Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 22 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 8...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mtakatifu..!Mtakatifu.!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni.
Tunakushukuru na kukusifu Dima...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa pumzi/uzima afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu

Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Yahweh
Uabudiwe Jehovah,Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya
ajabu,Hakuna kama wewe Mngu wetu,wewe ni mwamnzo na wewe
ni mwisho,Alfa na Omega,Mungu mwenye nguvu,Unatosha Yahweh..!

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Jehovah..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote walio tukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Yahweh utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah tunaomba utufunike kwa Damu ya mwanao mpendwa
Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti
kwakupigwa kwake sisi tumepata kupona..


Mungu amemfufua katika wafu Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ni Mchungaji Mkuu wa kondoo kwa sababu ya kumwaga damu yake iliyothibitisha agano la milele. Mungu wa amani awakamilishe katika kila tendo jema ili mtekeleze matakwa yake; yeye na afanye ndani yetu kwa njia ya Kristo yale yanayompendeza mwenyewe. Utukufu uwe kwake, milele na milele! Amina.

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Baba ukatupe
ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji nasi tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye
kuhitaji,Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto/wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwavyote
tunavyovimiliki,Mungu wetu ukatamalaki na kutuatamia,
Yahweh ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukawe na kiu ya
kukutafuta zaidi,Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya kusimamia
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Jehovah ukatupe amani ya moyo,utuwema,upendo,furaha,busara,
hekima na kuchukuliana..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze na tukawe na kiasi..


Nilimngojea Mwenyezi-Mungu kwa uvumilivu, akanielekea na kukisikia kilio changu. Aliniondoa katika shimo la hatari, alinitoa katika matope ya dimbwi, akanisimamisha salama juu ya mwamba, na kuziimarisha hatua zangu. Alinifundisha wimbo mpya, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu. Heri mtu anayemtumainia Mwenyezi-Mungu; mtu asiyejiunga na watu wenye majivuno, watu waliopotoka kwa kuabudu miungu ya uongo. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umetufanyia mengi ya ajabu, na mipango yako juu yetu haihesabiki; hakuna yeyote aliye kama wewe. Kama ningeweza kusimulia hayo yote, idadi yake ingenishinda. Wewe hutaki tambiko wala sadaka, tambiko za kuteketeza wala za kuondoa dhambi; lakini umenipa masikio nikusikie. Ndipo niliposema: “Niko tayari; ninayotakiwa kufanya yameandikwa katika kitabu cha sheria; kutimiza matakwa yako, ee Mungu wangu ni furaha yangu, sheria yako naishika kwa moyo wangu wote!” Nimesimulia habari njema za ukombozi, mbele ya kusanyiko kubwa la watu. Kama ujuavyo ee Mwenyezi-Mungu, mimi sikujizuia kuitangaza. Sikuuficha moyoni mwangu ukombozi ulionijalia, nimetangaza daima kuwa wewe ni mwokozi mwaminifu; sikulificha kusanyiko kubwa la watu fadhili zako na uaminifu wako. Ee Mwenyezi-Mungu, usininyime huruma yako! Fadhili zako na uaminifu wako vinihifadhi daima.

Baba wa Mbinguni leo tunarudisha Utukufu,sifa na shukrani kwa yote
ambayo tumekuomba na umetutendea,wema na fadhili zako
zadumu,Tutashangilia na kufurahia fadhili zako,Maana
wewe unaona dhiki za watoto wako na unajua hata taabu za nafsi
zetu,Utushibishe fadhili zako asubuhi,tushangilie na kufurahi maisha
yetu yote,Fadhili zako zipo mbele ya macho yetu,tunaishi kutokana
na uaminifu wako,Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi, na uaminifu
wako nyakati za usiku,Baba tunaomba uendelee kuwagusa na kuwatendea
wote wanaopitia majaribu mbalimbali,shida/tabu,watoto wako
wanaokutafuta kwa bidii na imani...


Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu; nafsi yangu yote ilisifu jina lake takatifu! Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu! Usisahau kamwe wema wake wote. Ndiye anayenisamehe uovu wangu wote, na kuniponya magonjwa yote. Ndiye aniokoaye kutoka kifoni, na kunijalia rehema na fadhili zake. Ndiye anayeniridhisha mema maisha yangu yote, hata nabaki kijana mwenye nguvu kama tai. Mwenyezi-Mungu huhukumu kwa haki; huwajalia wanaodhulumiwa haki zao. Alimjulisha Mose mwongozo wake, aliwaonesha watu wa Israeli matendo yake. Mwenyezi-Mungu ni mwenye rehema na huruma; ni mvumilivu na mwingi wa fadhili. Hatukemeikemei daima, wala hasira yake haidumu milele. Yeye hatuadhibu kama tunavyostahili; hatulipizi kadiri ya uovu wetu. Kama vile anga lilivyo juu mbali na dunia, ndivyo ulivyo mwingi wema wake kwa watu wanaomcha. Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo azitengavyo dhambi zetu mbali nasi. Kama vile baba amhurumiavyo mwanawe, ndivyo Mwenyezi-Mungu awahurumiavyo wote wamchao. Mungu ajua mfumo wa nafsi zetu; ajua kwamba sisi ni mavumbi. Walakini binadamu, maisha yake ni kama nyasi tu; huchanua kama ua shambani: Upepo huvuma juu yake nalo latoweka; na mahali lilipokuwa hapaonekani tena. Lakini fadhili za Mwenyezi-Mungu hudumu milele, kwa wale wote wanaomheshimu; na wema wake wadumu vizazi vyote, kwa wote wanaozingatia agano lake, wanaokumbuka kutii amri zake. Mwenyezi-Mungu ameweka kiti chake cha enzi mbinguni; yeye anatawala juu ya vitu vyote. Enyi malaika wakuu, msifuni Mwenyezi-Mungu; mnaotimiza amri zake na kutekeleza neno lake! Enyi jeshi lote la mbinguni, msifuni Mwenyezi-Mungu; enyi watumishi wake mnaotekeleza matakwa yake! Msifuni Mwenyezi-Mungu enyi viumbe vyake vyote; msifuni popote mlipo katika milki yake. Ee nafsi yangu, umsifu Mwenyezi-Mungu!

Kwa imani tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami..
Mungu awe nanyi na Amani,upendo,furaha viwe nanyi daima..
Mungu wetu akawatendee kama inavyompendeza yeye..
Damu ya Kristo Yesu ikawafunike..
Nawapenda.

Wamidiani wanashindwa kabisa

1Watu wa kabila la Efraimu wakamwuliza Gideoni, “Kwa nini umetutendea hivyo? Kwa nini hukutuita ulipokwenda kupigana na Wamidiani?” Wakamlaumu kwa ukali.
2Lakini Gideoni akawajibu, “Mambo niliyofanya mimi si kitu kabisa kama yakilinganishwa na yale mliyoyafanya nyinyi. Walichookota watu wa Efraimu baada ya mavuno ni chema na kizuri kuliko mavuno ya jamaa yangu ya Abiezeri. 3Mungu amewatia mikononi mwenu wakuu wa Midiani, Orebu, na Zeebu. Je, mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni alipokwisha sema hivyo, hasira yao dhidi yake ikatulia.
4Gideoni na wenzake 300 wakafika Yordani, wakavuka. Ingawa walikuwa wamechoka sana, waliendelea kuwafuatia adui zao.
5Basi, akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali wapeni wenzangu hawa mikate maana wamechoka sana; nami bado ninaendelea kuwafuatia wafalme Zeba na Salmuna wa Midiani.”
6Lakini viongozi wa Sukothi wakamwuliza, “Kwa nini tuwape mikate nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?”
7Gideoni akawaambia, “Sawa, lakini Mwenyezi-Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mikononi mwangu, nitaichanachana miili yenu kwa miiba na mbigili za jangwani.”
8Kutoka huko akawaendea watu wa Penueli, akawaomba namna ileile. Nao watu wa Penueli wakamjibu kama walivyomjibu watu wa Sukothi. 9Gideoni akawaambia, “Nitakaporudi kwa amani nitaubomoa mnara huu.”
10Zeba na Salmuna walikuwa huko Karkori pamoja na jeshi lao la watu 15,000 ambao ndio tu waliobaki kutoka jeshi la mashariki, maana wenzao 120,000 waliuawa. 11Gideoni akafuata njia ya magharibi iliyo mashariki mwa Noba na Yogbeha, akalishambulia jeshi hilo ambalo halikuwa tayari. 12Wafalme wa Midiani, Zeba na Salmuna walitoroka wakakimbia, lakini Gideoni aliwafuatia, akawakamata na kulitia jeshi lote hofu kubwa.
13Kisha, Gideoni, mwana wa Yoashi, akarudi kutoka vitani akipitia kwenye mteremko wa Heresi. 14Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumhoji. Kijana huyo akamwandikia majina ya viongozi na wazee mashuhuri wa Sukothi, jumla yao watu sabini na saba. 15Gideoni akarudi kwa watu wa Sukothi, akawaambia, “Si mtakumbuka mlivyonitukana mliposema, ‘Kwa nini tuwape mikate watu wako waliochoka sana nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?’ Haya basi, Zeba na Salmuna ndio hawa.” 16Basi, akawachukua wazee wa Sukothi na kuwapa funzo wanaume wote kwa kuichana miili yao kwa miiba na mbigili. 17Vilevile akaubomoa mnara wa Penueli na kuwaua wakazi wa mji huo.
18Kisha, akawauliza Zeba na Salmuna, “Watu wale mliowaua huko Tabori walikuwaje?” Wakamjibu, “Walifanana na wewe, maana walionekana kama wana wa mfalme.” 19Naye akawaambia, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu mzazi. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kama msingewaua, hata mimi nisingewaua.” 20Kisha akamwambia Yetheri, mzaliwa wake wa kwanza, “Simama, uwaue.” Lakini Yetheri aliogopa kuchukua upanga wake maana alikuwa bado kijana. 21Hapo Zeba na Salmuna wakasema, “Tuue wewe mwenyewe, maana hii ni kazi ya mtu mzima.” Gideoni akawaua yeye mwenyewe na kuchukua mapambo yao yaliyokuwa shingoni mwa ngamia wao.
22Kisha, Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Wewe na uwe mtawala wetu, na baada yako watutawale wazawa wako, kwa kuwa wewe umetukomboa kutoka kwa Wamidiani.” 23Gideoni akawajibu, “Mimi sitakuwa mtawala wenu wala mwanangu hatakuwa mtawala wenu. Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekuwa mtawala wenu.” 24Kisha akawaambia, “Ningependa kuwaomba kitu kimoja; naomba kila mmoja wenu anipe vipuli mlivyoteka nyara.” Wale Wamidiani kwa vile walikuwa Waishmaeli, walivaa vipuli vya dhahabu. 25Watu wakamjibu, “Tutakupa kwa hiari.” Wakatandaza nguo na kila mmoja akatupa humo vipuli walivyokuwa wameteka nyara. 26Uzito wa vipuli vyote alivyowataka wampe ulikuwa kilo ishirini. Zaidi ya hivyo, alipokea pia herini, mavazi ya urujuani yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani na mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao. 27Gideoni akazitumia kutengenezea kizibao ambacho alikiweka kwenye mji wake wa Ofra. Waisraeli wote wakaenda huko kukiabudu. Kizibao hicho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake. 28Basi, Wamidiani walishindwa kabisa wasiwe tishio kwa Israeli; na nchi ya Israeli ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini.

Kifo cha Gideoni

29Gideoni, yaani Yerubaali, mwana wa Yoashi akarudi nyumbani kwake na kukaa huko. 30Gideoni alikuwa na watoto wa kiume sabini, maana alioa wanawake wengi. 31Alikuwa na suria huko Shekemu ambaye alimzalia mtoto wa kiume, jina lake Abimeleki. 32Gideoni, mwana wa Yoashi, akafariki akiwa na umri mkubwa, akazikwa katika kaburi la Yoashi, baba yake, kwenye mji wa Ofra wa Wabiezeri.
33Mara baada ya kifo cha Gideoni, Waisraeli wakairudia miungu ya Baali na kuiabudu. Wakamfanya Baal-berithi kuwa mungu wao. 34Waisraeli wakamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, aliyewakomboa kutoka kwa maadui zao wengi waliowazunguka kila upande. 35Tena, hawakuitendea wema jamaa ya Yerubaali yaani Gideoni kwa mema yote aliyoyatenda katika Israeli.


Waamuzi 8;1-35

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: