Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 11 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 2..





Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..! Mungu wetu..
Muumba wetu,Muumba wa Mbingu, Nchi na vyote vilivyomo..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mlinzi wetu,Kimbilio letu,Muweza wa yote,
Hakuna jambo lolote lilogumu kwako Mungu wetu,Unatosha Yahweh..

Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yeremia mnamo mwaka wa kumi wa utawala wa Sedekia, mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Nebukadneza. Wakati huo, majeshi ya mfalme wa Babuloni yalikuwa yakiuzingira mji wa Yerusalemu, naye nabii Yeremia alikuwa amezuiliwa katika ukumbi wa walinzi uliokuwa ndani ya ikulu ya mfalme wa Yuda. Maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga Yeremia akisema, “Kwa nini unatabiri na kusema: ‘Mwenyezi-Mungu asema hivi: Tazama, mimi nautia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteka. Sedekia, mfalme wa Yuda, hataepa kutiwa mikononi mwa Wakaldayo; hakika atatekwa na mfalme wa Babuloni, ataonana naye uso kwa uso na kuongea naye ana kwa ana. Sedekia atachukuliwa hadi Babuloni, naye atakaa huko mpaka nitakapomchukulia hatua. Hata kama Sedekia atapigana na Wakaldayo, hatashinda.’” Yeremia akasema, Mwenyezi-Mungu alinena nami akasema: “Hanameli, mwana wa baba yako mdogo Shalumu, atakujia na kusema: ‘Nunua shamba langu lililoko Anathothi, maana wewe ni ndugu yangu kabisa, na unayo haki ya kulikomboa.’” Kisha binamu yangu Hanameli alinijia katika ukumbi wa walinzi kama alivyonifahamisha Mwenyezi-Mungu, akaniambia, “Nunua shamba langu lililoko Anathothi katika nchi ya Benyamini maana wewe una haki ya kulikomboa. Linunue kwa faida yako.” Ndipo nilipotambua kwamba lilikuwa kweli neno la Mwenyezi-Mungu. Basi, nililinunua shamba hilo lililoko Anathothi, kutoka kwa binamu yangu Hanameli, nikamlipa bei yake shekeli kumi na saba za fedha. Nikaitia sahihi hati ya kumiliki, nikaipiga mhuri, nikawaita mashahidi na kuipima ile fedha katika mizani. Kisha, nilichukua ile hati ya kumiliki niliyoipiga mhuri, ambayo ilikuwa na masharti na kanuni, pamoja na nakala nyingine iliyokuwa wazi. Nilimpa hiyo hati ya ununuzi Baruku mwana wa Neria mwana wa Maaseya, mbele ya binamu yangu Hanameli na mashahidi waliokuwa wametia sahihi hati ya ununuzi, na mbele ya Wayahudi wote waliokuwa wameketi katika ukumbi wa walinzi. Mbele ya watu wote hao, nilimpa Baruku maagizo yafuatayo: Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Chukua hati hizi zote mbili, hati hii ya kumiliki shamba iliyotiwa sahihi, na hii nyingine iliyo wazi, uziweke katika chungu ili zipate kuhifadhiwa kwa muda mrefu.” Maana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nyumba na mashamba, pamoja na mashamba ya mizabibu katika nchi hii yatanunuliwa tena.” Baada ya kumkabidhi Baruku mwana wa Neria, hati ya kumiliki shamba nilimwomba Mwenyezi-Mungu nikisema:
Unastahili kuabudiwa,Unasthahili kusifiwa,Unastahili kuhimidiwa
Hakuna kama wewe Mungu wetu..Alfa na Omega..!
Baba wa mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha,tukijiachilia mikononi mwako ..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Ee Mwenyezi-Mungu, ni wewe ambaye kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu, umeziumba mbingu na dunia; hakuna kisichowezekana kwako. Wewe unaonesha fadhili zako kwa maelfu ya watu; lakini pia unawaadhibu watu kwa sababu ya dhambi za wazee wao. Wewe ni Mungu mkuu, mwenye nguvu, Mwenyezi-Mungu wa Majeshi ndilo jina lako. Wewe unapanga kwa hekima na unafanya maajabu; njia za watu wote ziko wazi mbele yako, unamlipa kila mmoja kadiri ya njia zake na matendo yake. Katika nchi ya Misri ulifanya maajabu, ukatenda miujiza, na unaendelea kufanya hivyo mpaka leo miongoni mwa Waisraeli na katika mataifa mengine pia, jambo ambalo limekufanya ujulikane kila mahali. Kwa maajabu na miujiza uliyowatisha nayo Wamisri, uliwatoa watu wako Misri kwa nguvu zako nyingi na uwezo wako mkuu. Uliwapa nchi hii ambayo uliahidi kuwapa wazee wao, nchi inayotiririka maziwa na asali. Nao walifika, wakaitwa na kuimiliki. Lakini wao hawakukusikiliza, wala hawakufuata sheria zako. Hawakutenda mambo uliyoamuru. Ndiyo maana utawafanya wapatwe na balaa hii. Tazama, Wakaldayo wamechimba mahandaki kuuzunguka mji; wameuzingira ili wapate kuuteka; wanaushambulia. Vita, njaa na maradhi vitaufanya mji utekwe na watu hao. Kweli mambo uliyotabiri yametokea. Unaona mwenyewe. Lakini, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe uliyeniambia: “Nunua shamba kwa fedha na kuweka mashahidi,” ingawa mji wenyewe umetekwa na Wakaldayo. Ndipo Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Tazama, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa watu wote. Hakuna lolote linaloweza kunishinda. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninautoa mji huu kwa Wakaldayo na kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, naye atauteka. Wakaldayo wanaoushambulia mji huu wataingia na kuuchoma moto; watauteketeza pamoja na nyumba ambazo juu ya paa zake ubani ulifukiziwa mungu Baali na tambiko za divai zilimiminiwa miungu mingine, ili kunichokoza. Maana Waisraeli na watu wa Yuda hawakufanya chochote mbele yangu isipokuwa uovu tangu ujana wao; watu wa Israeli hawakufanya chochote isipokuwa kunikasirisha kwa matendo yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mji huu umechochea hasira yangu na kuniudhi tangu siku ulipojengwa mpaka leo hii. Kwa hiyo, nitautoa kabisa mbele yangu, kwa sababu ya uovu wote waliotenda watu wa Israeli na watu wa Yuda, pamoja na wafalme na viongozi wao, makuhani na manabii wao, na wakazi wa Yerusalemu. Wao walinipa kisogo badala ya kunigeuzia nyuso zao; ingawa nimewafundisha tena na tena, wao hawakusikiliza na kuyapokea mafundisho yangu. Waliweka sanamu za miungu yao ya kuchukiza katika nyumba hii inayojulikana kwa jina langu, wakaitia unajisi. Walimjengea mungu Baali madhabahu katika bonde la Mwana wa Hinomu, ili wamtolee mungu Moleki wavulana wao na binti zao, ingawa sikuwaamuru wala sikufikiria kwamba wangefanya hivyo, wakawafanya watu wa Yuda watende dhambi.”

Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,Biashara,masomo
na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe..

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Mungu wetu tunaomba tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


Mfalme wa Amani tunaomba amani yako itawale katika
Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,famila/ndugu
na wote wanaotuzunguka..

Mungu wetu tunaomba ulinzi wako,
Baba wa Mbinguni tunaomba utamalaki na kutuatamia..
Yahweh tunaomba Baraka zako,Upendo wetu ukadumu,
Hekima,Busara na tuchukulianae..

Yahweh tunaomba utupe neema ya kusimamia Neno lako,Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..

Baba wa Mbinguni utuepushe katika makwazo,migogoro,
kuumizana,chuki,tamaa,unafiki,dhuluma,hasira,kisasi, na yote yanayokwenda kinyume nawe/yasiyokupendeza Mungu wetu..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Roho mtakatifu atuongoze katika yote  tukapate kutambua/kujitambua
tukanene yaliyo yako na tukawe na kiasi..


Sasa basi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Yeremia, watu hawa wanasema kwamba, kwa vita, njaa na maradhi, mji huu utatiwa mikononi mwa mfalme wa Babuloni. Lakini nasema: Nitawakusanya watu kutoka nchi zote ambako kwa hasira na ghadhabu na chuki yangu kubwa, niliwatawanya. Nitawarudisha tena mahali hapa, na kuwafanya wakae salama. Nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao. Nitawapa moyo mmoja na nia moja, wapate kunicha mimi daima, kwa faida yao wenyewe na kwa faida ya watoto wao watakaofuata. Nitafanya nao agano la milele, kwamba sitaacha kamwe kuwatendea mema; nitaweka mioyoni mwao uchaji wangu ili wasiniache tena. Nitafurahi kuwatendea mema; nitawasimika daima katika nchi hii na kuwatendea kwa uaminifu. “Kama nilivyowaletea maafa watu hawa, ndivyo nitakavyowaletea mema niliyowaahidi. Mashamba yatanunuliwa katika nchi hii ambayo unasema imekuwa ukiwa bila watu wala wanyama, na kwamba imetolewa kwa Wakaldayo. Watu watanunua mashamba kwa fedha, watazitilia sahihi hati zake za kuyamiliki, watazipiga mhuri, na kuweka mashahidi katika nchi ya Benyamini, kandokando ya Yerusalemu, katika miji ya Yuda, katika miji ya nchi ya milima, katika miji ya Shefela, na katika miji ya jangwa la Negebu. Maana nitawastawisha tena. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako wote wenyew shida/tabu
wagonjwa,wenye njaa,waliokataliwa,waliokata tamaa,
wanaopitia magumu/majaribu,walio katika vifungo vya yule
mwovu na wote walio asi/kuanguka..
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,Baba ukawape uponyaji wa mwili na roho pia..
Yahweh ukawafungue na wakapate kuwa huru..
Mungu wetu ukawatendee  na ukaonekane katika shida zao..
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kuweza kujiombea
Yahweh ukasikie kulia kwao Baba ukawafute machozi yao..
Jehovah ukapokee sala/maombi yao wote wakuombao kwa moyo na imani..
Mungu wetu ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe Baba ukawanyanyue walioanguka na ukawafariji wafiwa..


Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami
Mungu Baba aendele kuwabariki na kuwatendea
sawasawa na mapenzi yake..

Amani na Upendo vikadumu ndani yenu
Nawapenda.


Yoshua anawatuma wapelelezi Yeriko

1 Taz Ebr 11:31; Yak 2:25 Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kwa siri kutoka Shitimu waende kufanya upelelezi, katika nchi ile na hasa mji wa Yeriko. Wakaenda, wakafika kwenye nyumba ya malaya mmoja aliyeitwa Rahabu wakalala humo.
2Mfalme wa mji wa Yeriko akaambiwa, “Tazama, wanaume wawili Waisraeli wameingia mjini leo usiku ili kuipeleleza nchi.” 3Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akisema: “Watoe nje watu waliokuja nyumbani kwako kwani wamekuja kuipeleleza nchi yote.” 4Lakini, yule mwanamke alikuwa amekwisha waficha watu hao wawili. Basi, akawaambia wajumbe hao, “Ni kweli kwamba hao watu walikuja kwangu, lakini mimi sikujua wametoka wapi. 5Wakati wa kufunga lango la mji, giza lilipoingia, hao watu waliondoka. Kule walikokwenda mimi sijui; wafuateni upesi nanyi mtawapata.” 6Lakini Rahabu alikuwa amewapandisha hao wapelelezi kwenye paa na kuwaficha kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandaza huko paani. 7Basi, wale watu waliotumwa na mfalme wakawafuatia kwa kupitia njia iliyokuwa imeelekea kwenye vivuko vya Yordani. Na mara tu walipoondoka mjini, lango la mji likafungwa. 8Rahabu akawaendea hao wapelelezi juu darini kabla hawajalala, 9akawaambia, “Mimi ninajua kwamba Mwenyezi-Mungu amewapa nchi hii; tumekumbwa na hofu juu yenu na wakazi wote wa nchi hii wamekufa moyo kwa sababu yenu. 10Taz Kut 14:21; Hes 21:21-35 Maana tumesikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu mlipotoka nchi ya Misri, na jinsi mlivyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, yaani Sihoni na Ogu, ambao mliwaangamiza kabisa. 11Mara tu tuliposikia mambo hayo, tulikufa moyo kabisa kwa sababu yenu, tukaishiwa nguvu kabisa. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu juu mbinguni na chini duniani! 12Kwa hiyo basi, tafadhali mniapie kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba mtanitendea kwa wema mimi na jamaa yangu kama vile mimi nilivyowatendeeni kwa wema, na mnipe uthibitisho kamili. 13Ahidini kwamba mtamsalimisha baba yangu na mama yangu, kaka zangu na dada zangu, na jamaa yao yote; hamtakubali tuuawe!”
14Wale watu wakamjibu, “Uhai wenu ni uhai wetu! Kama hamtaifichua siri yetu, Mwenyezi-Mungu atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa wema na uaminifu.”
15Basi, Rahabu akawashusha hao watu kwa kamba kupitia dirishani, kwa kuwa nyumba yake ilikuwa imejengwa ikiambatana na ukuta wa mji wa Yeriko. 16Akawaambia: “Nendeni mlimani mkajifiche huko ili wanaowafuatia wasiwakute. Kaeni huko kwa muda wa siku tatu, mpaka wanaowafuatia watakapokuwa wamerudi mjini, kisha mwende zenu.” 17Hao watu wakamwambia, “Sisi tutalitimiza kabisa jambo ulilotufanya tuahidi kwa kiapo. 18Tutakapokuja katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu kwenye dirisha ambalo umetuteremshia. Uwakusanye hapa kwako baba yako, mama yako na kaka zako na jamaa yote ya baba yako. 19Lakini mtu yeyote akitoka nje ya nyumba yako na kwenda mitaani hatutakuwa na lawama juu ya kifo chake. Lakini kama mtu yeyote atakayekuwamo ndani ya nyumba yako akiguswa tu, basi lawama ya kifo chake itakuwa juu yetu. 20Lakini kama ukimwambia mtu yeyote juu ya shughuli hii yetu, basi, sisi hatutabanwa na kiapo ulichotufanya tukuapie.” 21Naye akawaambia “Na iwe jinsi mlivyosema.” Kisha akawaruhusu waende zao, nao wakaondoka. Naye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.
22Wapelelezi hao waliondoka wakaenda milimani. Walikaa huko kwa muda wa siku tatu mpaka wale waliokuwa wanawafuatia waliporudi mjini Yeriko, baada ya kuwatafuta na kukosa kuwaona. 23Basi, hao wapelelezi wawili wakashuka kutoka milimani, wakavuka mto na kumwendea Yoshua, mwana wa Nuni; wakamwambia yote yaliyowapata. 24Wakamwambia “Hakika Mwenyezi-Mungu ameitia nchi yote mikononi mwetu. Tena wakazi wa nchi hiyo wamekufa moyo kwa sababu yetu.”


Yoshua 2;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: