Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 9 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 28...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu katika yote..
Mtakatifu.. Mtakatifu..Mtakatifu...! Baba wa Mbinguni, Tunasema asante kwa wema na fadhili zako, Asante kwakutulinda usiku mzima na kutuamsha tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..

Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni  tukijinyenyekeza na tukijiachilia mikononi mwako Mfalme wa Amani..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Baba wa mbinguni, kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua, kutojua..
Nasi tunaomba utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..

Yahweh..! Tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu, utufunike na Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Roho Mtakatifu akatuongoze  katika yote tupate kutambua na kujitambua Baba na tukawe na kiasi ..

Jehovah..! Tunaomba ukaibariki siku hii na ukatubariki katika Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vilaji/vinywaji,Tuingiapo/Tutokapo,Vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe..

Baba wa Mbinguni tunawaweka watoto wetu wanaofanya mitihani na wanaojiandaa na mitihani.. ukawaongoze vyema na kuwalinda wapate kuelewa na kukumbuka yote waliyofundishwa..ukawaondoe hofu na mashaka..
Mfalme wa Amani Tazama Yatima na wajane,wenye shida/Tabu, wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,wanaopitia magumu/majaribu, waliokwenye vifungo mbalimbali Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse na mkono wako wako wenye nguvu, ukawaponye na kuwaokoa, ukawafunike na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Wapate kupona kimwili na kiroho pia..



Baba wa Mbinguni ukawafariji wote wanaopitia wakati mgumu wa kuondokewa na wapendwa wao,Mungu wetu  ukawaguse na kuwafariji ukawape nguvu na uvumilivu katika wakati huu mgumu kwao, ukaonekane Yahweh.. na ukawaponye rohoni na wakawe na matumaini tena..wapitishe salama katika jaribu hili Baba kwani kwa binadamu ni kipindi kigumu mno..lakini kwa Neema yako na watavuka salama..

Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni; jina la Mungu wa Yakobo likulinde. Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake; akutegemeze kutoka mlima Siyoni. Azikumbuke sadaka zako zote; azikubali tambiko zako za kuteketezwa. Akujalie unayotamani moyoni mwako, aifanikishe mipango yako yote. Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako; tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu. Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote! Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua, atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni; kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa. Wengine hujigamba kwa magari ya vita; wengine hujigamba kwa farasi wao. Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Hao watajikwaa na kuanguka; lakini sisi tutainuka na kusimama imara. Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu; utujibu wakati tunapokuomba.



Asante Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako tukisifu na kushukuru katika yote..
Amina..!!

Asanteni sana wote  kwa kutembelea hapa..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Mavazi ya makuhani

(Kut 39:1-7)

1“Nawe Mose umlete kwangu Aroni ndugu yako, pamoja na wanawe: Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari utawateua miongoni mwa Waisraeli, ili wanitumikie kama makuhani. 2Utamshonea ndugu yako Aroni mavazi matakatifu ili apate kuonekana mwenye utukufu na mzuri. 3Waagize mafundi wote ambao nimewapa maarifa wamtengenezee Aroni mavazi ili awekwe wakfu kwa ajili ya kazi ya ukuhani. 4Waambie wamtengenezee vitu vifuatavyo: Kifuko cha kifuani, kizibao,28:4 kizibao: Kiebrania: Efodi; kizibao kitakatifu kilichovaliwa na kuhani mkuu. Juu yake kilibandikwa kifuko cha kifuani. kanzu, joho iliyonakshiwa, kilemba na mshipi. Aroni nduguyo na wanawe watayavaa ili wanitumikie kama makuhani. 5Hao mafundi watatumia sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na nyuzi za dhahabu na kitani safi iliyosokotwa.

Kizibao cha kuhani
6“Watakitengeneza kizibao cha kuhani kwa nyuzi za dhahabu na sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kukitarizi vizuri. 7Kitakuwa na kamba mbili za kukifungia mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili. 8Mkanda wa kukishikia utatengenezwa kwa vifaa hivyohivyo: Kwa nyuzi za dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa na kuwa kitu kimoja na kizibao hicho.
9“Kisha utachukua mawe mawili ya sardoniki ambayo utachora juu yake majina ya wana wa Israeli.28:9 Israeli: Israeli hapa ni sawa na Yakobo. 10Majina sita katika jiwe la kwanza, na majina sita yaliyobakia katika jiwe la pili; majina yafuatane kadiri ya kuzaliwa kwao. 11Utayachora majina hayo juu ya hayo mawe kama vile sonara achoravyo mhuri, kisha uyatie nakshi na kuyaingiza katika vijalizo vya dhahabu. 12Mawe hayo mawili yatawekwa juu ya kanda za kizibao kama kumbukumbu ya makabila kumi na mawili ya Israeli. Hivyo Aroni atavaa majina hayo mabegani mwake mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu kama ukumbusho. 13Utayatengenezea vijalizo viwili vya dhahabu, 14na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba. Utaifunga mikufu hiyo kwenye hivyo vijalizo.

Kifuko cha kifuani
(Kut 39:8-21)


15“Utatengeneza kifuko cha kifuani cha kauli28:15 kifuko cha kifuani cha kauli: Namna ya kifuko kilichobandikwa juu ya kizibao chenye mawe matakatifu (aya 30) ambayo yalitumiwa na kuhani kujulisha matakwa ya Mungu. cha maamuzi; kitengenezwe kwa ustadi sawa kama kilivyotengenezwa kile kizibao: Kwa dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa. 16Kifuko hicho ambacho kimekunjwa kitakuwa cha mraba, sentimita 22. 17Kitapambwa kwa safu nne za mawe ya thamani: Safu ya kwanza itakuwa ya akiki, topazi na almasi nyekundu; 18safu ya pili itakuwa ya zumaridi, johari ya rangi ya samawati na almasi; 19safu ya tatu itakuwa ya yasintho, akiki nyekundu na amethisto; 20na safu ya nne itakuwa ya zabarajadi, shohamu na yaspi; yote yatatiwa kwenye vijalizo vya dhahabu. 21Basi, patakuwa na mawe kumi na mawili yaliyochorwa majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Kila moja litakuwa kama mhuri, ili kuwakilisha makabila yale kumi na mawili. 22Kwa ajili ya kifuko hicho cha kifuani, utatengeneza mikufu ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba. 23Vilevile utatengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili ya kifuko cha kifuani na kuzitia kwenye ncha mbili za kifuko hicho, 24na mikufu miwili ya dhahabu uifunge kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani. 25Zile ncha mbili za mkufu wa dhahabu utazishikamanisha kwenye vile vijalizo viwili vya kile kibati ili zishikamane na kipande cha mabegani cha kizibao upande wa mbele. 26Pia utatengeneza pete mbili za dhahabu na kuzitia kwenye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibao. 27Kisha utatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kizibao kinapoungana na mkanda uliofumwa kwa ustadi. 28Kifuko cha kifuani kitafungwa kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho cha kifuani kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi.
29“Aroni anapoingia mahali patakatifu, atavaa kifuko cha kauli kimechorwa majina ya makabila ya wana wa Israeli; kwa namna hiyo mimi Mwenyezi-Mungu sitawasahau nyinyi kamwe. 30Taz Hes 27:21; Kumb 33:8; Ezra 2:63; Neh 7:65 Kwenye kifuko hicho utatia mawe ya kauli28:30 mawe ya kauli: Kiebrania: Urimu na Thumimu; yalikuwa mawe matakatifu yaliyotumika hapo awali kujua matakwa ya Mungu, taz. Hes 27:21; 1Sam 14:41; 28:6; Ezra 2:63; Neh 7:65. yaninginie kifuani mwa Aroni kila anapokuja mbele yangu. Nyakati hizo ni lazima kila mara kuvaa kifuko hicho, ili aweze kutambua matakwa yangu kuhusu Waisraeli.

Mavazi mengine ya kikuhani

(Kut 39:22-31)

31“Utashona kanzu ya kuvalia kizibao kwa sufu ya rangi ya buluu. 32Itakuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, na nafasi hiyo itazungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike. 33Taz Sira 45:9 Kwenye upindo wake wa chini, kuzunguka pande zote, itapambwa kwa makomamanga ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kutakuwa pia na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga: 34Komamanga, njuga, komamanga, njuga, kuizunguka kanzu yote. 35Aroni atavaa kanzu hiyo kutekeleza huduma yake ya ukuhani na sauti yake itasikika wakati anapoingia mahali patakatifu mbele yangu na wakati anapotoka, njuga hizo zitasikika, naye hatauawa.
36“Kisha, utatengeneza kibati cha dhahabu safi na kuchora juu yake kama mtu achoravyo mhuri, ‘Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.’28:36 Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu: Au Mtakatifu kwa Mwenyezi-Mungu. 37Kibati hicho utakifunga mbele ya kilemba kwa ukanda wa buluu. 38Aroni atakivaa kibati hicho kwenye paji la uso wake; kwa hicho kibati atachukua lawama ya makosa ambayo Waisraeli wanaweza kuwa wameyafanya katika kunitolea tambiko takatifu, nami nitazikubali tambiko zao. 39Utamtengenezea Aroni joho iliyonakshiwa kwa kitani safi na kumfumia kilemba cha kitani safi na ukanda ulionakshiwa vizuri.
40“Utawatengenezea wana wa Aroni majoho, mishipi na kofia ili waonekane wana utukufu na uzuri. 41Utamvalisha ndugu yako Aroni na wanawe mavazi hayo, kisha uwapake mafuta na kuwawekea mikono ili kuwaweka wakfu wanitumikie kama makuhani. 42Vilevile utawashonea suruali za kitani zitakazowafunika tangu kiunoni mpaka mapajani, ili wafunike uchi wao. 43Aroni na wanawe watavaa suruali hizo kila wanapoingia katika hema la mkutano, au wanapokaribia kwenye madhabahu, kufanya huduma za makuhani katika mahali patakatifu. Kwa njia hiyo hawataonesha uchi wao na kuwa na hatari ya kuuawa. Hiyo itakuwa kanuni ya kudumu kwa Aroni na wazawa wake.Kutoka28;1-40


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 8 May 2017

Neno la Faraja;Mungu atupe uvumilivu Ndugu/Familia yangu kwa kuondokewa na Ndugu yetu Christopher-Hamisi Mbegete na Watanzania kwa kuondokewa na Watoto wetu wanafunzi wa Lucky Vicent..

Pichani ni ndugu yetu,Kaka na Mpendwa wetu Christopher-Hamisi Mbegete
Naungana na Ndugu/ familia yangu huko nyumbani kwa wakati huu mgumu sana kwa kuondokewa na mpenzi ndugu yetu..
Daima tutakukumbuka, Sina Neno zuri  la kuweza kusema zaidi ya kumshukuru Mungu kwa maisha yako na kuwa nasi na sasa umetangulia..Mungu akatupe faraja na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu..Mungu akawasimamie na kuwaongoza  wote wanaoshiriki katika maandalizi ya kuulaza mwili wako.Na akawabariki na kuwaongezea zaidi ya walipojitoa, kwa Muda, Faraja na yote..
Ulale kwa Amani.


Niungane na familia, wanafunzi /walimu  na Watanzania wenzangu huko nyumbani na popote walipo kwa wakati huu mgumu kwenye Taifa letu
kwakuondokewa na watoto wetu,wadogo zetu wapendwa wetu Walimu na Wafanya kazi..
Mungu Baba akawape nguvu na uvumilivu kwa wakati huu mgumu,Poleni sana wazazi/ndugu na Watanzania..
Mungu akawafariji na kuwaongoza katika yote.
Mlale kwa Amani malaika  wetu,watoto wetu wapendwa..
ni kipindi kigumu sana lakini tumshukuru Mungu katika yote..






Shukrani kwa Mungu
3Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. 4Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu. 5Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye. 6Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji nyinyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi. 7Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu.[2wakorintho 1;3-7]






Bwana anakuja
13Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini.
15Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana, kwamba sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia. 16Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. 17Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. 18Basi, farijianeni kwa maneno haya.[1Wathesalonike 4;13-18]


Wapendwa/Waungwana leo tuungane na wenzetu katika kuombeleza Msiba huu..
Mniwie Radhi kesho kwa Neema ya Mungu tutaendelea.
Muwe na wakati mwema na msisahau kuwaweka katika maombi/sala/dua wote wanaopitia mapito haya.

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe sana.

Friday 5 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 27...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake kwetu..
Mungu wetu, Baba yetu, Muumba wetu, Muumba Mbingu na Nchi, Muumba wa vyote vilivyopo, Mume wa Wajane, Baba wa Yatima,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo, Yahweh..!! Jehovah nissi..!, Jejovah rapha..!, Jehovah shalom..! Jehovah jireh..! Jehovah Shammah..!Jehovah Rohi..!!
Asante Baba kwa wema na fadhili zako, Asante kwa ulinzi wako usiku mzima,Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii Baba wa Mbinguni..

Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kuomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua,kutojua Mfalme wa Amani tunaomba na sisi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukosea..
Baba tunaomba utuokoe na Mwovu na kazi zake zote, zikashindwe na ututakase  Miili yetu na Akili zetu na Utufunike  kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Baba ukatuponye rohoni na Roho mtakatifu akatuongoze katika yote na tupate kutambua/kujitambua na tukawe na kiasi..

Tukapendane na kusaidiana katika kweli,tusiwe watu wa kujikweza na kujitapa,tusiwe wenye kuhukumu, tusiwe watu wa kisasi,tusiwe wenye kiburi na kukoseana adabu.

Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Tukawe na Imani na kuwaombea wengine, Tukawe wavumilivu na wenye kushukuru..



Kwa hiyo, ndugu zangu, maadamu Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote: Mtoleeni Mungu miili yenu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu. Msiige mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu na kutambua jambo lililo jema, linalompendeza na kamilifu. Kutokana na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni nyinyi nyote: Msijione kuwa ni kitu zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kadiri ya kipimo cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.

Mfalme wa Amani tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia magumu/majaribu,shida/tabu,waliokwenyevifungo mbalimbali,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao, wanaotafuta watoto,wanaotafuta mume/mke,waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,wanaugua rohoni,waliokataliwa na walio njia panda hawaelewi waanzie wapi waishie wapi..maisha yamekuwa magumu hawana kazi wala biashara Baba ukawape ubunifu, Maarifa na ukawape hekima na busara kwenye maamuzi...

Mfalme wa Amani tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo na zitokazo, ukabariki tuingiapo/tutokapo,vilaji/vinywaji,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..
Ukamguse kila mmoja na kumbariki naye aweze kumbariki mwingine, iwe kwa chakula, iwe kwa kumuombea mwinzie, iwe kwa pesa, iwe kwa kumtakia maneno ya baraka na kumsamehe kabisa yule aliye mkosea na alikuwa kikwazo kwenye moyo wake..

Baba ukatende na kuponya mioyo yao, ukamalize kabisa uchungu moyoni, ukawape neema ya kupendana na kutakiana amani ya moyo..na wakawe na kiasi ili wasije kukwazana tena..

Ndugu yangu mpendwa yakabidhi hayo mapito yako kwa Mungu na umuombe akupe neema ya kutua hiyo mizigo uliyobeba..yanini kujitesa na mizigo mizito na yupo awezaye kukutua?Yanini kujitafutia mateso na kuugua rohoni na mponyaji yupo?
Mkabidhi Mungu nawe uwe huru na mwepesi..
Mungu wetu atupenda na alimtoa mwanawe mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo aliteseka ili sisi tupate kupona..

Matafuteni Bwana maadam anapatikana..
Kwa Mungu yote yanawezekana...
Sifa na utukufu tumrudishie Mungu wetu, Tunakushuru Mungu wetu na tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Amina..!
Asante kwa wote mnaotembelea hapa
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea zaidi..
Nawapenda.

Madhabahu

(Kut 38:1-7)

1“Utatengeneza madhabahu kwa mbao za mjohoro. Madhabahu hiyo itakuwa ya mraba, urefu wake mita27:1 mita: Vipimo hivyo awali ni dhiraa, urefu wa kutoka kiwiko cha mkono hadi ncha ya kidole cha kati. mbili na robo, na upana wake mita mbili na robo; kimo chake kitakuwa mita moja na robo. 2Katika kila pembe ya madhabahu hiyo utatengeneza upembe ambao utakuwa umeundwa kutokana na madhabahu yenyewe. Madhabahu hiyo yote utaipaka shaba. 3Utaitengenezea vyombo vyake: Vyungu vya majivu, sepetu, na mabirika, na nyuma na visahani vya kuchukulia moto. Vyombo vyake vyote utavitengeneza kwa shaba. 4Kisha utatengeneza wavu wa shaba wenye pete nne za shaba kwenye pembe zake nne. 5Wavu huo utauweka kwenye ukingo wa madhabahu upande wa chini ili ufike katikati ya madhabahu. 6Utatengeneza pia mipiko ya mjohoro ya kuibebea madhabahu; nayo utaipaka shaba. 7Mipiko hiyo itaingizwa kwenye zile pete kila upande wa madhabahu, wakati wa kuibeba. 8Utaitengeneza madhabahu kwa mbao, na iwe yenye mvungu ndani, kulingana na mfano niliokuonesha mlimani.

Kitalu cha hema la mkutano

(Kut 38:9-20)
9“Utatengeneza ua wa hema la mkutano. Upande wa kusini wa ua kutakuwa na vyandarua vilivyotengenezwa kwa kitani safi iliyosokotwa ambavyo vitakuwa na urefu wa mita 44 kwa upande mmoja. 10Vyandarua hivyo vitashikiliwa na nguzo ishirini za shaba zenye vikalio vya shaba. Lakini kulabu za nguzo hizo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. 11Hali kadhalika upande wa kaskazini, urefu wa chandarua utakuwa mita 44, na nguzo zake 20 za shaba, lakini kulabu za nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. 12Upande wa magharibi wa ua utakuwa na chandarua chenye urefu wa mita 22, na nguzo zake 10 na vikalio vyake 10. 13Upande wa mashariki kuliko na mlango, ua utakuwa na upana wa mita 22. 14Chandarua cha upande mmoja wa mlango kitakuwa na upana wa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. 15Vilevile katika upande wa pili wa mlango chandarua kitakuwa mita 6.5, pamoja na nguzo tatu na vikalio vyake vitatu. 16Mlango wenyewe wa ua utakuwa na pazia zito lenye urefu wa mita 9, lililotengenezwa kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri. Pazia hilo litashikiliwa na nguzo nne zenye vikalio vinne. 17Nguzo zote kuuzunguka ua zitashikamanishwa kwa fito za fedha, kulabu zake zitakuwa za fedha na vikalio vyake vitakuwa vya shaba. 18Ua huo utakuwa na urefu wa mita 44, upana wa mita 22, na kimo cha mita 2.25. Vyandarua vyake vitakuwa vya kitani safi na vikalio vyake vya shaba. 19Vyombo vyote vya hema takatifu vya matumizi ya kila aina, pamoja na vigingi vyote na hata vile vya ua vitakuwa vya shaba.

Taa
(Lawi 24:1-4)

20“Utawaamuru Waisraeli wakuletee mafuta safi kwa ajili ya taa, kuwe na taa inayowaka daima. 21Hiyo itakuwa ndani ya hema la mkutano nje ya pazia hilo mbele ya sanduku la maamuzi27:21 maamuzi: Au agano; Kiebrania: Eduti. na Aroni na wanawe wataitunza mbele yangu tangu jioni mpaka asubuhi. Agizo hili sharti lifuatwe daima na Waisraeli wote, kizazi hata kizazi.
Kutoka27;1-21


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 4 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 26...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu yu mwema sana..Tumshukuru na kulisifu jina lake..
kwa maana pasipo yeye sisi si kitu kabisa..

Asante Baba wa Mbinguni kwa kutulinda usiku mzima na kutuamsha salama..Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tazama Jana imepita Baba Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine..
Tunashuka mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Jehovah...!
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua au kutojua Mfalme wa Amani..

Tunaomba utupe nasi Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..

Yahweh..! Tunaomba utulinde na kutuokoa na yule mwovu na kazi zake zote..

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Tunaomba ututakase Miili yetu na Akili zetu na kutufunika na Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


Jehovah..! Tunaomba ukabariki Ridhiki zetu ziingiazo na zitokazo..zikawe baraka na tuweze kuwabariki na wengine wenye kuhitaji..
Mungu wetu tunaomba ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vilaji/vinywaji,vyombo vya usafiri, tuingiapo/tutokapo,na tumbeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah..!!


Baba tazama Yatima,Wajane,wenye shida/tabu,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka,wanaogua rohoni,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,waliokatika vifungo mbalimbali Baba tunaomba ukawafungue na kuwagusa na mkono wako wenye nguvu,ukawaponye kimwili na kiroho pia,ukaonekane kwenye shida zao Jehovah..!Ukasikie kulia kwao na ukapokee maombi yao,ukawanyanyue na kuwaongoza, ukawabariki na kuwafariji Yahweh..!!

Ndugu yangu mpendwa makabidhi Mungu shida zako yeye hatokuacha kamwe,Yeye anakujua zaidi ya yeyote,hakuna lililogumu kwakwe, Yeye hachoki binadamu anaweza kukuchoka na kukusimanga, binadamu anaweza kukuumiza zaidi,binadamu anaweza kukukwamisha zaidi,binadamu anaweza asikuelewe na kukuona mzigo,binadamu anaweza kukukatisha tamaa zaidi, binadamu anaweza asipende kuona maendeleo yako,Yupo mponyaji wa kweli, yeye anayependa na kufurahia maendeleo yako,yeye hufurahi zaidi ukimrudia na husamehe kabisa, Ukimwamini Mungu yote yanawezekana..Mtafute anapatikana,Mwite ataitika,Muombe atajibu, Muite atasikia..Kwa Mkono wake wenye nguvu atakugusa na kukubariki..


Tumtukuze Mungu wetu kwa nafasi tuliyonayo..
Kama muimbaji Muimbie na kumsifu kupitia uimbaji wako,kama mfinyanzi finyanga vyungu vya kuwekea maua tukapambe nyumba yake,Mungu ametupa vipawa tofauti, hakuna kidogo mbele zake..
hivyo ulivyo kuna karama Mungu amekupa, kwako unaweza  kuona ni ndogo lakini mbele za Mungu ni fahari na anamakusudi yake..Itumie vyema na kwa hiyari yako pasipo kulazimishwa..

Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.

Tukawe barua njema na tusomeke vyema..sawasawa na mapenzi yake..
Sifa na utukufu tumrudishie Mungu wetu,Tunayaweka haya yote mikononi mwako Baba wa Mbinguni..

Tukishukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu Leo na hata milele..
Amina..!

Mungu akawaguse na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake,msipungukiwe katika mahitaji yenu na muweze kuwabariki na wengine..
Asanteni sana kwakupita hapa Mungu awabariki mno..
Nawapenda.



Hema la mkutano

(Kut 36:8-38)

1“Zaidi ya hayo yote, utatengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu. Mapazia hayo utayapamba kwa michoro ya viumbe wenye mabawa waliotariziwa. 2Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 12 na upana wa mita 2. Mapazia hayo yawe ya kipimo kimoja. 3Utaunganisha mapazia matano yawe kipande kimoja na mapazia mengine matano yawe kipande cha pili. 4Utashonea vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, hali kadhalika utashonea vitanzi mwishoni mwa pindo la nje la kipande kingine cha pazia. 5Utatia vitanzi hamsini katika pazia moja na vitanzi vingine hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vielekeane. 6Kisha utatengeneza kulabu hamsini za dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, hivyo hema litakuwa kitu kimoja.
7“Pia utatengeneza kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi. 8Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote hayo 11 yatakuwa na kipimo kilekile. 9Utaunga mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja. Pazia la sita utalikunja mara mbili mbele ya hema. 10Kisha utafanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha pili. 11Utatengeneza kulabu hamsini za shaba na kuziingiza katika vile vitanzi hamsini ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia na hivyo kufanya pazia moja la hema. 12Ile nusu ya pazia iliyobaki utaitundika upande wa nyuma wa hema. 13Nusu mita ya urefu wa mapazia iliyo ya ziada utaikunja ininginie pande zote mbavuni mwa hema ili kulifunika. 14Utatengeneza pia kifuniko kingine cha hema kilichofanywa kwa ngozi laini ya kondoo dume na ngozi laini ya mbuzi.
15“Utatengeneza mbao za mjohoro za kusimama wima kwa ajili ya hema. 16Kila ubao utakuwa na urefu wa mita 4, na upana wa sentimita 66. 17Kila ubao utakuwa na ndimi mbili za kuunganishia. Utazifanyia mbao zote ndimi mbili. 18Basi, utatengeneza hizo mbao za hema hivi: Mbao ishirini kwa ajili ya upande wa kusini, 19na vikalio arubaini vya fedha chini ya hizo mbao ishirini, vikalio viwili chini kwa kila ubao ili kushikilia zile ndimi zake mbili na vikalio viwili viwe chini ya ubao mwingine ili kushikilia zile ndimi zake mbili. 20Upande wa kaskazini wa hema, utatengeneza mbao ishirini, 21na vikalio vyake arubaini vya fedha, vikalio viwili chini ya kila ubao. 22Kwa upande wa nyuma, ulio magharibi ya hema, utatengeneza mbao sita. 23Utatengeneza pia mbao mbili kwa ajili ya pembe za hema upande wake wa nyuma. 24Mbao hizo za pembeni ziachane chini lakini zishikamanishwe kwa juu kwenye pete ya kwanza. Mbao zote za pembeni zifanywe vivyo hivyo ili zifanye pembe mbili. 25Hivyo kutakuwa na mbao nane pamoja na vikalio vyake kumi na sita vya fedha: Vikalio viwili chini ya kila mbao na vikalio viwili chini ya ubao mwingine.
26“Utatengeneza pau za mjohoro; pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema, 27na pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi. 28Upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema utapenya katikati toka mwisho huu hadi mwisho mwingine wa hema. 29Mbao zote utazipaka dhahabu na kuzifanyia pete za dhahabu zitakazoshikilia hizo pau, ambazo pia utazipaka dhahabu. 30Hivyo utalitengeneza hema hilo kulingana na mfano niliokuonesha mlimani.
31“Utatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo utalitarizi kwa ustadi kwa viumbe wenye mabawa. 32Utalitundika pazia kwenye nguzo nne za mjohoro zilizopakwa dhahabu, zenye kulabu za dhahabu na vikalio vinne vya fedha. 33Taz Ebr 6:19; 9:3-5 Utalitundika pazia hilo kwenye vifungo, kisha ulilete lile sanduku la ushuhuda humo ndani kukiwa na vibao viwili vya mawe, nyuma ya pazia hilo. Pazia hilo litatenga mahali patakatifu na mahali patakatifu sana. 34Ndani ya mahali patakatifu utakiweka kile kiti cha rehema juu ya sanduku la maamuzi. 35Ile meza ya mjohoro utaiweka upande wa nje wa pazia hilo, na kile kinara cha taa utakiweka upande wa kusini wa hema, mkabala wa meza. Meza hiyo itakuwa upande wa kaskazini.
36“Kwa ajili ya mlango wa hema utatengeneza pazia zito kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri. 37Vilevile utatengeneza nguzo tano za mjohoro na kuzipaka dhahabu. Nguzo hizo zitakuwa na kulabu za dhahabu, na kila moja itakuwa na tako la shaba.

Kutoka26;1-37

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 3 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 25...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu..
Asante Baba wa Mbinguni, Mungu wetu, Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo ni mali yako,Mungu wa wajane,Mungu wa yatima,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..Yahweh..!Jehovah.!!El Shaddai..!! Elohim..!!El Olam..!!
Asante kwa kutulinda usiku mzima na kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..
Asante kwa wema wako na fadhili zako Baba..

Si kwamba sisi ni wema sana,Kwamba ni wazuri mno,Kwamba ni wajuaji sana,Si kwanguvu/utashi wetu Mungu..Hapana ni kwa Neema/Rehema zako Mungu wetu umetupa nafasi hii tena...

Mpendwa unayesoma hapa Tazama wengine wapo mahospitalini wanashindwa hata kuita jina la Mungu,wengine wamekata kauli wanashindwa hata kutubu,wengine wanashindwa hata kufumbua macho, wengine hata hawajitambui wala kutambua aliye pembeni yake..
Si kwamba ni wabaya sana,kwamba ni waovu mno..
Ni kwa mapenzi yake Mungu ametuchagua sisi..

Basi tumshukuru Mungu wetu ,Tumche yeye atoshaye.. hii nafasi tukaitumie vyema..tukatue mizigo yote isoyo lazima tuliyo ya ibeba,Iwe nafasi nzuri ya kumsamehe aliyekukosea, iwe nafasi nzuri ya kuweza kutubu mbele za Mungu, iwenafasi nzuri ya kuweza kuwabariki wengine,iwe nafasi nzuri yakuweza kuachilia,iwe nafasi nzuri ya kumuonyesha Upendo kwa mtu unayehisi anakuchukia,iwe nafasi nzuri ya kuachana na visasi kwani visasi si vyako.....

Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kulipiza kisasi ni shauri langu; mimi nitalipiza, asema Bwana.” Zaidi ya hayo, Maandiko yasema: “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake.” Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa wema.

Mungu wetu tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua,kutojua..

Baba wa Mbingu tunaomba utupe na sisi Neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukosea..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako.
Tunashuka mbele zako Baba tukijinyenyekeza na kuomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake..Tunaomba ututakase Miili yetu na Akili zetu na Utufunike na Damu ya Mwanao mpendwa Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti.Ukatupe macho ya rohoni na kutambua/kujitambua..
Mfalme wa Amani maisha yetu yapo mikononi mwako, tunaomba ukabariki Ridhiki zetu ziingiazo na zitokazo, zikawe baraka na tuweze kuwabariki na wenye kuhutaji Baba..
Ukatubariki tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri,tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..!!
Ukabariki Vilaji/vinywaji,Kazi zetu,Biashara,Masomo na ukabariki familia zetu, Baba ukawaguse na kuwaponga wote wanaopitia magumu/majaribu,shida/tabu,waliokuwa kwenye vifungo mbalimbali Baba ukawafungue na wapate kupona kimwili na kiroho..

Asante kwa sababu wewe ni Mungu unaye ponya,unayebariki,unayesikia na unayejibu..wewe ndiye Ndimi  Mwenyezi-Mungu Mungu wetu..!Tunayaweka haya yote mikononi mwako..tukishukururu na kukusifu daima..
Amina...!!
Mungu akaonekane na kuwaongoza,

Asanteni sana wote mliopita hapa Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.



Matoleo kwa ajili ya hema takatifu

(Kut 35:4-9)

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 2“Waambie Waisraeli wanipe michango ya matoleo, nawe upokee kwa niaba yangu. Utapokea kutoka kwa mtu yeyote atakayetoa kwa moyo mkunjufu. 3Utapokea matoleo yafuatayo: Dhahabu, fedha, shaba, 4sufu ya buluu, ya zambarau na nyekundu, kitani safi iliyosokotwa manyoya ya mbuzi; 5ngozi za kondoo dume zilizotiwa rangi nyekundu, ngozi za mbuzi, mbao za mjohoro, 6mafuta kwa ajili ya taa, viungo kwa ajili ya mafuta ya kuweka wakfu na kwa ajili ya ubani wenye harufu nzuri, 7vito vya sardoniki, na vito vingine kwa ajili ya mapambo ya kizibao cha kuhani25:7 kizibao cha kuhani: Kiebrania: Efodi; kizibao cha kuhani kilichovaliwa na kuhani mkuu, taz. Kut 28:6-14. na kifuko cha kifuani.25:7 kifuko cha kifuani: Namna ya kifuko kilichobandikwa juu ya kizibao cha kuhani, taz. Kut 28:15-18. 8Vilevile Waisraeli watanitengenezea hema takatifu, ili niweze kukaa kati yao. 9Utatengeneza hema hiyo na vifaa vyake kulingana na mfano nitakaokuonesha.

Sanduku la agano

(Kut 37:1-9)

10“Waisraeli watengeneze sanduku la mbao za mjohoro, lenye urefu wa sentimita 110, upana sentimita 66, na kimo sentimita 66. 11Utalipaka sanduku hilo dhahabu safi ndani na nje, na kulifanyia ukingo wa dhahabu pande zote. 12Kisha utalitengenezea pete nne na kuzitia miguuni pake, kila mguu pete moja. 13Utatengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu. 14Mipiko hiyo utaipitisha katika pete zilizo pande mbili za sanduku, kwa ajili ya kulibebea. 15Mipiko hiyo itabaki daima katika pete; isitolewe wakati wowote. 16Ndani ya sanduku hilo utaweka vibao viwili vya mawe vya ushuhuda.
17“Kisha utatengeneza kwa dhahabu safi kiti cha rehema,25:17 kiti cha rehema Tafsiri nyingine: Mahali pa kuondolea dhambi. Taz pia Ebr 9:5. urefu wake sentimita 110, na upana wake sentimita 66. 18Utatengeneza pia mfano wa viumbe hai viwili kwa kufua dhahabu, uviweke kwenye miisho miwili ya kiti hicho; 19kiumbe kimoja mwisho mmoja na kiumbe kingine mwisho mwingine. Viweke viumbe hivyo kwenye miisho ya kiti hicho, lakini viwe kitu kimoja na hicho kiti. 20Viumbe hivyo vitaelekeana, mabawa yake yamekunjuka kukifunika kiti cha rehema; nyuso zake zitaelekea kiti hicho. 21Ndani ya sanduku utaweka vibao viwili vya mawe na kukiweka kiti cha rehema juu yake. 22Mimi nitakutana nawe hapo; na kutoka juu ya kiti hicho cha rehema katikati ya viumbe hao walioko juu ya sanduku la ushuhuda, nitazungumza nawe na kukupa amri zote kwa ajili ya Waisraeli.

Meza ya mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu

(Kut 37:10-16)

23“Utatengeneza meza ya mbao za mjohoro yenye urefu wa sentimita 88, upana sentimita 44 na kimo sentimita 66. 24Hiyo meza utaipaka dhahabu safi na kuizungushia utepe wa dhahabu. 25Kisha utaizungushia ubao wenye upana wa sentimita 66. 26Utaitengenezea pete nne za dhahabu na kuzitia kwenye pembe zake miguuni pake. 27Pete hizo zitakuwa karibu na ule ubao wa kuizunguka meza na zitakuwa za kushikilia mipiko ya kuibebea hiyo meza. 28Utatengeneza mipiko ya mjohoro na kuipaka dhahabu; mipiko itakuwa ya kuibebea hiyo meza. 29Utatengeneza sahani na vikombe vya kuwekea ubani mezani, na pia bilauri na bakuli za kumiminia tambiko za kinywaji. Vifanye vyombo hivyo vyote kwa dhahabu safi. 30Taz Lawi 24:5-8 Meza hiyo utaiweka mbele ya sanduku la agano, na juu ya meza hiyo utaiweka ile mikate ya kuwekwa mbele yangu daima.

Kinara cha taa

(Kut 37:17-24)

31“Utatengeneza kinara cha taa kwa dhahabu safi. Tako lake na ufito wa hicho kinara vitakuwa kitu kimoja, kadhalika na vikombe vyake, matumba yake na maua yake, vyote vitafuliwa kwa kipande kimoja tu cha dhahabu. 32Matawi sita yatatokeza kila upande wa ufito wake, matawi matatu upande mmoja na matawi matatu upande mwingine. 33Katika kila tawi kutakuwa na vikombe vitatu mfano wa maua ya mlozi, kila kimoja na tumba lake na ua lake. 34Na katika ufito kutakuwa na vikombe vinne mfano wa maua ya mlozi, pamoja na vifundo vyake na maua yake. 35Mahali panapotokezea kila jozi ya matawi yale sita, chini yake patakuwa na kifundo kimojakimoja. 36Vifundo hivyo na matawi yake yatakuwa kitu kimoja na kinara hicho, na chote kitafuliwa kwa dhahabu safi. 37Utatengeneza pia taa saba kwa ajili ya kinara hicho na kuziweka juu yake ili ziangaze kwa mbele. 38Tengeneza pia koleo zake na visahani vyake kwa dhahabu safi. 39Utatumia kilo thelathini na tano za dhahabu safi kutengeneza kinara hicho na vifaa vyake. 40Taz Mate 7:44; Ebr 8:5 Hakikisha kwamba umevitengeneza kwa mfano uliooneshwa kule mlimani.

Kutoka25;1-40

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 2 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 24...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu na kumsifu daima..
Mtakatifu Baba wa Mbinguni..Asante kwa ulinzi wako usiku mzima ,Asante kwa kutuamsha tena,Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali  cha kuendelea kuiona leo hii..
Asante kwa wema wako na fadhili zako Baba wa mbinguni..
Tunakuja mbele zako  tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako mwako Mfalme wa Amani..Tunaomba ukaibariki siku hii iwe njema na yenye Amani,Upendo,Furaha na shukrani..
Ukabariki kazi zetu Baba Biashara,Masomo,Tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri,tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..!Vilaji/vinywaji na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia ukavitakase na ukatutakase Miili yetu na Akili kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Mungu wetu tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe..kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwajua/kutojua..
Baba tunaomba na sisi ukatupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Roho mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda,kutambua/kujitambua na tuwe na kiasi..


Yahweh..!! tunaiweka Nchi hii tunayoishi mikononi mwako na wote tunaoishi humu..Baba wa mbinguni tunaomba utubariki na kutulinda katika yote..Baba wa Mbinguni nyoosha mkono wako wenye nguvu na kutugusa na kutuponya kiroho na ukawe mtala mkuu..Mfalme wa Amani bariki mji huu na ukuu wako ukaonekane..
Mfalme wa Amani tunaiweka Tanzania mikononi mwako ukawe mtawala mkuu na kuibariki na ukawabariki wa Tanzania wote popote walipo..Ukatamalaki na kuwaongoza katika maisha yao..
Tunaiweka mikononimwako Afrika na Dunia yote wewe Mungu ukatuongoze katika yote,ukatawale na kuwaongoza wanaotuongoza wakatuongoze katika haki na kweli..
Mfamle wa Amani ukuwaponye na kuwagusa wote wanaopitia Magumu/majaribu,shida/tabu, waliokatika vifungo mbalimbali Yahweh..!! ukawafungue wapate kupona kimwili na kiroho pia..


Asante kwa yote Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba mbingu na Nchi na vyote vilivyomo,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..Jehovah nissi...!!Jehovah Rapha..!!Jehovah Jireh..!! Jehovaha Shammah..!!Jehovah Shalom....!!! Haleluyahhhhh...!!!


Mose akajenga madhabahu na kuiita, “Mwenyezi-Mungu ni Bendera Yangu”, akisema, “Inueni juu bendera ya Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu atapigana na Waamaleki kizazi hata kizazi!”
Amina..!!

Mungu wetu anatosha,Hakuna hatokuwepo kama yeye..Amini na kumtumainia yeye..atatenda alitenda na anaendelea kutenda..
Mungu aendelee kuwabariki...
Asanteni sana sana mnaopitia hapa Mungu awe nanyi Daima na msipungukiwe katika mahitaji yenu..
Nawapenda..Nawapendaa..!!



Agano linathibitishwa

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoni kwangu, wewe Aroni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli, mniabudu kwa mbali. 2Wewe Mose peke yako ndiwe utakayenikaribia, lakini wengine wasije karibu, na Waisraeli wasipande mlimani pamoja nawe.”
3Basi, Mose akaenda na kuwaambia watu wote maneno na maagizo yote Mwenyezi-Mungu aliyomwambia. Watu wote wakajibu kwa sauti moja, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.” 4Mose akayaandika maagizo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimpa. Kisha akaamka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili kulingana na idadi ya makabila kumi na mbili ya Israeli. 5Kisha akawatuma vijana wa Waisraeli wamtolee Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa na kumchinjia sadaka za amani za ng'ombe. 6Mose akachota nusu ya damu ya wanyama hao na kuiweka katika mabirika, na nusu nyingine akairashia ile madhabahu. 7Kisha akachukua kitabu cha agano la Mwenyezi-Mungu, akakisoma mbele ya watu, nao wakasema, “Hayo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya, nasi tutakuwa watiifu.” 8Taz Mat 26:28; Marko 14:24; Luka 22:20; 1Kor 11:25; Ebr 9:19-20; 10:29 Mose akaichukua ile damu na kuwanyunyizia watu, akisema, “Hii ndiyo damu ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”
9Kisha Mose, Aroni, Nadabu na Abihu na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, 10wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya johari ya rangi ya samawati, kikiwa safi kama mbingu angavu. 11Na Mungu hakuwadhuru hao viongozi wa watu wa Israeli. Walimwona Mungu, wakala na kunywa.
Mose mlimani Sinai

12Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Njoo kwangu juu mlimani, ungoje huko. Mimi nitakupa vibao viwili vya mawe vyenye sheria na amri nilizoandika kwa ajili ya kuwafunza Waisraeli.” 13Basi, Mose akaondoka pamoja na Yoshua, mtumishi wake, akaenda kwenye mlima wa Mungu. 14Mose aliwaambia wale wazee, “Tungojeni hapa mpaka tutakapowarudia. Aroni na Huri wako pamoja nanyi; yeyote aliye na tatizo na awaendee wao.”
15Basi, Mose akaenda mlimani, na wingu likaufunika mlima. 16Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukatua juu ya mlima Sinai na wingu likaufunika mlima kwa muda wa siku sita. Siku ya saba Mungu akamwita Mose kutoka katikati ya lile wingu. 17Utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulionekana mbele ya macho ya watu wa Israeli kama moto unaowaka juu ya mlima. 18Taz Kumb 9:9 Mose akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani. Alikaa huko kwa muda wa siku arubaini, mchana na usiku.

Kutoka24;1-18

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 1 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 23...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru sana Mungu wetu kwa Neema/Rehema hii ya kutuchagua tena kuendelea kuiona siku/wiki/mwezi huu..si kwa uwezo wetu bali ni kwa mapenzi yake..
Tunaomba Baba wa Mbinguni ukatubariki,Tazama  mwezi/wiki/siku mwingine/nyingine tena Baba tukakuja mbele zako tukishukuru kwa mema yote uliyotutendea na unayoendelea kututendea..Asante kwa pumzi na afya,Asante kwa ridhiki zako ,wema na fadhili zako,Asante kwa yote na tunaanza nawe Baba wa mbinguni kwa kila jambo, maisha yetu yapo mikononi mwako,Tunaomba ukatubariki na kututendea sawasawa na mapenzi yako..Tunaomba utuokoe na mwovu na kazi zake zote..Tunaomba utubariki tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri na tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Baba, kazi zetu,Biashara,Masomo,vilaji/vinywaji na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo yeye aliteseka ili sisi tupate kupona...Baba ukatutakase Akili na Miili yetu pia..
Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda,kutambua/kujitambua na tukawe na kiasi...
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mfalme wa Amani kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Tunaomba na sisi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea na tuwe na kiasi ili tusikwazane tena..
Tunawaweka mikononi mwako wote wanaopitia magumu/majaribu..Baba tazama wenye Shida/Tabu, wagonjwa,Wafiwa ukawe mfariji wao,waliokatika vifungo mbalimbali, waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye mashaka/hofu,waliomizwa moyoni,Baba wa mbinguni ukawaguse na kuwaponya..
Tazama Yatima na wajane,wanaotafuta watoto Mfalme wa Amani,wanaotafuta wenza mke/mume ukawapatie walio wao na kuwabariki katika mahitaji yao..
Baba tunaomba ukabariki Ridhiki zetu ziingiazo na zitokazo ukazifanye baraka na kuweza kusaidia wengine..
Yesu Anakataliwa na Wayahudi...!!
Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi. Naye Yesu akawa anatembea hekaluni katika ukumbi wa Solomoni. Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, “Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiwe Kristo, basi, tuambie wazi.” Yesu akawajibu, “Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia. Lakini nyinyi hamsadiki kwa sababu nyinyi si kondoo wangu. Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. Mimi nawapa uhai wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wala hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba. Mimi na Baba, tu mmoja.” Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie. Yesu akawaambia, “Nimewaonesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?” Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa ajili ya kazi njema, ila kwa sababu ya kumkufuru Mungu! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu.” Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika sheria yenu: ‘Mimi nimesema, nyinyi ni miungu?’ Mungu aliwaita miungu wale waliopewa ujumbe wake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima. Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: ‘Unakufuru,’ eti kwa sababu nilisema: ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’ Kama sifanyi kazi za Baba yangu, msiniamini. Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi, mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake.” Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao. Yesu akaenda tena ngambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko. Watu wengi walimwendea wakasema, “Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa.” Watu wengi mahali hapo wakamwamini.
Mwamini Mungu ndugu yangu..katika shida zako mwite yeye,katika Raha,Furaha mshukuru yeye...Yeye asiye lala wala kusinzia hatokuacha daima, binadamu hubadirika lakini Mungu yeye habadiriki kamwe ukimtumainia yeye na kufuata njia zake kamwe hutojuta....
Sifa na utukufu ni wako Mungu wetu, tunayaweka yote mikononi mwako,tukishukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu..
Amina..!!
Asanteni sana kwa wote mliopita hapa Mungu Baba muweza wa yote aendelee kuonekana katika mahitaji yenu na aendelee kuwabariki..
Nawapenda.

Haki na usawa

1“Usitoe habari za uongo. Usishirikiane na mtu mwovu ili kuwa shahidi mbaya. 2Usifuate genge la watu kutenda uovu, wala usijumuike na genge la watu kutoa ushahidi mahakamani ili kupotosha haki. 3Taz Lawi 19:15 Usiwe na upendeleo katika kesi ya maskini.
4“Ukimkuta ng'ombe au punda wa adui yako amepotea, utamrudishia mwenyewe. 5Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako.
6“Usiipotoshe haki anayostahili maskini katika kesi yake. 7Jitenge mbali na mashtaka ya uongo wala usiwaue wasio na hatia na waadilifu, maana mimi sitamsamehe mtu mwovu. 8Usipokee rushwa, maana rushwa huwapofusha wakuu na kupotosha mambo ya wenye haki.
9“Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri.

Mwaka wa saba

10“Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake. 11Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.
12“Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe. 13Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako.
Sikukuu tatu kubwa

(Kut 34:18-26; Kumb 16:1-17)

14“Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu. 15Taz Kut 12:14-20; Lawi 23:6-8; Hes 28:17-25 Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu. 16Taz Lawi 23:15-21, 39-43; Hes 28:26-31 Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno23:16 sikukuu ya kukusanya mavuno: Au sikukuu ya vibanda. mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu. 17Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.
18“Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi.
19 Taz Kut 34:26; Kumb 14:21; 26:2 “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.
“Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.23:19 desturi hiyo ilifanyika katika mila za kidini za Wakanaani.

Ahadi na maagizo

20“Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia. 21Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu. 22Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu. 23Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nikawaangamiza hao wote, 24msiiname mbele ya miungu yao kuiabudu, wala kuitumikia, wala msiige mambo yao. Bali mtawaangamiza kabisa na kuzivunjavunja nguzo zao. 25Mtanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawabariki kwa chakula na maji na kuyaondoa magonjwa kati yenu. 26Hakutakuwa na mwanamke yeyote atakayepoteza mimba wala kuwa tasa katika nchi yenu. Nami nitawajalia maisha marefu.
27“Nitapeleka kitisho mbele yenu na kuwavuruga watu wote mtakaowakabili, na adui zenu nitawafanya wageuke na kuwakimbia. 28Nitapeleka manyigu mbele yenu ambao watawafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti. 29Sitawaondoa watu hao katika mwaka mmoja, nchi isije ikabaki tupu na wanyama wa porini wakaongezeka mno na kuwazidi nguvu. 30Lakini nitawaondoa kidogokidogo mpaka hapo mtakapoongezeka na kuimiliki nchi hiyo. 31Mipaka ya nchi yenu itakuwa kutoka bahari ya Shamu hadi bahari ya Mediteranea, na kutoka jangwani mpaka mto Eufrate, maana nitawatia wakazi wa nchi hiyo mikononi mwenu, nanyi mtawafukuza wawaondoke. 32Msifanye agano lolote nao, wala na miungu yao. 33Msiwaruhusu waishi nchini mwenu wasije wakawafanya mtende dhambi dhidi yangu; maana kama mkiitumikia miungu yao, hakika hiyo itakuwa mtego wa kuwanasa.”

Kutoka23;1-33

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.