Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday 4 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli14...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Jehovah Nissi,Jehovah Jireh,
Jehovah Rapha,Jehovah Raah,Jehovah Shammah,Jehovah Shalom,
Emanueli-Mungu pamoja nasi...!!

Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah,
Uabudiwe Yahweh,Neema yako yatutosha Mungu wetu..!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Sifa na Utukufu ni wako ee Baba wa Mbinguni..!!


Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, ninaotamani sana kuwaoneni, nyinyi mlio furaha yangu na taji ya ushindi wangu, ndivyo basi mnavyopaswa kukaa imara katika kuungana na Bwana, enyi wapenzi wangu. Euodia na Suntike, nawaombeni na kuwasihi mpatane kama ndugu katika Bwana. Nawe ndugu yangu mwaminifu, nakutaka uwasaidie akina mama hao, kwani wamefanya kazi ya kueneza Injili kwa bidii pamoja nami na Klementi na wafanyakazi wenzangu wengine wote ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uhai. Basi, furahini daima katika kuungana na Bwana! Nasema tena: Furahini! Upole wenu ujulikane kwa watu wote. Bwana yu karibu. Msiwe na wasiwasi juu ya kitu chochote, ila kwa kila hali, mwombeni Mungu katika sala juu ya mahitaji yenu, kwa shukrani. Nayo amani ya Mungu ipitayo akili zote za watu italinda salama mioyo na akili zenu katika kuungana na Kristo Yesu. Hatimaye, ndugu zangu, zingatieni mambo mema na yanayostahili kusifiwa; mambo ya kweli na bora; mambo ya haki, safi, ya kupendeza na ya heshima. Tekelezeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu; mambo mliyosikia nimesema na kuona nimeyatenda. Naye Mungu anayetujalia amani atakuwa pamoja nanyi.

Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine..
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mfalme wa amani tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Jehovah utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika maisha yetu
Mungu Baba tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki tuingiapo/tutokapo..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki..
Jehovah tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Mungu wetu Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,Baba wa Mbinguni
ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Katika kuungana na Bwana nimepata furaha kubwa kwamba mwishoni mlipata tena fursa ya kuonesha kwamba mnanikumbuka. Kusema kweli mmekuwa mkinikumbuka daima ila tu hamkupata nafasi ya kuonesha jambo hilo. Sisemi hivyo sasa kwa sababu nahitaji kitu; maana nimejifunza kuridhika na vitu nilivyo navyo. Najua hali ya kutokuwa na vitu na hali ya kuwa na vingi. Nimejizoeza kuridhika katika kila hali na mahali; niwe nina cha kutosha au nina njaa; iwe nina ziada au nimepungukiwa. Naweza kuikabili kila hali kwani Kristo hunipa nguvu. Hata hivyo, nyinyi mlifanya vema kwa kushirikiana nami katika taabu zangu. Nyinyi Wafilipi mwafahamu wenyewe kwamba mwanzoni mwa kuhubiri Habari Njema, nilipokuwa naondoka Makedonia, nyinyi peke yenu ndio kanisa lililonisaidia; nyinyi peke yenu ndio mlioshirikiana nami katika kupokea na kuwapa wengine mahitaji. Nilipokuwa nahitaji msaada kule Thesalonike mliniletea, tena zaidi ya mara moja. Sio kwamba napenda tu kupokea zawadi; ninachotaka ni faida iongezwe katika hazina yenu. Basi, nimekwisha pokea vitu vyote mlivyonipa, tena ni zaidi kuliko nilivyohitaji. Nina kila kitu kwa vile sasa Epafrodito amekwisha niletea zawadi zenu. Zawadi hizi ni kama tambiko yenye harufu nzuri, sadaka inayokubaliwa na kumpendeza Mungu. Basi, Mungu wangu, kwa utajiri wake mkuu kwa njia ya Kristo, atawapeni mahitaji yenu yote. Utukufu uwe kwa Mungu wetu na Baba yetu, milele na milele. Amina.


Mungu wetu tazama wenye shida/tabu Mfalme wa Amani amani yako ikatawale kwa wote wenye hofu/mashaka..
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako mwenye nguvu na ukawaponya
walio wagonjwa,Yahweh ukawape uvumilivu wanaowauguza..
Mungu wetu ukawatendee wenye njaa,Baba wa Mbinguni ukabariki mashamba/vyanzo vyao Yahweh wakapate chakula cha kutosha kuweka akiba na kusaidia wengine...
Baba wa Mbinguni ukawaweke huru wale walio katika vifungo vya yule mwovu..
Mungu wetu ukawatendee walio magerezani pasipo na hatia
Mungu wetu haki ikatendeke..
Yahweh ukawavushe salama wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Jehovah ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru..
Mungu wetu ukawe mafariji kwa wafiwa,Baba wa Mbinguni ukawe tumaini kwa wote waliokata tamaa,waliokataliwa
Mfalme wa Amani tunaomba ukapokee sala/maombi yetu..


Nawasalimu watu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami hapa wanawasalimuni. Watu wote wa Mungu hapa, na hasa wale walio katika ikulu ya mfalme, wanawasalimuni. Nawatakieni nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.
kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami..
Rehema/neema za Mungu ziwe nanyi daima..
Nawapenda.

Kitendo cha ujasiri cha Yonathani

1Siku moja, Yonathani mwana wa mfalme Shauli alimwambia kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende ngambo kwenye ngome ya Wafilisti.” Lakini Yonathani hakumwambia baba yake. 2Shauli alikuwa amepiga kambi chini ya mkomamanga huko Migroni, nje ya mji wa Gibea, akiwa pamoja na watu wapatao 600. 3Ahiya, mwana wa Ahitubu ndugu yake Ikabodi mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi-Mungu mjini Shilo, alikuwa ndiye aliyevaa kizibao cha kuhani. Watu hawakujua kwamba Yonathani amekwisha ondoka.
4Kwenye kipito ambako Yonathani alipaswa apitie ili afike kwenye ngome ya Wafilisti, kulikuwa na miamba miwili iliyochongoka, upande huu na upande mwingine. Mwamba mmoja uliitwa Bosesi na mwingine uliitwa Sene. 5Mwamba mmoja ulikuwa kaskazini mwa mji wa Mikmashi na mwingine ulikuwa kusini mkabala na mji wa Gibea.
6Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende upande wa pili kwenye ile ngome ya hawa watu wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi-Mungu akatusaidia, maana Mwenyezi-Mungu haokoi kwa kutegemea wingi au uchache wa watu.”
7Yule kijana aliyembebea silaha akamwambia, “Fanya chochote unachotaka kufanya,14:7 chochote unachotaka kufanya: Makala ya Kiebrania: Chochote unachotaka kufanya. Geuka. mimi niko pamoja nawe kwani wazo lako ndilo wazo langu.”14:7 kwani … langu, Septuaginta: Makala ya Kiebrania haina sehemu hii. 8Yonathani akamwambia, “Tutavuka kuwaendea wale watu ili wapate kutuona. 9Kama wakituambia tuwangoje, hadi waje hapa tulipo basi, tutasimama papa hapa na wala hatutawaendea. 10Lakini wakisema sisi tuwaendee, basi tutawaendea kwani hiyo itakuwa ni ishara kuwa Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwetu.” 11Basi, wakajitokeza ili Wafilisti wawaone. Wafilisti walipowaona wakasema, “Angalieni wale Waebrania wanatoka kwenye mashimo walimokuwa wamejificha.” 12Wafilisti waliokuwa kwenye ngome wakamwita Yonathani na kijana aliyembebea silaha, “Njoni huku kwetu, nasi tutawaonesha kitu.”
Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Nifuate; Mwenyezi-Mungu amewatia mikononi mwa Israeli.” 13Basi, Yonathani akapanda kwa miguu na mikono, na yule kijana akamfuata. Yonathani aliwashambulia Wafilisti akiwaangusha chini huku yule kijana alifuata nyuma akiwaua. 14Katika mashambulizi hayo ya kwanza Yonathani, akiwa pamoja na kijana wake aliyembebea silaha, aliwaua watu kama ishirini katika eneo la nchi lipatalo nusu eka. 15Katika nchi nzima ya Wafilisti, wote walianza kufadhaika, wanajeshi kambini, watu mashambani, kwenye ngome, hata na washambuliaji walitetemeka; nchi ilitetemeka, na kulikuwa na woga mkubwa.

Kushindwa kwa Wafilisti

16Wapelelezi wa Shauli huko Gibea katika nchi ya Benyamini waliwaona watu wengi wakikimbia huku na huko. 17Shauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, “Hebu jihesabuni ili kujua ni akina nani waliotutoroka.” Walipojihesabu, waligundua kuwa Yonathani na kijana aliyembebea silaha walikuwa hawapo. 18Shauli akamwambia kuhani Ahiya, “Lilete hapa sanduku la Mungu.” (Wakati huo sanduku la agano la Mungu lilikuwa pamoja na Waisraeli.) 19Shauli alipokuwa anaongea bado na kuhani, ghasia kambini kwa Wafilisti ziliongezeka zaidi na zaidi. Kwa hiyo Shauli akamwambia kuhani, “Acha; usililete tena sanduku la agano.” 20Hivyo, Shauli na watu wake wakajipanga na kuingia vitani dhidi ya Wafilisti. Lakini Wafilisti walianza kushambuliana wenyewe kwa wenyewe kwa mvurugiko mkubwa. 21Waebrania waliokuwa upande wa Wafilisti, na waliokwenda nao huko kambini, wakageuka na kujiunga na Waisraeli waliokuwa pamoja na Shauli na Yonathani. 22Hata Waisraeli wengine waliokuwa wamejificha kwenye nchi ya milima ya Efraimu, waliposikia kuwa Wafilisti walikuwa wanakimbia, nao pia wakawafuatia na kuwapiga.
23Hivyo Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli ushindi.

Matukio baada ya vita

Vita vilienea mpaka kupita Beth-aveni. 24Siku ile, Waisraeli walisumbuliwa sana maana Shauli alikuwa amewaapisha watu, “Mtu yeyote atakayekula chakula kabla jua kutua, na kabla sijajilipiza kisasi cha adui zangu, na alaaniwe.” Hivyo, siku yote, hakuna mtu aliyeonja chakula chochote. 25Watu wote14:25 watu wote: Makala ya Kiebrania: Nchi yote. walipofika sehemu yenye msitu, walikuta asali kila mahali. 26Ingawa watu walipofika msituni na kukuta asali ikidondoka kila mahali hakuna mtu aliyethubutu kula asali hiyo kwa kuogopa kile kiapo walichoapishwa. 27Lakini Yonathani hakuwa amesikia baba yake alipowaapisha watu. Hivyo akainyosha fimbo aliyokuwa nayo, akaichovya kwenye sega la asali, akala asali hiyo. Hapo akajisikia kuwa na nguvu. 28Mtu mmoja akamwambia, “Baba yako aliwaapisha watu vikali, akisema, ‘Mtu yeyote atakayekula chakula leo na alaaniwe.’” Nao watu walikuwa hoi kwa njaa. 29Yonathani akajibu, “Baba yangu anawasumbua watu. Sasa mimi najisikia kuwa na nguvu kwa kuwa nimeonja asali hii kidogo. 30Kama tu askari wetu wangeweza kula kidogo kutoka nyara walizoteka kutoka kwa adui zao, wengi zaidi wa Wafilisti wangaliuawa.”
31Siku ile, Waisraeli waliwapiga Wafilisti, tangu Mikmashi mpaka Aiyaloni. Wakati huu Waisraeli walikuwa wamechoka kwa njaa. 32Basi walikimbilia nyara walizoteka, wakawachukua wanakondoo, fahali na ndama, wakachinja, wakala nyama na damu. 33Watu wengine wakamwambia Shauli, “Tazama watu wanatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu kwa kula nyama yenye damu.” Shauli akawaambia watu, “Nyinyi ni wahaini. Vingirisheni jiwe kubwa hapa14:33 hapa: Septuaginta: Makala ya Kiebrania: Leo. kwangu.” 34Akawaambia, “Nendeni mkawaambie watu wote walete ng'ombe na kondoo wao hapa, wawachinje na kuwala hapa. Wasitende dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, kwa kula nyama yenye damu.” Hivyo, usiku ule wote walipeleka ng'ombe wao na kuwachinjia hapo. 35Basi, Shauli akamjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu. Hiyo ilikuwa ndiyo madhabahu ya kwanza ambayo Shauli alimjengea Mwenyezi-Mungu.
36Kisha Shauli akawaambia watu, “Twendeni tukawafuatie Wafilisti usiku, tukawavamie na kupora mali zao mpaka asubuhi; hatutamwacha mtu yeyote hai.” Watu wakamwambia, “Fanya unachoona kuwa chema kwako.” Lakini kuhani akawaambia, “Kwanza tuombe shauri kwa Mwenyezi-Mungu.”
37Hivyo, Shauli akamwuliza Mungu, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Waisraeli?” Lakini Mungu hakujibu kitu siku hiyo. 38Shauli akasema, “Njoni hapa enyi viongozi wa watu, tujue ni dhambi gani tumetenda leo. 39Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai na ambaye huiokoa Israeli, hata kama ni mwanangu Yonathani, lazima auawe.” Lakini hakuna mtu aliyesema neno. 40Hivyo, Shauli akawaambia, “Nyinyi nyote simameni upande ule, halafu mimi na Yonathani mwanangu tutasimama upande huu.” Wao wakajibu, “Fanya chochote unachoona kinafaa.” 41Shauli akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, kwa nini hujanijibu mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu wa Israeli, ikiwa hatia iko kwangu au kwa Yonathani mwanangu, basi, amua kwa jiwe la kauli ya Urimu. Lakini ikiwa hatia hiyo iko kwa watu wako wa Israeli, amua kwa jiwe la kauli ya Thumimu.” Yonathani na Shauli walipatikana kuwa na hatia, lakini watu walionekana hawana hatia. 42Shauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Yonathani akapatikana kuwa na hatia. 43Ndipo Shauli akamwambia Yonathani, “Niambie ulilofanya.” Yonathani akajibu, “Nilikula asali kidogo kwa kutumia fimbo yangu. Niko hapa na niko tayari kufa.” 44Shauli akasema, “Mungu na anitendee mimi vivyo hivyo na hata na wengine. Yonathani ni lazima utauawa.”
45Lakini watu wakamwambia Shauli, “Mbona Yonathani aliyeiletea Israeli ushindi huu mkubwa, auawe? Jambo hilo liwe mbali. Twaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, hata unywele wa kichwa chake hautaanguka chini. Alichokifanya leo, amekifanya kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu.” Hivyo, watu walimkomboa Yonathani naye hakuuawa.
46Kisha Shauli aliacha kuwafuatia Wafilisti, nao Wafilisti wakarudi makwao.

Utawala wa Shauli na jamaa yake

47Baada ya Shauli kuwa mfalme wa Israeli, alipigana na adui zake kila upande: Wamoabu, Waamoni, Waedomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Kila alipopigana vita, alishinda. 48Alipigana kwa uhodari, akawashinda Waamaleki. Aliwaokoa Waisraeli kutoka kwa watu wote waliowashambulia.
49Watoto wa kiume wa Shauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-shua. Binti zake walikuwa wawili; mzaliwa wa kwanza aliitwa Merabu na mdogo aliitwa Mikali. 50Mkewe Shauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Kamanda wa jeshi la Shauli aliitwa Abneri, mwana wa Neri, mjomba wa Shauli. 51Baba wa Shauli alikuwa Kishi na baba wa Abneri alikuwa Neri mwana wa Abieli.
52Kulikuwa na mapigano makali dhidi ya Wafilisti muda wote Shauli alipokuwa mfalme; na kila mara Shauli alipompata mtu mwenye nguvu au shujaa alimchukua ajiunge na jeshi.


1Samweli14;1-52

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: