Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 17 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 5...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Nchi na Mbingu,
Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana,Muweza wa yote
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu mwenye nguvu,Mfalme wa amani,Alfa na Omega,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Hakuna kama wewe,Unatosha Baba wa Mbinguni...!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..

Sifa na utukufu tunakurudishia wewe..!!



Enyi watoto, watiini wazazi wenu Kikristo maana hili ni jambo jema. “Waheshimu Baba na mama yako,” hii ndiyo amri ya kwanza ambayo imeongezewa ahadi, yaani, “Upate fanaka na kuishi miaka mingi duniani.” Nanyi akina baba, msiwachukize watoto wenu ila waleeni katika nidhamu na mafundisho ya Kikristo.
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Jehovah..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu
Baba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
utufunike kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Enyi watumwa, watiini mabwana zenu hapa duniani kwa hofu na kutetemeka; fanyeni hivyo kwa unyofu wa moyo kana kwamba mnamtumikia Kristo. Fanyeni hivyo si tu wakati wanapowatazama ili mjipendekeze kwao, bali tumikieni kwa moyo kama atakavyo Mungu kwa sababu nyinyi ni watumishi wa Kristo. Muwe radhi kutumikia kwa ajili ya Bwana na si kwa ajili ya watu. Kumbukeni kwamba kila mtu mwenye kutenda mema, awe mtumwa au mtu huru, atapokea tuzo lake kutoka kwa Bwana. Nanyi mnaotumikiwa, watendeeni vivyo hivyo watumwa wenu, na acheni kutumia vitisho. Kumbukeni kwamba nyinyi pia kama vile wao, mnaye Bwana yuleyule mbinguni, naye hatendi kwa ubaguzi.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Yahweh tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji,Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe..


Mungu wetu tunaomba ukabariki Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Mfalme wa amani
tunaomba amani yako itawale katika maisha yetu,Mungu wetu tunaomba
ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki,Yahweh ukatamalaki
na kutuatamia,Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Jehovah ukatufanye chombo chema nasi tukatumike
 kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tupate kutambua/kujitambua
na tukawe na kiasi..



Hatimaye, nawatakeni muwe imara katika kuungana na Bwana na kwa msaada wa nguvu yake kuu. Vaeni silaha anazowapeni Mungu mpate kuzipinga mbinu mbaya za Ibilisi. Maana vita vyetu si vita kati yetu na binadamu, bali ni vita dhidi ya jeshi ovu la ulimwengu wa roho; tunapigana na watawala, wakuu na wenye nguvu, wanaomiliki ulimwengu huu wa giza. Kwa sababu hiyo, vaeni silaha za Mungu ili siku ile itakapofika mweze kuyapinga mashambulio ya adui; na mkisha pigana mpaka mwisho, mtakuwa bado imara. Basi, kaeni tayari. Ukweli na uwe kama mkanda kiunoni mwenu, uadilifu uwe kama vazi la kujikinga kifuani, na hamu ya kutangaza Habari Njema ya amani iwe kama viatu miguuni mwenu. Zaidi ya hayo yote, imani iwe daima kama ngao mikononi mwenu, iwawezeshe kuizima mishale ya moto ya yule Mwovu. Upokeeni wokovu kama kofia yenu ya chuma, na neno la Mungu kama upanga mnaopewa na Roho Mtakatifu. Salini daima, mkiomba msaada wa Mungu. Salini kila wakati kwa nguvu ya Roho. Kesheni bila kuchoka mkisali kwa ajili ya watu wote wa Mungu. Niombeeni nami pia ili niongeapo Mungu anijalie cha kusema, niweze kuwajulisha watu fumbo la Injili kwa uthabiti. Mimi ni balozi kwa ajili ya Injili hiyo ingawa sasa niko kifungoni. Ombeni, basi, ili niweze kuwa hodari katika kuitangaza kama inipasavyo.
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wote wanaopitia magumu/majaribu,wagonjwa,wenye shida/tabu,
waliokatika vifungo vya yule mwovu  Baba ukawape uponyaji wa mwili na
roho,ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako,wenye njaa
Mungu wetu ukawatendee na kubariki mashamba yao,wafiwa ukawe
mafariji wao,Mungu wetu ukafute machozi ya watoto wako na ukasikie
kuomba kwao,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!



Tukiko, ndugu yetu mpenzi na mtumishi mwaminifu katika kuungana na Bwana, atawapeni habari zangu zote mpate kujua ninachofanya. Namtuma kwenu awapeni habari zetu mpate kuwa na moyo. Ninawatakieni nyinyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami
Mungu wa rehema/neema aendelee kuwabariki na kuwatendea
sawasawa na mapenzi yake, Amani ya Kristo Yesu iwe nanyi Daima..
Nawapenda.

Wimbo wa Debora

1Siku hiyo, Debora na Baraki, mwana wa Abinoamu, wakaimba wimbo huu:
2“Viongozi walijitokeza kuongoza Israeli,
watu walijitolea kwa hiari yao.
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu!
3“Sikilizeni, enyi wafalme!
Tegeni sikio, enyi wakuu!
Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
4“Ee Mwenyezi-Mungu, ulipotoka huko Seiri,
ulipoteremka mlimani Edomu,
nchi ilitetemeka,
mbingu zilidondosha maji,
naam, mawingu yakaiangusha mvua.
5Milima ilitikisika mbele yako Mwenyezi-Mungu,
naam, mlima Sinai mbele yako Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
6“Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi,
katika wakati wa Yaeli,
misafara ilikoma kupita nchini,
wasafiri walipitia vichochoroni.
7Wakulima walikoma kuwako,
walikoma kuwako katika Israeli,
mpaka nilipotokea mimi Debora,
mimi niliye kama mama wa Israeli.
8Walijichagulia miungu mipya,
kukawa na vita katika nchi.
Lakini hakukupatikana mwenye upanga au ngao
kati ya watu 40,000 wa Israeli.
9Nawapa heshima makamanda wa Israeli
waliojitoa kwa hiari yao kati ya watu.
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu!
10“Tangazeni, enyi wapandapunda weupe,
enyi mnaokalia mazulia ya fahari,
nyinyi mnaotembea njiani, tangazeni jambo hilo.
11Imbeni kupita wanamuziki kwenye visima vya maji,
tangazeni ushindi wa Mwenyezi-Mungu,
ushindi kwa wakulima wake katika Israeli.
Ndipo watu wa Mwenyezi-Mungu waliposhuka malangoni.
12“Amka, amka, Debora!
Amka! Amka uimbe wimbo!
Amka, Baraki mwana wa Abinoamu,
uwachukue mateka wako.
13Mashujaa waliobaki waliteremka,
watu wa Mwenyezi-Mungu walikwenda kumpigania
dhidi ya wenye nguvu.
14Kutoka Efraimu waliteremka bondeni,5:14 bondeni: Makala ya Kiebrania; katika Maaleki.
wakafuata ndugu zao watu wa Benyamini;
kutoka Makiri walishuka makamanda,
kutoka Zebuluni maofisa wakuu.
15Wakuu wa Isakari wakafuatana na Debora,
watu wa Isakari waaminifu kwa Baraki;
wakamfuata mbio mpaka bondeni.
Lakini miongoni mwa koo za Reubeni
kulikuwamo kusitasita kwingi.
16Kwa nini walibaki mazizini?
Ili kusikiliza milio ya kondoo?
Miongoni mwa koo za Reubeni
kulikuwamo kusitasita kwingi.
17Kabila la Gileadi lilibaki ngambo ya Yordani.
Kabila la Dani, kwa nini mlibaki merikebuni?
Kabila la Asheri lilitulia huko pwani ya bahari,
lilikaa bandarini mwake.
18Watu wa Zebuluni ni watu
waliohatarisha maisha yao katika kifo.
Hata wa Naftali walikikabili kifo
kwenye miinuko ya mashamba.
19“Huko Taanaki, kando ya chemchemi za Megido,
wafalme walikuja, wakapigana;
wafalme wa Kanaani walipigana,
lakini hawakupata nyara za fedha.
20Nyota kutoka mbinguni zilishiriki vita,
zilifuata njia zao, zilipigana na Sisera.
21Mafuriko ya mto Kishoni yaliwachukua mbali,
naam, mafuriko makali ya mto Kishoni.
Songa mbele kwa nguvu, ee nafsi yangu!
22“Farasi walipita wakipiga shoti;,
walikwenda shoti na kishindo cha kwato zao.
23Malaika wa Mwenyezi-Mungu asema hivi:
‘Uapizeni mji wa Merosi,
waapizeni vikali wakazi wake;
maana hawakuja kumsaidia Mwenyezi-Mungu
hawakumsaidia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wenye nguvu’.
24“Abarikiwe kuliko wanawake wote
Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni.
Naam, amebarikiwa kuliko wanawake wote
wanaokaa mahemani.
25Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa;
alimletea siagi katika bakuli ya heshima.
26Kwa mkono mmoja alishika kigingi cha hema,
na kwa mkono wake wa kulia nyundo ya fundi;
alimponda Sisera kichwa,
alivunja na kupasuapasua paji lake.
27Sisera aliinama, akaanguka;
alilala kimya miguuni pake.
Hapo alipoinama ndipo alipoanguka, amekufa!
28“Mama yake Sisera alitazama dirishani
alichungulia katika viunzi vyake, akalalamika:
‘Kwa nini gari lake limechelewa?
Mbona vishindo vya magari yake vimechelewa kusikika?’
29Jibu akalipata kwa wanawake wenye hekima:
Akajituliza tena na tena kwa jibu hilo:
30‘Bila shaka wanatafuta na kugawana nyara;
msichana mmoja au wawili kwa kila askari,
vazi la sufu ya rangi kwa ajili ya Sisera.
Vazi la sufu iliyotariziwa,
na mikufu miwili ya nakshi kwa ajili ya shingo yangu!’
31“Ee Mwenyezi-Mungu, waangamie adui zako wote!
Lakini rafiki zako na wawe kama jua,
wakati linapochomoza kwa mwanga mkubwa!”
Nayo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini.


Waamuzi 5;1-31

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: