Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 13 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Ruthu 2...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na tukiwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwa uwezo wetu,wala si kwa nguvu/utashi wetu,si kwa akili zetu
wala si kwamba sisi ni wema sana zaidi ya wengine...
Ni kwa neema/rehema zako Baba ni kwa mapenzi yako Mungu wetu
sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Asifiwe Mwenyezi-Mungu Milele.!Amina..! Amina..!
Asifiwe Mwenyezi-Mungu,Mungu wa Israel,tangu milele na hata milele.!
Mwenyezi-Mungu yu hai..!Asifiwe  mwamba wa usalama wangu,Utukuzwe
Mungu wa wokovu wangu..!
Asifiwe Mwenyezi-Mungu maana hakuikataa sala yangu,
wala kuondoa fadhili zake kwangu..!
Mwenyezi-Mungu asifiwe siku kwa siku..! yeye hutubebea mizigo yetu,
yeye ndiye Mungu wa wokovu wetu..!


Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu; anga ladhihirisha kazi ya mikono yake. Mchana waupasha habari mchana ufuatao, usiku waufahamisha usiku ufuatao. Hamna msemo au maneno yanayotumika; wala hakuna sauti inayosikika; hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote, na maneno yao yafika kingo za ulimwengu. Mungu ameliwekea jua makao yake angani; nalo hutoka kama bwana arusi chumbani mwake, lafurahi kama shujaa aliye tayari kushindana. Lachomoza toka upande mmoja, na kuzunguka hadi upande mwingine; hakuna kiwezacho kuliepa joto lake.

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako ee Mungu wetu..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Jehovah tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona


Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti, huwapa hekima wasio na makuu. Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa, huufurahisha moyo; amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi, humwelimisha mtu. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema, na la kudumu milele; maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa, yote ni ya haki kabisa. Yatamanika kuliko dhahabu; kuliko dhahabu safi kabisa. Ni matamu kuliko asali; kuliko asali safi kabisa. Yanifunza mimi mtumishi wako; kuyafuata kwaniletea tuzo kubwa. Lakini nani aonaye makosa yake mwenyewe? Ee Mungu, niepushe na makosa nisiyoyajua. Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi, usikubali hayo yanitawale. Hapo nitakuwa mkamilifu, wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa. Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu na mkombozi wangu!

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Yahweh tunaomba
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji Jehovah tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah
ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mafalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu..
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu,popote tupitapo na ijulikane
kwamba upo Baba wa Mbinguni,Yahweh ukatawale,ukatamalaki na kutuatamia..Mungu wetu ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako,Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Enyi watu wote duniani mshangilieni Mungu! Imbeni juu ya utukufu wa jina lake, mtoleeni sifa tukufu! Mwambieni Mungu: “Matendo yako ni ya ajabu mno! Nguvu zako ni kubwa mno hata maadui zako wanajikunyata kwa hofu. Dunia yote inakuabudu; watu wote wanakuimbia sifa!” Njoni mkaone mambo aliyotenda Mungu; ametenda mambo ya kutisha kati ya watu: Aligeuza bahari kuwa nchi kavu, watu wakapita humo kwa miguu; hapo nasi tukashangilia kwa sababu yake. Anatawala milele kwa nguvu yake kuu; macho yake huchungulia mataifa yote. Mwasi yeyote asithubutu kumpinga. Msifuni Mungu wetu, enyi mataifa yote; tangazeni sifa zake zipate kusikika. Yeye ametujalia maisha, wala hakutuacha tuanguke. Umetupima, ee Mungu, umetujaribu kama madini motoni. Umetuacha tunaswe wavuni; umetubebesha taabu nzito. Umewaacha watu watukanyage; tumepitia motoni na majini . Lakini sasa umetuleta kwenye usalama. Nitakuja nyumbani kwako na sadaka za kuteketezwa, nitakutimizia nadhiri zangu, nilizotamka na kukuahidi mimi mwenyewe nilipokuwa taabuni. Nitakutolea sadaka za kuteketezwa nononono, tambiko za kuteketezwa za kondoo madume; nitatoa sadaka za ng'ombe na mbuzi. Enyi mnaomcha Mungu, njoni nyote mkasikilize, nami nitawasimulieni aliyonitendea. Mimi nilimlilia msaada kwa sauti, sifa zake nikazitamka. Kama ningalinuia maovu moyoni, Mwenyezi-Mungu hangalinisikiliza. Lakini kweli Mungu amenisikiliza; naam, amesikiliza maneno ya sala yangu. Asifiwe Mungu, maana hakuikataa sala yangu, wala kuondoa fadhili zake kwangu.

Yahweh tunaomba ukawaponye wagonjwa,Mungu wetu ukawape nguvu,uvumilivu wanaowauguza,,Baba wa Mbinguni ukawatendee 
Wajane na Yatima, Mungu wetu ukawavushe salama wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Yahweh ukawafungue na kuwaweka huru wale waliokatika vifungo vya yule mwovu Jehovah haki ikatendeke
kwa walio magerezani pasipo na hatia..Mungu wetu ukawasamehe na kuwasimamisha tena wale wote walikwenda kinyume nawe/walioanguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wote walioelemewa na mizigo Mungu wetu ukawape chakula wenye njaa
Baba wa Mbinguni ukawafariji wafiwa,Mungu wetu ukaonekane katika
shida/tabu za watoto wako,Jehovah ukasikie kulia kwao,Baba ukawafute
machozi ya watoto wako,Mungu wetu ukasikie,ukapokee na kujibu Sala/maombi yetu,Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
wote wanao kuomba kwa bidii/imani Ee Baba tunaomba utusikie..


Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni; jina la Mungu wa Yakobo likulinde. Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake; akutegemeze kutoka mlima Siyoni. Azikumbuke sadaka zako zote; azikubali tambiko zako za kuteketezwa. Akujalie unayotamani moyoni mwako, aifanikishe mipango yako yote. Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako; tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote! Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua, atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni; kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa. Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Hao watajikwaa na kuanguka; lakini sisi tutainuka na kusimama imara. Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu; utujibu wakati tunapokuomba.

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana,Mungu wa upendo
aendelee kuwabariki,Amani iwe nanyi pendo lenu likadumu
Msipungukiwe katika mahitaji yenu Baba wa Mbinguni
akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Ruthu anafanya kazi katika shamba la Boazi

1Naomi alikuwa na ndugu aliyeitwa Boazi, wa ukoo wa Elimeleki mumewe. Huyo alikuwa mtu mashuhuri na tajiri. 2Siku moja, Ruthu Mmoabu alimwambia Naomi, “Niruhusu niende shambani kukusanya masalio ya mavuno. Nina hakika kumpata mtu ambaye ataniruhusu niokote nyuma yake.” Naomi akamwambia, “Haya, nenda binti yangu.”
3Basi Ruthu akaenda shambani, akawafuata wavunaji huku anayaokota masuke waliyoyaacha. Na kumbe akajikuta katika shamba la Boazi, yule wa ukoo wake Elimeleki.
4Baada ya muda, Boazi alifika kutoka Bethlehemu akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi-Mungu awe nanyi.” Nao wakamjibu, “Mwenyezi-Mungu na akubariki.” 5Kisha Boazi akamwuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule msichana ni nani?” 6Huyo kiongozi wa wavunaji akajibu, “Ni msichana Mmoabu aliyekuja pamoja na Naomi kutoka katika nchi ya Moabu. 7Aliniomba nimruhusu awafuate nyuma wavunaji huku akiokota masazo kati ya miganda. Basi alikuja na amefanya kazi tangu asubuhi na ni sasa tu amekwenda kupumzika kibandani.”
8Ndipo Boazi akamwambia Ruthu, “Hebu sikiliza binti yangu. Usiende kuokota masuke mahali pengine ila katika shamba hili tu. Fuatana na wanawake hawa; 9angalia mahali wavunapo ujiunge nao. Nimewaonya vijana hawa wasikusumbue. Na ukiona kiu, nenda kwenye mitungi na unywe maji waliyoyateka hao vijana.”
10Hapo Ruthu akamwinamia Boazi mpaka chini kwa unyenyekevu, akamwambia, “Nimepataje kibali chako? Mbona unanihurumia na hali mimi ni mgeni tu?”
11Lakini Boazi akamjibu, “Nimeyasikia yote uliyomfanyia mama mkwe wako tangu mumeo afariki. Ninajua jinsi ulivyowaacha wazazi wako, ukaiacha nchi yako, na jinsi ulivyokuja kuishi kati ya watu ambao hukuwajua hapo awali. 12Mwenyezi-Mungu akujaze kwa yote uliyoyafanya. Mwenyezi-Mungu wa Israeli uliyemkimbilia akulinde chini ya mabawa yake, akupe thawabu kamilifu.”
13Ruthu akamjibu, “Bwana, wewe umenifanyia wema mkubwa sana. Ingawa mimi si kama mmoja wa watumishi wako, nimeridhika kwa kuwa umenifariji sana na kuongea nami kwa ukarimu.”
14Wakati wa chakula, Boazi alimkaribisha Ruthu akamwambia, “Karibu hapa, njoo ule mkate pia na uuchovye ndani ya divai.” Kwa hiyo Ruthu akaketi pamoja na wavunaji, na Boazi akampa nafaka iliyokaangwa, akala akashiba hata akabakiza. 15Na ikawa Ruthu alipoendelea kuokota mavuno, Boazi aliwaambia wafanyakazi wake, “Mwacheni akusanye hata mahali miganda ilipo wala msimkemee. 16Zaidi ya hapo, vuteni masuke kutoka katika matita na mumwachie aokote bila kumkaripia.”
17Basi Ruthu aliendelea kuokota masuke mpaka jioni; na baada ya kupura hiyo shayiri alipata debe moja na zaidi. 18Kisha akachukua mavuno hayo hadi mjini na kumwonesha mama mkwe wake kiasi alichookota. Pia alikitoa kile chakula alichobakiza baada ya kushiba, akampa. 19Basi mkwewe akamwuliza, “Uliokota wapi haya yote? Je, ulikuwa katika shamba la nani? Heri huyo aliyekufadhili.” Hapo Ruthu akamwambia Naomi kwamba alikuwa amefanya kazi katika shamba la mtu aliyeitwa Boazi. 20Basi, Naomi akamwambia mkwewe, “Mwenyezi-Mungu ambariki Boazi! Mungu hutimiza daima ahadi zake kwa walio hai na waliokufa.” Kisha akaendelea kusema, “Huyo mtu ni ndugu yetu wa karibu na ni mmoja wa wale wenye wajibu wa kututunza.”
21Kisha Ruthu Mmoabu akasema, “Isitoshe, aliniambia nijiunge pamoja na wafanyakazi wake mpaka wamalize mavuno yote.”
22Basi, Naomi akamwambia Ruthu, “Naam binti yangu. Ni vyema kufanya kazi pamoja na wanawake wengine katika shamba la Boazi, kwa maana labda ungesumbuliwa kama ungekwenda katika shamba la mtu mwingine.” 23Kwa hiyo, Ruthu akafanya kazi nao, akaokota masuke mpaka mavuno ya ngano na shayiri yalipomalizika. Wakati huo wote alikuwa anakaa na mama mkwe wake.

Ruthu2;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


No comments: