Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Swahili na Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 14 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 2...Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu.!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mungu wa Wajane,Baba wa Yatima,Muweza wa yote,Mponyaji wetu,
Utukuzwe Yahweh,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uabudiwe Jehovah,
Uhimidiwe Mungu wetu,Unatosha Baba wa Mbinguni,Hakuna kama wewe
wewe ni alfa na Omega,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..!

Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima. Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli. Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu. Maana kwa kuja kwake Kristo, sheria imefikia kikomo chake, ili wote wanaoamini wafanywe waadilifu.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Yahweh..
Tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya kwakuwaza,
kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Mungu wetu..
Tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na yule
mwovu na kazi zake zote..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
 Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..Kuhusu kuwa mwadilifu kwa kuitii sheria, Mose aliandika hivi: “Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya sheria ataishi.” Lakini kuhusu kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: “Usiseme moyoni mwako: ‘Nani atapanda mpaka mbinguni?’ (yaani, kumleta Kristo chini); wala usiseme: ‘Nani atashuka mpaka kuzimu?’ (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu).” Maandiko Matakatifu yasema hivi: “Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako” nao ndio ile imani tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu; na hukiri kwa kinywa akaokolewa. Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.”

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Jehovah
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji Yahweh
nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji,Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa
zetu,watoto/wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu ukatubariki,ukatamalaki na kutuatamia,Jehovah ukatupe
neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Baba ukatuepushe na roho za kiburi,kujiona kujisifu,Mungu wetu na vyote vinavyokwenda kinyume nawe..
Jehovah ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupenda wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!” Lakini wote hawakuipokea hiyo habari njema. Maana Isaya alisema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu.” Tena nauliza: Je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni wa kwanza kujibu: “Nitawafanyeni muwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu.” Tena Isaya anathubutu hata kusema: “Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionesha kwao wasiouliza habari zangu.” Lakini kuhusu Israeli anasema: “Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii.”


Tazama wenye shida/tabu Mungu wetu, Tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu,wagonjwa wakapate uponyaji wako,wenye njaa ukawapatie chakula,wanaopitia magumu/majaribu ukawavushe Mungu wetu,walio katika vifungo vya yule mwovu ukawafungue Jehovah ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako,Nuru ikaangaze katika
maisha yao,wakapate uponyaji wa mwili na roho pia...

Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakunisoma
Mungu aendelee kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani,Upendo na Baraka ziwe nanyi siku zote..
Nawapenda.

Mwenyezi-Mungu anawagombeza watu wake

1Malaika wa Mwenyezi-Mungu aliondoka Gilgali, akaenda Bokimu, akawaambia Waisraeli, “Niliwatoa nchini Misri na kuwaleta katika nchi ambayo niliwaahidi kwa kiapo babu zenu. Nilisema kwamba sitalivunja agano langu nanyi kamwe. 2Na kwa upande wenu niliwaamuru msifanye agano na wenyeji wa nchi hii na kwamba madhabahu zao mtazibomoa. Lakini nyinyi hamkuitii amri yangu. Kwa nini mambo haya? 3Kwa hiyo sasa nasema: Sitawafukuza tena wakazi wa nchi hii bali watawataabisha, nayo miungu yao itakuwa mtego kwenu.” 4Malaika wa Mwenyezi-Mungu alipowaambia watu wote wa Israeli maneno haya, walipaza sauti zao na kulia. 5Wakapaita mahali hapo Bokimu.2:5 Bokimu: Jina hili katika Kiebrania linamaanisha “Wanaolia”. Hapo wakamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu.

Kifo cha Yoshua

6Baada ya Yoshua kuwaaga Waisraeli, kila mmoja alikwenda kwenye eneo lake alilogawiwa ili kuimiliki nchi. 7Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha ya Yoshua na baada ya kifo chake muda wote walioishi wale wazee waliosalia ambao waliyaona matendo makuu ambayo Mwenyezi-Mungu aliwatendea Waisraeli. 8Yoshua mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alifariki akiwa na umri wa miaka 110. 9Wakamzika katika sehemu aliyogawiwa iwe yake huko Timnath-heresi, katika nchi ya milima ya Efraimu kaskazini ya mlima Gaashi. 10Kisha watu wote wa kizazi chake walifariki, kikafuata kizazi kingine ambacho hakikumjua Mwenyezi-Mungu wala matendo aliyowatendea watu wa Israeli.

Waisraeli wanamwasi Mwenyezi-Mungu

11Basi, Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali. 12Walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao, ambaye aliwatoa katika nchi ya Misri, wakaifuata miungu mingine, miungu iliyoabudiwa na watu walioishi kandokando yao. Waliisujudia miungu hiyo, wakamkasirisha sana Mwenyezi-Mungu. 13Walimwacha Mwenyezi-Mungu, wakatumikia Mabaali na Maashtarothi. 14Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya Israeli, naye akawaacha wanyanganyi wapore mali zao. Aliwakabidhi kwa adui zao waliowazunguka hata wasiweze tena kuwapinga. 15Kila walipokwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi-Mungu uliwakabili kuwaletea balaa, kama alivyokuwa amewaonya na kuapa. Nao wakawa katika huzuni kubwa.
16Ndipo Mwenyezi-Mungu akawapa waamuzi ambao waliwaokoa mikononi mwa watu waliopora mali zao. 17Hata hivyo, Waisraeli hawakuwasikiliza waamuzi wao, maana walifanya kama wazinzi kwa kufuata miungu mingine na kuisujudia. Waliacha upesi nyayo walizofuata babu zao ambao walitii amri za Mwenyezi-Mungu; bali wao hawakufanya hivyo. 18Kila mara Mwenyezi-Mungu alipowapelekea mwamuzi, yeye mwenyewe alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa mikononi mwa adui zao muda wote wa uhai wa mwamuzi huyo. Aghalabu, Mwenyezi-Mungu aliwaonea huruma aliposikia kilio chao kutokana na mateso na dhuluma walizofanyiwa. 19Lakini kila mara mwamuzi alipofariki walirudia mienendo yao ya zamani, wakaishi vibaya kuliko babu zao. Waliifuata miungu mingine, wakaitumikia na kuisujudia, wala hawakuyaacha matendo yao wala ukaidi wao. 20Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi ya Waisraeli, akasema, “Kwa kuwa watu hawa wamevunja agano nililofanya na babu zao, wakakataa kutii sauti yangu, 21sitayafukuza tena mataifa ambayo Yoshua aliyabakiza, wakati alipofariki. 22Nitayatumia mataifa hayo kuwajaribu Waisraeli nione kama watairudia njia yangu kama babu zao au sivyo.” 23Basi, Mwenyezi-Mungu akayaacha mataifa hayo, wala hakuyafukuza mara moja, wala hakumpa Yoshua ushindi juu ya mataifa hayo!

Waamuzi 2;1-23

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: