Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 22 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli5...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake
kwetu...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi
Muumba wa vyote vilivyopo vinavyoonekana na visivyo onekana
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Baba wa Upendo,Baba wa Baraka
Mungu wenye nguvu,Mungu wa walio hai,Muweza wa yote,Alfa na Omega
Unastahili sifa Baba wa Mbinguni,Unastahili kuabudiwa Jehovah,Unastahili kuhimidiwa Yahweh..Unatosha Baba wa Mbinguni...!!


Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu; unifundishe nifuate unayotaka. Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha, kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu; ninakutegemea wewe kila siku. Uikumbuke huruma yako ee Mwenyezi-Mungu; uzikumbuke na fadhili zako kuu, ambazo zimekuwako tangu kale. Usikumbuke dhambi na makosa ya ujana wangu; unikumbuke kadiri ya fadhili zako, kwa ajili ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia. Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu; naam, huwafundisha hao njia yake. Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu, kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake.
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Mungu Baba..!!


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote walio tukosea..
Mfalme wa amani tunaomba  utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni tunaomba utuokoe na yule mwovu na Kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kila usemapo, maneno yako ni ya kweli; na katika hukumu, wewe hushinda.” Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu? Labda utasema: “Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!” Ni sawa na kusema: Tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili!

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Yahweh tunaomba ukatupe
ubunifu na maarifa Katika ufanyaji/utendaji Yahweh nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Jehovah
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..


Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Baba wa Mbinguni ukatubariki na mkono wako wenye nguvu ukatuguse...
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki..
Mungu Baba tunaomba ukatupe macho ya rohoni,masikio ya kusikia sauti yako na kuitii,tukawe salama moyoni na ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako,Yahweh tuka nene yaliyo yako..
Mungu wetu ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu! Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu. Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka. Vinywa vyao vimejaa laana chungu. Miguu yao iko mbioni kumwaga damu, popote waendapo husababisha maafa na mateso; njia ya amani hawaijui. Hawajali kabisa kumcha Mungu.” Tunajua kwamba sheria huwahusu walio chini ya sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kushika sheria; kazi ya sheria ni kumwonesha tu mtu kwamba ametenda dhambi.

Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu
Mungu wetu tunaomba ukawavushe salama wale wanaopitia magumu/majaribu
mbalimbali...
Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa Yahweh ukawape uvumilivu na nguvu wale wanaowauguza..
Jehovah tunaomba ukawape chakula wenye njaa Yahweh ukawe tumaini kwa walio kata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka Baba wa Mbinguni ukawasamehe wale wote walikwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawe faraja kwa waliofiwa
Yahweh ukawape neema ya kujiombea kufuata njia zako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana Wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo ikatawale katika maisha yenu..
Nawapenda.




Sanduku la agano kati ya Wafilisti

1Baada ya Wafilisti kuliteka sanduku la Mungu, walilibeba kutoka mji wa Ebenezeri hadi mji wao wa Ashdodi. 2Kisha, wakalipeleka sanduku la Mwenyezi-Mungu kwenye hekalu la mungu wao Dagoni na kuliweka karibu naye. 3Kesho yake asubuhi, watu wa mji wa Ashdodi walipoamka waliona sanamu ya Dagoni imeanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Mungu. Wakaisimamisha tena sanamu ya Dagoni na kuiweka tena mahali pake. 4Lakini, kesho yake asubuhi walipoamka, waliona kuwa sanamu ya Dagoni imeanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu, kichwa, miguu na mikono ya sanamu hiyo, vyote vilikuwa vimekatika, vikawa vimelala chini kwenye kizingiti cha mlango. Kiwiliwili cha sanamu ya Dagoni ndicho tu kilikuwa kimebakia. 5Ndio maana makuhani wa Dagoni na wote wanaoingia kumwabudu Dagoni huko Ashdodi, wanapoingia kwenye hekalu la Dagoni hawakanyagi kizingiti cha hekalu la Dagoni hadi leo.
6Mwenyezi-Mungu aliwaadhibu vikali na kuwatisha watu wa Ashdodi. Aliwaadhibu, hata na majirani zao, kwa kuwaletea ugonjwa wa majipu. 7Wakazi wa Ashdodi walipoyaona mambo yaliyowapata, wakasema, “Mungu wa Israeli anatuadhibu vikali sisi pamoja na mungu wetu Dagoni. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu haliwezi kukaa kwetu.” 8Walituma wajumbe na kuwakusanya wakuu wote wa Wafilisti na kuwauliza, “Je, tutafanya nini na sanduku hili la Mungu wa Israeli?” Wakuu wao wakajibu, “Sanduku hilo la Mungu wa Israeli lipelekeni Gathi.” Basi, wakalipeleka kwenye mji wa Gathi. 9Lakini baada ya kulipeleka huko Gathi, Mwenyezi-Mungu akauadhibu mji huo, akisababisha hofu kuu mjini, na akawapiga wanaume wa mji huo, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. 10Hivyo, wakalipeleka sanduku hilo la Mungu kwenye mji wa Ekroni. Lakini sanduku hilo la Mungu lilipofika huko, watu wa mji huo walipiga kelele, “Wametuletea sanduku la Mungu wa Israeli ili kutuua sisi na watu wetu.” 11Kisha wakatuma ujumbe na kukusanya wakuu wa Wafilisti na kuwaambia, “Lirudisheni sanduku la Mungu wa Israeli mahali pake, ili lisituue sisi pamoja na watu wetu.” Walifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na hofu kubwa katika mji mzima kwa sababu Mungu alikuwa anawaadhibu vikali. 12Nao wale ambao hawakufa walipatwa na majipu hata kilio cha mji kilifika mbinguni.


1Samweli5;1-12

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: