Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 6 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 11 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!
Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu..
Muumba wa Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo..
Muweza wa yote,Utukuzwe Mungu wetu,Uabudiwe daima..
Uhimidiwe Baba wa Mbinguni,Unatosha Jehovah..
Hakuna kama wewe Yahweh..!


Basi, sasa na tumsifu Mungu! Yeye anaweza kuwaimarisheni katika ile Habari Njema niliyohubiri juu ya Yesu Kristo, na katika ile siri iliyofunuliwa na ambayo ilikuwa imefichika kwa karne nyinyi zilizopita. Lakini, sasa ukweli huo umefunuliwa kwa njia ya maandiko ya manabii; na kwa amri ya Mungu wa milele umedhihirishwa kwa mataifa yote ili wote waweze kuamini na kutii. Kwake Mungu aliye peke yake mwenye hekima, uwe utukufu kwa njia ya Yesu Kristo, milele na milele! Amina.


Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha  kuendelea kuiona leo hii..
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikonono mwako..
Mungu Baba tunaomba utusamehe dhambi zetu zote..
Tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Mungu wetu tazama wajane na yatima Baba wa mbinguni tunaomba ukawabariki na ukawatendee,ukawaongoze na ukaonekane kwenye shida/tabu zao..
Yahweh tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu..
 ukuwaponye wagonjwa,wenye shida/tabu..
wanaopitia magumu/ majaribu mbali mbali,waliokata tamaa..
Mungu wetu tunaomba ukawape uponyaji wa mwili na roho..
Jehovah ukawape neema ya kuweza kujiombea..
Kusimamia Neno lako,Amri na sheria zako nazo zikawaweke huru..


Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.” Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini. Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo....
Mungu wetu nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu tunaomba ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah..!tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
ukabariki nyumba/ndoa zetu,Amani na upendo vikatawale..
Ukawabariki watoto wetu ukawaongoze katika ukuaji wao nasi ukatupe neema ya hekima na busara katika malezi yetu..
Ukawabariki wazazi/wazee wetu,Ndugu,Jamaa na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu ukatupe Amani,Upendo,Furaha ..
tukashirikiane kwa upendo na tukaonyane kwa upendo..

Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni. Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia; ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.” Tena Maandiko yasema: “Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake.” Na tena: “Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni.” Tena Isaya asema: “Atatokea chipukizi katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia.” Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Ukatufanye chombo chema Mungu Baba na tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Sifa na utukufu tunakurudishia Muumba wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni kwa kuwa nami wapendwa..
Mungu aendelee kuwabariki..
upendo wenu katika Kristo Yesu na udumu..
Nawapenda.

Ukuu wa Mwenyezi-Mungu


1“Kwa ajili hiyo, mpendeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kushika siku zote kanuni zake, masharti yake, maagizo yake na amri zake. 2Fikirini kwa makini, kwa sababu ya watoto wenu ambao hawakujua wala hawakuona adhabu ya Mwenyezi-Mungu, uwezo wake na nguvu zake, 3ishara zake na maajabu yake aliyoyatenda kule Misri kwa Farao mfalme wa Misri na nchi yake yote; 4aliyoyatendea majeshi ya Misri, farasi wao na magari yao ya vita, jinsi alivyozamisha jeshi hilo katika bahari ya Shamu, na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoliangamiza hata hivi leo. 5Pia kumbukeni aliyowafanyieni Mwenyezi-Mungu jangwani kabla hamjafika hapa, 6na mambo aliyowatenda Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, mwana wa Reubeni; jinsi mbele ya watu wote wa Israeli nchi ilivyofunuka na kuwameza pamoja na jamaa zao, mahema yao, wanyama na watumishi wao wote. 7Maana macho yenu yameona matendo yote haya makubwa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafanya.

Neema za nchi ya ahadi

8“Tiini amri zote ninazowaamuru siku hii ya leo, ili muweze kuingia na kuimiliki nchi mnayoiendea, 9mpate kuishi kwa muda mrefu katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali; nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliahidi kuwapa babu zenu na wazawa wao. 10Kwa kuwa nchi mnayokwenda kuimiliki si kama nchi ya Misri mlikotoka, ambako mlipanda nafaka, mkamwagilia maji kwa miguu kama mashamba ya mboga. 11Lakini nchi mnayokwenda kuimiliki, ni nchi ya milima na mabonde, nchi ambayo hupata maji ya mvua kutoka mbinguni, 12nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huitunza; Mwenyezi-Mungu huiangalia daima tangu mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka.
13“Basi, mkizitii amri zangu ninazowapeni leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkamtumikia kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote, 14yeye ataipatia mvua nchi yenu wakati wake, mvua za masika na mvua za vuli, nanyi mtavuna nafaka yenu, divai yenu na mafuta yenu. 15Ataotesha majani mashambani kwa ajili ya ng'ombe wenu, nanyi mtakula na kushiba. 16Jihadharini, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, 17nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi yenu, akazifunga mbingu hata pasiwepo mvua na nchi ikaacha kutoa mazao yake, halafu mkaangamia upesi kutoka katika nchi nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu anawapa.
18“Yawekeni maneno yangu haya mioyoni mwenu na rohoni mwenu. Yafungeni mikononi mwenu kama alama na kuyavaa katika paji la uso. 19Wafundisheni watoto wenu maneno haya mkiyazungumzia mketipo katika nyumba zenu, mnapotembea, mnapolala na mnapoamka. 20Ziandikeni katika vizingiti vya nyumba zenu, na katika malango yenu, 21ili nyinyi na watoto wenu mpate kuishi maisha marefu katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliapa kuwapa babu zenu, siku zote mbingu zitakapodumu juu ya dunia.
22“Mkijihadhari kutenda amri zote ambazo nimewapa: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote na kuambatana naye, 23basi Mwenyezi-Mungu atayafukuza mataifa yote hayo mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi iliyo mali ya mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi. 24Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; nchi yenu itaenea kutoka jangwani, upande wa kusini, hadi milima ya Lebanoni upande wa kaskazini, na kutoka mto Eufrate upande wa mashariki, hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi. 25Hakuna mtu yeyote atakayeweza kuwakabili. Popote mtakapokwenda katika nchi hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatia watu hofu wawaogope, kama alivyowaahidi.
26“Angalieni, leo hii nawawekea mbele yenu baraka na laana: 27Baraka, kama mtatii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo nawapeni hivi leo; 28na laana, kama hamtazitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuiacha njia ninayowaamuru, mkaabudu miungu mingine ambayo hata hamjawahi kuijua. 29Mwenyezi-Mungu atakapowafikisha kwenye nchi mnayokwenda kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka mlima Gerizimu, na laana kutoka mlima Ebali. 30(Milima hii iko ngambo ya mto Yordani, magharibi ya barabara kuelekea machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waishio Araba mkabala wa Gilgali). 31Itawabidi kuvuka mto Yordani mwingie kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni. Basi, mtakapoimiliki na kukaa humo, 32muwe waangalifu kutimiza masharti yote na maagizo ninayowapa leo.


Kumbukumbu la Sheria 11:1-32

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: