Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 28 May 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 1Mambo ya Nyakati 13...





Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Haleluyah ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwamba sisi tumetenda mema sana wala si kwa nguvu zetu
si kwa utashi wetu wala si kwa akili zetu si kwamba sisi
ni wazuri mno si kwa uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu....

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudshia Mungu wetu....!!



Na sasa sikilizeni enyi matajiri! Lieni na kuomboleza kwa sababu ya taabu zitakazowajieni. Mali zenu zimeoza, na nguo zenu zimeliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha vimeota kutu, na kutu hiyo itakuwa ushahidi dhidi yenu, nayo itakula miili yenu kama vile moto. Nyinyi mmejirundikia mali katika siku hizi za mwisho! Hamkuwalipa mishahara watumishi waliofanya kazi katika mashamba yenu. Sikilizeni malalamiko yao! Kilio cha hao wanaovuna mashamba yenu kimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmeishi duniani maisha ya kujifurahisha na ya anasa. Mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmemhukumu na kumuua mtu asiye na hatia, naye hakuwapingeni!


Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tuaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya 
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
 kuwasamehe wale wote waliotukosea
Jehovah usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuepushe
na yule mwovu na kazi zake zote
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza 
ili sisi tupate kupona...




Basi, ndugu zangu, muwe na subira mpaka Bwana atakapokuja. Tazameni mkulima anavyongoja kwa subira mimea yake itoe mavuno ya thamani. Yeye hungojea kwa subira mvua za masika na za vuli. Nanyi pia mnapaswa kuwa na subira; imarisheni mioyo yenu, maana siku ya kuja kwake Bwana inakaribia. Ndugu zangu, msinung'unikiane nyinyi kwa nyinyi msije mkahukumiwa na Mungu. Hakimu yu karibu, tayari kuingia. Ndugu, mkitaka kuona mfano wa subira na uvumilivu katika mateso, fikirini juu ya manabii ambao walinena kwa jina la Bwana. Tunawaita hao wenye heri kwa sababu walivumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wa Yobu, na mnajua jinsi Bwana alivyomtendea mwishoni. Maana Bwana amejaa huruma na rehema.



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa 
katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza
kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo vimiliki
Yahweh tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Baba wa Mbinguni ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tukawe salama rohoni
Mfalme wa amani amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia 
sauti yako na kuitii
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote 
za maisha yetu
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu
Neema zako zikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu
Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi



Zaidi ya hayo yote, ndugu zangu, msiape kwa mbingu, wala kwa dunia, wala kwa kitu kingine chochote. Semeni “Ndiyo” kama maana yenu ni ndiyo, na “La” kama maana yenu ni la, na hapo hamtahukumiwa na Mungu. Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. Je, yuko mgonjwa kati yenu? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa, nao watamwombea na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Wakiomba kwa imani mgonjwa ataponyeshwa; Bwana atampatia nafuu, na dhambi alizotenda zitaondolewa. Basi, ungamanieni dhambi zenu, na ombeaneni, ili mpate kuponywa. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda mengi. Elia alikuwa binadamu kama sisi. Aliomba kwa moyo mvua isinyeshe, nayo haikunyesha nchini kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. Kisha akaomba tena, mvua ikanyesha kutoka angani na nchi ikatoa mazao yake. Ndugu zangu, mmoja wenu akipotoka kuhusu ukweli, na mwingine akamrudisha, fahamuni kwamba, huyo anayemrudisha mwenye dhambi kutoka njia yake ya upotovu, ataiokoa roho yake kutoka kifo, na dhambi nyingi zitaondolewa.

Mungu Baba tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu
wote wanaopotia magumu/majaribu mbalimbali
watoto wako wanaokuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
 kila mmoja na mahitaji yake 
Yahweh tunaomba ukaonekane katika maisha yao
Jehovah tunaomba ukawaokoe,ukawavushe salama na  kuwalinda
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako
wakasimaie Neno lako nalo likaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukasikie kuomba kwetu
Baba wa Mbinguni ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea 
kama inavyompendeza yeye....
Nawapenda.


Sanduku la agano lasimamishwa Kiriath-yearimu

(2Sam 6:1-11)

1Daudi alishauriana na makamanda wa vikosi vya maelfu na vikosi vya mamia, pamoja na viongozi wote. 2Kisha akawaambia Waisraeli wote waliokusanyika, “Ikiwa mtakubaliana nami, na ikiwa ni mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, na tufanye hivi: Tutume wajumbe waende wakawaite ndugu zetu waliobaki nchini Israeli, pamoja na makuhani na Walawi walioko katika miji yao na malisho yao, waje wajumuike pamoja nasi. 3Kisha twende tukalichukue sanduku la agano la Mungu wetu, maana hatukulijali wakati wa utawala wa mfalme Shauli.” 4Watu wote walikubaliana na pendekezo hilo kwani waliliona kuwa jambo jema.
5Hivyo, Daudi aliwakusanya Waisraeli wote nchini; toka kijito cha Shihori kilichoko Misri, hadi maingilio ya Hamathi ili kulileta sanduku la Mungu toka Kiriath-yearimu. 6Daudi, akiandamana na Waisraeli wote, akaenda hadi mjini Baala, yaani Kiriath-yearimu, nchini Yudea, ili kulichukua toka huko sanduku la Mungu linaloitwa kwa jina lake Mwenyezi-Mungu akaaye kwenye kiti chake cha enzi juu ya viumbe vyenye mabawa. 7Basi, wakalichukua sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Abinadabu kwa gari jipya. Uza na Ahio waliliendesha gari hilo. 8Daudi na Waisraeli wote wakawa wanacheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mungu. Waliimba huku wanapiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, matoazi na tarumbeta.
9Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza aliunyosha mkono wake kulishikilia sanduku la agano kwa sababu ng'ombe walijikwaa. 10Mara Mwenyezi-Mungu akamkasirikia Uza kwa kulishika sanduku, akamuua. Uza akafa papo hapo mbele ya Mungu. 11Daudi alikasirika kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimuua Uza akiwa na hasira. Kwa sababu hiyo, mahali hapo huitwa Peres-uza13:11 Peres-uza: Kiebrania maana yake “Pigo la Uza”. hadi leo. 12Siku hiyo Daudi akamwogopa Mungu, akasema, “Sasa, nitawezaje kulichukua sanduku la Mungu nyumbani mwangu?” 13Basi, Daudi hakulichukua sanduku mpaka mji wa Daudi,13:13 mji wa Daudi: Yaani: Yerusalemu. bali alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. 14Sanduku hilo la Mungu lilikaa huko kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu, naye Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya Obed-edomu na mali yake yote.


1Mambo ya Nyakati13;1-14


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: