Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 3 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 30 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..! Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi na vyote
vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mfalme wa Amani,Baba wa Upendo,Baba wa Baraka..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Muweza wa yote,hakuna lisilowezekana juu yako..
Unatosha Baba wa Mbinguni,Hakuna kama wewe.
Alfa na Omega,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya Ajabu..



Yahusu sasa vyakula vilivyotambikiwa sanamu: Tunajua kwamba sisi sote tuna ujuzi, lakini ujuzi huo huwafanya watu wawe na majivuno; lakini mapendo hujenga. Anayefikiri kwamba anajua kitu, kwa kweli hajui chochote kama inavyompasa. Lakini anayempenda Mungu, huyo anajulikana naye. Kwa hiyo, kuhusu vyakula vilivyotambikiwa sanamu, twajua kwamba sanamu si kitu duniani; twajua kwamba Mungu ni mmoja tu. Hata kama viko vitu viitwavyo miungu duniani au mbinguni, na hata kama wako miungu na mabwana wengi, hata hivyo, kwetu sisi yuko Mungu mmoja tu; Baba, Muumba wa vyote, ambaye kwa ajili yake sisi tuko. Pia yuko Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake vitu vyote viliumbwa, na sisi twaishi kwa njia yake.


Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tazama jana imepita Baba wa Mbinguni Leo ni siku mpya Jehovah Kesho ni siku nyingine..
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na tukijiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mizimu,Nguvu za mapepo,nguvu za mpinga Kristo
Zishindwe katika jina lililokuu kupita majina yote 
jina la Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yahweh tunaomba ututakase na utufunike kwa Damu ya 
Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..
kwakupigwa kwakwe sisi tumepona..


Nani aliyeamini mambo tuliyosikia? Nani aliyetambua kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu ulihusika? Maana, mbele yake Mwenyezi-Mungu, mtumishi wake alikua kama mti mchanga, kama mzizi katika nchi kavu. Hakuwa na umbo wala sura ya kutupendeza, wala hakuwa na uzuri wowote wa kutuvutia. Alidharauliwa na kukataliwa na watu, alikuwa mtu wa uchungu na huzuni. Alikuwa kama mtu kinyaa kwa watu; alidharauliwa na tukamwona si kitu. Hata hivyo alivumilia majonzi yetu, na kubeba huzuni zetu. Sisi tulifikiri amepata adhabu, amepigwa na Mungu na kuteswa. Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu. Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai; kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Jehovah ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mfalme wa Amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukavitakase na Ukavifunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo...

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Amani na upendo vikatawale katika Nyumba/Ndoa zetu
Watoto/wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanao tuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako wakati wote..
Baba wa Mbinguni ukatamalaki na kutuatamia..
Jehovah ukatupe hekima,busara na tukawe baraka kwa wengine..
Tukanene yaliyo yako,tukasikie sauti yako na ukatupe macho ya rohoni
tukapate kutambua na kujitambua..
Tukasaidiane na kuhurumiana,tukaelimishane kwa upendo na tukachuliane...
Ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Tukawe barua njema popote tupitato na tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..


Basi, nasema hivi: Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe. Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya sheria. Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: Uzinzi, uasherati, ufisadi; kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano; husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: Watu wanaotenda mambo hayo hawataupata ufalme wa Mungu uwe wao. Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Hakuna sheria inayoweza kupinga mambo hayo. Wale walio na Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake. Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na
 Utukufu hata Milele..
Amina...!
Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwakuwa nami..
Baba wa Baraka na upendo awe nanyi daima..
Mkono wake wenye nguvu ukawaguse na Amani ya
Kristo iwe nanyi daima..
Nawapenda. 


Matumaini mema kwa siku zijazo

1Mose akaendelea kusema, “Nimewapeni uchaguzi kati ya baraka na laana. Mambo hayo yote yakiwapata nanyi mkiyatafakari popote mlipo miongoni mwa mataifa ambamo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakuwa amewatawanya, 2mkamrudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi na watoto wenu, mkatii kwa moyo wote na roho yote neno lake ninalowaamuru leo, 3hapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawarudishieni mema yenu na kuwahurumia na kuwakusanya tena kutoka katika mataifa ambamo atakuwa amewatawanya. 4Na hata kama mmetawanywa katika sehemu mbali kabisa duniani, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawakusanya na kuwarudisheni, 5ili muimiliki tena nchi ambamo waliishi wazee wenu. Naye atawafanya mfanikiwe zaidi na kuwa wengi kuliko wazee wenu. 6Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafanyeni nyinyi na wazawa wenu muwe na moyo wa utii ili mumpende yeye kwa moyo wenu wote na roho yenu yote, mpate kuishi. 7Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atazifanya laana hizi zote ziwapate adui zenu ambao waliwatesa. 8Nanyi mtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu na kuzishika amri zake zote ninazowapeni leo. 9Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawafanya mfanikiwe katika kila mtakalofanya; mtakuwa na watoto wengi na ng'ombe wengi na mashamba yenu yatatoa mazao. Maana atapenda tena kuwafanya mfanikiwe kama vile alivyopenda kuwafanikisha wazee wenu, 10ikiwa mtiatii sauti yake na kushika amri na masharti yake yaliyoandikwa katika kitabu hiki cha sheria na kumrudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wote na roho yote.
11“Amri ninazowapa leo si ngumu mno kwenu, wala haziko mbali nanyi. 12Haziko mbinguni hata mseme, ‘Nani atakayepanda juu mbinguni kutuletea ili tupate kuzisikia na kuzitii?’ 13Wala haziko ngambo ya bahari, hata mseme, ‘Nani atakayevuka bahari atuletee ili tuzisikie na kuzitii.’ 14Sivyo, ila zipo karibu nanyi, vinywani mwenu na mioyoni mwenu, mpate kuzitekeleza.
15“Leo hii nawapeni uchaguzi kati ya mema na mabaya; kati ya uhai na kifo. 16Kama mkitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo ninawapa leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata njia zake na kushika masharti na maagizo yake, basi, mtaishi na kuongezeka; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,30:16 mkitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu: Kiebrania hakina maneno hayo. atawabariki katika nchi ambayo mnakwenda kuimiliki. 17Lakini mkipotoshwa na kukataa kumsikiliza, mkavutwa kuabudu miungu mingine na kuitumikia, 18mimi nawatangazieni leo hii kwamba mtaangamia. Hamtaishi kwa muda mrefu katika nchi mnayokwenda kuimiliki, ngambo ya mto wa Yordani. 19Naziita mbingu na dunia zishuhudie juu yenu leo hii, kwamba nimewapeni uchaguzi kati ya uhai na kifo, kati ya baraka na laana. Basi, chagueni uhai nyinyi na wazawa wenu mpate kuishi, 20mkimpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkiitii sauti yake na kuambatana naye. Maana kufanya hivyo kunamaanisha kwamba mtapata maisha marefu na kuishi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaahidi wazee wenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwamba atawapeni.”


Kumbukumbu la Sheria 30:1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: