Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 27 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 11...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu ametuchagua na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu
na Nchi,Muumba wa vyote vilivyomo,vinavyoonekana na visivyooneka
Muweza wa yote,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe Daima,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni
Uabudiwe Jehovah,Hakuna kama wewe Yahweh,Matendo yako ni 
makuu mno,Matendo yako ni ya ajabu,Unatosha Ee Mungu wetu..!



Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa). Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: “Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!” Yesu aliposikia hivyo, akasema, “Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe.” Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi. Kisha akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni tena Yudea!” Wanafunzi wakamwambia, “Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?” Yesu akajibu, “Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu. Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake.” Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha.” Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, ikiwa amelala, basi atapona.” Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro. Basi, Yesu akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa; lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake.” Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, “Twendeni nasi tukafe pamoja naye!”

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari katika majukumu yetu
Sifa na Utukufu ni wako Baba wa Mbinguni...!!


Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne. Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu, umbali upatao kilomita tatu. Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao. Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani. Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa! Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.” Yesu akamwambia, “Kaka yako atafufuka.” Martha akamjibu, “Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho.” Yesu akamwambia, “Mimi ndimi ufufuo na uhai. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi; na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?” Martha akamwambia, “Ndiyo Bwana! Mimi naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.”


Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Yahweh..
Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Ee Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu Jehovah
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba 
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwambia faraghani, “Mwalimu yuko hapa, anakuita.” Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu. Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki. Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza. Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwambia, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!” Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni. Kisha akawauliza, “Mlimweka wapi?” Wakamwambia, “Bwana, njoo uone.” Yesu akalia machozi. Basi, Wayahudi wakasema, “Tazameni jinsi alivyompenda!” Lakini baadhi yao wakasema, “Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?”

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu Mungu wetu
ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji Yahweh nasi
tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye
kuhitaji..Yahweh tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah
tunaomba utupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa Amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Yahweh tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote
tunavyovimiliki,Mungu wetu  Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
ukatupe neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na 
sheria zako siku zote za maisha yetu,tukanene yaliyo yako,ukatupe
macho ya rohoni masikio ya kusikia sauti yako na kutii..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe. Yesu akasema, “Ondoeni hilo jiwe!” Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, “Bwana, amekwisha anza kunuka; amekaa kaburini siku nne!” Yesu akamwambia, “Je, sikukuambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?” Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, “Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza. Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma.” Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: “Lazaro! Toka nje!” Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, “Mfungueni, mkamwache aende zake.”



Tazama wenye shida na tabu Mungu wetu,wagonjwa,wenye njaa,
waliokatika vifungo vya yule mwovu,wanaopitia magumu/majaribu
mbalimbali,waliokata tamaa,waliokataliwa,waliokwenda kinyume nawe
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba ukawaokoe na kuwavusha,Mungu wetu ukawaponye kimwili na kiroho
Baba ukawape chakula na ukabariki mashamba yao,Yahweh ukawasamehe
na kuwaongoza,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Jehovah ukawape
neema ya kujiombea na kufuata njia zako,wafiwa ukawe mfariji wao..
Baba ukapokee sala/maombi yetu,ukasikie kuomba kwetu na ukawatendee
sawasawa na mapenzi yako..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako tukiamini  na kukushukuru
 Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nayi Daima..
Nawapenda.



1Huko Gileadi kulikuwa na mpiganaji hodari aitwaye Yeftha, mwana wa mama mmoja malaya, na baba yake aliitwa Gileadi. 2Gileadi alikuwa pia na wana wengine kwa mke wake wa halali. Watoto wa mke huyo walipokuwa wakubwa, walimfukuza Yeftha kutoka nyumbani, wakamwambia, “Wewe huna haki ya kupata urithi kutoka kwa baba yetu, maana wewe ni mtoto wa mwanamke mwingine.” 3Basi, Yeftha akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu. Huko watu ovyo wakakusanyika kujiunga naye, wakamfuata katika safari zake za mashambulio.
4Baada ya muda fulani, Waamoni waliwashambulia Waisraeli. 5Wakati vita vilipopamba moto, wazee wa Gileadi wakaenda kumleta Yeftha kutoka nchi ya Tobu, 6wakamwambia, “Njoo utuongoze katika vita vyetu na Waamoni.” 7Lakini Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Je, si mlinichukia hata mkanifukuza kutoka kwa jamaa ya baba yangu? Kwa nini mnanijia sasa mkiwa katika taabu?” 8Hao wazee wa Gileadi wakamwambia “Ndio maana tumekujia ili uende nasi kupigana na Waamoni, nawe utakuwa kiongozi wetu na wa wakazi wote wa Gileadi.” 9Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Kama mkinirudisha nyumbani kupigana na Waamoni halafu Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu, mimi nitakuwa kiongozi wenu.” 10Wale wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, “Mwenyezi-Mungu atakuwa shahidi kati yetu. Hakika tutafanya kama ulivyosema.” 11Yeftha akafuatana na wazee wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi wao. Yeftha akasema masharti yake huko Mizpa mbele ya Mwenyezi-Mungu
12Yeftha akapeleka ujumbe kwa mfalme wa Amoni akamwambia, “Una ugomvi gani nasi hata uje kuishambulia nchi yetu?” 13Mfalme wa Amoni akawajibu hao wajumbe, “Waisraeli walipotoka Misri, walichukua nchi yangu kutoka mto Arnoni hadi mto Yaboki na mto Yordani. Sasa nirudishie nchi hiyo kwa amani.”
14Yeftha akatuma tena wajumbe kwa mfalme wa Amoni 15wamwambie kwa niaba yake, “Waisraeli hawakuchukua nchi ya Wamoabu wala nchi ya Waamoni. 16Lakini Waisraeli walipotoka Misri, walisafiri jangwani hadi bahari ya Shamu mpaka Kadeshi. 17Kisha Waisraeli wakatuma wajumbe kwa mfalme wa Edomu wakimwomba awaruhusu kupita katika nchi yake, lakini mfalme wa Edomu akakataa. Basi wakamwomba ruhusa mfalme wa Moabu naye pia akakataa. Kwa hiyo Waisraeli wakabaki Kadeshi. 18Kisha wakasafiri wakipitia jangwani kuzunguka nchi ya Edomu na Moabu mpaka walipofika upande wa mashariki wa Moabu, wakapiga kambi ngambo ya mto Arnoni. Lakini hawakuingia eneo la Moabu. Mto Arnoni ndio uliokuwa mpaka wa Moabu. 19Hapo Waisraeli walituma wajumbe kwa mfalme Sihoni wa Waamori huko Heshboni wakamwomba awaruhusu kupita katika nchi yake waende katika nchi yao. 20Lakini Sihoni hakuwakubali Waisraeli wapite katika nchi yake. Basi, Sihoni akakusanya watu wake wote, akapiga kambi huko Yahasa, akawashambulia Waisraeli. 21Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni pamoja na watu wake mikononi mwa Waisraeli, wakawashinda. Hivyo Waisraeli wakachukua nchi yote ya Waamori ambao walikuwa wanaishi huko. 22Walilichukua eneo lote la Waamori tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki na tangu jangwani upande wa mashariki hadi mto Yordani magharibi. 23Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, akawafukuza Waamori mbele ya Waisraeli. Je, wewe unataka kutunyanganya nchi yetu? 24Tosheka na kile ambacho mungu wako Kemoshi amekupa. Lakini nchi yoyote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, amewafukuza wakazi wake, akatupa sisi, hiyo ni mali yetu sisi. 25Je, unadhani wewe una nguvu kuliko Balaki mwana wa Zipora aliyekuwa mfalme wa Moabu? Yeye hakushindana na Waisraeli au kupigana nao. 26Wakati wote Waisraeli walipoishi mjini Heshboni na vijiji vyake, na mji wa Aroeri na vijiji vyake pamoja na miji yote iliyo ukingoni mwa mto Arnoni kwa muda wa miaka 300, kwa nini hukulikomboa eneo hilo wakati huo? 27Mimi sijakukosea kitu na ndio maana unafanya kosa unaponishambulia. Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mwamuzi ataamua leo hii kati ya Waisraeli na watu wa Amoni.” 28Lakini mfalme wa Amoni alipuuza ujumbe huo wa Yeftha.
29Kisha roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Yeftha, naye akaondoka na kupitia Gileadi na Manase, akarudi Mizpa katika nchi ya Gileadi na kuendelea hadi Amoni. 30Yeftha akamwapia Mwenyezi-Mungu akisema, “Kama utawatia Waamoni mikononi mwangu, 31basi, yeyote atakayetoka nje kutoka nyumbani mwangu kuja kunilaki nitakapokuwa narudi baada ya kuwashinda Waamoni, huyo atakuwa wako wewe Mwenyezi-Mungu. Huyo nitakutolea sadaka ya kuteketezwa.”
32Basi, Yeftha akavuka mto, akapigana na Waamoni, naye Mwenyezi-Mungu akawatia Waamoni mikononi mwake. 33Akajipatia ushindi mkubwa, akateka maeneo ishirini yaliyokuwa kati ya Aroeri, sehemu zilizozunguka Minithi na Abel-keramimu. Basi Waamoni wakashindwa kabisa na Waisraeli.
34Yeftha alipokuwa anarudi nyumbani kwake huko Mizpa, binti yake akatoka kuja kumlaki akicheza na kupiga matari. Msichana huyo alikuwa ndiye mtoto wake wa pekee. Yeftha hakuwa na mtoto mwingine wa kiume wala wa kike. 35Yeftha alipomwona, alirarua mavazi yake kwa huzuni na kusema, “O binti yangu! Umenivunja moyo. Wewe umekuwa chanzo kikubwa cha matatizo kwangu. Nimekwisha mwapia Mwenyezi-Mungu nami siwezi kuvunja kiapo changu.”
36Naye akamwambia, “Baba, kama umemwapia Mwenyezi-Mungu kitu, basi nitendee kama ulivyoahidi, kwa vile sasa amekuwezesha kuwalipiza kisasi adui zako Waamoni.” 37Kisha, akamwambia baba yake, “Nakuomba jambo hili moja, nipatie muda wa miezi miwili, niende na rafiki zangu milimani, niomboleze kufariki kwangu kabla ya kuolewa.” 38Baba yake akamruhusu aende huko kwa miezi miwili. Naye akaenda pamoja na rafiki zake, wakaomboleza kufa kwake kabla ya kuolewa. 39Baada ya miezi miwili akarudi nyumbani; kisha baba yake akamtendea kulingana na nadhiri yake. Msichana huyo hakuwa amemjua mwanamume yeyote. Basi, tangu wakati huo kukawa na desturi hii katika Israeli: 40Kila mwaka wanawake wa Israeli huenda kuomboleza kwa siku nne kifo cha bintiye Yeftha wa Gileadi.


Waamuzi 11;1-40

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: