Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 22 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo45...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa Mema aliyotutendea/anayoendelea kututundea..

Tumkaribie Mungu

19Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu. 20Yeye ametufungulia njia mpya, njia ya uhai, kupitia lile pazia, yaani mwili wake mwenyewe. 21Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu. 22Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa kutokana na dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi. 23Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu. 24Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema. 25Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, siku ile ya Bwana inakaribia.[Waebrania 10:19-25]
Asante Mungu wetu, Muumba mbingu na Nchi, Bwana wetu na Mwokozi wetu,Mfalme wa Amani,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Bwana wa Majeshi,Muweza wa yote..
Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuiona leo hii Baba..
Si kwa Uwezo wetu,Nguvu/utashi wetu..Si kwamba sisi ni wema sana Baba hapana..Ni kwa Neema /Rehema zako Muumba wetu...
Mtakatifu Baba wa Mbinguni tunaiweka siku hii mikononi mwako..Ukatuongoze na kutubariki Baba.. Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji,Hatua zetu ziwe nawe Baba..Vyombo vya usafri na tutembeapo Baba wa Mbingu usituache..
Tunaomba ubariki kazi zetu,Biashara,Masomo, na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase..
Ukabariki Ridhiki zetu Baba zinazoingia na zinazotoka..zikawe na ulinzi wako..Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda tukatende sawasawa na mapenzi yako..Utufanye chombo chema Baba nasi tukatumike sawaswa na mapenzi yako..
Utusamehe dhambi zetu Baba wa Mbinguni, tulizokosa kwa kuwaza/kutenda..kwa makusudi/kutokukusudia,Tunazozijua/kutojua..
Nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Bariki Yatima na Wajane Baba, Wenye Shida/Tabu na wote wanaopitia Magumu/Majaribu Baba ukawaponye na kuwaweka huru..
Sifa na utukufu ni zako Baba wa Mbinguni..
Tunashukuru na kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina....!!

37Maana kama yasemavyo Maandiko:
“Bado kidogo tu,
na yule anayekuja, atakuja,
wala hatakawia.
38Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi;
walakini akirudi nyuma,
mimi sitapendezwa naye.”

39Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tumo na wale wanaoamini na kuokolewa.[Waebrania 10:37-39]


Yosefu anajitambulisha

1Hapo Yosefu akashindwa kujizuia mbele ya wote walioandamana naye, akawaamuru watoke nje. Hivyo Yosefu alikuwa peke yake alipojitambulisha kwa ndugu zake. 2Lakini alilia kwa sauti kubwa hata Wamisri wakamsikia, hali kadhalika na watu wa jamaa ya Farao nao wakamsikia. 3Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu. Je, baba yangu angali hai?” Lakini ndugu zake wakapigwa na bumbuazi mbele yake, hata wakashindwa kumjibu. 4Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri. 5Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu. 6Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno. 7Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa. 8Kwa hiyo, si nyinyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Ndiye aliyenifanya kama baba kwa Farao, msimamizi wa nyumba yake yote na mtawala wa nchi yote ya Misri. 9Basi, fanyeni haraka, mwende kwa baba na kumwambia, ‘Yosefu, mwana wako, anasema: Mungu amenifanya kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri. Basi, usikawie kuja kwangu. 10Utakaa karibu nami katika eneo la Gosheni: Wewe, wana wako na wajukuu wako, mifugo yako na mali yako yote. 11Utakapokuwa Gosheni, mimi nitakutunza wewe, jamaa yako pamoja na mifugo yako ili msije mkafa njaa, kwani bado miaka mitano zaidi ya njaa.’” 12Kisha Yosefu akasema, “Nyinyi wenyewe mmeona kwa macho yenu na hata ndugu yangu Benyamini ameona kwa macho yake kwamba ni mimi mwenyewe Yosefu ninayezungumza nanyi. 13Ni lazima kumwambia baba yangu juu ya fahari yangu huku Misri na yote mliyoyaona. Basi, fanyeni haraka, mkamlete baba yangu huku.” 14Kisha Yosefu akamkumbatia Benyamini, nduguye, akalia; Benyamini naye akalia, huku wamekumbatiana. 15Akiwa bado analia, Yosefu akawakumbatia ndugu zake na kuwabusu. Hapo ndipo ndugu zake walipoweza kuzungumza naye.

Farao anamwalika Yakobo aje Misri

16Habari hizo zilipofika ikulu ya mfalme, kwamba ndugu za Yosefu wamekuja, zikamfurahisha sana Farao na watumishi wake. 17Kwa hiyo, Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako wawapakie punda wao mizigo, warudi nchini Kanaani, 18wamlete hapa baba yao na jamaa zao wote. Mimi nitawapa sehemu nzuri kabisa ya nchi ya Misri, ambako wataweza kufurahia matunda yote ya nchi hii. 19Waambie pia wachukue kutoka hapa magari ya kukokotwa ya kuwaleta watoto wao wachanga na wake zao na wala wasikose kumleta baba yao. 20Waambie wasijali juu ya mali zao maana sehemu nzuri kuliko zote katika nchi ya Misri itakuwa yao.”
21Basi, wana wa Israeli wakafanya kama walivyoagizwa. Yosefu akawapa magari kulingana na maagizo ya Farao na chakula cha njiani. 22Aliwapa kila mmoja wao mavazi ya kubadili, lakini akampa Benyamini vipande 300 vya fedha na mavazi matano ya kubadili. 23Tena alimpelekea baba yake zawadi hizi kwa ajili ya safari yake: Punda kumi waliobeba bidhaa bora za Misri, punda jike kumi waliobeba nafaka, mikate na vyakula vingine. 24Basi, Yosefu akaagana na ndugu zake. Walipokuwa wanaondoka aliwaonya akisema, “Msigombane njiani!”
25Basi, wakatoka Misri na kurudi nyumbani kwa baba yao Yakobo, nchini Kanaani. 26Wakamwambia baba yao, “Yosefu yu hai! Yeye ndiye mtawala wa nchi yote ya Misri!” Hapo baba yao akapigwa na bumbuazi, kwani hakuweza kuyasadiki maneno yao. 27Lakini, walipomsimulia yote waliyoagizwa na Yosefu na alipoyaona magari aliyopelekewa na Yosefu kumchukua, moyo wake ukajaa furaha kupita kiasi. 28Israeli akasema, “Sasa nimeridhika; mwanangu Yosefu yu hai! Nitakwenda nimwone kabla sijafa.”
Mwanzo45;1-28

Bible Society of Tanzania


"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: