, wewe hutaweza kupata fursa ya kuwa mfalme wa nchi hii? Sasa nenda ukamlete hapa kwangu, kwa kuwa lazima auawe.” 32Yonathani akamjibu, “Kwa nini auawe? Amefanya nini?” 33Lakini Shauli mara akamtupia Yonathani mkuki ili amuue. Naye Yonathani akatambua kuwa baba yake alikuwa amepania kumwua Daudi. 34Hapo Yonathani, huku akiwa amekasirika sana, aliondoka mezani kwa haraka, wala hakula chakula chochote siku hiyo ya pili ya sherehe za mwezi mwandamo. Yonathani alihuzunika sana juu ya Daudi kwa sababu baba yake alikuwa amemwaibisha.
35Kesho yake asubuhi, Yonathani alikwenda kule shambani, kukutana na Daudi kama walivyoagana. Alikwenda huko na kijana mmoja wa kiume. 36Alipofika huko alimwambia yule kijana wake, “Kimbia ukaitafute mishale ambayo nitapiga.” Yule kijana alipokuwa anakimbia, Yonathani akapiga mshale mbele yake. 37Yule kijana alipofika mahali ambapo mshale uliangukia, Yonathani akamwita, “Mshale uko mbele yako. 38Fanya haraka na usisimame tu mahali hapo.” Yule kijana alikusanya mishale na kumwendea bwana wake. 39Lakini yule kijana hakujua chochote juu ya maana ya kitendo hicho. Waliojua ni Yonathani na Daudi tu. 40Yonathani akamkabidhi yule kijana silaha zake na kumwambia “Nenda urudi mjini.”
41Mara yule kijana alipokwisha ondoka, Daudi akainuka na kutoka mahali alipojificha karibu na rundo la mawe.20:41 rundo la mawe: Makala ya Kiebrania: Kusini. Aliinama chini kwa heshima mara tatu mbele ya Yonathani. Wote wawili, Daudi na Yonathani, wakakumbatiana na kulia. Daudi alikuwa na uchungu zaidi kuliko Yonathani.20:41 Daudi … Yonathani: Makala ya Kiebrania si dhahiri. 42Halafu Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani. Tumekwisha apa wote kwa jina la Mwenyezi-Mungu, kuwa Mwenyezi-Mungu awe shahidi kati yetu milele, na kati ya wazawa wangu na wazawa wako milele.” Daudi akainuka na kwenda zake, naye Yonathani akarudi mjini.


1Samweli20;1-42
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: