Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 25 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 19...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu ni muweza wa yote..Tumshukuru na Kumsifu daima..
Yeye aliyetuumba,Yeye aliyetupa kibali  cha kuendelea na kuiona tena Leo hii,Yeye kwa Mapenzi yake, Neema/Rehema zake ametuamsha tena,

yeye aliyetuchagua sisi,Yeye ni Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba mbingu na Nchi, Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo, Baba yetu,Mfalme wa Amani, Muweza wa yote, Yeye ni mwanzo na yeye ni mwisho,Hakuna kama yeye na hatokuwepo,Yeye ni Alfa na Omega..Jehovah Nissi..!! Jehovah Rapha..!! Jehovah Jireh..!! Jehovah Shammah..!!El shaddah..!!!
Unatosha Baba, Neema  zako zatutosha, hakuna wa kufanana nawe Baba..!!Sifa na utukufu ni kwako daima..!!
Tunashuka mbele zako Baba ili wewe uinuliwe Daima... Tunakuja mbele zako, tunajiachilia mikononi mwako Baba na kujinyenyekeza...
Tunaomba utuokoe na kututakasa kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana wetu  na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Ututakase miili yetu na Akili zetu. tupate kujitambua/kutambua..
Ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo , Vilaji/Vinywaji, Tuingiapo/tutokapo, Hatua zetu zikawe nawe Yahweh..!! Tazama vyote tunavyoenda kugusa/kutumia navyo tunaomba ukavitakase...
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Baba.. kwakuwaza,kwakunena, kwakutenda,kwakujua,kutojua..Mfalme wa Amani tunaomba nasi utupe Neema yakuweza kuwasamehe wote waliotukosea..
Tunakwenda kinyume na mwovu na kazi zake zote..

Baba wa Mbinguni utuokoe..
Baba wa Mbinguni tazama wenyeshida/tabu,wagonjwa,waliomagerezani pasipo na hatia,waliofungwa na mwovu Baba,wafiwa ukawe mfariji wao, Yatima na Wajane Mungu wangu na wote wanaopitia magumu/majaribu..
Tunaomba Baba ukawaponye na kuwaokoa, ukawaguse na mkono wako wenye nguvu..Uponyaji wa kweli una wewe..Ukawaweke huru Baba na wakapatekupona kimwili na kiroho.. Ukuu wako ukaonekane Baba wa Mbingu..
Asante Mungu wetu katika yote.. Maisha yetu yapo mikononi mwako..
Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako na Tunakushuru na kukusifu..
Tukiamini wewe ni Mungu wetu na Mlinzi wetu..kwako wewe hakuna linaloshindikana..Tunakuabu siku zote na Imani, Tumaini la kweli lipo kwako..


Utuonee huruma, ee Mungu, utubariki; utuelekezee uso wako kwa wema; dunia yote ipate kutambua njia yako, mataifa yote yajue nguvu yako ya kuokoa. Watu wote wakutukuze, ee Mungu; watu wote na wakusifu! Mataifa yote yafurahi na kuimba kwa furaha; maana wawahukumu watu kwa haki, na kuyaongoza mataifa duniani. Watu wote wakutukuze, ee Mungu; watu wote na wakusifu! Nchi imetoa mazao yake; Mungu, Mungu wetu, ametubariki. Mungu aendelee kutubariki. Watu wote duniani na wamche.
Amina..!!!

Asanteni wote mliopitia hapa Mungu aendelee kuwabariki katika mahitaji yenu.
Nawapenda.

Waisraeli mlimani Sinai

1Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu tangu walipotoka nchini Misri, watu wa Israeli walifika katika jangwa la Sinai. 2Walipoondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, huko walipiga kambi mbele ya mlima Sinai. 3Basi, Mose akapanda juu mlimani kwa Mungu. Hapo Mwenyezi-Mungu akamwita Mose kutoka huko juu mlimani, akamwambia, “Hivi ndivyo utakavyowaambia wazawa wa Yakobo, hao Waisraeli, 4‘Nyinyi wenyewe mmeona nilivyowatenda Wamisri na jinsi nilivyowachukua kama tai anavyochukua watoto wake kwa mabawa, nikawaleta kwangu. 5Taz Kumb 4:20; 7:6; 14:2; 26:18; Tito 2:14 Sasa basi, kama mkiitii sauti yangu na kulishika agano langu, mtakuwa watu wangu wateule kati ya mataifa yote, maana dunia yote ni yangu. 19:5-6 Taz 1Pet 2:9 6Taz Ufu 1:6; 5:10 Mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Hayo ndiyo maneno utakayowaambia Waisraeli.”
7Basi, Mose akarudi, akawakusanya pamoja wazee wa Waisraeli na kuwaambia maneno hayo aliyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 8Watu wote wakaitikia kwa pamoja wakisema, “Mambo yote aliyoyasema Mwenyezi-Mungu, tutayafanya.” Mose akamjulisha Mwenyezi-Mungu jibu hilo la watu. 9Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Haya, mimi nitakujia katika wingu zito ili Waisraeli wapate kunisikia ninaposema nawe na kukuamini siku zote.”
Kisha Mose akamwambia Mungu jinsi watu walivyosema. 10Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa watu uwatakase leo na kesho. Waambie wayafue mavazi yao 11wawe tayari kwa kesho kutwa, maana siku hiyo ya tatu mimi Mwenyezi-Mungu nitashuka juu ya mlima Sinai mbele ya watu wote. 12Taz Ebr 12:18-20 Tena wewe utawawekea watu mpaka kuzunguka mlima. Utawakanya wajihadhari sana wasipande juu mlimani wala kuugusa mpaka wake. Yeyote atakayeugusa mlima, atauawa. 13Mtu asimguse mtu huyo; atauawa kwa kupigwa mawe au mshale awe ni mtu au ni mnyama, hataishi. Wakati mbiu itakapopigwa mfululizo, watu wote watakaribia mlimani.”
14Basi, Mose akashuka mlimani na kuwaendea watu, akawatakasa, nao wakayafua mavazi yao. 15Kisha akawaambia watu wote, “Kesho kutwa muwe tayari, na mwanamume yeyote asimkaribie mwanamke.”
16 Taz Ufu 4:5 Basi, siku ya tatu asubuhi, kukatokea ngurumo na umeme na wingu zito juu ya mlima. Ikasikika pia sauti kubwa ya mbiu ambayo iliwatetemesha watu wote kambini. 19:16-18 Taz Kumb 4:11-12 17Kisha Mose akawaongoza watu wote kutoka kambini, wakaenda kukutana na Mungu. Wote walikwenda wakajipanga chini ya mlima.
18Mlima wa Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi wa tanuri kubwa na mlima wote ulitetemeka kwa nguvu. 19Sauti ya mbiu ilizidi kuongezeka, na Mose akaongea na Mungu. Mungu naye akamjibu katika ngurumo.
20Mwenyezi-Mungu alishuka juu ya mlima Sinai, akamwita Mose kutoka huko juu, naye Mose akapanda mlimani. 21Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Shuka chini ukawaonye watu wote wasije kunitazama; la sivyo wengi wao wataangamia. 22Hata makuhani ambao hunikaribia wanapaswa kujitakasa; la sivyo nitawaadhibu.” 23Mose akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Watu hawa hawawezi kuupanda mlima wa Sinai kwani wewe mwenyewe ulituamuru tuweke mpaka kuuzunguka mlima.” 24Mwenyezi-Mungu akasema, “Teremka chini kisha urudi pamoja na Aroni. Lakini usiwaruhusu makuhani na watu wengine wapite mpaka na kuja kwangu, la sivyo nitawaadhibu.” 25Basi, Mose akashuka na kuwaambia Waisraeli mambo yote aliyoagizwa.

Kutoka19;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: