Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 26 June 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mambo Ya Walawi..22...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?

Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Asante kwa ktuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi ni wema sana au wazuri mno zaidi ya wengine waliotangulia/fariki leo hii au walio vitandani kwa magonjwa mbalimbali..
wengine wanahitaji hata kuita jina la Mungu lakini hawawezi..
Tumempa nini Mungu?Hapana ni kwa Rehema/Neema zake tuu Mungu wetu..

Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho. Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe. Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu. Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana. Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo.
Basi Mungu wetu akatuongoze  tukatumie wakati huu vizuri..

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako..
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizoziwaza,tulizozinena,tulizozitenda,kwakujua/kutojua..Mungu wetu tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Utuepushe na majaribu,utuokoe na yule mwovu na kazi  zake zote..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu,Utufunike kwa Damau ya Mwanao Mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tupate kutambua na kujitambua na tukawe na kiasi..
Tunayakabidhi maisha yetu mikononi mwako Jehovah...

Maadamu nyinyi mmemkubali Kristo Yesu aliye Bwana, basi, ishini katika muungano naye. Muwe na mizizi ndani yake, mjijenge juu yake na kuwa imara katika imani kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele. Angalieni, basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe! Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu, nanyi mmepewa uhai kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote. Katika kuungana na Kristo nyinyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi. Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo mlifufuliwa pia pamoja naye kwa kuamini katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka kwa wafu. Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu nyinyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa nyinyi uhai pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani. Huko Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake. Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya mwezi mpya au Sabato. Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo. Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganyifu za kidunia na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu.

Ukatubariki na kubariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda tukafanye sawasawa na mapenzi yako..
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..

Tazama wenye shida/tabu,wamaotaabika na kukata tamaa,wenye hofu/mashaka,waliokatika vifungo mbalimbali,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali..
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,Ukawape macho ya kuona na masikio ya kusikia, ukawaonyeshe njia na wakafute sheria na Amri zako..Wakapate kuijua kweli nayo itawaweka huru na kuwaponya kiroho na kimwili..wakapate Ulinzi uliowako na kusimamia Neno lako..
wakajue jinsi ulivyo na kwamba wewe ni muweza wa yote..
Tunakwenda kinyume na roho zote mbaya,nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga Kristo..
Zishindwe katika Jina lililokuu Jina la  Bwana wetu Yesu Kristo...


Nyinyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa katika nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti: “Msishike hiki,” “Msionje kile,” “Msiguse kile!” Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu. Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima kwa namna ya ibada wanayojishurutishia, unyenyekevu, na kuutendea mwili kwa ukali; lakini hayafai chochote kuzuia tamaa za mwili.
Wapendwa Mungu wetu yupo na ni mwema sana..
Tumtafute kwa bidii na kufuata njia zake ili tupate kupona..

Asante Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
tukiamini na kushukuru daima..
Sifa na utukufu tunakurudishia  wewe Baba wa Mbinguni....

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asante sana waungwana/wapendwa kwa kuwanami/kunisoma..
Mungu aendelee kuwabariki na msipungukiwe  katika mahitaji yenu..
na Mungu akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.
 

Utakatifu wa sadaka
1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Mwambie Aroni na wanawe makuhani waviheshimu vitu ambavyo Waisraeli wameniwekea wakfu, wasije wakalikufuru jina langu takatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. 3Waambie hivi: Kama mmoja wa wazawa wenu katika vizazi vyenu vyote atavikaribia vitu vitakatifu ambavyo Waisraeli wameviweka wakfu kwangu mimi Mwenyezi-Mungu akiwa najisi, mtu huyo atatengwa nami. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. 4Mtu yeyote wa nasaba ya Aroni akiwa na ugonjwa wa ukoma au anatokwa usaha asile vitu vitakatifu mpaka atakapokuwa safi. Mtu yeyote akimgusa mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa, 5au akigusa kiumbe chochote chenye kutambaa ambacho husababisha mtu kuwa najisi au mtu ambaye aweza kumtia unajisi wa aina yoyote ile, 6mtu huyo, atakuwa najisi mpaka jioni na haruhusiwi kula vyakula vitakatifu mpaka hapo atakapokuwa ameoga. 7Jua litakapotua ndipo atakapokuwa safi. Baada ya hapo ataweza kula vyakula vitakatifu kwani hicho ndicho chakula chake. 8Kuhani asile nyama yoyote ya mnyama aliyekufa peke yake au kuuawa na mnyama wa porini, asije akajitia unajisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. 9Kwa hiyo, ni lazima makuhani walishike agizo langu, wasije wakafanya dhambi na kuuawa. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu.
10“Mtu asiye wa ukoo wa makuhani haruhusiwi kula chakula kitakatifu. Hata mgeni wa kuhani au mwajiriwa wake haruhusiwi kula. 11Lakini kama kuhani amemnunua mtumwa ili kuwa mali yake, basi, huyo mtumwa anaruhusiwa kula na pia wale waliozaliwa nyumbani kwake. 12Kama binti yake kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, haruhusiwi kula sadaka ya vitu vitakatifu. 13Lakini kama binti yake kuhani ni mjane au amepewa talaka na hana mtoto, naye amerudi nyumbani kwa baba yake, akakaa naye kama alipokuwa kijana, basi, anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mgeni haruhusiwi kula vyakula hivyo. 14Kama mtu mwingine akila vyakula vitakatifu bila kujua, basi, atalipa asilimia ishirini ya thamani ya alichokula na kumrudishia kuhani. 15Kuhani asivitie unajisi vitu ambavyo Waisraeli wamemtolea Mwenyezi-Mungu 16na hivyo kusababisha watu wawajibike uovu na hatia yao kwa kula vitu vyao vitakatifu. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayeviweka wakfu vitu hivyo.”
17Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 18“Mwambie Aroni na wanawe makuhani na Waisraeli wote hivi: Kama mtu yeyote miongoni mwenu au mgeni yeyote aishiye katika Israeli akitoa sadaka yake, iwe ni ya kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari ya kumtolea Mwenyezi-Mungu kwa kuteketezwa, 19ili apate kukubalika, atatoa katika ng'ombe dume au katika kondoo dume asiye na dosari. 20Ni marufuku kutoa chochote kilicho na dosari kwani hakitakubaliwa kwa faida yenu. 21Mtu yeyote anapomtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya amani ili kutimiza nadhiri au sadaka ya hiari kutoka katika kundi lake la mifugo, ili akubaliwe ni lazima awe ni mnyama mkamilifu; mnyama huyo asiwe na dosari yoyote. 22Usimtolee Mwenyezi-Mungu mnyama yeyote aliye kipofu, kilema, aliyevunjika mahali, anayetokwa na usaha, mwenye upele au ukurutu, wala usiwatoe kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu. 23Fahali au mwanakondoo aliye na kiungo kimoja kirefu au kifupi kuliko kawaida waweza kumtoa sadaka ya hiari; lakini huyo usimtoe kuwa sadaka ya kutimiza nadhiri. 24Mnyama ambaye kiungo chake cha kiume kimejeruhiwa, kimepondwa, kimevunjwa au kimekatwa, kamwe usimtolee Mwenyezi-Mungu; usifanye kitu cha namna hiyo nchini mwako. 25Wala usipokee kutoka kwa wageni wanyama wa namna hiyo na kunitolea mimi Mungu wako kama chakula. Wanyama hao wana dosari kwa vile wamekatwa na hawatakubaliwa kwa faida yenu.”
26Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 27“Fahali, kondoo dume au beberu akizaliwa atabaki na mama yake kwa siku saba. Lakini tangu siku ya nane anaweza kutolewa kwa Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa kwa moto. 28Lakini usimchinje ng'ombe au kondoo siku moja pamoja na ndama wake. 29Utakaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya shukrani utaitoa kwa namna ambayo itakufanya ukubaliwe. 30Mnyama huyo ni lazima aliwe siku hiyohiyo; msimbakize mpaka kesho yake asubuhi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
31“Kwa hiyo mtazishika na kuzitekeleza amri zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. 32Msilikufuru jina langu takatifu, kwani ni lazima niheshimiwe miongoni mwa watu wa Israeli. Mimi Mwenyezi-Mungu ndiye ninayewaweka wakfu. 33Mimi ndimi niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”

Mambo Ya Walawi22;1-24


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: