Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 16 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 4...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba wa Vyote vilivyopo..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa wote walio hai..
Baba wa Yatima,Mume wa wajane,Baba wa Upendo,Mungu wa huruma Muweza wa yote,Mponyaji wetu,Jehovah..!Yahweh..!Adonai..!
El Shadai..!Elohim..!El Elyon..!El Olam..!El Qanna..!Emanueli..!Mungu pamoja nasi..!

Utukuzwe ee Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,
Unatosha Mungu wetu,Hakuna kama wewe..!




Laiti mngenivumilia kidogo, hata kama mimi ni mjinga kiasi! Naam, nivumilieni kidogo. Ninawaoneeni wivu lakini ni wivu wa Mungu; maana nyinyi ni kama bikira safi niliyemposa kwa mwanamume mmoja tu ambaye ndiye Kristo. Lakini naogopa kwamba, kama vile yule nyoka kwa hila zake za uongo alimdanganya Hawa, fikira zenu zaweza kupotoshwa, mkauacha uaminifu wenu wa kweli kwa Kristo. Maana mtu yeyote ajaye na kumhubiri Yesu aliye tofauti na yule tuliyemhubiri, nyinyi mwampokea kwa mikono miwili; au mnakubali roho au Injili tofauti kabisa na ile mliyopokea kutoka kwetu! Sidhani kwamba mimi ni mdogo kuliko hao “mitume wakuu.” Labda sina ufasaha wa lugha, lakini elimu ninayo; jambo hili tumelionesha wazi kwenu, kila mahali na kila wakati.

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba tumetenda mema sana,si kwa nguvu/utashi wetu,si kwa akili zetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii Mungu wetu,Ni kwa Neema/rehema zako
Ni kwa mapenzi yako Mungu wetu kuwa hivi tulivyo..

Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na Kesho ni siku
Nyingine Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Mungu wetu
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..





Mimi niliihubiri kwenu Habari Njema ya Mungu bila kudai mshahara; nilijinyenyekesha ili nipate kuwakweza nyinyi. Je, nilifanya vibaya? Nilipofanya kazi kati yenu, mahitaji yangu yaligharimiwa na makanisa mengine. Kwa namna moja au nyingine niliwapokonya wao mali yao nipate kuwatumikia nyinyi. Nilipokuwa nanyi sikumsumbua mtu yeyote nilipohitaji fedha; ndugu waliotoka Makedonia waliniletea kila kitu nilichohitaji. Nilikuwa mwangalifu sana nisiwe mzigo kwa namna yoyote ile, na nitaendelea kufanya hivyo. Naahidi kwa ule ukweli wa Kristo ulio ndani yangu, kwamba hakuna kitakachoweza kunizuia kujivunia jambo hilo popote katika Akaya. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu eti siwapendi nyinyi? Mungu anajua kwamba nawapenda! Nitaendelea kufanya kama ninavyofanya sasa, ili nisiwape nafasi wale wanaotafuta nafasi, nafasi ya kujivuna kwamba eti wanafanya kazi kama sisi. Maana, hao ni mitume wa uongo, wafanyakazi wadanganyifu wanaojisingizia kuwa mitume wa Kristo. Wala si ajabu, maana hata Shetani mwenyewe hujisingizia kuwa malaika wa mwanga! Kwa hiyo si jambo la kushangaza ikiwa na hao watumishi wake wanajisingizia kuwa watumishi wa haki. Mwisho wao watapata kile wanachostahili kufuatana na matendo yao.


Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Mungu wetu ukatupe
Ubunifu,Maarifa katika ufanyaji/utendaji nasi tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..



Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na
kwa vyote tunavyovimiliki,Baba wa Mbinguni ukatawale,ukatamalaki na
kutuatamia,Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu,Baba ukatuokoe
katika majivuno,masengenyo,ugomvi,makwazo na vyote vinavyokwenda
kinyume nawe,Mungu wetu ukatupe neema ya kusaidiana,kupendana na tukafurahi pamoja na tukalie pamoja inapobidi..
Baba tukafuate njia zako,Tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu,Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Ee.. Baba ..!tunaomba upokee maombi/sala zetu..





Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo. Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu. Maadamu wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna. Nyinyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu! Mnamvumilia hata mtu anayewafanya nyinyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni! Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu – nasema kama mtu mpumbavu – mimi nathubutu pia. Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi. Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi – nanena hayo kiwazimu – ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi. Mara tano nilichapwa vile viboko arubaini kasoro kimoja vya Wayahudi. Nilipigwa fimbo mara tatu, nilipigwa mawe mara moja; mara tatu nilivunjikiwa meli baharini, na humo nikakesha usiku kucha na kushinda mchana kutwa. Kila mara safarini nimekabiliwa na hatari za mafuriko ya mito, na hatari za wanyama; hatari kutoka kwa wananchi wenzangu na kutoka kwa watu wa mataifa mengine; hatari za mjini, hatari za porini, hatari za baharini, hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. Nimefanya kazi na kutaabika, nimekesha bila usingizi mara nyingi; nimekuwa na njaa na kiu; mara nyingi nimefunga na kukaa katika baridi bila nguo. Na, licha ya mengine mengi, kila siku nakabiliwa na shughuli za makanisa yote. Kama mtu yeyote ni dhaifu, nami pia ni dhaifu; mtu yeyote akikwazwa, nami pia huwa na wasiwasi. Ikinilazimu kujivuna, basi, nitajivunia udhaifu wangu. Mungu na Baba wa Bwana Yesu – jina lake litukuzwe milele – yeye anajua kwamba sisemi uongo. Nilipokuwa Damasko, mkuu wa mkoa, aliyekuwa chini ya mfalme Areta, alikuwa akiulinda mji wa Damasko ili anikamate. Lakini, ndani ya kapu kubwa, niliteremshwa nje kupitia katika nafasi ukutani, nikachopoka mikononi mwake.



Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wagonjwa
wakapate uponyaji wako,wenye njaa ukawapatie chakula na ukabariki
mashamba yao wapate mavuno ya kutosha na kuweka akiba,
wanaopitia magumu/majaribu Mungu wetu ukawavushe,walio magerezani pasipo na hatia Baba ukawatete na kuwatendea,waliokatika vifungo vya
yule mwovu Mungu wetu ukawafungue na ukawaweke huru,Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na Nuru yako
ikaangaze katika maisha yao..
Kwa imani tunayaweka haya yote mikononi mwako,tukiamini
wewe ni Mungu wetu Jana leo kesho na hata Milele..
Sifa na Utukufu ni wako Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!


Asanteni sana wapendwa kwakuwa nami,Baba wa Mbinguni aendelee
kuwa nanyi,Amani,Upendo na Baraka zisipungue katika maisha yenu..
Nawapenda.

Debora na Baraki

1Baada ya kifo cha Ehudi, Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. 2Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, ambaye aliishi huko Hazori. Kamanda wa jeshi lake alikuwa Sisera, mwenyeji wa Harosheth-hagoimu. 3Mfalme Yabini alikuwa na magari ya vita 900 ya chuma. Aliwakandamiza sana Waisraeli kwa miaka ishirini; nao wakamlilia Mwenyezi-Mungu awasaidie.
4Wakati huo, kulikuwa na nabii mwanamke aliyeitwa Debora, mke wa Lapidothi, aliyekuwa mwamuzi wa Waisraeli wakati huo. 5Debora alikuwa na mazoea ya kuketi chini ya mtende uliokuwa kati ya mji wa Rama na mji wa Betheli katika nchi ya milima ya Efraimu. Watu wa Israeli walimjia ili awaamulie mashauri yao. 6Siku moja alimwita Baraki mwana wa Abinoamu wa Kedeshi katika nchi ya Naftali. Alipokuja alimwambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anakuamuru hivi: ‘Nenda ukusanye watu wako mlimani Tabori, uchague watu 10,000 kutoka makabila ya Naftali na Zebuluni. 7Mimi nitamchochea Sisera, jemadari wa jeshi la Yabini, aje na majeshi na magari yake kupigana nawe kwenye mto Kishoni, na kumtia mikononi mwako.’” 8Baraki akamwambia Debora, “Kama utakwenda pamoja nami, nitakwenda. Lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.” 9Debora akamjibu, “Sawa. Nitakwenda pamoja nawe; lakini hutapata heshima yoyote ya ushindi, maana Mwenyezi-Mungu, atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.” Basi, Debora akafuatana na Baraki kwenda Kedeshi. 10Baraki akayaita makabila ya Naftali na Zebuluni huko Kedeshi; watu 10,000 wakamfuata. Debora akaenda pamoja naye.
11Wakati huo, Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake ambao ni wazawa wa Hobabu, baba mkwe wa Mose. Alikuwa amepiga hema lake mbali huko kwenye mwaloni wa Zaananimu, karibu na Kedeshi.
12Sisera alipopata habari kwamba Baraki mwana wa Abinoamu amekwenda mlimani Tabori, 13alikusanya jeshi lake lote na magari yake mia tisa ya chuma, akaondoka Harosheth-hagoimu, akaenda kwenye mto Kishoni. 14Debora akamwambia Baraki, “Inuka! Leo ni siku ambayo Mwenyezi-Mungu atamtia Sisera mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu anakwenda mbele yako.” Basi, Baraki akashuka kutoka mlimani Tabori akiwaongoza watu wake 10,000. 15Baraki akafanya mashambulizi, naye Mwenyezi-Mungu akamtimua Sisera na jeshi lake lote mbele ya Baraki kwa upanga. Sisera akatoka katika gari lake, akakimbia kwa miguu. 16Baraki akalifuatia jeshi hilo na magari mpaka Harosheth-hagoimu na kuwaua wanajeshi wote wa Sisera kwa mapanga; hakubaki hata mtu mmoja.
17Lakini Sisera alikimbia kwa miguu mpaka hemani kwa Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni. Alifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na amani kati ya mfalme Yabini wa Hazori na jamaa ya Heberi. 18Yaeli akatoka kumlaki Sisera, akamwambia, “Bwana wangu, karibu kwangu, wala usiogope.” Akaingia hemani mwake, akamfunika kwa blanketi. 19Sisera akamwambia Yaeli, “Tafadhali, nipe maji kidogo ninywe, maana nina kiu.” Akampa maziwa badala ya maji, kisha akamfunika tena. 20Sisera akamwambia, “Simama mlangoni mwa hema. Mtu yeyote akija kukuuliza kama kuna mtu yeyote hapa, mwambie hakuna.” 21Lakini Yaeli, mke wa Heberi, akachukua kigingi cha hema na nyundo, akamwendea polepole akakipigilia kile kigingi cha hema katika paji la uso wake kikapenya mpaka udongoni, kwa maana alikuwa amelala fofofo kwa uchovu. Basi, Sisera akafa papo hapo. 22Naye Baraki alipokuwa anamfuatilia Sisera, Yaeli akatoka nje kumlaki akamwambia, “Njoo nami nitakuonesha yule unayemtafuta.” Baraki akaingia ndani ya hema la Yaeli na kumkuta Sisera chini, amekufa, na kigingi cha hema pajini mwake.
23Hivyo, siku hiyo Mungu akawapa Waisraeli ushindi juu ya mfalme Yabini wa Kanaani. 24Waisraeli wakaendelea kumwandama Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka walipomwangamiza.


Waamuzi 4;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: