Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 21 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo24....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Nimatumaini yangu mmeanza siku hii na Mungu..
Tumshukuru sana Mungu kwa Pumzi/Uzima,Afya na kutupa kibali cha kuiona leo hii..Ikawe yenye Baraka,Amani,Upendo,Furaha na Kumpendeza Mungu wetu muumba wa vyote..
Akatubariki Kuingia/Kutoka kwetu,Kazi,Biashara,Elimu,Vilaji/Vinywaji, Vyombo vya usafiri na tutembeapo Baba wa mbinguni awe nasi na kuvitakasa vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..
Roho mtakatifu akatuongoze kwenye kunena na kutenda,Mungu baba aka
tupe na ukutuongezea Hekima,Busara,Uvumilivu,Utambuzi/kujitambua na kuheshimiana.
Mfalme wa Amani ukawafariji wafiwa,Ukawaponye na kuwaokoa Wenye Shida/Tabu,Wagonjwa,waliokata tamaa, wenyevifungombalimbali na wote wanaopitia Magumu/Majaribu yoyote.
Mfalme wa Amani ukatawale maisha yetu na ukatupe sawasawa na Mapenzi yako..
Tunajikabidhi mikononi mwako Baba wa mbinguni,Tukishukuru na kuamini kwamba wewe ni Bwana na mwokozi wetu..
Amina...!!
Muwe na Imani na Amani.


Isaka anaoa
1Sasa Abrahamu alikuwa mzee wa miaka mingi, naye Mwenyezi-Mungu alikuwa amembariki katika kila hali. 2Siku moja Abrahamu akamwambia mtumishi wake aliyekuwa mzee kuliko wengine na msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako mapajani mwangu, 3nami nitakuapisha kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu na dunia, kwamba hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ninaoishi nao. 4Niapie kwamba utakwenda mpaka katika nchi yangu, kwa jamaa zangu, umtafutie mwanangu Isaka mke.” 5Mtumishi akamwambia, “Huenda mwanamke huyo atakataa kufuatana nami kuja huku, ikiwa hivyo, je, ni lazima nimrudishe mwanao nchini ulikotoka?” 6Abrahamu akamwambia, “La! Angalia sana usimrudishe mwanangu huko. 7Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, aliyenitoa nyumbani kwa baba yangu na kutoka katika nchi nilimozaliwa, na ambaye alisema nami, aliniapia kwamba atawapa wazawa wangu nchi hii. Yeye atamtuma malaika wake mbele yako ili umletee mwanangu mke kutoka huko. 8Iwapo mwanamke huyo hatapenda kufuatana nawe hadi huku, basi kiapo changu hakitakufunga, lakini kwa vyovyote vile usimrudishe mwanangu huko.” 9Basi, mtumishi huyo akaweka mkono wake mapajani mwa Abrahamu, bwana wake, akaapa kuhusu jambo hilo.
10Kisha, huyo mtumishi akachukua ngamia kumi wa bwana wake akaondoka akiwa na zawadi nzuri za kila aina. Akasafiri kwenda katika mji alimokaa Nahori, nchini Mesopotamia. 11Alipowasili, aliwapigisha magoti ngamia wake kando ya kisima kilichokuwa nje ya mji. Ilikuwa jioni wakati ambapo wanawake huenda kisimani kuteka maji. 12Naye akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba unijalie nifaulu leo na umfadhili Abrahamu bwana wangu. 13Niko hapa kando ya kisima ambapo binti za wenyeji wa mji huja kuteka maji. 14Basi, msichana nitakayemwambia atue mtungi wake wa maji anipatie maji ninywe, naye akanipa mimi pamoja na kuwanywesha ngamia wangu, na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Jambo hilo litanionesha kwamba umemfadhili bwana wangu.”
15Kabla hajamaliza kuomba, mara Rebeka, binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu yake Abrahamu, akafika amebeba mtungi wake begani. 16Msichana huyo alikuwa na sura ya kuvutia sana, na bikira ambaye hakuwa amelala na mwanamume yeyote. Basi, akateremka kisimani, akaujaza mtungi wake maji na kupanda. 17Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali, nipatie maji ya kunywa kutoka mtungi wako.” 18Msichana akamjibu, “Haya kunywa bwana wangu.” Na papo hapo akautua mtungi wake, akiushikilia ili amnyweshe. 19Alipokwisha kumpatia maji, akamwambia, “Nitawatekea maji ngamia wako pia, wanywe mpaka watosheke.” 20Basi, akafanya haraka, akawamiminia ngamia maji ya mtungi wake katika hori, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na kuwanywesha ngamia wake wote. 21Yule mtu akawa anamtazama kwa makini bila kusema lolote, apate kufahamu kama Mwenyezi-Mungu ameifanikisha safari yake au sivyo.
22Ngamia walipotosheka kunywa maji, yule mtu akampa huyo msichana pete ya dhahabu yenye uzito upatao gramu sita, na bangili mbili za dhahabu za gramu kumi kila moja. 23Akamwuliza, “Niambie tafadhali: Wewe ni binti nani? Je, kuna nafasi ya kulala nyumbani kwenu?” 24Rebeka akajibu, “Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori. 25Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha na mahali pa kulala wageni.” 26Ndipo yule mtu akainamisha kichwa chake, akamwabudu Mwenyezi-Mungu 27akisema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hajasahau fadhili zake na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mwenyezi-Mungu ameniongoza mimi mwenyewe moja kwa moja hadi kwa jamaa ya bwana wangu!”
28Kisha yule msichana akakimbia kwenda kuwapa habari jamaa za mama yake. 29Rebeka alikuwa na kaka yake aitwaye Labani. Labani akatoka mbio kukutana na yule mtu kisimani. 30Labani alikuwa ameiona ile pete na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia mambo Rebeka aliyoambiwa na huyo mtu. Labani alimkuta yule mtu amesimama karibu na ngamia wake kando ya kisima. 31Labani akamwambia, “Karibu kwetu wewe uliyebarikiwa na Mwenyezi-Mungu. Mbona unasimama nje? Mimi mwenyewe nimekwisha tayarisha nyumba na mahali kwa ajili ya hawa ngamia wako!” 32Basi, mtumishi huyo wa Abrahamu akaingia nyumbani. Labani akawafungua ngamia na kuwapatia majani ngamia wake, akampa yeye na watu wake maji ya kunawa miguu. 33Basi, wakamwandalia chakula, lakini yeye akasema, “Sitakula mpaka nimesema ninachotaka kusema.” Labani akamwambia, “Haya, tuambie.”
34Yule mtu akasema, “Mimi ni mtumishi wa Abrahamu. 35Mwenyezi-Mungu amembariki sana bwana wangu, naye amekuwa mtu maarufu. Amempa makundi ya kondoo na mifugo mingi, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda! 36Sara, mke wa bwana wangu katika uzee wake, alimzalia bwana wangu mtoto; na bwana wangu amempa huyo mtoto mali yake yote. 37Bwana wangu aliniapisha mimi akisema, ‘Hutamwoza mwanangu msichana yeyote miongoni mwa binti za Wakanaani ambao ninaishi katika nchi yao. 38Bali utakwenda mpaka nchi yangu, kwa jamaa zangu, ili umtafutie mwanangu Isaka mke.’ 39Nami nikamwambia bwana wangu, ‘Huenda mwanamke huyo akakataa kufuatana nami kuja huku.’ 40Lakini yeye akasema, ‘Mwenyezi-Mungu aniongozaye maishani mwangu, atamtuma malaika wake aende pamoja nawe na kukufanikisha katika safari yako; nawe utamtwalia mwanangu mke kutoka kwa jamaa yangu na nyumba ya baba yangu. 41Kama utakapofika kwa jamaa zangu hawatakupa huyo msichana, basi, hutafungwa na kiapo changu.’
42“Leo nilipofika kisimani nimeomba, ‘Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, nakuomba nifaulu leo katika safari yangu na umfadhili Abrahamu bwana wangu. 43Niko hapa kando ya kisima. Msichana atakayekuja kuteka maji ambaye nitamwomba anipatie maji kidogo ya kunywa kutoka mtungi wake, 44naye akanipa na kuwatekea maji ngamia wangu, basi huyo na awe ndiye uliyemchagua kuwa mke wa mwana wa bwana wangu.’
45“Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, mara Rebeka alifika na mtungi wake wa maji begani, akateremka kisimani na kuteka maji. Nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ya kunywa.’ 46Naye akautua mtungi wake haraka kutoka begani mwake, akasema, ‘Haya, kunywa bwana wangu. Nitawatekea maji ngamia wako pia.’ Basi mimi nikanywa na ngamia wangu pia akawapa maji. 47Ndipo nilipomwuliza, ‘Je, wewe ni binti wa nani?’ Akaniambia, ‘Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka, mkewe Nahori.’ Ndipo nilipompa pete na kumvisha bangili mikononi. 48Kisha nikainama na kumwabudu Mwenyezi-Mungu; nikamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye ameniongoza moja kwa moja kwa binti wa ukoo wa bwana wangu kwa ajili ya mwanawe. 49Sasa, basi, niambieni kama mko tayari kumtendea bwana wangu kwa uaminifu na haki; kama sivyo, basi semeni, nami nitajua cha kufanya.”
50Baada ya kusikia hayo, Labani na Bethueli wakamjibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi-Mungu, sisi hatuwezi kuamua lolote. 51Rebeka huyu hapa; mchukue uende. Na awe mke wa mwana wa bwana wako kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.” 52Mtumishi wa Abrahamu aliposikia maneno hayo, alimsujudia Mwenyezi-Mungu. 53Kisha akatoa vito vya fedha na dhahabu na nguo, akampa Rebeka. Pia aliwapa ndugu na mama yake Rebeka mapambo ya thamani kubwa.
54Mtumishi wa Abrahamu na watu aliokuja nao wakala, wakanywa na kulala huko. Walipoamka asubuhi, mtumishi yule akasema, “Naomba kurudi kwa bwana wangu.” 55Lakini ndugu na mama yake Rebeka wakasema, “Mwache msichana akae nasi muda mfupi, kama siku kumi hivi; kisha anaweza kwenda.” 56Lakini yeye akasema, “Tafadhali, msinicheleweshe, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha fanikisha safari yangu; naomba mniruhusu kurudi kwa bwana wangu.” 57Nao wakasema, “Basi, tumwite msichana mwenyewe, tumwulize.” 58Wakamwita Rebeka na kumwuliza, “Je, utakwenda na mtu huyu?” Naye akajibu, “Nitakwenda.” 59Basi, wakamwacha Rebeka na yaya wake aende na mtumishi wa Abrahamu na watu wake. Yaya wake Rebeka pia aliandamana naye. 60Basi, wakambariki Rebeka wakisema,
“Ewe dada yetu!
Uwe mama wa maelfu kwa maelfu;
wazawa wako waimiliki miji ya adui zao.”
61Kisha, Rebeka na wajakazi wake wakapanda ngamia na kumfuata huyo mtumishi wa Abrahamu; nao wote wakaondoka.
62Wakati huo, Isaka alikuwa ameondoka Beer-lahai-roi, akawa anakaa huko pande za Negebu. 63Siku moja jioni, Isaka alikwenda mashambani kutafakari. Basi, akatazama akaona ngamia wanakuja. 64Naye Rebeka alipotazama na kumwona Isaka, alishuka chini 65na kumwuliza mtumishi wa Abrahamu, “Ni nani yule mtu anayetembea kule shambani, anakuja kutulaki?” Yule mtumishi akasema, “Ni bwana wangu.” Basi, Rebeka akatwaa shela yake, akajifunika uso. 66Yule mtumishi akamsimulia Isaka yote aliyokuwa ameyafanya. 67Basi, Isaka akamchukua Rebeka ndani ya hema iliyokuwa ya Sara mama yake, akawa mke wake. Isaka akampenda Rebeka na kupata faraja baada ya kifo cha mama yake.
Mwanzo24;1-67
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Monday 20 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo23...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana, Anastahili kusifiwa,Anastahili kuabudiwa,Ahimidiwe,Mungu wetu asiyelala,Mungu wetu aponyae,Mungu wetu afanyae njia pasipo na njia,Yeye ni Alpha na Omega..!!
Tunamshukuru sana  kwa Neema/Rehema  ya kuiona leo hii,
Asante Baba wa Mbinguni kwa kutupa kibali cha kuendelea kuwepo leo hii..
Sisi si kwamba ni wema sana,Wazuri sana,Wajuaji, wenyenguvu/Utashi..Hapana ni kwa mapenzi yako tuu wewe uliyetuumba, na kuumba Mbingu na nchi na vyoote vilivyopo..
Ukaibariki siku hii Baba wa Mbinguni, Tuingiapo/Tutokapo,Vyombo vya Usafiri,Tutembeapo,Vilaji/Vinywaji,Kazi,Biashara,Elimu na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Mfalme wa Amani ukavitakase..
kuwaguse na kuwaponya wote wanaopitia Magumu/Majaribu,Vifungo mbalimbali vya mwovu,Wagonjwa,Wafiwa,Waliokata tamaa,wenyeshida/Tabu mbalimbali..
Mfalme wa Amani ukatawale katika maisha yetu, Ukatawale na kuwaongoza wanaotuongoza wakaongoze kwa haki na kweli,Ukaibariki nchi hii tunayoishi Baba,Ukaibariki Tanzani,Afrika na Dunia yote Mfalme wa Amani ukatawale..
Tunakwenda kinyume na Mwovu, Tunajiachilia mikononi mwako Bwana Mungu wetu, Tunashukuru na Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
Amina..!!!!!!
Tuanze wiki na Mungu yeye atosha..
Mbarikiwe.


Kifo cha Sara
1Sara aliishi miaka 127. Hiyo ndiyo iliyokuwa miaka ya maisha yake Sara. 2Alifia huko Kiriath-arba, yaani Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abrahamu akaomboleza na kumfanyia matanga Sara mkewe. 3Abrahamu akaiacha maiti ya mkewe, akatoka kwenda kuzungumza na Wahiti, akawaambia, 4 “Mimi ninaishi kama mgeni miongoni mwenu. Nipatieni sehemu ya ardhi ya kaburi, ili nipate kumzika marehemu mke wangu.” 5Wahiti wakamjibu, 6“Ee bwana wetu, tusikilize; wewe ni kiongozi maarufu miongoni mwetu. Mzike marehemu mkeo katika kaburi lolote utakalojichagulia; hakuna yeyote miongoni mwetu atakayekunyima kaburi lake, wala kukuzuia kumzika marehemu mkeo.” 7Hapo Abrahamu akasimama na kuinama kwa heshima mbele ya wananchi Wahiti, 8akawaambia, “Ikiwa mnaniruhusu nimzike marehemu mke wangu, tafadhali mwombeni Efroni mwana wa Sohari, kwa niaba yangu, 9aniuzie lile pango lake la Makpela lililo mpakani mwa shamba lake. Msihini aniuzie nilifanye makaburi yangu; anipatie kwa bei ya haki papa hapa mbele yenu.”
10Efroni mwenyewe alikuwa miongoni mwa Wahiti hao waliokuwa wamekutanika penye lango la mji. Basi, Efroni Mhiti, akamjibu Abrahamu, mbele ya Wahiti wote hapo langoni, 11“La, bwana; tafadhali unisikilize. Ninakupa shamba lote na pango lililomo humo; tena ninakupa mbele ya wananchi wenzangu. Mzike humo marehemu mkeo.”
12Abrahamu akainama tena kwa heshima mbele ya wananchi, 13akamwambia Efroni, wananchi wote wakisikia, “Nakuomba, tafadhali unisikilize. Nitakulipa bei kamili ya shamba lako, na ninakuomba upokee malipo haya, ili nipate kumzika humo marehemu mke wangu.” 14Efroni akamjibu Abrahamu, “Bwana, nisikilize; 15shamba lenye thamani ya shekeli 400 tu za fedha ni nini kati yako na mimi? Mzike marehemu mke wako.” 16Abrahamu akakubaliana na Efroni, akampimia kiasi cha fedha alichotaja mbele ya Wahiti wote, fedha shekeli 400, kadiri ya vipimo vya wafanyabiashara wa wakati huo.
17Basi, shamba la Efroni lililoko huko Makpela, mashariki ya Mamre, pango na miti yote iliyokuwamo pamoja na eneo zima, likawa lake 18Abrahamu mbele ya Wahiti wote waliokutanika penye lango la mji. 19Baada ya hayo, Abrahamu akamzika Sara mkewe katika pango hilo lililokuwamo katika shamba la Makpela, mashariki ya Mamre (yaani Hebroni) katika nchi ya Kanaani. 20Shamba na pango lililokuwamo humo lilithibitishwa na Wahiti liwe mali yake Abrahamu apate kuzika humo wafu wake.
Mwanzo23;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Friday 17 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo22..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu ni mwema sana,Tunamshukuru na Kumsifu, Unastahili kuabudiwa ee Mungu Baba wa Mbinguni,Sifa na Utukufu ni kwake Mungu wetu,Bwana wa Mabwana,Mume wa wajane,Baba wa Yatima,Mungu asiye lala,Mungu anayejibu,Aponya,Anaokoa,Yeye anatosha kwa kila uliombalo Ukimkabidhi yeye na kuamini anatenda...
Yanini kung'ang'ana na mizigo yako?kwanini wakata tamaa?Kwanini kupoteza muda,Gharama,Kutafuta kisicho chako?Yupo awezae yote,Njoo kwakwe naye atakutua mizigo yako,Mgeukie Baba Mungu muumba nchi na Mbingu yeye ni Mfalme wa Amani,Upendo,Faraja,Furaha,Ushindi,mpe/mkabidhi maisha yako leo na hutojutia,Omba na kusifu pasipo kikomo,Muite leo ataitika, Mwambie yote yeye anasikia..
Acha kutangatanga kwa wanadamu/mataifa hawatakusaidia kitu pasipo Mungu...
Mungu aendelee kutubariki/Kutulinda, Kuingiakwetu/Kutokakwetu,Vilaji/Vinywaji,Vyombo vya Usafiri,Tutembeapo,Kazi,Biashara,Masomo na Vyote tunavyoenda kugusa/Kutumia Baba wa Mbinguni akavitakase..
Akatupe sawa sawa na Mapenzi yake.
Tunakwenda kinyume na mwovuTunajikabidhi na kujiachilia mikononi mwako baba wa Mbinguni, Tukiamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu sasa na hata milele..
Amina..!!!
Mungu awe nanyi katika yote.


Abrahamu anamtoa Isaka sadaka
1Baada ya muda fulani, Mungu alimjaribu Abrahamu. Mungu alimwita, “Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam nasikiliza.” 2Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, Isaka, mwanao wa pekee umpendaye, uende mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuonesha.” 3Basi, kesho yake, Abrahamu akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Akatayarisha kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akaanza safari kuelekea mahali alipoambiwa na Mungu. 4Mnamo siku ya tatu, Abrahamu aliinua macho akapaona mahali hapo kwa mbali. 5Akawaambia wale watumishi wake, “Ngojeni hapa na huyu punda. Mimi na mwanangu tutakwenda mpaka kule, tukamwabudu Mungu, kisha tutawarudiani.”
6Basi, Abrahamu akazitwaa zile kuni, akamtwika Isaka mwanawe; yeye mwenyewe akachukua moto na kisu mkononi; wakaondoka pamoja. 7Isaka akamwuliza baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?” 8Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atatujalia mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.” Basi, wakaendelea na safari yao.
9 Walipofika mahali ambapo Mungu alimwagiza, Abrahamu akajenga madhabahu na kupanga kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe na kumlaza juu ya kuni juu ya madhabahu. 10Abrahamu akaunyosha mkono wake, akatwaa kisu tayari kumchinja mwanawe.
11Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita kutoka mbinguni, “Abrahamu! Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam, nasikiliza!” 12Malaika akamwambia, “Usimdhuru mtoto wala usimfanye lolote! Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwani hukuninyima hata mwanao wa pekee.” 13Ndipo Abrahamu akatazama, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake kichakani. Basi, akaenda, akamchukua huyo kondoo, akamtoa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14Kwa hiyo, Abrahamu akapaita mahali hapo, “Mwenyezi-Mungu hujalia.” Kama isemwavyo hata leo, “Katika mlima wa Mwenyezi-Mungu, watu hujaliwa.”
15Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwita Abrahamu mara ya pili kutoka mbinguni, 16 akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: Nimeapa kwa nafsi yangu kwamba kwa kuwa umefanya hivi, wala hukuninyima mwanao wa pekee, 17 hakika nitakubariki, na wazawa wako nitawazidisha kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ufuoni mwa bahari. Wazawa wako wataimiliki miji ya adui zao. 18 Kutokana na wazawa wako mataifa yote duniani yatabarikiwa kwa sababu wewe umeitii amri yangu.” 19Basi, Abrahamu akawarudia wale watumishi wake, nao kwa pamoja wakaondoka, wakarudi Beer-sheba; Abrahamu akakaa huko Beer-sheba.

Watoto wa Nahori

20Baada ya matukio hayo Abrahamu alipata habari kwamba Milka pia amemzalia Nahori, nduguye, watoto wa kiume: 21Usi mzaliwa wa kwanza, Buzi ndugu yake, Kemueli baba yake Aramu, 22Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli. 23Bethueli alimzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori, ndugu yake Abrahamu, watoto hao wanane. 24Zaidi ya hayo, Reuma, suria wa Nahori, pia alimzalia watoto: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.
Mwanzo22;1-24
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday 16 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi; Mwanzo21..


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Nimatumaini yangu mmeamka salama..Tunamshukuru Mungu kwa leo hii,Ametupa kibali cha kuiona tena..Wengi walitamani kuiona siku hii lakini wameshindwa,wengine ni wagonjwa wanashindwa hata kuinuka,Wengine hawana hata kauli, Sisi ni nani basi tumepewa hii Neema /Rehema ya kuwa Hai na wenye Afya na tushindwe kumuabudu Mungu,Kumshukuru Mungu,Kumsifu Mungu?
Tumempanini Mungu kwa uzima huu, sisi si kwamba ni wema sana zaidi ya wenzetu,si kwa nguvu/utashi wetu kuiona leo hii bali ni kwamapenzi ya Mungu wetu Muumba nchi na mbingu, Yeye ni mwingi wa Neema/Rehema, Yeye ni mtetezi wetu,Yeye asiye lala,Yeye ni mwokozi wetu,Yeye atupaye ridhiki zetu, Yeye awezae yote,Yeye ni mwamzo na yeye ni mwisho,Hakuna kama Yeye na hatokuwepo..
Mkabidhi Shida/Tabu zako,Magonjwa,Vifungo mbalimbali,Waliokata tamaa lipo Tumaini la kweli,Wafiwa yupo mfariji wa kweli,Wanaopitia Magumu/Majaribu yoyote mgeukie Mungu yeye anaweza..Akisema atakubariki hakuna wakupinga,Weka juhudi ya kumtafuta naye utamuona, Omba pasipokuchoka,Mwite na ataitika na kukutendea sawasawa na mapenzi yake.
Mungu Baba ukabariki Kuingia/Kutoka kwetu,Kazi,Biashara,Masomo,Vyombo vya usafiri na tutembeapo,Baba ukavitakase na damu yako vyote Tunavyoenda kuvitumia/kuvigusa..
Ukatuokoe na mwovu..Tunakuja mbele zako na kujiachilia mikononi mwako,Tukiamini wewe ni Bwana na mwokozi wetu..
Amina..!!!
Mbarikiwe.

Kuzaliwa kwa Isaka

1Mwenyezi-Mungu alimkumbuka Sara, akamtendea kama alivyoahidi. 2Basi, Abrahamu akiwa mzee, Sara akapata mimba, akamzalia mtoto wa kiume, wakati uleule Mungu alioutaja. 3Abrahamu akampa huyo mwanawe ambaye Sara alimzalia jina Isaka. 4Isaka alipotimiza umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri kama alivyoamriwa na Mungu. 5Abrahamu alikuwa na umri wa miaka 100 wakati mwanawe Isaka alipozaliwa. 6Naye Sara akasema, “Mungu amenipatia kicheko; yeyote atakayesikia habari hizi, atacheka pamoja nami.” 7Kisha akaongeza, “Ni nani angeweza kumwambia Abrahamu kwamba mimi Sara nitanyonyesha watoto? Tena nimemzalia mtoto wa kiume katika uzee wake!”
8Isaka akaendelea kukua, na siku alipoachishwa kunyonya, Abrahamu akafanya sherehe kubwa.

Hagari anafukuzwa
9Baadaye Sara alimwona Ishmaeli, mtoto wa Abrahamu aliyezaliwa na Hagari, Mmisri, akicheza na Isaka mwanawe. 10Basi, Sara akamwambia Abrahamu, “Mfukuzie mbali mjakazi huyu na mwanawe. Haiwezekani kabisa mtoto wa mjakazi kurithi pamoja na mwanangu Isaka.” 11Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa kuwa Ishmaeli pia alikuwa mtoto wake. 12Lakini Mungu akamwambia Abrahamu, “Usihuzunike kwa sababu ya mtoto huyu, wala huyo mtumwa wako wa kike. Lolote akuambialo Sara lifanye; kwa kweli wazawa wako watatokana na Isaka. 13Na kuhusu huyo mwana wa mjakazi wako, nitamfanya awe baba wa taifa kubwa kwa kuwa yeye pia ni mtoto wako.”
14Hivyo, asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari na kumtwika begani; akamfukuza pamoja na mwanawe. Hagari akaondoka, akawa anatangatanga nyikani Beer-sheba.
15Ikawa maji yalipomwishia katika kile kiriba, Hagari akamlaza mwanawe chini ya mti. 16Naye akaenda kando, akaketi umbali wa kama mita 100 hivi, akisema moyoni mwake, “Heri nisimwone mwanangu akifa.” Na alipokuwa ameketi hapo, mtoto akalia kwa sauti.
17Mungu akamsikia mtoto huyo akilia, na malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni, akamwambia, “Una shida gani Hagari? Usiogope; Mungu amesikia sauti ya mtoto huko alipo. 18Simama umwinue mtoto na kumshika vizuri mikononi mwako, kwani nitamfanya awe baba wa taifa kubwa.” 19Mungu akamfumbua Hagari macho, naye akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, akamnywesha mtoto wake.
20Mungu akawa pamoja na huyo mtoto, naye akaendelea kukua. Alikaa nyikani na akawa mpiga upinde hodari sana. 21Alikuwa akikaa katika nyika za Parani, na mama yake akamwoza mke kutoka nchi ya Misri.
Agano kati ya Abrahamu na Abimeleki
22Wakati huo, Abimeleki pamoja na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, alimwendea Abrahamu, akamwambia, “Mungu yuko pamoja nawe katika kila kitu unachofanya. 23Kwa hiyo niapie kwa jina la Mungu kwamba hutanifanyia hila mimi au watoto wangu au wazawa wangu. Kadiri mimi nilivyokuwa mwaminifu kwako, vivyo hivyo nawe uwe mwaminifu kwangu na kwa nchi hii unamokaa.” 24Abrahamu akasema, “Naapa.”
25Wakati huo Abrahamu alikuwa amemlalamikia Abimeleki juu ya kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamemnyanganya. 26Abimeleki akamwambia, “Mimi sijui nani aliyefanya hivyo; mpaka leo hii wewe hukuniambia; wala mimi sijapata kusikia habari hizi hadi leo.” 27Basi, Abrahamu akachukua kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki nao wawili wakafanya agano baina yao. 28Abrahamu akatenga wanakondoo wa kike saba. 29Abimeleki akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini unawatenga hao wanakondoo wa kike saba?” 30Abrahamu akamjibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba ninakupa kwa mkono wangu mwenyewe kama shahidi wangu kwamba mimi ndimi niliyechimba kisima hiki.” 31Kwa hiyo kisima hicho kikaitwa Beer-sheba, maana wote wawili walikula kiapo mahali hapo. 32Hivyo, wakafanya agano huko Beer-sheba. Abimeleki na Fikoli, mkuu wa jeshi lake, akaondoka na kurudi katika nchi ya Wafilisti. 33Abrahamu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu, akamwabudu Mungu, Mungu wa milele. 34Abrahamu alikaa katika nchi ya Wafilisti muda mrefu.
Mwanzo21;1-34
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday 15 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo20..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Natumaini mmeamka salama na Mungu yu pamoja nanyi..
Asante Baba wa Mbinguni kwa siku hii uliyo tupa kibali kuiona tena..
Si kwa uwezo/Utashi wetu bali kwa Neema/Rehema zako..
Tunaomba uibariki ikawe njema yenye mafanikio, Heri na Fanaka..
Ukabariki kuingiakwetu/Kutoka kwetu,Vilaji/Vinywaji,Vyombo vya Usafiri,Tutembeapo,Kazi,Biashara,Masomo na Vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase..
Roho mtakatifu akatuongoze kwenye kunena na kutenda..Sema nasi Baba wa Mbinguni ..
Ukawaguse na kuwaponya wote wanaopitia Magumu/Majaribu, Vifungo mbalimbali vya mwovu,Wagonjwa,Wafiwa,Walio Magerezani pasipo na hatia..Wewe ni Mungu uwezaye yote,Ufanya njia pasipo na njia,Unastahili kuabudiwa,Bwana wa Mabwana,Mungu usiye lala,Mfalme wa Amani ukatawale Nchi hii na Ukatawale Tanzania,Afika nzima na Dunia yote..Ukawaongoze wanaotuongoza na waongoze katika haki na kweli siku zote..Mamlaka ni yako,Nguvu na Utukufu,Jana,Leo,Kesho na hata Milele..
Amina..!!!!
Mungu awe nanyi katika yote ,Muwe na wakati mwema.


Abrahamu na Abimeleki

1Toka Mamre, Abrahamu alisafiri kuelekea eneo la Negebu, akafanya makao yake kati ya Kadeshi na Shuri, kisha akaenda kukaa kwa muda huko Gerari. 2Akiwa huko, Abrahamu alisema kuwa mkewe Sara ni dada yake. Kwa hiyo, mfalme Abimeleki wa Gerari akamchukua Sara. 3Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku, akamwambia, “Wewe utakufa kwa sababu ya mwanamke uliyemchukua, kwani ana mumewe.”
4Abimeleki ambaye bado hakuwa amelala na Sara, akajibu, “Bwana, utawaua watu wasio na hatia. 5Abrahamu mwenyewe ndiye aliyesema kuwa huyu ni dada yake. Tena hata Sara mwenyewe alisema kuwa Abrahamu ni kaka yake! Mimi nimefanya nilivyofanya kwa moyo mnyofu na sina hatia.” 6Basi, Mungu akamwambia katika hiyo ndoto, “Sawa. Najua kwamba umefanya hivyo kwa moyo mnyofu, na mimi ndiye niliyekuzuia kutenda dhambi dhidi yangu; ndiyo maana sikukuruhusu umguse huyo mwanamke. 7Sasa mrudishe huyo mwanamke kwa mume wake. Abrahamu ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini usipomrudisha, ujue kwa hakika kwamba wewe utakufa pamoja na watu wako wote.”
8Basi, Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumishi wake wote na kuwaeleza mambo aliyoyaona katika ndoto; nao wakaogopa sana. 9Ndipo Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwuliza, “Umetutendea nini? Nimekukosea nini hata ukaniletea balaa hili mimi na ufalme wangu? Umenitendea mambo yasiyostahili kutendwa.” 10Tena Abimeleki akazidi kumwuliza, “Ni kitu gani kimekusukuma kufanya hivyo?”
11Abrahamu akamjibu, “Nilifanya hivyo kwa kuwa hakuna amchaye Mungu mahali hapa, na kwamba mngeniua ili mumchukue mke wangu. 12Zaidi ya hayo, kwa kweli, yeye ni dada yangu: Baba yake na baba yangu ni mmoja, lakini mama tofauti; ndiyo maana akawa mke wangu. 13Wakati Mungu aliponifanya niiache nyumba ya baba yangu na kwenda ugenini, nilimwambia mke wangu, ‘Popote tutakapokwenda tafadhali useme kwamba mimi ni kaka yako!’”
14Abimeleki akamrudishia Abrahamu mke wake Sara, akampa na kondoo, ng'ombe na watumwa wa kiume na kike. 15Tena Abimeleki akamwambia Abrahamu, “Tazama, nchi hii yote ni yangu! Basi, chagua popote upendapo, ukae.” 16Kisha, akamwambia Sara, “Tazama, mimi nimempa ndugu yako vipande 1,000 vya fedha ili kuwaonesha wote walio pamoja nawe kwamba huna hatia; umethibitishwa huna lawama.”17Kisha Abrahamu akamwomba Mungu, naye akamponya Abimeleki, mkewe na mjakazi wake, hata wakaweza kupata tena watoto. 18Hapo kwanza Mwenyezi-Mungu alikuwa amewazuia wanawake wote wa nyumba ya Abimeleki kupata watoto kwa sababu ya Sara, mke wa Abrahamu.
Mwanzo20;1-18

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Tuesday 14 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo19..

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tunamshukuru Sana Mungu kwa leo hii na ikawe yenye Baraka,Amani, Furaha,Upendo na Faida...Mungu akawe nasi katika Kazi,Biashara,Masomo na akabariki Vyombo vya usafiri,Tutembeapo, Tuingiapo/Tutokapo,Vilaji/Vinywaji na akatakase vyote tunavyoenda kugusa/kutumia na Damu yake..
Akawakomboe/Kuwaponya wenye Shida/Tabu, Waliokata tamaa,Waliokataliwa/Kutengwa, Wenye vifungo mbalimbali na wote wanaopitia Magumu/Majaribu..
Akatupe sawaswa na mapenzi yake..
Yeye akisema atakubariki hakuna wa kupinga, Akisema ndiyo nani aseme hapana?Mungu wetu yu macho na anaweza yote..Mkadhi leo mizigo yako naye atakutua..Tuombe pasipo kukoma..
Mungu anatosha..!!!
Muwe na Wakati mwema.


Uovu wa watu wa Sodoma
1Wale malaika wawili wakawasili mjini Sodoma jioni. Loti ambaye alikuwa ameketi penye lango la mji wa Sodoma, alipowaona, aliinuka kuwalaki, akainama kwa heshima, 2akasema, “Bwana zangu, karibuni nyumbani kwangu mimi mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala kwangu usiku wa leo. Asubuhi na mapema mtaweza kuendelea na safari yenu.” Lakini, wao wakasema, “La! Sisi tutalala huku mtaani.” 3Loti akawasihi sana, mwishowe wakakubali, wakageuka na kuingia nyumbani kwake. Loti akawaandalia karamu, akaoka mikate isiyotiwa chachu, wakala.
4Lakini kabla ya kulala usiku, wanaume wote wa mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, bila kubaki hata mmoja, wakaizingira nyumba ya Loti. 5Wakamwita Loti na kumwuliza, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako? Watoe nje. Tunataka kulala nao.”
6Loti akatoka nje, akafunga mlango nyuma yake, 7akawaambia, “Ndugu zangu, nawasihi msitende uovu huo. 8Tazama, ninao binti wawili ambao bado hawajalala na mwanamume. Mniruhusu niwapeni hao wasichana muwatendee kama mpendavyo. Lakini msiwatende lolote wanaume hawa kwa sababu ni wageni wangu.”
9Lakini wao wakasema, “Tupishe! Wewe ulikuja huku ukiwa mgeni na sasa wajifanya hakimu! Basi, tutakutenda mabaya zaidi ya hao wageni wako.” Hapo wakamsukuma Loti nyuma hata karibu wauvunje mlango wake. 10Lakini wale wageni wakanyosha mikono yao, wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kuufunga mlango. 11Kisha wakawapiga kwa kuwapofusha macho wanaume wote waliokuwapo mlangoni, wakubwa kwa wadogo, hata wakataabika kuutafuta ule mlango, wasiupate.
Loti anatoka Sodoma
12Wale watu wawili wakamwambia Loti, “Je, una mtu mwingine hapa, pengine wana, mabinti, wachumba wa binti zako au watu wengine wa jamaa yako wanaoishi mjini humu? Watoe mahali hapa haraka, 13kwa maana kilio kilichomfikia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wakazi wa hapa ni kikubwa mno, naye ametutuma tuje kuwaangamiza.”
14Basi, Loti akawaendea wachumba wa binti zake, akawaambia, “Haraka! Tokeni mahali hapa, maana Mwenyezi-Mungu atauangamiza mji huu.” Lakini wao wakamwona kama mtu mcheshi tu.
15Kulipokucha, malaika wakamhimiza Loti wakisema, “Amka, mchukue mkeo na hawa binti zako wawili msije mkaangamia wakati mji huu unapoadhibiwa.” 16Loti akawa anasitasita. Lakini kwa vile Mwenyezi-Mungu alivyomhurumia Loti, wale malaika wakamshika yeye, mkewe na binti zake wawili, wakamtoa nje ya mji. 17Walipowatoa nje ya mji, malaika mmoja wao akawaambia, “Kimbieni kwa usalama wenu. Msiangalie nyuma wala kusimama popote bondeni. Kimbilieni milimani, msije mkaangamia.”
18Loti akawaambia, “La, bwana zangu! 19Ni kweli kwamba mimi mtumishi wenu nimepata fadhili mbele yenu, nanyi mmenionea huruma sana kwa kuyaokoa maisha yangu; lakini milimani ni mbali mno. Maangamizi haya yatanikuta kabla sijafika huko, nami nitakufa. 20Tazameni, kule kuna mji mdogo ambao naweza kuukimbilia kwani uko karibu. Basi, mniruhusu nikimbilie huko. Ule ni mji mdogo tu, na huko nitasalimika.”
21Naye akamjibu, “Sawa, nimekubali ombi lako. Sitauangamiza mji ulioutaja. 22Harakisha! Kimbilia huko, nami sitafanya lolote mpaka utakapowasili huko.” Hivyo mji huo ukaitwa Soari.
Kuangamizwa kwa Sodoma na Gomora
23Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Loti alipowasili mjini Soari. 24Ndipo Mwenyezi-Mungu akateremsha moto mkali wa kiberiti kutoka mbinguni juu ya Sodoma na Gomora, 25akaiangamiza miji hiyo, bonde lote, wakazi wake wote na mimea yote katika nchi hiyo. 26Lakini mkewe Loti aliyekuwa nyuma ya Loti, akatazama nyuma, akageuka nguzo ya chumvi.
27Asubuhi na mapema, Abrahamu alikwenda mahali alipokuwa amesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu. 28Akiwa hapo, akatazama chini pande za Sodoma na Gomora na eneo lote la bondeni, akashangaa kuona moshi ukipanda, moshi kama wa tanuri kubwa. 29Mungu alipoiangamiza miji ya bondeni alimokuwa anakaa Loti, alimkumbuka Abrahamu kwa kumtoa Loti katika miji hiyo, ili Loti asije akaangamia pamoja nayo.
Asili ya Wamoabu na Waamoni
30Loti aliogopa kuishi mjini Soari, kwa hiyo akauhama mji huo, yeye pamoja na binti zake wawili, wakaenda kuishi pangoni, milimani. 31Wakiwa huko, binti mkubwa akamwambia dada yake, “Baba yetu ni mzee, na hakuna mwanamume nchini wa kutuoa tupate watoto. 32Basi, tumlevye baba kwa divai, ili tupate kulala naye na kudumisha uzawa kwa kupata watoto kwake.” 33Usiku huo wakamlevya baba yao kwa divai, na yule binti wa kwanza akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka.
34Kesho yake, yule binti wa kwanza akamwambia yule mdogo, “Jana usiku mimi nililala na baba; leo pia tumlevye kwa divai, kisha wewe utalala naye, na hivyo sote tutadumisha uzao kwa kupata watoto.” 35Basi, usiku huo pia wakamlevya baba yao kwa divai, kisha yule binti mdogo akaenda akalala naye. Lakini baba yake hakujua wakati bintiye alipolala naye, wala alipoondoka. 36Hivyo, binti wote wawili wa Loti wakapata mimba kutokana na baba yao. 37Yule binti wa kwanza akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Moabu. Huyo ndiye baba wa Wamoabu hadi leo. 38Yule mdogo pia akajifungua mtoto wa kiume, akamwita Ben-ami. Huyo ndiye baba wa Waamoni hadi leo.
Mwanzo19;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.