Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Sunday 17 July 2016

Natumai Jumapili inaishia vyema;Burudani,Bwana Wa Majeshi na Nimesogea.by Paul S.Mwangosina -Sandra-Neema birthday, Shukrani na utukufu kwa Mungu wetu...


Wapendwa/Waungwana natumaini mlikuwa/mnaendelea vyema na Jumapili hii..
Mungu aendelee kuwatunza na kuwalinda, Kiroho na kimwili,Muingiapo na mtokapo,Vilaji na vinywaji, Msipungukiwe na Amani ya moyo,Baraka na Furaha kila iitwapo leo...

Kwetu kuanzia ijumaa mpaka leo tulikuwa na wakati mzuri sana,
15/7 kila mwaka tunaungana na binti yetu mpendwa kwa kumbukumbu yake ya kuzaliwa.
Ni zawadi iliyo njema  kwetu kutoka kwa Mungu,Tunamshukuru sana Mungu kwa baraka hii
kwenye maisha yetu,"Sandra-Neema" alikuwa baraka tangu alipofika mikononi mwetu na anaendelea kuwa baraka kwetu,Miaka 18 ni mingi na kwa wengine ni dada mkubwa lakini kwetu sisis wazazi kila siku utakuwa mtoto kwetu.

Mungu aendelee kukulinda,kukuongoza katika masomo na maisha yako yote yawe mikononi mwake
kila hatua unayopitia umtangulize Mungu iwe mchana iwe usiku,liwe giza iwe Nuru,kunena na kutenda,Uzidi kukuwa kiroho na kimwili, Uendelee kuwa baraka kwetu kama wazazi, walezi, ndugu,Jamaa , marafiki na jamii pia.Mungu azidi kukuinua katika yote yaliyo mema.

Shukrani;Viongozi wetu katika imani,washarika wenzetu na wote tunaomba pamoja
bila kuchoka katika yote.Mungu aendelee kuwabariki sana kwa kuwa pamoja nasi.
Shukrani;kwa Ndugu,Jamaa,marafiki zetu wote kwa Zawadi na  mchongo wenu kwenye makuzi ya binti yetu na yote,
tunaamini mtoto hulelewa na wengi si wazazi tuu,Mungu awabariki sana na tunawathamini mno.

Ngoja niishie hapa kwa leo Mungu yu mwema sana na tunauona mkono wa Bwana.

"Happy birthday da'Sandra-Neema".



1Kisha malaika akanionesha mto wa maji ya uhai maangavu kama kioo, yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. 2Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uhai unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa. 3Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo.
Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu. 4Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao. 5Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.



Neno La Leo;Ufunuo 22: 1-21


Kuja kwa Yesu
6Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaoneshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde.
7“Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.”
8Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona, nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionesha mambo hayo, nikataka kumwabudu. 9Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!”10Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia. 11Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.”
12  “Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake. 13Mimi ni Alfa na Omega, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho.”
14Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, wapate kuwa na haki ya kula tunda la mti wa uhai, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake.15Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji.
16“Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!”
17Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo.

Hatima
18Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki.19Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uhai, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki. 20Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Kweli naja upesi.”
Amina. Njoo Bwana Yesu!
21Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amina.

Biblia Habari Njema 


"Swahili Na Waswahili"Muwe na wakati Mwema.

No comments: