Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 15 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 18 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahweh..!Jehovah..!Eli Shaddai..!Eli Him..!El Elyon..!El Olam..!El Qanna..!Emanueli..!Mungu pamoja nasi..!
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Unastahili kutukuzwa..
Unatosha Baba wa Mbinguni,Matendo yako ni ya Ajabu..!



Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu. Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi, na uaminifu wako nyakati za usiku, kwa muziki wa zeze na kinubi, kwa sauti tamu ya zeze. Ee Mwenyezi-Mungu, matendo yako yanifurahisha; nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda. Matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, ni makuu mno! Mawazo yako ni mazito mno! Mtu mpumbavu hawezi kufahamu, wala mjinga hajui jambo hili: Kwamba waovu waweza kustawi kama nyasi, watenda maovu wote waweza kufanikiwa, lakini mwisho wao ni kuangamia milele, bali wewe, ee Mwenyezi-Mungu, u mkuu milele.

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii..
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..



Oneni, basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu. Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba, wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo. Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa. Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria. Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote. Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona wala kumjua Kristo. Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa. Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi. Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu. Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi.

Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu ..
Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu..
Mfalme wa amani utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ..

Mumngu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Yahweh ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu..
Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunayakabidhi maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,Watoto,Wazazi/Wazee wetu,familia/Ndugu na
Wote wanaotuzunguka Mungu wetu tunaomba ulinzi wako,
Amani,Upendo,Hekima,Busara na kuchukuliana..



Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana! Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema! Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia nyinyi. Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uhai kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo. Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uhai wa milele ndani yake. Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu. Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu? Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.

Baba wa Mbinguni ukatufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Ukatuokoe na vyote vinavyoenda kinyume nawe..
Yahweh ukatupe neema ya kusimamia Neno lako,Amri na Sheria zako..

Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu. Kwa maana, hata kama dhamiri zetu zatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu. Wapenzi wangu, kama dhamiri zetu hazina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu, na kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza. Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Yesu Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru. Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.
Baba wa Mbinguni ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia na yote tunayoenda kutenda Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Ukatufanye Barua njema nasi  tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Asante Baba Mungu yote tuyaweka mikononi mwako..
Tukiamini wewe ni Mungu wetu hakuna kama wewe..
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/Waungwana kwakuwa nami..
Mungu Baba aendelee kuwabariki..
Nawapenda.

Fungu la makuhani

1“Makuhani Walawi, yaani kabila lote la Lawi wasiwe na sehemu wala urithi katika Israeli. Wao watakula sehemu ya sadaka za Mwenyezi-Mungu. 2Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; Mwenyezi-Mungu ndiye urithi wao kama alivyoahidi.
3“Na hii itakuwa haki ya makuhani kutoka kwa watu wanaotoa sadaka iwe ni ng'ombe au kondoo: Watampa kuhani mguu wa mbele, mashavu na matumbo. 4Mtawapa sehemu ya kwanza ya mazao yenu ya nafaka, divai, mafuta yenu na sufu ya kwanza ya kondoo wenu. 5Katika makabila yenu yote, Mwenyezi-Mungu amechagua kabila la Walawi limtumikie kama makuhani milele.
6“Ikiwa Mlawi yeyote atapenda mwenyewe anaweza kutoka mji wowote ule wa Israeli kwenda pale mahali Mwenyezi-Mungu alipochagua, 7na hapo anaweza kuhudumu kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama wale Walawi wengine wanaohudumu mbele ya Mwenyezi-Mungu. 8Watapata mafungu yao sawa ya kula, ingawa wanayo mapato kutokana na mauzo ya mali za jamaa zao.18:7 Kiebrania hakieleweki.

Onyo dhidi ya desturi ngeni

9“Mtakapofika katika ile nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawapa, msifuate desturi za kuchukiza za mataifa hayo. 10Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu atakayemtambika mtoto wake wa kiume au wa kike kwa moto, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, 11wala mchawi, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu. 12Maana yeyote atendaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; na kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu. 13Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Ahadi ya kupewa nabii

14“Mataifa haya ambayo mtaimiliki nchi yao hufuata maongozi ya waaguzi na wapiga ramli; lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu hawaruhusu nyinyi kufanya hivyo.
15“Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawateulieni nabii aliye kama mimi kutoka miongoni mwenu, nanyi mtamsikiliza huyo. 16Hicho ndicho mlichomwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule Horebu, siku ile mlipokusanyika na kusema, ‘Tusisikie tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wala tusiuone tena moto huu mkubwa, tusije tukafa!’ 17Naye Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Wamesema ukweli. 18Nitawateulia miongoni mwa ndugu zao wenyewe nabii kama wewe; nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. 19Yeyote ambaye hatasikia maneno atakayosema nabii huyo kwa jina langu, mimi mwenyewe nitamwadhibu. 20Lakini nabii yeyote atakayesema kwa jina la miungu mingine, au atakayejaribu kusema neno kwa jina langu hali mimi sikumwambia aseme, huyo nabii atakufa.’
21“Lakini nyinyi mwaweza kusema, ‘Tutawezaje kutambua neno ambalo Mwenyezi-Mungu hakulisema?’ 22Kama nabii akisema kitu ati kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na kitu hicho hakifanyiki au hakiwi kweli, jambo hilo hakulisema Mwenyezi-Mungu; nabii amelisema kwa ufidhuli, nanyi msitishwe na jambo hilo.



Kumbukumbu la Sheria 18:1-22


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: