Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 31 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mambo Ya Walawi..4...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?

Tumshukuru Mungu wetu yeye yu mwema..

Haleluyah..!Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo, Muweza wa yote,Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Alfa na Omega..!Yahweh..!Jehovah..!Unatosha Baba.. Hakuna kama wewe..!

Tazama Jana imepita Baba wa Mbinguni Leo ni siku mpya Kesho ni siku nyingine...!!
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako,Umekuwa nasi usiku wote na wakati wote..
Asante kwa kutupa kibali cha kuendelea tena kuiona Leo hii ..

Tunakuja Mbele zako tukijinyenyekeza,Tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tunaomba utusamehe pale tupokwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua...
Mungu wetu tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe nasi waliotukosea..
Tunaomba utuepushe na majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake..

Tunaomba ututakase Miili yetu na Akili zetu na utufunike na Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena na kutenda na tukawe na kiasi..


Tunaomba ukabariki kuingia kwetu/kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri,tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..

Ukabariki vilaji/vinywaji,Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda Kugusa/Kutumia Mfalme wa Amani ukavitakase kwa Damu  ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Ukabariki Ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi utupe Neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji Baba wa Mbinguni..


Ukawaguse na mkono wako wenye Nguvu wote wanaopitia Magumu/majaribu Mbalimbali,walio kwenye vifungo mbalimbali na Ukawainue wanyonge na waliodhulumiwa wakapate haki yao..
Ukaonekane Jehovah..!! kwenye shida/tabu zao na wote wanaokulilia ukawafute machozi,wanaokuomba Baba ukawajibu sawasawa na mapenzi yako.
Wapendwa yanini mteseke na mizigo ?
Yanini kuteseka na kuugua rohoni?
Yanini kukata tamaa na kuwa na hofu/mashaka?
Baba anawapenda sana..
Asema..


 Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha...!!


Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza. “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia. Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”


Mfalme wa Amani tuyaweka maisha yetu mikononi mwako..Baba wa Mbinguni Tazama watoto wetu wanaondelea na mitihani na wanaojindaa na mitihani ukawabariki na ukawaguse na mkono wako wenye nguvu..wapate kukumbuka na kuelewa yote waliyofundishwa.. wakawe kichwa na si mkia..


Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafanya kuwa wa kwanza kwa nguvu na sio wa mwisho. Mtaendelea mbele na sio kurudi nyuma kama mkishika amri zake ambazo ninawapeni leo na kuwa waangalifu kuzitekeleza, bila kugeuka kulia au kushoto kuifuata miungu mingine na kuitumikia.
Asante Mungu wetu Baba yetu Tunaweka Ndoa zetu Mikononi mwako Mfalme wa Amani ..Kila mmoja akafuate/kufanya jukumu lake..
Mke na akawe mke kama ulivyoagiza,Mume na akawe Mume kama ulivyoagiza..ukatupe kuelewa na kujtambua katika Nyumba zetu na tufuate Neno lako Mungu wetu na si Maneno ya Binadamu..



Kila mmoja amstahi mwenzake kwa sababu ya heshima mliyo nayo kwa Kristo. Wake wawatii waume zao kama kumtii Bwana. Maana mume anayo mamlaka juu ya mkewe, kama vile Kristo alivyo na mamlaka juu ya kanisa; naye Kristo mwenyewe hulikomboa kanisa, mwili wake. Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, vivyo hivyo, wake wawatii waume zao katika mambo yote. Nanyi waume, wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, akajitoa mwenyewe sadaka kwa ajili yake. Alifanya hivyo ili kwa neno lake, aliweke wakfu kwa Mungu, baada ya kulifanya safi kwa kuliosha katika maji, kusudi ajipatie kanisa lililo takatifu na safi kabisa, kanisa lisilo na doa, kasoro au chochote cha namna hiyo. Basi, waume wanapaswa kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. ( Hakuna mtu yeyote auchukiaye mwili wake; badala ya kuuchukia, huulisha na kuuvika. Ndivyo naye Kristo anavyolitunza kanisa, maana sisi ni viungo vya mwili wake). “Kwa sababu hiyo, mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mkewe, nao wawili watakuwa mwili mmoja.” Kuna ukweli uliofichika katika maneno haya, nami naona kwamba yamhusu Kristo na kanisa lake. Lakini yanawahusu nyinyi pia: Kila mume lazima ampende mkewe kama nafsi yake mwenyewe, naye mke anapaswa kumstahi mumewe.
Kanisa linaanzia Nyumbani ..!
 Hasa wa mama mmhh..tumekuwa na mambo mengi mengi kisingizio Maombi,Mikutano,Makundi,Kusaidiana,kushikamana,sisi tunaosema hivyo ndiyo sisi wakwanza kusahau majukumu yetu..Maombi yooote,Mungu tunayemtafuta saa zooote, Mafundisho tunayopeana kila wakati sijui yanaishia wapi..?

 Msinielewe Vibaya  sipingani na haya mambo ya wamama hapana .. Basi yakazae matunda na tuwe na kiasi ..

Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini.

Ee-Mungu Baba tusaidie tuijue kweli yako na tujitambue..
Mungu akinipa kibali cha kuongelea hili ipo siku nitaongea..

Asante Mungu wetu.Tunakushukuru na kukuabudu wewe..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakua Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata milele..
Amina..!!

Asanteni sana kwa wote mnaotembelea hapa..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea 

sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda sana.



Sadaka kwa ajili ya dhambi zisizokusudiwa
1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Waambie watu wa Israeli hivi: Kama mtu ametenda dhambi bila kukusudia, akafanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, atafanya kama ifuatavyo: 3Ikiwa kuhani ambaye amepakwa mafuta ndiye aliyetenda dhambi hata akawatia watu hatiani, basi huyo atamtolea Mwenyezi-Mungu fahali mchanga asiye na dosari awe sadaka ya kuondoa dhambi. 4Atamleta huyo fahali mchanga kwenye mlango wa hema la mkutano, mbele ya Mwenyezi-Mungu; naye ataweka mkono wake juu ya kichwa cha fahali huyo na kumchinja mbele ya Mwenyezi-Mungu. 5Huyo kuhani, aliyepakwa mafuta atachukua kiasi cha damu na kuingia nayo ndani ya hema la mkutano. 6Atachovya kidole chake katika damu hiyo na kuirashia mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu upande wa mbele wa pazia la mahali patakatifu. 7Kuhani atachukua sehemu ya damu na kuzipaka pembe za madhabahu ya kufukizia ubani wa harufu nzuri, mbele ya Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka iliyoko karibu na mlango wa hema la mkutano. 8Kisha atayaondoa mafuta yote ya ng'ombe huyo: Mafuta yanayofunika matumbo, 9figo mbili na mafuta yaliyo juu yake na yale yaliyo kiunoni, na yale yaliyoshikamana na figo na ini; hizi ni sehemu zilezile zinazoondolewa kwa mnyama wa sadaka ya amani. 10Kuhani atazichukua na kuziteketeza juu ya madhabahu ya kuteketezea sadaka. 11Lakini ngozi ya huyo ng'ombe, nyama, kichwa, miguu, matumbo na mavi yake, 12yaani ng'ombe mzima aliyesalia atampeleka na kumteketeza nje ya kambi mahali safi ambapo majivu hutupwa, naye atamchoma kwa moto juu ya kuni; atachomwa moto hapo mahali pa kumwagia majivu.
13“Iwapo jumuiya yote nzima ya Israeli imetenda dhambi bila ya kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu 14mara dhambi hiyo itakapojulikana, jumuiya yote itatoa fahali mchanga awe sadaka ya kuondoa dhambi. Watamleta kwenye hema la mkutano. 15Wazee wa jumuiya ya watu wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo fahali, kisha atachinjwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. 16Yule kuhani aliyeteuliwa rasmi kwa kupakwa mafuta ataleta sehemu ya damu ya huyo fahali ndani ya hema la mkutano. 17Atachovya kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza mbele ya pazia mara saba, mbele ya Mwenyezi-Mungu. 18Kisha, sehemu ya damu atazipaka pembe za madhabahu iliyoko katika hema la mkutano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka iliyo karibu na mlango wa hema la mkutano. 19Mafuta yote ya mnyama huyo atayachukua na kuyateketeza kwenye madhabahu. 20Kwa hiyo atamfanya fahali huyu kama alivyomfanya yule mwingine wa sadaka ya kuondoa dhambi. Basi, huyo kuhani atawafanyia watu ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, nao watasamehewa. 21Kisha atamchukua fahali huyu na kumpeleka nje ya kambi na kumteketeza kwa moto kama alivyomfanya yule mwingine. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi ya jumuiya.
22“Ikiwa mtawala ametenda dhambi bila kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, na hivyo akawa na hatia, 23mara akijulishwa dhambi hiyo aliyotenda, ataleta sadaka yake ya beberu asiye na dosari. 24Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha beberu na kumchinjia mahali wanapochinjia sadaka za kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. 25Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka. 26Mafuta yote ya beberu huyo atayateketeza madhabahuni, kama afanyavyo na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa hiyo kuhani atamfanyia mtawala ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.
27 # Taz Hes 15:27-28 “Kama mtu wa kawaida ametenda dhambi bila kukusudia, kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu na hivyo akawa na hatia, 28mara atakapojulishwa kuwa ametenda dhambi, ataleta sadaka ya mbuzi jike asiye na dosari kwa ajili ya kuondoa dhambi aliyotenda. 29Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mbuzi huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa. 30Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu iliyobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu. 31Mafuta yote ya mbuzi huyo atayaondoa kama aondoavyo mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, naye kuhani atayateketeza madhabahuni, na harufu yake nzuri itampendeza Mwenyezi-Mungu. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu hiyo ibada ya upatanisho, naye atasamehewa.
32“Ikiwa mtu huyo ataleta mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, basi, ataleta mwanakondoo jike asiye na dosari. 33Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mwanakondoo huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali pale wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa. 34Kisha kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu. 35Kisha atayaondoa mafuta yote kama aondoavyo mafuta ya mwanakondoo wa sadaka ya amani, na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka zitolewazo kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Naye kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.”

Mambo Ya Walawi4;1-35


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: