Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 16 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 33...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote.
Asante Baba wa Mbinguni, Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba mbingu na Nchi, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo..Yahweh..!Jehovah..!El Shaddai..!Elohim..!Adonai..!
Asante kwa wema na Fadhili zako, Asante kwa ulinzi wako na kutumsha salama..
Asante kwa kutuchagua na kutupa Kibali cha kuendelea kuiona Leo hii..
Tunashuka mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..

Tunaomba utusamehe pale tulipo kwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda, kwakujua/kutojua..
Baba tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika kunena na kutenda,tukawe na kiasi na  tukawe chombo chema  tukatumike sawasawa na mapenzi yako..


Tunashukuru kwa uponyaji na ulinzi wako Mfalme wa Amani.. Asante kwa ridhiki zako Mungu wetu, Asante kwa kazi ulizotupa Baba wa Mbinguni, Asante kwa Biashara na Masomo pia..Asante kwa familia zetu na nyumba zetu Mfalme wa Amani..Asante kwa yote tuliyoyanena na tuliyoyaacha Baba wa Mbinguni unayajua na wewe unatujua vyema..
Tunaomba ukavibariki na kutubariki katika yote na tusipungukiwe katika mahitaji yetu na ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Baba ukawabariki na wengine wanaohitaji na wataabikao,wenye shida/Tabu,waliovifungoni,wagonjwa, wafiwa ukawe mfariji wao, wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Jehovha tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu.. ukawaponye na kuwainua, ukaonekane kwenye Taabu zao Baba wapate kupona kimwili na kiroho pia..

Jehovah..! Tunawaweka watoto wetu mikononi mwako, wewe ukawe mlinzi mkuu katika maisha yao, ukawaongoze katika masomo na ujana wao, makuzi yao na hatua zao za ukuaji ziwe nawe..wapate kukujua wewe katika maisha yao..Ukawabariki na wakawe Baraka kwa wazazi/walezi,Ndugu,walimu na jamii pia..



Mwanangu, moyo wako ukiwa wenye busara, moyo wangu pia utakuwa wenye furaha. Moyo wangu utashangilia, mdomo wako utakaposema maneno yaliyo sawa.


Baba ukatuongoze wazazi/walezi katika malezi yetu..tusipotoke na huu ulimwengu wa leo wenye mambo mengi ya kutisha tunayodhania ni maendeleo na usasa..ukatupe hekima na busara katika malezi,ukatupe kiasi,Upendo na upole kiasi..tukawe wasimamizi wema na mfano bora kwa watoto wetu..

Usiache kumrudi mtoto; ukimchapa kiboko hatakufa. Ukimtandika kiboko, utayaokoa maisha yake na kuzimu.
Asiyemwadhibu mtoto wake hampendi; lakini ampendaye mwanawe humrudi mapema.

Wazee huwaonea fahari wajukuu zao; watoto huwaonea fahari wazazi wao.
Eeh -Mungu wetu tunaomnba utuongoze..!!
Tunarudisha sifa na utukufu ni wako..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako Baba wa Mbinguni,Tukishukuru na kuamini kwako wewe yote yanawezekana..
Amina..!!
Asanteni wote mliopita/mnaondelea kupita hapa..
Mungu Baba akawabariki katika yote..
Nawapenda.


Mungu amwamuru Mose waanze safari

1 Taz Mwa 12:7; 26:3; 28:13 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Anza safari uondoke hapa, wewe na watu hao uliowatoa nchini Misri, mwende katika nchi niliyomwapia Abrahamu, Isaka na Yakobo, nikisema, ‘Nitawapa wazawa wenu nchi hii’. 2Nitamtuma malaika awaongoze; nitawafukuza Wakaanani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 3Nendeni katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali. Lakini kwa sababu nyinyi ni wenye vichwa vigumu sitakwenda pamoja nanyi, nisije nikawaangamiza njiani.”
4Watu walilia waliposikia habari hizi mbaya; wala hakuna aliyevaa mapambo yake. 5Walifanya hivyo kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Nyinyi ni watu wenye vichwa vigumu; nikienda pamoja nanyi kwa muda mfupi tu, nitawaangamiza. Hivyo vueni mapambo yenu ili nijue namna ya kuwatendea.’” 6Basi, Waisraeli waliyavua mapambo yao tangu walipoondoka mlimani Horebu.

Hema la mkutano

7Mose alikuwa na desturi ya kulichukua lile hema na kulisimika nje ya kambi. Hema hilo alilipa jina, Hema la Mkutano. Mtu yeyote aliyetaka shauri kwa Mwenyezi-Mungu alikwenda kwenye hema la mkutano nje ya kambi. 8Kila mara Mose alipotoka kwenda kwenye hema hilo, kila mtu alisimama penye mlango wa hema lake na kumwangalia Mose mpaka alipoingia ndani ya hilo hema. 9Wakati Mose alipoingia ndani ya hilo hema, mnara wa wingu ulitua kwenye mlango wa hema, na Mwenyezi-Mungu akaongea naye. 10Watu wote walipouona ule mnara wa wingu umesimama mlangoni mwa hema, kila mmoja wao alisimama na kuabudu mlangoni mwa hema lake. 11Hivyo ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyokuwa akiongea na Mose uso kwa uso, kama mtu na rafiki yake. Kisha Mose alirudi tena kambini. Naye kijana Yoshua mwana wa Nuni ambaye alikuwa mtumishi wake hakuondoka hemani.

Mwenyezi-Mungu aahidi kuwa na watu wake

12Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tazama! Wewe waniambia, ‘Waongoze watu hawa,’ lakini hujanijulisha ni nani utakayemtuma anisaidie. Hata hivyo umesema kwamba unanijua kwa jina na pia kwamba nimepata fadhili mbele zako. 13Sasa basi, nakusihi, kama kweli nimepata fadhili mbele yako, nioneshe sasa njia zako, ili nipate kukujua na kupata fadhili mbele zako. Naomba ukumbuke pia kwamba taifa hili ni watu wako.”
14Mungu akasema, “Mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nawe, na nitakupa faraja.” 15Mose akasema, “Kama wewe binafsi hutakwenda pamoja nami, basi, usituondoe mahali hapa. 16Maana nitajuaje kuwa nimepata fadhili mbele zako, mimi na watu wako kama usipokwenda pamoja nasi? Ukienda pamoja nasi itatufanya mimi na watu wako kuwa watu wa pekee miongoni mwa watu wote duniani.”
17Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa kuwa umepata fadhili mbele yangu, nami nakujua kwa jina lako, jambo hilihili ulilolisema nitalifanya.” 18Mose akasema, “Nakusihi unioneshe utukufu wako.” 19Taz Rom 9:15 Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Nitapita mbele yako na kukuonesha wema wangu wote nikilitangaza jina langu, ‘Mwenyezi-Mungu’. Mimi nitamrehemu yule ninayependa kumrehemu, na kumhurumia yule ninayependa kumhurumia. 20Lakini hutaweza kuniona uso maana hakuna mwanadamu yeyote atakayeniona na kuishi.” 21Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kuna mahali karibu nami ambapo utasimama juu ya mwamba; 22na utukufu wangu utakapokuwa unapita, nitakutia katika pango mwambani na kukufunika kwa mkono wangu, mpaka nitakapokuwa nimepita. 23Halafu nitauondoa mkono wangu nawe utaniona nyuma, lakini uso wangu hutauona.”Kutoka33;1-23


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: