Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Swahili na Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 24 February 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mwanzo27....

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana,Yeye awezaye yote,Mfalme wa Amani,Mungu ni pendo apenda watu,Anayefanya njia pasipo na njia,
Akisema atakubariki na atafanya hivyo,Unastahili kuabudiwa,Kutukuzwa Baba wa mbinguni,Wewe Uliyetuumba,wewe ni habari njema,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Kuamka wazima na wenye Afya ni kwa Neema/Rehema ya Mungu tuu na si kwa uwezo,Nguvu/Utashi na uelewa wetu,Mungu wetu si mtu hata aseme uongo,Ahadi zake ni Amina na kweli..


Mwachie Mwenyezi-Mungu mzigo wako naye atakutegemeza,Kamwe hamwachi mwadilifu ashindwe.{Zaburi55;22]
Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako,Mtumainiye yeye naye atafanya kitu.{Zaburi37:5}
Sasa ndugu yangu mpendwa yanini kutangatanga,Kujibebesha mizigo isiyo yako na usiyoiweza?Mpe leo maisha yako Mungu ukiamini na yeye anatosha, na kufuata njia zake kamwe hatokuacha, Furaha ipo kwakwe,Tumaini ni yeye,Upendo wa kweli unapatikana kwakwe,Faraja ya kweli ipo kwa Mungu...
Mtumainiye Mqwenyezi-Mungu na kutenda mema,Upate kuishi katika nchi na kuwa salama{Zaburi37:3}
Mungu akatubariki kuingiakwetu/Kutoka kwetu,Vyombo vya usafiri na Tutembeapo,Vilaji/Vinywaji,Kazi,Biashara,Elimu na vyote tunavyoenda kutumia/kugusa Mungu akavitakase na kuvifunika na damu ya Mwokozi..


Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, nadamu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.{1Yohane 1:7}

Tunajiachilia Mikononi mwako Baba wa Mbingu,Tukishukuru na Kuamini wewe ni Bwana na Mwokozi wetu..
                                      Amina..!!
                                       Mungu akaonekane kwenye Maisha yenu.
                                    


Isaka anambariki Yakobo

1Isaka alikuwa amezeeka na macho yake yalikuwa hayaoni. Basi, alimwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu!” Naye akaitika “Naam baba, nasikiliza!” 2Isaka akasema, “Tazama, mimi ni mzee, wala siku ya kufa kwangu siijui. 3Basi, chukua silaha zako, yaani podo na upinde wako, uende porini ukaniwindie mnyama. 4Halafu unitengenezee chakula kitamu, kile nipendacho, uniletee ili nile, nipate kukubariki kabla ya kufa kwangu.”
5Kumbe, wakati huo Isaka alipokuwa akiongea na Esau mwanawe, Rebeka alikuwa anasikiliza. Kwa hiyo, Esau alipokwenda porini kuwinda, 6Rebeka alimwambia mwanawe Yakobo, “Nimemsikia baba yako akimwambia kaka yako Esau, 7amwindie mnyama na kumtengenezea chakula kitamu, ili ale, apate kumbariki mbele ya Mwenyezi-Mungu kabla ya kufa kwake. 8Sasa mwanangu, sikiliza maneno yangu na utii ninayokuagiza. 9Nenda kwenye kundi la mbuzi uniletee wanambuzi wawili wazuri, nimtengenezee baba yako chakula kitamu, kile apendacho. 10Kisha utampelekea baba yako ale, apate kukubariki kabla hajafa.”
11Lakini Yakobo akamwambia mama yake Rebeka, “Kumbuka kaka yangu Esau amejaa nywele mwilini, hali mimi sina. 12Labda baba atataka kunipapasa, nami nitaonekana kama ninamdhihaki, kwa hiyo nitajiletea laana badala ya baraka.” 13Mama yake akamwambia, “Laana yako na inipate mimi, mwanangu; wewe fanya ninavyokuagiza: Nenda ukaniletee hao wanambuzi.”
14Basi, Yakobo akaenda, akachukua wanambuzi wawili, akamletea mama yake; naye akatayarisha chakula kitamu, kile apendacho Isaka baba yake. 15Kisha Rebeka akatwaa mavazi bora ya Esau, mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo, mwanawe mdogo. 16Akamvika pia ngozi za wale wanambuzi mikononi na kwenye sehemu laini shingoni mwake. 17Kisha akampa kile chakula kitamu na mkate aliokuwa ametayarisha.
18Basi, Yakobo akaingia ndani kwa baba yake, akamwita, “Baba!” Naye akaitika, “Naam! Ni nani wewe mwanangu?” 19Yakobo akamjibu baba yake, “Ni mimi Esau, mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniagiza. Tafadhali baba, kaa kitako ule mawindo yangu ili upate kunibariki.” 20Lakini Isaka akamwuliza, “Imekuwaje umepata mawindo upesi hivyo, mwanangu?” Yakobo akamjibu, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amenifanikisha.”
21Ndipo Isaka akamwambia Yakobo, “Basi, mwanangu, karibia nipate kukupapasa ili nijue kweli kama wewe ndiwe mwanangu Esau au la.” 22Yakobo akamkaribia baba yake Isaka, naye akampapasa na kusema, “Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau.” 23Hakumtambua kwa sababu mikono yake ilikuwa yenye nywele nyingi kama ya Esau kaka yake; kwa hiyo akambariki. 24Akamwuliza tena, “Kweli wewe ndiwe mwanangu Esau?” Naye akamjibu, “Ndiyo.” 25Basi, baba yake akasema, “Niletee hiyo nyama nile mawindo yako mwanangu, nikubariki.” Hapo Yakobo akampelekea chakula, naye akala; akampelekea divai pia, akanywa. 26Ndipo baba yake Isaka, akamwambia, “Sogea karibu, mwanangu, unibusu.” 27Basi, Yakobo akamkaribia baba yake na kumbusu, na baba yake aliposikia harufu ya mavazi yake, akambariki akisema,
“Tazama, harufu nzuri ya mwanangu
ni kama harufu ya shamba alilobariki Mwenyezi-Mungu!
28Mungu akumiminie umande wa mbinguni;
akupe ardhi yenye rutuba,
nafaka na divai kwa wingi.
29Jamii za watu zikutumikie,
na mataifa yakuinamie kwa heshima.
Uwe mtawala wa ndugu zako,
watoto wa kiume wa mama yako wakuinamie kwa heshima.
Kila akulaaniye na alaaniwe,
kila akubarikiye na abarikiwe!”

Esau anaomba baraka

30Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, naye Yakobo alipokuwa ndio tu ametoka mbele ya baba yake Isaka, Esau kaka yake Yakobo, akarudi kutoka mawindoni. 31Esau pia akatengeneza chakula kitamu, akampelekea baba yake, akamwambia, “Haya baba, inuka ule mawindo yangu mimi mwanao, ili upate kunibariki!” 32Isaka akauliza, “Wewe ni nani?” Naye akamjibu, “Ni mimi mwanao Esau, mzaliwa wako wa kwanza.” 33Hapo Isaka akatetemeka mno, akasema, “Ni nani basi yule aliyewinda na kuniletea mawindo, nami nimekwisha kula kabla hujaja? Tena nimekwisha mbariki; naam, amekwisha barikiwa!”
34Esau alipoyasikia maneno ya baba yake, akaangua kilio cha uchungu. Kisha akamwambia baba yake, “Ee baba yangu, nibariki na mimi, tafadhali!” 35Lakini Isaka akasema, “Ndugu yako alikuja kwa hila, naye amechukua baraka yako.” 36Esau akasema, “Ndio maana anaitwa Yakobo! Amechukua nafasi yangu mara mbili. Kwanza alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua baraka Zangu.” Kisha akamwuliza baba yake, “Je, hukunibakizia baraka yoyote?” 37Isaka akamjibu, “Nimekwisha mfanya Yakobo kuwa mtawala wako, na kumpa ndugu zake wote kuwa watumishi wake. Nimempatia nafaka na divai. Nikufanyie nini sasa, wewe mwanangu?” 38Esau akamwambia baba yake, “Baba, kwani una baraka moja tu? Nibariki hata mimi, ee baba!” Hapo Esau akalia kwa sauti kubwa. 39Ndipo Isaka, baba yake, akamwambia,
“Makao yako yatakuwa mbali na ardhi yenye rutuba,
na mbali na umande wa mbinguni.
40Utaishi kwa upanga wako,
na utamtumikia ndugu yako;
lakini utakapoasi
utaivunja kongwa yake shingoni mwako.”
41Basi, Esau akamchukia Yakobo kwa sababu ya baraka aliyokuwa amepewa na baba yake. Esau akawaza, “Siku za matanga ya baba zitakapokwisha, ndipo nitakapomuua ndugu yangu Yakobo.” 42Lakini Rebeka alipojua nia ya mwanawe mkubwa, akamwita mwanawe mdogo Yakobo, akamwambia, “Jihadhari, ndugu yako Esau anajifariji kwa kupanga kukuua. 43Kwa hiyo, mwanangu, sikiliza maneno yangu. Ondoka ukimbilie kwa kaka yangu Labani kule Harani. 44Kaa naye kwa muda, mpaka ghadhabu ya nduguyo itakapopoa. 45Ghadhabu yake itakapopoa, naye atakapokuwa amesahau uliyomtendea, nitatuma mtu akurudishe. Kwa nini nifiwe na nyinyi wote wawili siku moja?”

Yakobo anatumwa kwa Labani

46Rebeka akamwambia Isaka, “Sina raha kabisa maishani kwa sababu ya hawa wanawake wa Esau Wahiti. Ikiwa Yakobo ataoa mmojawapo wa wanawake hawa Wahiti, maisha yangu yana faida gani?”
Mwanzo27;1-46

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN):
Jifunze zaidi

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: