Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 29 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 28 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)





Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..! Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Baba wa Mbinguni,Baba wa Upendo..
Baba wa Faraja,Baba wa Baraka,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote..
Jehovah Jireh..!,Jehovah Nissi..!,Jehovah Shammah..!
Jehovah Shalom...!,Jehovah Raah..!Emanuel..!
Mungu pamoja nasi...!!



Mimi mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda nyinyi, kwa sababu ukweli unakaa nasi milele. Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo. Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru. Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: Tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri mliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: Mnapaswa nyote kuishi katika upendo. Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu, na mwili wa kibinadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni mpinzani wa Kristo. Basi, jihadharini nyinyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishughulikia, bali mpate tuzo lenu kamili. Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana. Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu. Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu. Ninayo mengi ya kuwaambieni, lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike.
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..
Si kwamba tumekutenda mema sana,si kwa nguvu wala uwezo wetu..
Ni kwa neema/rehema zako tuu sisi kuwa hivi tulivyo..

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Mfalme wa Amani tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu..
Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


Mfalme wa Amani tunaomba ukatawale na kutamalaki 
katika Nyumba/ndoa zetu,


Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno, kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu. Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi. Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu. Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao. Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Nyinyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote. Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uhai anaowapeni Mungu. Hapo sala zenu hazitatiliwa kizuizi.
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na 
wote wanaotuzunguka Mungu wetu ukawe mlinzi mkuu..
Baba wa Mbinguni ukatubariki,ukatutakase na kutufunika kwa 
Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako
Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..


Mwisho nasema hivi: Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kindugu, kuwa wapole na wanyenyekevu nyinyi kwa nyinyi. Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, ajizuie asiseme mabaya aepe kusema uongo. Ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia. Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu.” Ni nani atakayeweza kuwadhuru nyinyi kama mkizingatia kutenda mema? Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu.

Tukawe barua njema nasi tukasoke kama inavyokupendeza wewe..
Roho mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Mkono wako wenye nguvu ukawaguse na kuwaponya wote
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Mungu wetu ukawaokoe
wote wali katika vifungo vya yule mwovu..
wakapate uponyaji wa mwili na roho pia..
ukawape neema ya kujiombea na ukapokee sala/maombi yao
ukaonekane katika mapito yako na ukawape sawasawa na mapenzi yako..



Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa katika maji, ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa nyinyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki katika yote yampendezayo..
Muwe na wakati mwema..
Nawapenda.


Baraka kwa wanaotii

(Lawi 26:3-13; Kumb 7:12-24)

1“Kama mkiitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu na kuzingatia kwa uangalifu amri ambazo ninawaamuru leo, yeye atawaweka juu ya mataifa yote duniani. 2Kama mkitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtapewa baraka zifuatazo;
3“Miji yenu itabarikiwa na mashamba yenu.
4“Mtabarikiwa mpate wazawa wengi, mavuno mengi, ng'ombe na kondoo wengi.
5“Vikapu vyenu vya nafaka vitabarikiwa na vyombo vyenu vya kukandia. 6Mtabarikiwa mnaporudi nyumbani na mnapotoka nje. 7Maadui zenu wakiwashambulia, Bwana atawapeni ushindi juu yao. Wakija kuwashambulia kwa njia moja watawakimbieni kwa njia saba. 8Baraka za Mwenyezi-Mungu zitakuwa katika ghala zenu za nafaka na katika shughuli zenu zote. Atawabariki katika nchi ambayo anawapeni.
9“Mwenyezi-Mungu atawafanyeni kuwa watu wake watakatifu kama alivyowaahidi, kama mkizitii amri zake yeye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata njia zake. 10Mataifa yote duniani yakiona kwamba nyinyi mnaitwa kwa jina la Mwenyezi-Mungu yatawaogopa. 11Mwenyezi-Mungu atawafanikisha kwa wingi: Watoto, mifugo na mavuno shambani katika nchi aliyowaapia wazee wenu kuwa atawapeni, 12Mwenyezi-Mungu atawafungulieni hazina yake nzuri kutoka mbinguni na kunyesha mvua katika nchi kwa wakati wake, na kubariki kazi zenu. Mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. 13Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafanya kuwa wa kwanza kwa nguvu na sio wa mwisho. Mtaendelea mbele na sio kurudi nyuma kama mkishika amri zake ambazo ninawapeni leo na kuwa waangalifu kuzitekeleza, 14bila kugeuka kulia au kushoto kuifuata miungu mingine na kuitumikia.

Kukosa utii

(Lawi 26:14-46)

15“Lakini kama hamtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, au msipokuwa waangalifu kutekeleza amri zake zote na masharti ninayowaamuru leo, basi mtapatwa na laana hizi zote: 16Mtapata laana katika miji yenu na mashamba yenu. 17Vikapu vyenu vya nafaka vitalaaniwa na vyombo vyenu vya kukandia mkate. 18Watoto wenu watalaaniwa na mazao yenu ya nchi; mifugo yenu italaaniwa isiongezeke. 19Mtalaaniwa mnapoingia na mnapotoka.
20“Mwenyezi-Mungu atawaleteeni maafa, vurugu na kukata tamaa katika shughuli zenu zote mpaka mmeangamia upesi kwa sababu ya uovu wa matendo yenu na kwa sababu ya kumwacha Mwenyezi-Mungu. 21Atawaleteeni maradhi mabaya mpaka wote muangamie kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki. 22Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa kifua kikuu, homa, majipu, joto kali, ukame, dhoruba na ukungu; mambo hayo yatawaandama mpaka mmeangamia. 23Mbingu zitakauka kama shaba nyeusi bila mvua, na nchi itakuwa kama chuma. 24Mwenyezi-Mungu ataifanya vumbi na mchanga kuwa mvua yenu, vumbi litawanyeshea mpaka mmeangamizwa.
25“Mwenyezi-Mungu atawafanya mshindwe na adui zenu. Nyinyi mtakwenda kuwakabili kwa njia moja, lakini mtawakimbia kwa njia saba. Nanyi mtakuwa kinyaa kwa watu wote duniani. 26Maiti zenu zitakuwa chakula cha ndege wala hapatakuwa na mtu atakayewafukuza. 27Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa majipu yaliyowapata Wamisri, atawapeni vidonda, upele na kuwashwa ambavyo hamwezi kuponywa. 28Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa pigo la kuwa na wazimu, mtakuwa vipofu na kuvurugika akili. 29Mtakwenda kwa kupapasapapasa mchana kama vipofu wala hamtafanikiwa katika shughuli zenu. Mtakuwa mkidhulumiwa kila mara na hakutakuwa na mtu wa kuwasaidieni.
30“Mtachumbia wasichana lakini watu wengine watalala nao. Mkijenga nyumba watu wengine watakaa ndani yake. Mkipanda mizabibu watu wengine watavuna. 31Ngombe wenu watachinjwa mbele ya macho yenu lakini hamtaonja hata kipande cha nyama yao. Punda wenu watachukuliwa kwa nguvu mbele ya macho yenu wala hamtarudishiwa. Kondoo wenu watapewa adui zenu, na hakuna mtu atakayeweza kuwasaidia. 32Watoto wenu wa kiume na wa kike watatolewa kwa watu wengine huku mkikodoa macho mchana kutwa kuwatazamia warudi, lakini hamtakuwa na nguvu ya kufanya chochote.
33“Taifa msilolijua litachukua mazao yote ya nchi yenu na matunda ya jasho lenu, nanyi mtadhulumiwa na kuteswa daima, 34hata mtapata wazimu kwa mambo mtakayoona kwa macho yenu wenyewe. 35Mwenyezi-Mungu atayashambulia magoti yenu na miguu yenu kwa majipu mabaya ambayo hamtaweza kuponywa; yatawaenea tangu utosini mpaka nyayo za miguu.
36“Mwenyezi-Mungu atawapeleka nyinyi na mfalme wenu mtakayejichagulia, mpaka kwa taifa ambalo nyinyi hamkulijua wala wazee wenu. Na huko mtatumikia miungu mingine ya miti na mawe. 37Nanyi mtakuwa kinyaa, dharau na mshangao miongoni mwa watu wote wa nchi ambako Mwenyezi-Mungu atawapeleka. 38Mtapanda mbegu nyingi lakini mtavuna kidogo tu kwa kuwa nzige watakula mazao yenu. 39Mtapanda mizabibu na kuitunza, lakini hamtavuna mizabibu hiyo wala kunywa divai yake, maana wadudu wataila. 40Mtakuwa na mizeituni mahali pote nchini mwenu, lakini hamtakuwa na mafuta ya kujipaka; kwa sababu zeituni hizo zitapukutika. 41Mtazaa watoto wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wenu, watachukuliwa uhamishoni. 42Matunda yenu yote na mazao yenu mashambani vitamilikiwa na nzige.
43“Wageni waishio katika nchi yenu watazidi kupata nguvu huku nyinyi mkizidi kufifia zaidi na zaidi. 44Wao watawakopesha nyinyi, lakini nyinyi hamtakuwa na uwezo wa kuwakopesha. Wao watakuwa wa kwanza kwa nguvu nanyi mtakuwa wa mwisho.
45“Hayo yote yatawapateni nyinyi na kuwaandama mpaka muangamizwe kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kuhusu kushika amri zake na masharti aliyowapa. 46Lakini hizo zitakuwa ushahidi wa hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwenu na wazawa wenu milele.
47“Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwabariki katika kila njia, lakini nyinyi hamkumtumikia kwa moyo wa furaha na mkunjufu. 48Kwa hiyo mtawatumikia maadui zenu ambao Mwenyezi-Mungu atawatuma dhidi yenu, kwa njaa, kiu na uchi, na kutindikiwa kila kitu. Atawafungeni nira ya chuma mpaka awaangamize.
49“Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi. 50Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana; 51litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize. 52Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni. 53Wakati wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui wenu, mtakula watoto wenu ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni. 54Hata mtu mpole kabisa na aliyelelewa vizuri sana atamnyima chakula ndugu yake, mkewe ampendaye na mtoto wake atakayesalia; 55wala hatamgawia hata mmoja wao nyama ya watoto wake atakaowala. Hamtabakiwa na chochote wakati huo wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui katika miji yenu yote. 56Hata mwanamke yule ambaye ni mpole sana na aliyelelewa vizuri na mwororo hata hajawahi kukanyaga udongo kwa kisigino chake hataweza kufanya vingine. Wakati huo wa kuzingirwa kutakuwa na njaa hata 57atamla mtoto wake mchanga na kile kinachotoka baada ya kuzaliwa mtoto bila hata mumewe mpenzi au mmoja wa watoto wake kutambua.
58“Kama msipokuwa waangalifu kutekeleza maneno yote ya sheria hii iliyoandikwa katika kitabu hiki na msipoliheshimu na kulitukuza jina tukufu la kuogofya la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, 59basi, Mwenyezi-Mungu atawaleteeni nyinyi na wazawa wenu mateso yasiyo ya kawaida, mateso makali yasiyoponyeka na ya kudumu, na magonjwa makali ya kudumu. 60Atawaleteeni tena yale magonjwa mliyoyaogopa nchini Misri, nayo yatawaandama daima. 61Atawaleteeni magonjwa ya kila aina na mateso mengine ambayo hayakutajwa katika kitabu hiki cha sheria mpaka muangamie. 62Ijapokuwa nyinyi ni wengi kama nyota za mbinguni, lakini mtakuwa wachache tu kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 63Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyopendezwa kuwafanikisha na kuwafanya kuwa wengi, vivyo hivyo Mwenyezi-Mungu atapendezwa kuwaletea maafa na kuwaangamiza. Nanyi mtaondolewa katika nchi hiyo ambayo mnakwenda kuimiliki. 64Mwenyezi-Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka pembe moja ya dunia hadi nyingine na huko mtaitumikia miungu mingine ya miti na mawe, miungu ambayo nyinyi wala wazee wenu hawakuijua. 65Hamtakuwa na raha yoyote mahali penu wenyewe pa kutulia wala miongoni mwa mataifa hayo. Ila Mwenyezi-Mungu atawapeni huko wasiwasi wa moyo, kufifia kwa macho na mahangaiko ya rohoni.
66“Maisha yenu yatakuwa mashakani, mchana na usiku mtakuwa na hofu na hamtakuwa na usalama wa maisha. 67Mioyo yenu itajaa woga wa kila mtakachoona. Asubuhi mtasema, ‘Laiti ingekuwa jioni,’ jioni itakapofika mtasema, ‘Laiti ingekuwa asubuhi.’ 68Mwenyezi-Mungu atawarudisheni Misri kwa meli, safari ambayo aliahidi kwamba hamngeifanya tena. Huko mtajaribu kujiuza kwa maadui zenu kuwa watumwa, lakini hakuna mtu atakayewanunua.”



Kumbukumbu la Sheria 28:1-68

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: