Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 13 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 11...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mtakafitufu,Mtakatifu,Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni
Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na nchi
Muumba wa Vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyooneka
Mungu mwenye nguvu,Mungu  wa walio hai,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mponyaji wetu,Mume wa wajane,Baba wa yatima,Baba wa upendo,Baba wa Baraka,Muweza wa yote Alfa na Omega,Emanueli-Mungu pamoja nasi Neema yako yatutosha ee Mungu wetu..!!
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote 
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi,uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe Baba wa Mbinguni..!!


Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa. Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote. Nasema tena wazi: Kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika sheria yote. Kama mnatazamia kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu. Kwa upande wetu, lakini, sisi tunangojea kwa matumaini kwa nguvu ya Roho tufanywe waadilifu kwa njia ya imani. Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo. Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi, aliyewazuia kuuzingatia ukweli? Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni. “Chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!” Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba nyinyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni – awe nani au nani – hakika ataadhibiwa.


Tazama jana imepita ee Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea
Mungu wetu utuepushe katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona....


Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote. Laiti hao wanaowavurugeni wangejihasi wenyewe! Nyinyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo. Maana sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako...

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia,/ndugu na wote wanaotuzunguka
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Yahweh tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Baba wa Mbinguni ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Yahweh ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu,upendo kati yetu ukadumu,utu wema na fadhili na yote yanayokupendeza wewe..
Mungu wetu ukatuepushe na roho za kiburi,uongo,unafiki,ugombanishi,makwazo,chuki,choyo na yote yanayokwenda kinyume nawe..
Mungu wetu ukatuguse na mkono wako wenye nguvu Yahweh ukatuongoze na ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni,Neema yako ikawe nasi Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Jehovah ukatupe neema ya kufuata njia zako yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Basi, nasema hivi: Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe. Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya sheria. Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: Uzinzi, uasherati, ufisadi; kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano; husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: Watu wanaotenda mambo hayo hawataupata ufalme wa Mungu uwe wao. Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Hakuna sheria inayoweza kupinga mambo hayo. Wale walio na Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake. Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.


Ee Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa,Yahweh ukawape chakula wenye njaa,Mungu wetu ukawe tumaini kwa walio kata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka..
Jehovah tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu Yahweh tunaomba ukawafungue walio katika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia Yahweh haki ikatendeke..
Baba wa Mbinguni ukawavushe wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Yahweh ukawe faraja kwa wafiwa,Mungu wetu ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na kusimamia Neno lako nalo liwaweke huru..Mungu wetu tunaomba ukasikie kulia kwao Baba wa Mbinguni tunaomba ukawafute machozi ya watoto wako wanaokutafuta,kukuomba kwa bidii na imani..Ee Baba tunaomba ukasikie sala/maombi yetu Mungu wetu ukapokee Baba wa Mbinguni ukajibu sawasawa na mapenzi yako...
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele...
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu wetu mwenye mamlaka,Nguvu na Utukufu akawatendee kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.


Daudi na Bathsheba
1Hata ikawa katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Daudi alimtuma Yoabu na maofisa wake pamoja na Waisraeli wote kupigana; nao waliteka nyara Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi alibaki Yerusalemu.
2Siku moja, wakati wa jioni, Daudi aliamka kitandani akaenda kwenye paa ya ikulu. Alipokuwa anatembea huko juu, alimwona mwanamke mmoja akioga na mwanamke huyo alikuwa mzuri sana. 3Daudi akatuma mtu kuuliza mwanamke huyo ni nani. Mtu huyo akamwambia Daudi “Mwanamke huyo ni Bathsheba binti wa Eliabu, na ni mke wa Uria Mhiti.” 4Basi, Daudi alituma wajumbe wamlete. Basi Bathsheba akaja kwa Daudi, naye Daudi akalala naye; (mwanamke huyo alikuwa ndio tu amejitakasa baada ya hedhi yake); kisha akarudi nyumbani kwake. 5Mwanamke huyo akapata mimba, naye akatuma habari kwa Daudi kuwa ana mimba yake.
6Basi, Daudi akamtumia Yoabu ujumbe, “Mtume Uria, Mhiti kwangu.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. 7Uria alipofika kwake, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, watu wote, na hali ya vita. 8Halafu Daudi alimwambia Uria, “Rudi nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Uria alitoka nyumbani kwa mfalme, na mara mfalme akampelekea zawadi. 9Lakini Uria hakurudi nyumbani kwake, bali alilala pamoja na watumishi wote wa bwana wake kwenye lango la ikulu. 10Daudi alipoambiwa kwamba Uria hakwenda nyumbani kwake, Daudi alimwuliza Uria, “Wewe umetoka safari, kwa nini hukuenda nyumbani kwako?” 11Uria alimjibu Daudi “Sanduku la agano, pamoja na majeshi yote ya Israeli na Yuda yanakaa kwenye vibanda vitani. Bwana wangu Yoabu na watumishi wake wote wamepiga kambi mbugani; je ni sawa mimi niende nyumbani nikale na kunywa na kulala na mke wangu? Kama uishivyo na roho yako inavyoishi, sitafanya kitu cha namna hiyo.” 12Kisha, Daudi akamwambia Uria, “Basi, kaa hapa leo pia, na kesho nitakuacha urudi.” Hivyo Uria akabaki mjini Yerusalemu siku hiyo. Siku iliyofuata, 13Daudi alimwalika Uria kula na kunywa huko kwake, akamfanya Uria alewe. Hata hivyo, usiku ule Uria hakwenda nyumbani kwake, ila alilala kwenye kochi lake pamoja na watumishi wa bwana wake.
14Asubuhi yake, Daudi alimwandikia Yoabu barua akampa Uria aipeleke kwa Yoabu. 15Katika barua hiyo Daudi aliandika hivi: “Mweke Uria kwenye mstari wa mbele, mahali ambako mapigano ni makali kabisa, kisha umwache huko na kurudi nyuma ili apigwe, afe.” 16Basi, Yoabu alipokuwa anauzingira mji alimweka Uria mahali ambapo alijua wazi wanajeshi wa adui walikuwa hodari sana. 17Wakazi wa mji huo walitoka katika mji wao na kupigana na Yoabu. Baadhi ya watumishi wa Daudi, waliuawa. Uria Mhiti naye aliuawa pia. 18Kisha, Yoabu alipeleka habari zote kwa Daudi akimweleza juu ya vita. 19Yoabu akamwamuru huyo mtumishi aliyemtuma hivi, “Baada ya kumweleza mfalme mambo yote kuhusu vita, 20akikasirika na kukuuliza, ‘Kwa nini mlikwenda karibu na mji mlipokuwa mnapigana? Hamkujua kwamba wangewapiga mishale kutoka kwenye kuta za mji wao? 21Nani alimuua Abimeleki mwana wa Yerubeshethi? Si alikuwa mwanamke mmoja mjini Thebesi ambaye alitupa jiwe la kusagia kutoka kwenye ukuta nalo likamuua Abimeleki? Kwa nini basi, mlikwenda karibu na ukuta?’ Basi, wewe utamwambia hivi, ‘Hata mtumishi wako Uria Mhiti, naye amekufa.’”
22Yule mjumbe alikwenda kwa Daudi na kumwambia yote aliyotumwa na Yoabu ayaseme. 23Yule mjumbe akamwambia Daudi, “Adui zetu walituzidi nguvu, wakatoka nje ya miji na kutushambulia nyikani. Hata hivyo sisi tuliwarudisha mpaka kwenye lango la mji. 24Halafu wakatupiga mishale sisi watumishi wako kutoka ukutani. Baadhi ya watumishi wako waliuawa. Hata mtumishi wako Uria, Mhiti, naye amekufa.” 25Daudi akamwambia yule mjumbe, “Utamwambia hivi Yoabu, ‘Jambo hili lisikusumbue kwani upanga hauna macho, vita huua yeyote yule. Bali, imarisha mashambulizi dhidi ya mji, hadi umeuangamiza mji huo’. Ndivyo utakavyomtia moyo Yoabu.”
26Bathsheba mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe Uria amekufa, alimwombolezea mumewe. 27Muda wa matanga ulipokwisha, Daudi aliagiza Bathsheba achukuliwe na kupelekwa nyumbani kwake. Bathsheba akawa mke wa Daudi, naye akamzalia Daudi mtoto wa kiume. Lakini jambo hilo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi-Mungu.

2Samweli11;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.


No comments: