Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 29 March 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo50...Mwisho wa Kitabu cha Mwanzo..Mungu wetu yu Mwema Sana..!!

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa mema mengi aliyotutendea/anayotutendea..
Sifa na Utukufu ni kwake Daima..



Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu; anga ladhihirisha kazi ya mikono yake. Mchana waupasha habari mchana ufuatao, usiku waufahamisha usiku ufuatao. Hamna msemo au maneno yanayotumika; wala hakuna sauti inayosikika; hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote, na maneno yao yafika kingo za ulimwengu. Mungu ameliwekea jua makao yake angani; nalo hutoka kama bwana arusi chumbani mwake, lafurahi kama shujaa aliye tayari kushindana. Lachomoza toka upande mmoja, na kuzunguka hadi upande mwingine; hakuna kiwezacho kuliepa joto lake. Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu, humpa mtu uhai mpya; masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti, huwapa hekima wasio na makuu. Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa, huufurahisha moyo; amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi, humwelimisha mtu. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema, na la kudumu milele; maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa, yote ni ya haki kabisa. Yatamanika kuliko dhahabu; kuliko dhahabu safi kabisa. Ni matamu kuliko asali; kuliko asali safi kabisa. Yanifunza mimi mtumishi wako; kuyafuata kwaniletea tuzo kubwa. Lakini nani aonaye makosa yake mwenyewe? Ee Mungu, niepushe na makosa nisiyoyajua. Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi, usikubali hayo yanitawale. Hapo nitakuwa mkamilifu, wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa. Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu, mwamba wangu na mkombozi wangu!

Yeye aliyetupa Kibali cha kuiona Leo hii..
Yeye ni Mungu wetu ,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi,Yeye atosha,Yeye Mwanzo na Yeye ni Mwisho..Yeye asiyesinzia wala kulala.. Mchana yupamoja nasi Usiku yupamoja nasi Jana,Leo, Kesho na hata Milele yeye atabaki kuwa Mungu, Ije mvua lije jua Mungu yu mwema sana...!!!!Hakuna wa kufanana naye,Hakuna na hatakuwepo kama yeye..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...Jehovah..!! Yahweh..!! wewe ni Mkuu wa Yote..
Tunajinyeyekeza mbele zako Baba  na kujiachilia mikononi mwaka Leo na siku zote..Utubariki Baba wa Mbinguni,Tuingiapao/Tutokapo, Tutembeapao,Hatua zetu ziwe nawe Yahweh..
Ubariki Vinywaji/Vilaji,Vyombo vya usafari na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase na Damu ya Mwanao, Bwana wetu Na Mwokozi wetu..Yesu Kristo wa Nazareti....!!!!
Ututakase Miili yetu na Akili zetu Baba..
Roho mtakatifu akatuongoze kwenye kunena/kutenda..Kutambua/kujitambua..
Baba ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo na Ridhiki zetu Baba ziingiapo na zitokapo Mfalme wa Amani..!!!!
Utusamehe dhambi zetu Baba tulizozitenda kwa kujua/kutojua..
Baba utupe Neema ya kuweza nasi kuwasamehe waliotukosea...
Baba ukawawaponye na kuwaokoa wenye Shida/Tabu, wanaopitia Majaribu/Magumu,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,Waliomagerezani pasipokuwa na hatia,waliofungwa na mwovu, Baba nyoosha mkono wako ukawaguse na kuwaokoa wawe huru kimwili na kiroho..
Mfalme wa Amani Ukatawale na kuibariki Nchi hii tunayoishi, Ukabariki Tanzania Baba, Afrika yote na Dunia nzima..
Ukawaongoze wanaotuongoza nao wakatuongoze katika haki na kweli..
Tunakwenda kinyume na Mwovu Baba..
Tunakuja mbele zako Yahweh..! Sifa na Utukufu ni wako Jehovah..!!tunashukuru na kuaminia kwamba  wewe ni Bwana wetu

na Mwokozi wetu..Yote tunaweka mikononi mwako..
Amina..!!

Muwe na wakati mwema.

1Hapo Yosefu akamkumbatia baba yake akilia na kumbusu. 2Kisha, akawaagiza waganga wake wampake Israeli, baba yake, dawa ili asioze, nao wakafanya hivyo. 3Kama kawaida, siku arubaini zilihitajika kwa kazi hiyo. Wamisri nao wakaomboleza kifo cha Yakobo kwa muda wa siku sabini.
4Baada ya matanga kumalizika, Yosefu akawaambia watu wa jamaa ya Farao, “Ikiwa nimekubalika mbele yenu, tafadhali zungumzeni na Farao kwa niaba yangu kwamba baba yangu aliniapisha, akisema, 5‘Mimi karibu nitafariki. Yakupasa kunizika katika kaburi nililojichongea katika nchi ya Kanaani.’ Kwa hiyo namwomba aniruhusu niende kumzika baba yangu, kisha nitarudi.” 6Farao akajibu, “Nenda ukamzike baba yako kama alivyokuapisha.” 7Basi, Yosefu akaondoka kwenda kumzika baba yake akifuatana na watumishi wote wa Farao, wazee wa nyumba ya Farao, pamoja na wazee wa nchi nzima ya Misri. 8Hali kadhalika, Yosefu alifuatana na jamaa yake yote, ndugu zake na jamaa yote ya baba yake Yakobo. Katika eneo la Gosheni walibaki watoto wao tu pamoja na kondoo, mbuzi na ng'ombe wao. 9Pia waliandamana naye wapandafarasi na magari; lilikuwa kundi kubwa sana.
10Walipofika katika uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, ngambo ya mto Yordani, waliomboleza kwa huzuni kubwa, naye Yosefu akamfanyia baba yake marehemu matanga ya siku saba. 11Wakanaani wenyeji wa nchi hiyo, walipoyaona maombolezo yaliyofanywa kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, wakasema, “Maombolezo haya ya Wamisri, kweli ni makubwa!” Kwa hiyo, mahali pale pakaitwa Abel-misri, napo pako ngambo ya mto Yordani.
12Wana wa Yakobo walimfanyia baba yao kama alivyowaagiza: 13Walimchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika katika pango lililokuwa katika shamba kule Makpela, mashariki ya Mamre. Pango pamoja na shamba hilo Abrahamu alikuwa amelinunua kwa Efroni Mhiti, ili pawe mahali pake pa kuzikia. 14Baada ya kumzika baba yake, Yosefu alirudi Misri pamoja na ndugu zake na watu wote waliokuwa wameandamana naye kwenda kumzika baba yake.

Yosefu awaondolea shaka ndugu zake

15Baada ya kifo cha baba yao, ndugu zake Yosefu walisemezana, “Huenda Yosefu atatuchukia na kutulipiza mabaya yote tuliyomtendea.” 16Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakisema, “Baba yako, kabla hajafariki, aliagiza hivi, 17‘Mwambieni Yosefu kwa niaba yangu: Tafadhali uwasamehe ndugu zako makosa yao mabaya na maovu yote waliyokutendea.’ Sasa basi, tafadhali usamehe uovu tuliokutendea sisi watumishi wa Mungu wa baba yako.” Yosefu alipopata ujumbe huu, alilia. 18Kisha ndugu zake wakamjia, wakainama mpaka chini mbele yake, wakasema, “Tazama, sisi tu watumishi wako.” 19Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope, je, mimi ni badala ya Mungu? 20Nyinyi mlitaka kunitendea vibaya, lakini Mungu alikusudia mema ili watu wengi wapate kuwa hai kama mwonavyo leo. 21Haya, msiogope. Mimi nitawapeni chakula pamoja na watoto wenu.” Basi akawafariji na kusema nao vizuri.

Kifo cha Yosefu
22Yosefu akaendelea kukaa katika nchi ya Misri pamoja na jamaa yote ya baba yake. Aliishi kwa muda wa miaka 110. 23Yosefu alijaliwa kuwaona watoto na wajukuu wa mwanawe Efraimu, na pia kuwapokea kama wanawe watoto wa Makiri mwana wa Manase.
24Baadaye Yosefu aliwaambia ndugu zake, “Mimi sasa ninakaribia kufa. Lakini Mungu hakika atawajia kuwasaidia. Atawatoa katika nchi hii na kuwapelekeni katika nchi aliyowaapia Abrahamu, Isaka na Yakobo.” 25Kisha Yosefu akawaapiza wana wa Israeli, akisema, “Mungu atakapowajia kuwasaidia, hakikisheni kwamba mmeichukua mifupa yangu kutoka huku.”
26Basi, Yosefu akafariki kule Misri, akiwa na umri wa miaka 110. Nao wakaupaka mwili wake dawa usioze, wakauweka katika jeneza kule Misri.
Mwanzo50;1-26
Bible Society of Tanzania

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: