Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Swahili na Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 22 June 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mambo Ya Walawi..20..


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?

Ni siku nyingine tena Mungu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Kwa wema na fadhili zake ametulinda usiku na wakati wote,Ametupa neema/rehema hii ya kuamka salama wenye afya na kuendelea na kazi/mambo yetu katika kutafuta ridhiki na yote yanayotukabili mbele yetu yeye akatuongoze  kwa maana peke yetu hatutaweza..


Mwenyezi-Mungu asipoijenga nyumba, waijengao wanajisumbua bure. Mwenyezi-Mungu asipoulinda mji, waulindao wanakesha bure.
Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe pale tulikwenda kinyume nawe kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..

Ututakase Miili yetu na Akili zetu,Utufunike kwa Damu ya Mwanao Mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..Yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena. Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mmegundua kwamba Bwana ni mwema.” Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule na la thamani kubwa. Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea tambiko za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Tazama! Naweka jiwe huko Siyoni, jiwe la msingi, teule na la thamani. Mtu atakayemwamini huyo hataaibishwa.” Kwenu nyinyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, “Jiwe walilolikataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.” Tena Maandiko yasema: “Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu.” Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo. Lakini nyinyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu. Wakati mmoja nyinyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa nyinyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmepokea huruma.


Mungu wetu ukatufanye chombo chema na tukatumike sawasawa na mapezni yako..


Asante Mungu wetu tunaomba ukaibariki siku hii na ukabariki vyote tunavyoenda kutenda/kufanya na tukafanye sawaswa na mapenzi yako..
Vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mungu wetu ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako Mungu wetu tuliyanena na tusiyoyanena Mungu wetu unayajua na kutujua vyema kuliko tujijuavyo sisi..
Tunakushukuru na kukusifu Daima..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..

Amina..!

Asanteni sana kwakuwanami/kunisoma..
Mungu aendelee kuwabariki na msipungukiwe na neema yake..
Nawapenda sana.Adhabu kwa ajili ya maovu

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Waambie Waisraeli hivi: Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli au mgeni anayekaa miongoni mwenu, akimtoa sadaka mtoto wake yeyote kwa mungu Moleki ni lazima mtu huyo auawe. Wananchi wa hapo watamuua kwa kumpiga mawe. 3Mimi mwenyewe nitamkabili mtu huyo na kumtenga na watu wake kwa sababu alimtoa mmoja wa watoto wake sadaka kwa mungu Moleki na hivyo kupachafua mahali pangu patakatifu na jina langu takatifu. 4Kama wananchi wa mahali hapo hawatamwadhibu mtu huyo kwa kumuua, 5mimi mwenyewe nitamkabili mtu huyo na jamaa yake. Nitawatenga kutoka watu wao, yeye mwenyewe pamoja na wote waliokosa uaminifu kwangu kwa kumwendea mungu Moleki.
6“Kama mtu yeyote anawaendea waaguzi wa mizimu na wachawi na hivyo kukosa uaminifu kwangu, nitamkabili mtu huyo na kumtenga na watu wake. 7Kwa hiyo, jiwekeni wakfu muwe watakatifu; kwani mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 8Shikeni masharti yangu na kuyatekeleza. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa. 9Mtu yeyote amlaaniye baba yake au mama yake, ni lazima auawe. Amemlaani baba au mama yake, kwa hiyo damu yake itakuwa juu yake.
10“Kama mwanamume akizini na mke wa jirani yake, ni lazima wote wawili wauawe. 11Mwanamume akilala na mmoja wa wake za baba yake, anamwaibisha baba yake; wote wawili ni lazima wauawe. Damu yao itakuwa juu yao wenyewe. 12Mwanamume yeyote akilala na mke wa mwanawe, wote wawili ni lazima wauawe. Wamefanya zinaa ya maharimu; wanawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe. 13Kama mwanamume yeyote akilala na mwanamume mwenzake kana kwamba ni mwanamke, basi, wote wawili ni lazima wauawe kwani wamefanya jambo lililo chukizo; watawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe. 14Kama mwanamume akioa mke na pia kumwoa mama yake, huo ni uovu; wote watatu ni lazima wateketezwe kwa moto kwani wamefanya uovu. Mtafanya hivyo ili uovu usiwe miongoni mwenu. 15Kama mwanamume yeyote akilala na mnyama ni lazima auawe; na mnyama huyo lazima auawe. 16Kama mwanamke akimkaribia mnyama na kulala naye ni lazima mwanamke huyo auawe na mnyama huyo pia; damu yao itakuwa juu yao wenyewe.
17“Kama mwanamume yeyote akimwoa dada yake, binti ya baba yake au mama yake, na binti huyo akakubaliana na mwanamume huyo ambaye ni kaka yake, na kulala naye, hilo ni chukizo, ni lazima watengwe na rika lao kwani wamefanya jambo la aibu. Ni lazima mwanamume huyo awajibike kwa uovu wake. 18Kama mwanamume akilala na mwanamke aliye mwezini, wote wawili ni lazima watengwe na watu wao; huyo mwanamume amelala na mwanamke aliye na hedhi, na huyo mwanamke amelala na mwanamume akiwa na hedhi. 19Usilale na dada ya mama yako wala na shangazi yako, maana hao ni jamaa yako wa karibu. Wote watendao hayo watawajibika kwa uovu wao. 20Kama mtu akilala na mke wa baba yake, mkubwa au mdogo, anamwaibisha baba yake mkubwa au mdogo; wote wawili watawajibika kwa dhambi yao; wote wawili watakufa bila watoto. 21#Taz Lawi 18:16 Kama mwanamume akimwoa mke wa ndugu yake, anamwaibisha ndugu yake, huo ni unajisi; wote wawili watakufa bila watoto.
22“Mnapaswa kushika na kutekeleza masharti na maagizo yangu yote; la sivyo nchi ile ambamo ninawapeleka itawatapika. 23Msizifuate desturi za taifa ninalolifukuza mbele yenu; kwani waliyafanya hayo yote, nami nikawachukia sana. 24Lakini, nimekwisha waambia, ‘Mtarithi nchi yao, mimi nawapa nchi hiyo muimiliki, nchi inayotiririka maziwa na asali.’ Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu niliyewatenga na mataifa mengine. 25Kwa hiyo, ni lazima mtofautishe kati ya mnyama asiye najisi na aliye najisi, kati ya ndege asiye najisi na aliye najisi. Msijifanye kuwa najisi kwa kugusa mnyama au ndege au chochote kitambaacho duniani ambacho nimekitenga kuwa ni najisi. 26Kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni mtakatifu, nami nimewatenga nyinyi na mataifa mengine ili muwe mali yangu, mtakuwa watakatifu.
27“Mwanamume au mwanamke yeyote aliye mlozi au mchawi, ni lazima auawe kwa kupigwa mawe. Wote watawajibika kwa umwagaji wa damu yao wenyewe.”

Mambo Ya Walawi20;1-27


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: