Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday 15 December 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Ruthu 4...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..! Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu Baba yetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mungu mwenye nguvu,Baba wa upendo,Baba wa Yatima,Mungu wa Wajane
Mungu wa walio hai,Muweza wa yote,Kimbilio letu,Mungu uponyaye
Unastahili sifa Baba wa Mbinguni,Unastahili kuabudiwa Mungu wetu,
Unastahili kuhimidiwa Jehovah,Unastahili kutukuzwa Yahweh..

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakatiwote..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwa nguvu zetu wala si kwa utashi wetu,si kwamba sisi ni wema sana
si kwa akili zetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Jehovah ni kwa neema/rehema zako ni kwa mapenzi yako Mungu wetu
Sifa na Utukufu tunakuridishia wewe...!!

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na 
kujiachilia mikononi mwako Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mfalme wa amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukose..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya Mwanao Mpendwa
Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza
ili sisi tupate kupona..



“Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu; kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu. Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako? Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyomo jichoni mwako na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako. “Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua nyinyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.


Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Jehovah tunaomba
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji Baba wa Mbinguni
tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yhaweh nasi utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Mfalme wa Amani tunaomba utusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe kama inavyokupendeza wewe..


Maana, yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye mlango hufunguliwa. Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe? Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka? Kama basi nyinyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: Atawapa mema wale wanaomwomba. “Yote mnayotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndiyo maana ya sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Jehovah tunaomba
ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na 
wote wanaotuzunguka Mungu wetu tunaomba amani yako ikatawale
upendo wetu ukadumu kati yetu,Yahweh tunaomba ulinzi wako
kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki Mungu wetu ukatamalaki na 
kutuatamia,Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako,Jehovah
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Mungu wetu ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi. Lakini njia inayoongoza kwenye uhai ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
Mungu wetu tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Yahweh tunaomba ukawaponye wagonjwa na ukawape uvumilivu ,nguvu na moyo wote wanaouguza,Baba wa Mbinguni wakawape chakula wenye njaa..
Jehovah tunaomba ukawafungue na kuwaweka huru wote walio
katika vifungo vya yule mwovu,Mungu wetu ukawe tumaini kwa wote
waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka Mungu wetu
ukaonekane na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..


“Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali. Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La! Basi, mti mzuri huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni. Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.

kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu wetu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na 
mapenzi yake,Amani ikatawale katika maisha yenu..
Nawapenda.





Boazi anamwoa Ruthu

1Boazi alikwenda mahali pa kufanyia mkutano huko kwenye lango la mji akaketi chini. Kisha yule ndugu ya Elimeleki ambaye Boazi alikuwa amemtaja, akapita karibu na hapo. Boazi akamwita, akasema, “Njoo, uketi hapa ndugu.” Basi huyo mtu akaja na kuketi hapo. 2Ndipo Boazi akawaita wazee kumi wa mji, akawaomba wao pia waketi hapo. Wakaketi. 3Ndipo Boazi akamwambia yule ndugu yake, “Sasa Naomi ambaye amerudi kutoka Moabu, anataka kuliuza shamba ambalo lilikuwa la jamaa yetu Elimeleki. 4Basi mimi nimeona afadhali nikujulishe habari hii. Sasa ikiwa unalitaka shamba hili, toa fidia ulichukue mbele ya wazee wa watu wangu. Ikiwa unalitaka au hulitaki sema basi kwa kuwa nafasi ya kwanza ya kulifidia ni yako na yangu ni ya pili.” Naye akasema, “Mimi nitalifidia.”
5Boazi akasema, “Ni vyema, lakini ukilichukua hilo shamba kutoka kwa Naomi, basi utakuwa unamchukua pia Ruthu Mmoabu, mjane ambaye ni jamaa ya marehemu ili kwamba shamba hilo libaki katika jamaa ya huyo marehemu.”
6Yule jamaa aliyekuwa wa karibu akajibu, “Ikiwa ni hivyo, sitalifidia shamba hilo, kwa sababu yaonekana kuwa nitauharibu urithi wangu. Afadhali haki yangu ya kulichukua nikupe wewe, maana mimi siwezi kulifidia.” 7Siku zile, katika Israeli ikiwa watu walitaka kukomboa au kubadilishana kitu, ilikuwa ni desturi kwa mtu kuonesha ishara kwa kuvua kiatu chake na kumpa mwingine. Kwa ishara hiyo Waisraeli walionesha kwamba mambo yamesawazishwa.
8Basi, mtu huyo alimwambia Boazi, “Lifidie shamba,” kisha alivua kiatu chake na kumpa. 9Ndipo Boazi akawaambia wazee na watu waliokuwa hapo, “Leo nyinyi ni mashahidi wangu. Mmeona kwamba nimenunua kutoka kwa Naomi, vyote vilivyokuwa vya Elimeleki, na vya Kilioni na Mahloni. 10Zaidi ya hayo, Ruthu Mmoabu mjane wa Mahloni, nimemnunua ili awe mke wangu. Mapatano haya yatafanya mali ya jamaa ya marehemu na ukoo wake kubakia kwa watu wake katika mji huu. Nyinyi ni mashahidi.”
11Basi wazee waliokuwa langoni na watu wote waliokuwapo walijibu, “Ndiyo, sisi ni mashahidi. Mwenyezi-Mungu amfanye mke wako awe kama Raheli na Lea, ambao wote wawili waliijenga nyumba ya Israeli. Nawe upate kustawi katika jamaa ya Efratha, uwe na sifa katika Bethlehemu. 12Kwa sababu ya watoto Mwenyezi-Mungu atakaokupatia ambao mwanamke huyu atakuzalia, nayo nyumba yako iwe kama nyumba ya Peresi ambaye Tamari alimzalia Yuda.”

Boazi na vizazi vyake

13Kwa hiyo, Boazi akamchukua Ruthu akawa mke wake. Mwenyezi-Mungu alimjalia Ruthu naye akachukua mimba, akajifungua mtoto wa kiume. 14Ndipo wanawake wa mji huo wakamwambia Naomi, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye hakukuacha leo bila kuwa na jamaa aliye karibu wa kukutunza; naye awe mwenye sifa kubwa katika Israeli. 15Yeye atakurudishia uhai wako na atakutunza katika uzee wako; maana mkwe wako anayekupenda ambaye ana thamani kubwa zaidi kwako kuliko watoto wa kiume saba, ndiye amemzaa.” 16Basi Naomi alimchukua mtoto huyo akamweka kifuani mwake na kumlea.
17Wanawake majirani walimwita mtoto huyo Obedi wakisema, “Mtoto amezaliwa kwa Naomi.” Hatimaye Obedi akamzaa Yese aliyemzaa Daudi.
18Na hivi ndivyo vizazi vya Peresi: Peresi alimzaa Hesroni, 19Hesroni akamzaa Rami, Rami akamzaa Aminadabu, 20Aminadabu akamzaa Nahshoni, Nahshoni akamzaa Salmoni, 21Salmoni akamzaa Boazi, Boazi akamzaa Obedi, 22Obedi akamzaa Yese na Yese akamzaa Daudi.


Ruthu4;1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: